JITIHADA ZETU ZILENGE
KUJITOA KATIKA HALI YA UCHUMI TEGEMEZI
Mapema mwezi huu kulikuwa
na semina ya wazalishaji wakubwa ambayo iliandaliwa na Chama ili kubadilishana
mawazo juu ya maswala mbalimbali. Ufuatao ni muhtasari wa hotuba ya mwenyekiti
wa Chama, Mwalimu Julius Nyerere, wakati akifunga semina hiyo kwenye Chuo cha
Usimamizi wa Fedha, Dar es Salaam.
Ndugu Rais na ndugu wanasemina,
Sasa imefikia wakati tuifunge semina hii. Hatuna muda mrefu sana
wa kutumia kwa kufunga, na kwa sababu haya nitakayoyasema hayakuandikwa sina
hakika yatachukua muda gani, lakini wale ambao mmefunga mtaniwia radhi nikivuka
muda kidogo.
Sasa kwanza mimi ningeanza na shukrani... ninalazimika kuanza kwa
shukrani kwa sababu mbili. Kwanza, semina hii niliitaka mimi. Niliiomba mimi na
ninawashukuru wote waliojitahidi kuandaa mpaka ikawezekana.
Pili, ninawashukuru sana watoa mada wa leo. Bahati mbaya muda
umekwisha, sikuwapa nafasi ya kurudia. Wenzao niliwapa nafasi ya lakini watoa
mada wa leo sikuwapa nafasi. Lakini watoa mada wote nawashukuru kwa ubora wa
mada zao na jinsi walivyozitoa kwetu. Nawashukuru sana.
Tatu, nawashukuru wote walioshiriki kwenye mjadala huu. Kwa upande
wangu mimi na kwa upande wetu wale tuliofikiria kuandaa hii, tumeona kama
mazungumzo haya yamekuwa mazungumzo ya manufaa.
Baadhi yetu nasema pengine semina hii isiwe mara moja lakini kwa
baadhi yetu nadhani hata kama haitakuwa katika hali sasa, hatuwezi kila wakati
tunamchukua Rais mara nyingine hivi tukae nae siku tatu maana Rais anazo kazi
nyingi huko.
Lakini tunaweza kutafuta njia nyingine ya kuweza kuendelea na mazungumzo
yanayotuchanganya changanya. Watu wa namna hii katika ngazi mbalimbali si
lazima tuwe na Rais na baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali
ambao wanazo kazi zao.
Lakini nasema kwa kifupi napenda kuwashukuru sana wote
waliotusaidia kutufikisha mazungumzo haya kwa ubora wa mazungumzo na kwamba
mmeweza kusema waziwazi. Mimi nimefarijika sana na kwamba mmeweza kusimama na
kusema kila mtu anavyoona.
Kama nilivyosema nilipokuwa nikifungua semina, mimi sasa hivi nina
kofia mbili. Kofia moja, mwenyekiti wa Chama chenu, na kofia nyingine
Mwenyekiti wa Tume ya Kusini. Kusema
ukweli, kazi zote mbili zinafanana, lakini ni matatizo tu. Tunazungumza
matatizo yetu haya na miaka miwili mitatu nimeweza kuyaona matatizo haya.
Ninalosema karne ya 21 bado
kuna miaka 11 tu inakuja, tatizo letu la msingi ni la nchi za Kusini zote. Nalo
ni hili, uchumi wetu una sifa mbili. Sifa ya kwanza ya uchumi, duniani; uchumi
huu unapitanapitana. Uchumi wa Tanzania ni tofuti na uchumi wa Brazil au wa
India au wa China au hata wa Zimbabwe. Na huu ni uchumi duni kwa maana mbili.
Maana ya kwanza, maana ya hali halisi ni hii inachanganya zote, maana ya hali
halisi ni kwamba ukienda kwa mfano tu, sisi tunalima kwa jembe la mkono,
tunatumia mikokoteni. India, mpaka leo, wanatumia mikokoteni ya ng’ombe, pale
New Delhi ziko sekta utazikuta ni sekta za maendeleo lakini ni uchumi wa namna
hii, nasema ni duni kwa namna hii. Namna ya kwanza ni hiyo hiyo ni kweli kwa
sababu bado kuna shughuli nyingine zinafanywa katika hali ya nyuma kabisa.
