Tuesday, October 9, 2018

TAKE THE STAIRS - PANDA NGAZI



Success is never owned, it is only rented and the rent is due every day". 

Kitabu rejea;TAKE THE STAIRS (7 steps to achieving true success).By Rory Vaden.

Katika maisha yetu wanadamu kila mtu huwa anapenda kufanikiwa kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni kwenye biashara,taaluma,ama ujuzi alionao.Ila watu wanashindwa kufahamau njia bora za kufikia mafanikio yatakayowapa raha na furaha ya kudumu.Mafanikio yoyote yanapatikana kwa hatua na si jambo lijalo kwa ghafla tu,na tatizo linalowamaliza watu ni kuishi kwa kudhani mafanikio unaweza yafikia kwa mfano wa kupanda lift ya ghorofa na punde ukajikuta umeshafika ghorofa ya tano,lakini mafanikio hayapo hivo,mtu yeyote ukitaka kufanikiwa ni lazima upande ngazi(hatua) ili uende hatua kwa hatua,labda jiulize swali dogo tu je, upandapo lift katika ghorofa mwili wako huwa unapata faida ipi? ,hebu mtazame mtu apandae ghorofa kwa kutumia ngazi,mtu huyu hupata faida nyingi ,kwanza mwili wake unapotoa jasho huujenga na kupunguza sukari isiyotakiwa mwilini  na faida nyingine kadha wa kadha.Huu ni mfano tu wa ngazi za kupanda katika jengo,basi ndivyo yalivyo na mafanikio  ya mtu huwa yanahitaji kuyaendea kwa kufuata hatua ili uweze kuwa na uchungu nayo pale ukishayapata,jitoe mapema kwenye ESCALATOR MENTALITY ili usizidi kuupoteza muda.

Mafanikio ya mtu yeyote yanajengwa kwa mtu kuwa na nidhamu kubwa na si kwa njia za mikato kama watu wadhaniavyo.Kuwa na nidhamu binafsi (self discipline) si jambo jepesi hata kidogo,uonapo watu wamefanikiwa jua kwamba walitengeneza nidhamu zao binafsi,hawakungoja kusukumwa sukumwa katika kutenda yale wapendayo kuyatenda na ndipo walijikuta wakifika kule walipotamani kufika.Mpendwa msomaji nikuambie tu wazi,utakapo amua leo kujijengea nidhamu binafsi jua si jambo ambalo utalipata kwa wakati mfupi na pia hutalipata kwa gharama ndogo,jipange kujitoa kwelikweli ili ujijengee nidhamu binafsi katika kazi yako,biashara yako,kipaji chako n.k.

Pia watu wengi hupenda na hutamani kufikia hatua kubwa za mafanikio lakini sumu kubwa inayowamaliza ni tabia ya kupenda kuhairisha mambo.Unakuta mtu anatamani kuwa mfanyabiashara mkubwa lakini kila siku husema nitaanza kesho Mwandishi mmoja alisema "successful people form the habit of doing things that failures don't like doing".Na hivi ndivyo watu wakubwa wanavyofanikiwa ni kwa sababu hawaghairishi mambo na nidhamu zao za hali ya juu ndizo zinazowasaidia kuviishi  viapo vyao.

Lakini pia watu hudhani watu waliofanikiwa walikutana utajiri wa kifedha,kuwa na biashara kubwa,ama ubobezi katika fani fulani kwa siku moja,lakini si kweli,ukirudi na kufuatilia watu wote waliofanikiwa walipita maisha ya kufanya mambo madogo madogo yaliyo na tija katika maisha yao na baadaye wakajikuta yakiwaletea matokeo makubwa(small choices yield big results),anza kujijengea nidhamu katika mambo madogo madogo nawe utajishuhudia ukipiga hatua siku baada ya siku.

