Bonde la Olduvai - Picha kwa hisani ya blogu husika
|
Waziri mkuu wa kwanza wa Kongo Picha kwa hisani ya blogu husika |
Bara letu tukufu la Afrika, kwa mara nyingine limo tena katika migogoro baina yetu wenyewe. Bara Afrika lenye nchi zaidi ya hamsini lilianza kujipatia uhuru wake zaidi ya miaka hamsini iliyopita. Ghana ilikuwa nchi ya mwanzo kabisa, yenye waafrika weusi wengi zaidi, kujipatia uhuru wake chini ya ndugu Kwame Nkurumah. Na mara ya mwisho nchi ya Afrika kujipatia uhuru wake ilikuwa ni Namibia? tarehe 21 Marchi 1990. Ukiacha Sudani Kusini iliyopata uhuru wake toka kwa ndugu yake Sudani tarehe 9 Julai 2011. Afrika Kusini; iliyopata uhuru wa watu weusi walio wengi mwaka 1994 ilikuwa na hali ya kipekee sana; ilivamiwa na wazungu walioifanya nchi hiyo kuwa nyumbani kwao. Nguvu ya Umma haikuzuilika tena na ilikuwa lazima wananchi walio wengi wapate haki yao. Kwa utangulizi huu, ingawa mfupi mno kwa bara lenye kila aina ya utajiri, binafsi nadhani bara hili, japokuwa ni changa kwa umri wa mataifa ya kisasa lakini kongwe kihistoria kwakuwa ndo nyumbani kwa binadamu wa kwanza; tazama Olduvai Gorge, ilitakiwa tuwe na uwezo wa kujitawala na kujisimama wenyewe.
Afrika ina utajiri anuwai na wenye kupatikana katika nchi nyingi za barani mwetu. Pamoja na utajiri tulionao tunaendelea kuonekana kama masikini wa kutupwa. Wayuropa na Wamarekani na hata Waasia wanatufanya sisi (ama sisi wenyewe ) kama binadamu wa daraja la pili. Matokeo yake ni kubweteka, kukosa fikra zetu wenyewe, kuwa tegemezi na kusubiria misaada toka kwa hao wajomba wasiozaliwa tumbo moja na mama zetu.
Utegemezi upo kwenye nyanja nyingi sana za maisha yetu; toka kwenye mipango ya maendeleo hadi kwenye masuala ya vyakula vyetu wenyewe. Nchi zetu (kupitia viongozi tulionao) ni kama hazijui tunahitaji kitu gani na tunataka kwenda wapi. Utasikia mpango wa maendeleo tunanakili toka Ulaya na Marekani kama ilivyo ili hali tukibadilisha majina na mahitaji yetu mahususi tu. Jambo hili linadumaza hata fikra za vijana wetu shuleni na vyuoni; kwanini kuwa mbunifu ili hali mawazo yangu hayatumika popote, anajiuliza mwanafunzi. Badala ta kutumia muda mwingi kujenga fikra binafsi sahihi ni afadhali kufuatisha mawazo ya watu wengine. Utegemezi unatufanya tushindwe kujenga mambo yetu wenyewe. Mathalani kwenye elimu fursa za kimasomo zinazotolewa nje ya nchi; bila shaka ni kwa lengo zuri tu la kusaidia kujenga wataalamu toka katika nchi zinazokuwa. Hata hivyo ni vyema kutazama misaada ya aina hiyo kwa jicho la kichunguzi; inawezekana kabisa nyuma yake kuna fursa ama bidhaa zinazohitajika toka nchi zetu hivyo unazilainisha nchi hizi zinazoendelea kwa misaada midogo kama hiyo. Nasema midogo kwa sababu nchi zetu za kiafrika zina wajibu wa kujenga shule na vyuo vikuu vyenye sifa na hadhi kubwa kidunia kwa sababu vinavyohitajika kufanya hivyo vipo hapa barani. Tutazame mifano wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Kongo. Kwenye makala hii nitatumia zaidi jina KONGO