Pili, uchumi duni kwa
kulinganisha na wenzetu wa Kaskazini. Ukitazama sisi na ukitazama uchumi wao,
uchumi wetu uko nyuma. Sifa ya kwanza ya uchumi wetu ni duni, hii sifa ya uduni
ni mbaya lakini si mbaya sana hii, inawezekana ikawa ni kama la kawaida. Kwa
nini? Kwa sababu kama kuna duni kule ni uchumi ulioko nyuma kama maana yake
ingekuwa uchumi mchanga, uchumi ambao haujakomaa. Juzi nilitumia mti, mti mmoja
umepandwa ni mkubwa umestawi na ndege wa anga wanakuja mle wanastawi. Mti
mwingine wa mbegu ile ile umepandwa lakini bado ni mdogo lakini wa aina ile ile
na bado unakua.
Sasa unaweza ukawa na mti
huu umekomaa, huu bado lakini ni mti. Hali yake ni nzuri tu, upe muda na kuumwagia
maji na siku moja mti huu kwa namna yake utakuwa imara na kuanza kutoa matunda.
Kwa maana hiyo, uduni huo ni uchumi uko nyuma isingekuwa mbaya kama ingekuwa
sifa hiyo peke yake tu tungeweza kuutilia mbolea uchumi ule utabadilika.
Lakini uchumi huu una sifa
ya pili, ni uchumi tegemezi. Ni uchumi unaotegemea Kaskazini, tena sifa ile ya
kutegemea inaupa ugonjwa. Kwa hiyo, utegemeaji ule ni kama maradhi; maradhi
hayatokani na uduni peke yake, maradhi, hasa ya uchumi wetu ni ule utegemezi
wake kama kama hivyo, ni duni tu kwa maana ya uchumi mchanga, haujakomaa lakini
una afya. Ni sawa na mtoto, unakua tu, lakini ni uchumi tegemezi. Ni ugonjwa.
Ni kilema. Ni uchumi kilema.
Safari moja jeshi letu
nadhani lilikuwa likiadhimisha miaka 20 ya kuanzishwa jeshi. KamaCommander-in-Chief,
nilikwenda pale uwanjani na jeshi letu lilipitisha silaha zake na zana za vita.
Zilikuwa nyingi, gwaride zuri, nikaziona zote – zote zinatoka nje, zote kabisa.
Leo siku ya kujivunia kidogo, jeshi letu limetimiza miaka 20. Kwa hiyo ni siku
ya kujivuna, lakini hii paredi, tunaparedi nini? Hatuparedi jeshi, tunaparedi
biashara. Huwa ni gwaride la namna hii. Tangu hapo huwa natembea nakwenda
kwenye nchi za ndugu zetu, siku zingine nakaribishwa nayaona maparedi hayo
hayanivutii, isipokuwa yanavutia kwa ufanisi wa Kaskazini wa kuvuta pesa za
maskini hawa wa Kusini.
Kwa hiyo, kama unatazama
magwaride ya kijeshi, kama unatazama viwanja vya ndege, sisi hatuna ndege
nyingi sana, lakini hata Dar es Salaam nenda uone ndege ziko pale. Hata Dar es
Salaam utakuta ndege pale. Magwaride ya majeshi, viwanja vya ndege, hata nchi
zenyewe ziwe zina mali nyingi kama vile nchi zenye uwezo wa kutoa mafuta,
utakuta zimejaa tele viwanja vya madege makubwa makubwa ya kila aina.
Mabarabara yetu katika nchi
za Kusini yamejaa magari tele, ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam. Kwa baadhi ya
nchi zingine, hata bidhaa madukani, maduka yamejaa tele – zimetengenezwa wapi?
Yote hayo kama magwaride, kama ni viwanja vya ndege, kama magari, kama ni
bidhaa madukani nasema kwa baadhi ya nchi fulani fulani hata kama ni Coca-Cola
ni maonyesho, ni magwaride ya utegemezi kote katika nchi zetu.
Kwa Coca-Cola, kwa sababu
Marekani wao wana nguvu sana kwa Coca-Cola, Marekani sasa anataka wote tuwe ni
wanywa Coca-cola. Ndugu Mengi mkipenda msipende, mtatuuzia tu Coca-Cola basi
Coca-Cola inauzwa tu.
Sasa uchumi wetu basi ni
uchumi tegemezi. Uchumi wa nchi zetu hizi zote una sifa hizo mbili. Hili tatizo
letu kubwa la msingi. Uchumi wetu ni uchumi duni, lakini uduni peke yake si
kitu sana, lakini tatizo kubwa kabisa kabisa ni uchumi tegemezi.