Ukiwa na nidhamu maishani utaishi maisha unayoyapenda ikiwa ni katika biashara yako,katika kazi yako au ujuzi wako na maisha hayo ya furaha hayatakuwa ya muda bali  yatakuwa ni ya kudumu maishani mwako,kumbuka kuwa mafanikio hayana umiliki wa kudumu ni kama kitu kilichokodishwa tu na gharama yake ya kulipia ni nidhamu.Ikiwa unataka uwe na afya bora lazima uwe na nidhamu katika ulaji wako,ukiwa unataka mafanikio ya kibiashara ni lazima uwe na nidhamu katika biashara yako,ukiwa unataka ndoa yako iwe yenye furaha lazima uwe na nidhamu katika ndoa yako n.k.

Nenda kafanyie kazi haya machache niliyokushirisha ukilianza vyema juma hili la 41 katika mwaka wetu 2018,na nitaendelea kukushirikisha hatua 7 saba muhimu za kufikia mafanikio yoyote makubwa,njia hizi amezielezea vyema mwandishi Rory Vaden.Nikutakie heri wewe unaeenda kuchukua hatua ya kuyafanyia kazi yale ambayo umejifunza.

Na mwanafunzi wa kudumu wa shule ya maisha, Mchambuzi wa vitabu na Mshairi;
Marko Kinyafu.
+255 714 129 520.
Dar es salaam,Tanzania.

Kupata maarifa ni bure ila kulipa gharama ya ujinga ni kazi kubwa kuliko gharama unayoikimbia sasa ya kupata kile kilichobora kwa ukombozi wa fikra zako.


Sunday, October 7, 2018

WHO WILL CRY WHEN YOU DIE? - NANI ATALIA UTAKAPOKUFA?



Tafakuri ya leo; Uchambuzi wa kitabu kiitwacho WHO WILL CRY WHEN YOU DIE Na Robin Sharma.

Habari mpendwa msomaji wa makala hizi naamini unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku,basi leo nimetamani tupate muendelezo na tuendelee kujifunza katika mambo mazuri ambayo mwandishi Robin Sharma ametushirikisha katika kitabu chake cha Who will cry when you die.Kwenye makala iliyopita tulipata kuona mambo tisa kati ya 101 basi leo tuendelee kujifunza mambo mengine machache ambayo tukiyatenda hakika itakuwa ni faida kwetu na kwa vizazi vijavyo.

Jambo la kwanza ni kuishi kinyenyekevu(be humble),mtu yeyote aishiye maisha ya unyenyekevu kwanza kabisa huwa tayari kujifunza kwa wengine lakini pia hujijengea mahusiano bora na watu wanaomzunguka na jamii kwa ujumla,hivyo unyenyekevu ni silaha kubwa sana ya kuishi nayo,jamii itakuwa ikijifunza kwako na itamani kuendelea kuwa na wewe na hata siku ukifa itakukumbuka na kukulilia sana.

Jitoe kubeba hatari kubwa(risks).Siku zote mtu aliyeradhi kubeba hatari kubwa huwa ndiye anayepata matokeo makubwa,hivyo basi usiwe muoga kubeba hatari kubwa katika maisha yako binafsi,jamii na hata kwa taifa kwa ujumla.

Acha kuwa na hofu na vitu ambavyo huna uwezo wa kuvibadilisha.Hii pia ni moja ya changamoto kubwa sana watu wanayokutana nayo katika maisha yao ya kila siku,unakuta mtu anawaza mambo makubwa na ya hatari ambayo hayawezi kutokea ama hana uwezo nao wa kuyabadilisha,ndugu yangu acha kuwaza vitu vilivyo nje ya uwezo wako,maana hatari yake ni kuwa utajikuta ukipoteza nishati nyingi huku ukipata matokeo kidogo na hii ni hasara.