KONGO - Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Kongo ni "JITU" lililolala. Nchi hii ina utajiri asilia wa kila namna. Nchi Kongo kuna misitu asilia, madini ya kila namna, watu wenye nguvu na akili, ardhi/ wenye rutuba, mito, nguvu ya umeme, bahari, tamaduni nyingi nzuri na kadhalika. Pamoja na utajiri mkubwa usiodikika, wananchi wengi nchini Kongo hushindia mlo mmoja tena mara nyingi usio kamili. Wafanyakazi wengi nchi humo hupitisha miezi bila malipo, bidhaa nyingi zinazopatikana huko hutoka nchi jirani. Kongo ilipopata uhuru wake toka mikononi mwa Ubelgiji (kinchi kidogo kikilitawala jitu kubwa vile) tarehe 30 Juni 1960 chini ya uongozi wa rais wa kwanza Joseph Kasa vubu na waziri mkuu wa kwanza Patrice Lumumba ambaye alikuwa na mawazo mengi mazuri juu ya bara zima la Afrika, Siku ya uhuru wa nchi yake, kama ilivyokuwa huko Ghana kwa Kwame Nkurumah, aliyesema kuwa Ghana sana u huru milele, Lumumba yeye alisema Kongo itakuwa muhimili wa mambo mengi makubwa Afrika na duniani (si maneno yake moja kwa moja - mengi ni tafsiri na vionjo vyangu zaidi). Leo miaka zaidi ya hamsini kisha uhuru hakuna kiongozi wa jitu hilo kubwa aliyeweza kufikia mawazo ya mwana Afrika huyu halisi. Toka kifo chake nchi hii imekuwa itawaliwa kwa namna isiyokubalika, hususani kipindi cha rais aliyeiongoza nchi hiyo kwa muda mrefu Mobutu Sese Seko. Ndugu huyu aliifanya nchi kuwa mali yake binafsi na kufanya alivyotaka. Msemo wa Kiswahili; "Mungu si Athumani" bwana huyu aliondolewa madarakani na vikosi vya Laurent Kabila mwaka 1997. Laurent Kabila, kama ilivyo kwa historia za wapigania uhuru wengi wa Afrika, alishiriki shughuli za kisiasa toka ujana wake kwenye kikosi cha vijana cha Patrice Lumumba. Ndugu huyu alikuwa na matamanio na nia njema sana ya kuleta uhuru wa kweli kwa watu wa Kongo, lakini alishindwa kwa kuwa alikuwa amefungamana na makundi yaliyokuwa na uchu mkubwa wa mali za nchi hiyo. Hivyo miaka minne baadaye aliuwawa. Toka kuuwawa kwake bado hakujawa na uimara thabiti japokuwa Joseph Kabila, mtoto wa rais kabila, anajitahidi kuongoza nchi hiyo kubwa. Hata hivyo kuna waasi wanaoibuka na madai mbalimbali juu ya Kongo.
Hivi karibuni kumezuka kikundi kingine cha waasi maarufu kwa jina M23. Hili ni moja kati ya makundi mengi ambayo tayari yamekwishaibuka ili kudai wanachoita kuwa haki zao. Yamewahi kuibuka makundi mengine kadhaa wa kadhaa "Banyabulenge" na mengine. Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, mashirika ya kikanda na mashirika mengine mbalimbali duniani yamejaribu kuleta amani ya kudumu bila mafanikio ya kweli kwa muda mrefu sasa. Binafsi nadhani suluhu kwa machafuko ya Kongo imo mikononi mwetu Waafrika na nadhani tunaweza kujilinda na kujiletea maendeleo ya kweli. Kongo ina utajiri mkubwa mno kiasi kwamba wengi wanaokwenda kupatanisha wanaingia kwenye mtego wa kujichukulia utajiri huo japokuwa kidogo- ni vigumu kupata ushahidi wa kuandikwa katika haya lakini kuna mambo mengi yanaendelea. Umoja wa Afrika kwa makubaliano ya Kongo unaweza kujenga jeshi imara na kulinda amani itakayoleta maendeleo ya kweli kwa nchi hiyo. Naamini kuwa uchumi wa Kongo ukiwa imara uchumi wa bara zima utanufaika na kukua vyema zaidi. Afrika tuna uwezo na wa kufanya mambo yetu wenyewe shida ni huko kupumbazwa na Wayuropa na Wamarekani - matokeo yake tunajihisi kuwa hatuwezi. Afrika simama mwenyewe imara unaweza!