Kwa hiyo tunajivunia ule
ugonjwa… tunajivunia ule ugonjwa wala hatuuonei haya… unaparedi silaha za
wakubwa, unaparedi madege ya wakubwa, unaparedi bidhaa za wakubwa, unaparedi
ma-Coca-Cola ya wakubwa na unajivuna tu, unasema sisi tumeendelea. Ukimwambia
umeendelea kwa nini atakwambia njoo uone barabara yetu.
Sasa nasema hilo ndilo
tatizo letu la msingi watu wote – nchi zote za Kusini na hapa tujenge uchumi.
Pamoja na kwamba uwe ni uchumi haulingani na wa wakubwa lakini ni uchumi
unaokua.
Kwa hiyo jitihada zetu ziwe
ni kujitoa katika hali hii hasa sifa hii ya pili. Kwa sababu bila kuitoa sifa
hii ya pili ni vigumu sana kupambana na sifa ya kwanza. Kwa nini? Kwa sababu
katika nchi kama Tanzania…, Tanzania si mfano mzuri sana lakini upo, zipo
sehemu mbili. Acha ile Ndugu Idi Simba alikuwa anasema ‘informal sector’
na ‘formal sector ‘. Ipo tunayo sisi hapa na zipo katika sehemu
zetu zote.
Tunao uchumi tunaweza
kuuita wa kisasa. Uchumi wa kisasa ni ule uchumi uliochuma. Uchumi wa kisasa
katika nchi hizi ni wa kigeni. Kwa hiyo, Coca-Cola, chombo cha kigeni ni mtambo
unapokea tu pale.
Eh! Yuko Mhindi mmoja
Kiswahili chake kilikuwa kizuri sana kuliko cha Babu Patel, aliniambia:
‘‘Mwalimu ee wewe sema nakwishakata mirija, lakini bomba je kwishakata?’’ Sasa
mabomba… sasa uchumi wetu ule wa kisasa ni wa mabomba, mwanzo wake huko nje.
Utazameni wote. Utazameni. Ni wa mabomba, na madhali hii sekta ‘modern’
ni ya mabomba, hii sekta ‘modern’ hii msingi wake ni nje, ni tegemezi si
yako. Ni vigumu kwamba ‘modernisation’ ya ya sekta nyingine ambayo si ‘modern’
itatokana na nguvu yako, itatokanaje na nguvu yako? Si yako hii sekta ‘modern’,
si yako hii.
Hivi upewe na Marekani
kiwanda chake cha Coca-Cola hapa halafu ukiendeshe kwa madhumuni yako? Ndivyo
kweli kwa kitu kingine chochote mtakachokubaliana naye umwendeshee hapa
Tanzania kwa masharti yake, mnamwendeshea chake kwa masharti yake kwa faida
yake. Sasa nasema hilo ndilo Tatizo namba moja kwa nchi zetu.
Na nchi zote tunazosema,
zote ziwe za kibepari ama za kijamaa, madhali tatizo hili ni la kawaida kwao,
hazina budi zipambane nalo. Ni yao yote ikiwa ni mabepari, wakiwa wajamaa ni
tatizo. Na kweli, tatizo la nchi ni tatizo linawahusu wote.
Nyingine nasema lazima
tushirikiane. Nasema kushirikiana humu si rahisi. Sasa mimi wenzangu nadhani
tutafanya mapendekezo. Mapendekezo yetu katika kupambana na tatizo hili na
msingi mmoja ni umoja. Ninasema tunaona jinsi tutakavyofanya na tutaiambia kila
nchi tumieni uwezo wenu wa ndani wote kwa ajili ya maendeleo. Hapana kukimbia.
Mnatoka nje haraka haraka kabla ya kuonekana uwezo wenu wote wa nyumbani unapatikana.
Lakini tutasema vilevile tumieni kikamilifu ushirikiano wenu kwa ajili ya
maendeleo.