Penda kazi yako.Kuna msemo unasema "kazi mbaya ukiwa nayo",hii huonyesha ni jinsi gani watu hudharau kazi zao pindi pale wanapokuwa wakizifanya na kujiona kama wao ni watu duni tofauti na wengine,lakini dhana hii ni potofu,unachotakiwa ni kuipenda kazi yako hata kama ni ndogo kiasi gani au wewe unaiona ni dunia kiasi gani utakapoipenda kazi yako utaifanya kwa ufanisi na hata wale uwapao huduma yako watavutiwa sana na watakukumbuka sana hata siku ukiwa haupo tena duniani.

Pia tuwapo katika shughuli zetu za kazi baada ya kumaliza wakati mwingine hujikuta tukiwa tumechoka na wenye mawazo mengi sana,lakini unachotakiwa kufanya ni kutafuta namna ya kuondoa hayo mawazo ya kazi kabla haujafika kwenye mlango wa nyumbani,kumbuka kwamba na familia nayo inatamani uwepo wako hivyo unapofika huku ukiwa na mawazo hutakuwa na uwezo wa kushirikiana vyema na familia yako na hii hupelekea kupunguza mahusiano mazuri na familia yako.Unaweza sikiliza miziki tulivu hii itakusaidia kukuweka sawa kiakili kabla hujafika nyumbani.

Kusanya nukuu(Quotes) zote uzipendazo.Nukuu za watu wakubwa ama wabobezi wa jambo fulani ni moja kati ya vitu muhimu sana vinavyozidisha hamasa(inspiration) kwa mtu mwingine kutenda jambo kama hilo.Kusanya nukuu uzipendazo zitakusaidia kukupa msukumo wa kufanya mambo makubwa.

Andika tena historia ya maisha yako.Uandishi wa historia za maisha yetu ni jambo muhimu sana japo si wengi wenye utamaduni wa kufanya hivyo,wengi huupuuzia tu na kuona kuwa hamna haja ya kufanya hivyo,lakini wakiwa hawajui kuwa wanapoteza kitu kikubwa sana.Unapoandika historia ya maisha yako husaidia kujitathimini kwa siku za mbeleni kuwa wapi ulipotoka na wapi ulipo sasa,lakini pia kuacha historia yako siku ukifa ni alama pia.

Piga picha nyingi kadiri uwezavyo.Katika jambo jingine muhimu sana japo laonekana kama ni la kawaida kawaida ni hili la upigaji wa picha.Picha zina faida nyingi kwanza ni kumbukumbuku,lakini pia hukuonyesha taswira halisi ya maisha yako wapi ulipokuwa na wapi ulipo sasa,siku ukifa watu watazitazama picha zako na kuendelea kukukumbuka daima,anza leo kupiga picha na uziweke kwenye kumbukumbu nzuri ikiwa ni kwenye nakala tete(soft copy) au hata kwenye nakala ngumu(hard kopi).

Wenye hekima wakubwa walioishi miaka ya zamani walisema; ukitaka kuishi maisha ya kikamilifu fanya vitu vitatu kabla hujafikwa na umauti,vitu hivyo ni,ZAA MTOTO,PANDA MTI na ANDIKA KITABU,hivi vitu vitatu si lazima uvifanye vyote japo ukiweza kuvitenda vyote ni heri.Ukifanikiwa kuwa navyo vitu hivi huwa ni urithi mkubwa utakaokuja kuuacha duniani,hata siku ukifa lakini hazina hii itaishi kwa miaka mingi sana.

Mwisho kabisa Ishi maisha ya kikamilifu ili uje kufa ukiwa mtu mwenye furaha.Hapa lipo somo kubwa sana watu wamekuwa wakiishi mambo ambayo sio kusudio lao waliloitiwa duniani,unakuta mtu anasoma uhasibu kwa sababu familia yao nzima ni wahasibu lakini yeye fani hiyo haikiwa wito wake, na hii hupelekea watu kuishi maisha yenye huzuni na mateso makubwa,inachotakiwa ni mtu uishi kikamilifu katika lile kusudio lako uliloitiwa hii itakufanya uishi kwa amani na hata siku ukifa utakufa ukiwa na furaha.