Tukitaka sisi washauri
tutakwenda nje, tunaletewa wabovu zaidi kuliko hawa, wengine wamefundishwa na
hawa hawa. Sasa tumieni watu wa nyumbani hapa. Tumieni kikamilifu uwezo wenu wa
ndani. Pili, kama nyumbani hawapo uliza Kenya – vunja hii kasumba yako hii,
uliza Kenya, uliza Uganda, uliza Zimbabwe, uliza Malawi , potelea mbali. Kwa
sababu katika hii lazima tushirikiane wote… Uliza Malawi : ‘‘Tunataka
mtaalamu wa aina fulani hivi, hamna hapo mtaalamu huyu?’’ Uliza Malawi, uliza
Zimbabwe, uliza Msumbiji, kama huna uliza sehemu nyingine Afrika. Hakuna. Uliza
India. Hata hii akili tegemezi kwamba India ni nchi yenye nguvu za nyuklia
kwamba haina washauri ambao wanaweza wanaweza kukusaidia nyie hapa. Huu ni
ukoloni. Nasema tutapendekeza hilo hapa.
Kwanza tumieni kikamilifu
uwezo wetu wa ndani kujitegemea. Pili, tumieni kikamilifu uwezo wenu wa
ushirikiano katika ngazi mbalimbali. Nchi mbili, nchi tatu, nchi nne. Fanyeni
hivyo na muuone utegemezi kuwa ni adui. Muuone hivyo na muupige vita, hivyo
msiufurahie, mnafurahia maradhi. Mnafurahia ukoloni. Sasa nasema hii si rahisi.
Kwa nini nasema si rahisi? Labda nitalisemea nitakapofika katika sehemu yetu ya
pili.
Dunia imegawanyika hivyo
sehemu ya wakubwa wana nguvu za uchumi na wanaitumia kuendeleza nguvu hizo.
Nilisema Ndugu Kaunda alijaribu kuacha Coca-Cola nikamwambia : ‘‘Sasa
utafanyaje?’’ Alisema: ‘‘Mwalimu, tunaanza mtambo wetu pale wa vinywaji vya
nyumbani, unaweza kufanikiwa.’’ Nikamwambia: ‘‘Ken, huwezi… huwezi kwa sababu
wako Wazambia pale watakuletea taabu kwelikweli.’’ Nimeambiwa
jana kwamba nadhani sasa Coca-Cola watarudi. Wamesharudi kwa sababu sasa mapambano
hayo dhidi ya ukoloni mamboleo si rahisi. Ndugu Mengi, ni magumu zaidi kuliko
mapambano dhidi ya ukoloni kwa sababu tulipokuwa tukipambana na ukoloni ilikuwa
ni rahisi zaidi kuunganisha nguvu za ndani. Ilikuwa rahisi vilevile kwa nchi
changa kushirikiana. Kwa Tanzania kushirikiana na India; TANU kushirikiana na
KANU, kushirikiana na Indian Congress, kushirikiana na UNIP, kushirikiana na
African Congress. Tulikuwa tunaweza kufanya kazi pamoja na marafiki bila
tatizo, lakini sio sasa.
Sasa niiache hii niende
haraka haraka. Nasema hili ni tatizo letu. Kwa hiyo tatizo la Tanzania ni hilo
na pia ni la wenzetu wote; uchumi wetu ni duni kwa maana zote mbili. Kama
nilivyowaambia juzi, tungeweza kulima kwa ng’ombe tungekuwa na maendeleo
makubwa sana. Kwa hiyo, uchumi wetu uko nyuma, wenzetu wako mbali. Sisi tuko
nyuma, uchumi wetu ni tegemezi. Ni uchumi tegemezi. Lazima tuutoe katika hali
hii ya kuwa uchumi tegemezi. Na katika hali hii ya kwamba tunataka uchumi wa
Tanzania uwe uchumi unaojitegemea ndio lazima wote tuwe pamoja kwa sababu
tunamkabili mtu wa nje. Hii haina itikadi, ni uzalendo tu.
Wajapani wanaulinda uchumi
wao. Wanaulinda kwa mbinu za ajabu ajabu, na washindani wao wa Kaskazini,
wengine hata hawazijui mbinu hizo. Wajapani anakwenda kwenye mkutano,
wanaambiwa : ‘‘Lakini ninyi Wajapani namna gani, soko lenu gumu sana
kuliingia.’’ Wanasema: ‘‘Tutajaribu kuona njia za kuweza kusaidia saidia.’’
Wanakwenda, sijui wanafanyafanya mambo yao huko, inabaki ngumu.
Wajapani mnauza magari
mengi sana katika nchi yetu, hapo Mjapani anacheka kimoyomoyo: ‘Ah! Si mmesema
tushindane bwana? Kwani tunayaleta kwa nguvu, si watu wenu wanayaagiza?’ Lakini
namna yalivyokuwa rahisi kuliko hayo ya Uingereza, kuliko hayo ya Ujerumani,
kuliko hayo ya Ufaransa, kuliko hayo ya Mmarekani, Mjapani anajua mwenyewe ni
madhubuti kwelikweli, lakini ziko njia nyingine ndio… ndio… lakini si bepari
yule? Kwani katika jambo hilo la kusema biashara ya Japani lazima iwe ya
Japani, huu ni uzalendo. Kwa hiyo, nchi ya kijamaa inasema hivyo, na nchi ya
kibepari inasema hivyo.
Kwa hiyo, sisi hapa Tanzania
tutakaposema tunataka kiwanda cha Tanzania kiwe cha Tanzania lazima wote tuseme
hivyo. Mimi niseme hivyo, Mengi useme hivyo, Patel aseme hivyo, Shomari
aseme hivyo. Wote. Lazima iwe ni biashara yetu, lazima … lazima tujenge
biashara ya Tanzania. Sisi si watoto wadogo, dunia inabadilika hii bwana.
Tumesomesha watu bwana. Kulikuwa kuna wakati tunaweza kusema kijingajinga,
lakini sasa tumesomesha watu wote, yani watu wote hawa tumewasomesha. Kazi yetu
nyinyi mtujengee tegemezi. Sasa nyinyi mtukwamue. Ndio hamuwezi kwenda
mnakwenda kwenye Benki ya Taifa tumekupanga kwenye Benki ya Taifa mnakwenda
kuomba fedha katika Benki ya Taifa kusudi kutusaidia kujenga uchumi tegemezi,
haiwezekani. Mtusaidie kutukwamua. Katika hiyo lazima tuungane wote. Ujumbe
namba moja; Somaia unanisikia? … Ndio ujumbe namba moja, hili halina itikadi;
Waingereza wanafanya hivyo, wamekuwa wakifanya hivyo.
Nyinyi wadogo mkiambiwa muungane mnasema “tunapotezwa na
aliyetwambia”. Mnapotezwa; ni walewale wakubwa. Sasa nasema tujenge uchumi wa
Tanzania. Kazi hiyo ya kujitoa katika ukoloni mamboleo tegemezi lazima
mshirikiane – mabepari na msiokuwa mabepari, sekta ya umma na sekta binafsi;
katika kazi hii lazima tufanye kazi moja. Tujenge uchumi wa Tanzania ambao sio
uchumi tegemezi. Sasa ujumbe huo nadhani niubakize hapohapo.
Sasa baada ya kusema hivyo, nasema nianze kusema ule mgawanyiko wa
nje na ndani. Mgawanyiko kati ya Kaskazini na Kusini, unaoleta unyonge,
unawezekana pia ndani; katika nchi yetu nako tunaweza. Sasa hivi
nasema. Ngoja nitumie kofia yangu ya tume ya ushirikiano nizungumze, lakini
nizungumze mambo yale yale.
Kaskazini na Kusini naona sana ni mgawanyiko kati ya kaskazini
inayotawala na kusini inayotawala. Nasema lazima tusaidiane kwa sababu tunaishi
katika dunia moja. Wote ni binadamu; sehemu ndogo iliyoendelea ya Kaskazini
iendelee kututawala wengi tulio Kusini kana kwamba si watu sisi. Hii hatuwezi
kuikubali hata kidogo.
Ujumbe huu lazima uende Kaskazini kutoka Kusini. Haiwezekani
tuishi katika dunia moja halafu tukakubali. Kule kutawaliwa kwa nguvu shauri
nyingine, lakini kukubali ni aibu. Mnatukana Mungu. Mnakubali unyonge. Kwa
nini? Kwa hiyo lazima kutuma ujumbe huo. Sasa naivua kofia yangu naiweka.
Sasa ndani ya Tanzania: kwamba mgawaniko kati ya Kaskazini na
Kusini inaweza kuwa nchi. Kwa hiyo, kutakuwa Kaskazini kugawa Kusini katika
Tanzania. Tutakuwa na watu Tanzania wanaishi maisha ya Kaskazini tu kana kwamba
hawako Kusini. Hii si kweli, haiwezekani…
Walio wengi hawawezi kukubali hata kidogo. Hawatakubali, walio wengi hawa miaka
11 kufika karne ya 21; hawawezi kukubali mgawanyiko huo.