Haya ni machache niliyotamani nikushirikishe mpenzi msomaji,utakapopata wasaa wa kukisoma kitabu hiki hakika utajifunza mengi zaidi.Ruhusa kuwashirikisha na wengine tunaoona wana kiu ya kupata maarifa na kama utakuwa unahitaji kitabu hiki utanipata kwa barua pepe na namba za simu nitakazo kuachia.Nikutakie heri sana wewe unaenda kuchukua hatua ya kufanyia kazi.

Na mwanafunzi wa kudumu wa shule ya maisha, mchambuzi wa vitabu na mshairi;

Marko Kinyafu
+255 714 129 520
Dar es salaam,Tanzania.

HAIJALISHI UMESHAPOTEZA MUDA KWA KIASI GANI,NAFASI YA KUFIKA KULE UNAPOTAKA KUFIKA BADO IPO KAMA UKIAMUA LEO.


Friday, October 5, 2018

WHO WILL CRY WHEN YOU DIE - NANI ATAKULILIA SIKU UKIFA?


Tafakuri ya uchambuzi wa kitabu kiitwacho: WHO WILL CRY WHEN YOU DIE (Nani atakulilia siku ukifa?),Na Robin Sharma.

Habari mpenzi msomaji makala hizi,ninatumai u mzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku,leo nimekuja na uchambuzi wa kitabu cha mwandishi Robin Sharma(WHO WILL CRY WHEN YOU DIE)  nakukaribisha nawe usome uchambuzi huu naamini kuna mengi utaenda kujifunza.

Kwanza kabisa katika maisha haya tunayoishi lazima tukumbe kuwa ipo siku yana ukomo wake,hakuna ambaye ataishi milele.Sasa je ulishawahi kujiuliza nani atakulilia siku ukifa?,mwandishi Robin Sharma anaeleza mambo 101 katika kitabu hiki lakini embu twende kuona haya machache na siku baada ya siku tutazidi kujifunza mengine.Karibu,

1.Chunguza na ujue wito wako ni upi? yaani uliletwa duniani ili uje kufanya nini? ukikaa na kupata jawabu,anza kuishi kwa lile kusudi uliloitiwa kuja kulifanya duniani ili uache alama yenye kukumbukwa na kila mtu hata siku ukiwa haupo tena duniani.

2.Jifunze kuwa na shukrani kwa watu,jijengee tabia ya kushukuru hata kama ulichopewa ni kidogo ila ukiweza kuthamini kilicho kidogo basi utaweza kuthamini hata kilicho kikubwa pia.

3.Simamia mitazamo yako,ili utimize lile kusudi ulilolipanga kulitekeleza.

4.Jifunze kuwa na nidhamu binafsi(self discipline),hii itakusaidia kuwa na nidhamu katika utendaji wa mambo yako bila ya kuyumbishwa tena utayatimiza kwa wakati muafaka.

5.Weka kumbukumbu ya yale uyafanyayo kila siku,andika katika notibuku yako ili uweke kumbukumbu na upate tathimini ni wapi pa kujirekebisha.

6.Jijengee tabia ya kuwa muaminifu.Unapotoa ahadi na ukashindwa kuitekeleza jua kwamba uaminifu wako unapotea kwa watu na mwisho wa siku utajikuta ukiangukia katika mahusiano mabaya na watu.Kaa chini kisha jitafakari ni mambo mangapi uliyoahidi ndani ya wiki na hujayatekeleza? ukipata jibu tafuta njia ya kujiboresha ili usirudie makosa.

7.Anza siku yako vizuri.Asubuhi ukiamka tenga japo dakika 30 za kujipanga kwa siku yako ujue kuwa itakwendaje na angalia tathimini ya siku yako iliyopita ila leo ufanye mambo kwa uzuri zaidi.