Kwa hiyo, mnaweza hata
ndani ya Tanzania kuwa na kikundi cha watu wachache kinachotawala uwezo wa
uchumi na kwa hiyo kutawala uwezo wa kisiasa. Na wale walio wengi ambao
ukiwauliza wanasema sisi tuna uchumi tegemezi, hapa ndio wote wataitwa wa ‘informal
sector’. Eh! Idi anasema wengi nchini Peru. Nilikuwa nchini Peru, sasa
wanakuwa ni watu wa aina hiyo wengi wao. Tunaweza kuwa na mgawanyiko huo pia
hapa. Sasa mimi kwa kofia yangu ya pili, wenzangu, nasema hilo hatuwezi
kulikubali wote hapa katika itikadi yoyote.
Tunakubali hiki kitu
tunachopambana nacho kimataifa tukionee haya kupambana nacho ndani, ambako tuna
uwezo? Kwa sababu ulimwenguni uwezo wetu ni mdogo; ndani tuna uwezo.
Kwamba tutakuwa wanafiki
tu, tunawaambia wa Kaskazini kwamba mgawanyiko haukubaliki wakati huo huo
nchini Tanzania sisi-sisi tunajenga mgawanyiko huo, na tunadhani tunakuwa
waaminifu mbele ya nani? Si mbele yetu wenyewe, si mbele ya Mungu, si mbele ya
nani. Tutakuwa waaminifu mbele ya nani kama tutafanya hivyo?
Sasa wenzangu mmesimama
hapa. Patel kasimama hapa akasema vizuri kabisa: ‘Tunasukuru kwa ushirikiano
mzuri kwa Watanzania.’ Hapa amani nzuri hakuna utengano wa ukabila au nini!
Yote kasema sawa, ni kweli. Mengi alisema vilevile, tuko hapa, tusingekuwa hapa
bila msimamo wa Chama – tusingekuwa hapa. Sawa sawa, tuna utulivu safi kabisa,
hii ni kweli kabisa; kitu chetu cha kujivunia kikubwa kabisa ni hicho tu – tuna
utulivu wa hali ya juu katika nchi hii. Eh! Mwakitwange alirudia katika mada
yake kusifu utulivu.
Lakini Waswahili wanasema
ukiona vyaelea vimeundwa. Vimeundwa. Sio tu utulivu umekuja wenyewe tu. Utulivu
wa Tanzania sio kwamba Azimio la Arusha limeondoa umaskini hata kidogo.
Umaskini si huu bado tunaendelea nao? Si huu mpaka leo? Uchumi si huu huu bado
tunasumbuka nao? Si kwamba Azimio la Arusha limeondoa umaskini hata kidogo,
wala halikutoa ahadi hiyo. Azimio la Arusha limetoa ahadi ya matumaini. Ya
haki, ahadi ya matumaini kwa wengi, ndio watu wengi wa Tanzania wanaendelea na
kuwa na matumaini hayo. Madhali yapo matumaini hayo, mtaendelea kuwa na amani.
Hapa tuna umaskini Tanzania, lakini hakuna ‘social cancer’. Inawezekana,
sijui kama kameanza anza kidogo, sijui; lakini hatuna ‘social cancer’.
Hakuna ‘volcano’ inayojengeka kwamba ukiweka sikio chini hivi,
unasikia hiyo ‘volcano’ inajengeka na kwamba siku moja italipuka
tu. Hatujafika hapo bado kwa sababu watu bado wana matumaini yanayotokana na
msimamo wa Azimio la Arusha. Halikuondoa umaskini lakini limewapeni wote nyinyi
wa chumba hiki, mabepari na wajamaa, limewapeni nafasi hiyo – kwamba mjenge
nchi ina matumaini kwa wengi. Bila hivyo hamna, watakataa; na mtawafanyaje?
Hivi kweli mtawafanyaje?
Hivi kweli Waswahili wachache nyinyi mtawale Watanzania kwa nguvu bila
matumaini, halafu watakaa tu kwa amani – amani ya matumaini – matumaini
yakiisha kutakuwa na ghasia za kijamii na nitawashangaa Watanzania hawa wakatae
kufanya ghasia. Kwa nini?
Hivi sasa katika kofia
yangu ile nawaambia Wazungu wa Kaskazini. Nasema hivi, msingi wa amani duniani
ni haki. Kwa hiyo, kama mnataka amani ya kweli sio kwamba mashariki na
magharibi mzungumze yaishe, hata kidogo. Kwa hiyo, mtakuwa mnaondoa migogoro
yenu mtaona mmetengeneza namna moja ya haki, lakini bila kuondoa migogoro ya
Kaskazini na Kusini, amani tutaikataa sisi. Haitakuwa dunia ya amani kwa sababu
ni watu sisi na ndani ya kila nchi ni hivyo hivyo. Uingereza ni hivyo hivyo,
Marekani ni hivyo hivyo, Ujerumani ni hivyo hivyo na Tanzania ni hivyo hivyo.
Kama wengi hawana matumaini, tunajenga ‘volcano’. Siku moja italipuka na lazima ilipuke. Isipokuwa watu hao
wajinga. Wengi wa nchi hiyo wajinga, wanakubali kutawaliwa hivi hivi. Kuonewa
hivi hivi na wingi wanao, wajinga hao. Kwa hiyo, Watanzania hawa watakuwa
wajinga, wapumbavu, kama wataendelea kukubali kuonewa na watu wachache katika
nchi yao. Kwa nini?
Kwa hiyo hatuwezi tukasema
sasa eti umefikia wakati tukasema Azimio la Arusha tulisahau. Msijidanganye
hivyo. Hiyo ni sawa na mjinga ametumia ngazi amepanda amefika juu, halafu
anaipiga teke ile ngazi. Unaipiga teke ile ngazi, haya kaa huko maana tutakata
jiti sasa. Sisi tuko chini, wewe uko juu; ngazi umekwishaipiga teke,
tutaliangusha sasa jiti – nalo ni refu hili. Kishindo chako cha kuanguka bwana
kitakuwa kikubwa kweli, tusiseme hivyo.
Sasa nasema hiyo nayo
inatosha, baada ya kusema hapo inatosha; lazima tukubali msingi wetu, msingi
wetu wa kujenga hiyo amani tuendelee na imani tuendelee. Wananchi wa Tanzania
waendelee kuamini Chama, kuamini serikali, kuamini nyinyi wenye nafasi –
wawaone nyinyi ni wenzao, wasiwaone nyinyi ni maadui zao. Waamini Chama,
waamini serikali – nyinyi mliopata nafasi maana hakuna nchi watu wote sawa.
Hata vidole vyangu hivi si sawa, hakuna usawa wa namna hiyo.
Lakini waamini serikali.
Wakiamini Chama chao, wawaamini nyinyi mliotangulia mbele wawaone kwamba kwa
kweli wote pamoja, kwamba mmetangulia lakini shabaha yetu ni ile ile: kujenga
nchi ya haki. Hapo tukikubali msingi huo sasa nasema tushindane. Tushindane
katika hali hiyo tunaendelea kujenga sekta ya umma. Kwa nguvu. Tunaipunguzia
udhaifu wake; zingine za ovyo ovyo, zingine za kijinga-jinga. Tunazipunguza
kujenga sekta ya umma, hata kidogo, msije mkadanganyika hata kidogo.
Tutazidi kuongeza sekta ya
umma na kuifanya imara. Sio dhaifu hata kidogo. Lakini sekta ya binafsi ipo
tangu 1967 na kabla, sasa fanyeni kazi nzuri lakini tukabiliane na watu wa nje
kwa pamoja. Mtu ambaye tutamkataa sisi ni yule ambaye kazi yake yeye ni
kutufanya sisi tu ni wafanyakazi wa nchi za Kaskazini. Huyo si mwenzetu hata
kidogo. Si mwenzetu, Mengi. Jifanye bepari mzalendo, tutakuunga mkono asilimia
mia moja kama bepari mzalendo. Hatutakusaidia, tutapambana nawe kama utajaribu
kuifanya nchi hii koloni mamboleo kwa ajili ya mtu mwingine nje ya Tanzania.
Tuelewane hivyo. Kuwa bepari, tengeneza fedha, lakini fedha hizo kwa ajili ya
Tanzania – kwa ajili ya kujitegemea kwa nchi yetu – lakini tukupe uwanja wa
nchi yetu uutumie kutufanya wafanyakazi wa watu wengine, hatukubali hata
kidogo. Tutapambana na nyinyi mkiwa namna hiyo. Ndio maana sasa hivi tunasema
waziwazi. Tujenge nchi yetu. Hatutaji, katika hali ya kujaribu kuutoa uchumi
wetu katika hali hii ya ovyo, tutatumia uwezo wetu wa ndani kwa ajili ya
maendeleo, ubepari na ujamaa. Tutazichanganya zote hizi kwa nguvu kabisa kabisa
kujenga uchumi wa nchi yetu.