8.Jifunze kusema hapana.Hapa ipo shida kwa wengi,watu wanashindwa kujizuia kufanya mambo hata ambayo hayana faida yoyote kwao,embu jijengee tabia ya kusema hapana sio kila kitu ukiambiwa utende basi unakuwa mwepesi kutenda,ukifanya hivi itakusaidia kuokoa muda wako na kufanya mambo kwa uzuri zaidi.

9.Tenga siku yako ya mapumziko,jiwekee muda wako hata kama si siku nzima ila tenga masaa utakayopumzika na kupumzisha akili,ikiwa ni pamoja na kukaa na familia ama ndugu kisha ujipange kwa mwanzo mpya wa juma linalofuata.

Machache haya yanaweza kukusaidia endapo utachukua hatua ya utendaji,nami nikutakie kila heri katika hatua unayoenda kuchukua ya kufanya maamuzi ya kutenda.

Na mwanafunzi wa kudumu wa shule ya maisha,mshairi na mchambuzi wa vitabu;
Marko Kinyafu
+255 714 129 520
Kinyafumarcos@gmail.com.

AMKA HAPO ULIPOKAA KUNA MAVUMBI,SIMAMA UJIFUTE NA UANZE KUSONGA MBELE.

Thursday, October 4, 2018

THE POWER OF READING BOOKS - NGUVU YA USOMAJI VITABU



Tafakuri ya  kitabu cha THE POWER OF READING BOOKS(Nguvu ya usomaji vitabu) Na. Shemeji Melayeki.

Mpendwa rafiki natumai haujambo,kwa wasaa mwingine natamani nikushirikishe mambo machache ambayo mwandishi Shemeji Melayaki ameyaelezea katika hiki kifupi kabisa chenye kurasa 14 tu,lakini kikiwa kimesheheni somo kubwa sana,basi nawe karibu twende pamoja.

Watu wakubwa waliowahi kuwapo na waliopo duniani mafanikio yao ukiwafuatilia utawakuta walikuwa ni wasomaji wakubwa wa vitabu,tabia ya usomaji vitabu imekuwa ni ngumu sana kwa watu kuiigia kutokana na uvivu mkubwa watu walionao na hali ya kupenda kuhairisha mambo na hii hujikuta kuona kama suala la usomaji wa vitabu ni la watu fulani au la watu wachache lakini hii si kweli,ila mtu yeyote atakae kufanikiwa sharti asome vitabu ili apate maarifa thabiti katika lile eneo analotaka kujinoa ikiwa ni katika kipaji,biashara,ujuzi,nk.Tabia huathiriwa na tabia hivyo tabia ya kutopenda kusoma vitabu itaathiriwa pale tu utakapo chukua uamuzi leo wa kuanza kusoma vitabu.

Description: 📚Yapo mambo mengi sana mtu hupata faida baada ya kusoma vitabu,machache miongoni mwa hayo ni kama;

-Maarifa humuongezea mtu nguvu ya kujiamini na kufanya mambo makubwa kwasababu anakuwa ana uhakika na lile alifanyalo.

-Maarifa yanamuongezea mtu nguvu ya ushawishi katika kutekeleza mambo makubwa,kwa sababu vipo vitabu vingi vinavyolezea jinsi watu walivyofanikiwa katika maisha yao mfano kitabu cha I CAN,I WILL,I MUST the keys of success kitabu hiki kinaeleza jinsi Dr Regnald Mengi alivyopitia changamoto nyingi hadi kufikia hapa alipo sasa,hivyo nawe kupitia kusoma kitabu utapata nguvu ya ushawishi wa kuona kuwa kumbe mambo makubwa yanawezekana endapo tu ukiamua kweli kuchukua hatua.

-Kitabu huyaunganisha mawazo ya msomaji na mwandishi wa kitabu kwa kupitia njia ya usomaji.

-Viongozi wote ni wasomaji vitabu(all leaders are readers),huwezi kuongoza kama hupendi kusoma vitabu.

-Maarifa ya vitabuni huunoa ujuzi wako na kukufanya uwe bora zaidi katika eneo lako unalofanyia kazi ikiwa ni biashara,kipaji,huduma n.k,Mungu mwenyewe hutumia kitabu kuweka taarifa zake,je si zaidi sana sisi wanadamu? ,Kutoka 32:33
*BWANA akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu.*

Description: 📖MBINU ZA KUANZA KUWA MSOMAJI VITABU.

~Kwanza kabisa tafuta vitabu vya eneo ambalo unapenda kujifunza hii itakufanya uwe na hamasa ya kupenda kujifunza kila siku.

~Anza kwa kusoma kitabu kidogo kwa kuanza na kurasa chache chache mwisho utajikuta ukipiga hatua siku hadi siku kama vile wenye hekima walivyosema kuwa haba na haba mwisho hujaza kibaba.

~Soma kila siku.Usiache tabia ya kusoma japo kwa kurasa chache mwisho utajikuta hii itakuwa ni tabia yako ya kudumu.

~Fanya tafakuri ya yale uliyojifunza.Kufanya tafakuri ni sawa na mmeng'enyo wa chakula baada ya mtu kumaliza kula,nawe ukimaliza kusoma kitabu yaangalie yale uliyojifunza kwa kupiga picha na jinsi maisha yako halisi yalivyo,kisha chukua hatua ya kutendea kazi.

~Shirikisha wengine yale unayojifunza.Usiwe mchoyo wa kuwapa wenzio yale uyajauyo,kwa jinsi unavyozidi kushirikisha watu kile ukijuacho ndipo unapozidi kuwa bora zaidi(master) katika eneo hilo.

Anza leo kusoma vitabu ukianzia kwa hatua ndogondogo huku ukiweka nia ya kutamani kupiga hatua zaidi.Aonaye kununua kitabu ni gharama kubwa basi asubiri kulipa gharama kubwa zaidi atayoilipa kwa kutosoma vitabu.Mtu asiyesoma vitabu uhisi dunia ni kama sehemu ndogo ambayo unaweza kuizunguka na kuimaliza punde kama vile uzungukavyo kijiji,lakini si kweli,ila uhalisia ni kuwa dunia ina vitu vingi sana ambavyo kila siku tunatakiwa kujifunza na hatutavimaliza hadi siku tunakufa,basi anza leo nawe kuishi kiutoshelevu ili uje kufa ukiwa tupu.

Nikutakie heri wewe uendaye kuchukua hatua katika kutenda na hakika ipo siku utajishuhudia jinsi utakavyo kuwa mtu mpya siku baada ya siku katika eneo la maarifa.


Mimi Mwanafunzi wa shule ya maisha,Mchambuzi na mshairi.
Marko Kinyafu.
Description: 📞📩+255 714 129 520
Dar es salaam, Tanzania.

_Kuyatawala maisha huanza kwa kuitawala siku moja na siku yenyewe ndio leo_


THE POWER OF READING USEFUL BOOKS - KUSOMA VITABU VIFAAVYO HUONGEZA MAARIFA!


Ndugu msomaji wa blogu ya Wajenga Dunia,

Habari za siku nyingi? Bila shaka u mzima wa afya tele. Napenda kukukaribisha kwa mara nyingine katika ukurasa huu ili uendelee kujipatia maarifa yafaayo maishani.

Kuanzia sasa nakufahamisha kuwa tutakuwa tukifanya tafakari ya vitabu mbalimbali vyenye kukupatia maarifa na ujuzi wa mambo anuwai. Karibu sana. Kwa kila tafakari kutakuwa na mawasiliano ya mwandishi wa makala ama tafakari husika ili kama ukitaka kuwasiliana naye basi ufanye hiyo.

Martin Mandalu
+255 767 864 379