Lakini hatutajifanya kwamba
eti tukisahau msingi wa Azimio la Arusha tutaendelea kubaki na amani katika
nchi. Uwongo, haiwezekani. Kwa hiyo, lazima tukubali kushirikiana hivyo kwa
msingi huo.
Sasa, mwisho kabisa nitasema haraka haraka. Jamani nyie katika
jitihada hizi za kuanza kujitegemea kidogo, mambo machache yafuatayo
tukubaliane tuyafanye. Kwanza, lazima tujitegemee kwa chakula. Lazima tuseme
kwamba tutaacha kuombaomba chakula. Sasa nchi inajitegemea kwa chakula… sijui
Patel zile eka zako 12,000 unalima nini? Pilipili? Lazima tujitegemee kwa
chakula. Hilo liko katika uwezo wetu. Kusema kwamba Watanzania hawawezi
kujitegemea kwa chakula ni uongo. Tunaweza kujitegemea kwa chakula.
Sasa tufanye hivyo basi, maana aibu sana watu wazima kuomba
chakula kila siku. Na matajiri hawa hawana haya. Waswahili tunaona haya
kumsimulia mtu kitu kama chakula. Kumsimulia mtu kwa chakula ni kumsemasema.
Unampa chakula halafu unamsema kwamba watu hawa bwana kwao hawali. Akija kwako
hapo atakaa wee haondoki, na anasikia hivyo. Sasa waswahili hawapendi tabia
hiyo. Mtu unaweza kumsimulia kitu kingine chochote lakini chakula; chakula
hasimuliwi mtu bwana. Lakini wenzetu hawa wakubwa, anakupa chakula huku
anakusema bwana. Anakupa chakula kwanza halafu wakati uleule wanatuwekea
vikwazo sisi tusijitegemee katika jambo la kilimo. Wao wanatoa ruzuku kwa
kilimo chao, wana mapesa mengi kwa hiyo vilimo vyao ni vyenye ufanisi kabisa.
Kilimo cha Wamarekani hakiwezi kushindana wakiondoa ruzuku.
Waondoe; kama hodari kiasi hicho si waondoe ruzuku! Maana sisi wametuambia
tuondoeb ruzuku, tumeondoa. Ndugu Rais, na wao waondoe basi maana wanajidai
hodari sana hawa. Waondoe, waache kuwapa wakulima wao pesa za bure. Wakulima
wao na wakulima wa Kusini tushindane tu; kama wanatuweza, waondoe kesho. Si
wanajidai hodari sana. Sitaki kusema zaidi, nasema ingawa kilimo
jamani, ndugu Rais, tujilishe wote hawa tunaolima, tujilishe. Hilo la kwanza,
tujilishe kwa chakula; sisi tunaingia karne ya 21 bado hatujilishi kwa chakula.
Majitu mazima, tumesomesha watu wengi sana, wasomi tele.
Pili, mavazi. Tulipofanya rasilimali zile kubwa katika viwanda
tukasema tunalima pamba sisi. Sasa tunalima pamba, halafu pamba yetu tunauza
nje. Watu wazima tunalima pamba, tunauza nje; sasa
angalau tuanze kutengeneza nguo. Kwa hiyo, lengo letu la mwanzo, tulikuwa
tunataka – tulitaka kutumia pamba yetu asilimia 60 ndani na asilimia 40 kuuza
nje. Sasa sijui tunauza kiasi gani… Tunatumia theluthi moja, kama asilimia 30.
Kwa hiyo, kwa vyovyote vile hatujafikia, lakini rasilimali inatosheleza. Kwamba
kama viwanda hivi vingekuwa vikitumika kwa uwezo wao wote, pengine vingesogelea
hapo au hata kuvuka viwanda tulivyonavyo. Sasa ninasema katika hilo uwezo
tunao. Ingawa bado uwezo wa kutengeneza viwanda vyetu wenyewe hatuna, lakini
viwanda hivyo tulivyonavyo tuvitumie basi angalau tujitosheleze kwa nguo – kwa
mavazi – kwa maana ya mavazi, yaani nguo zenyewe na viatu. Sisi tuna ng’ombe,
tuna mbuzi; tunaendelea, watu wazima tunauza ngozi nje, ngozi hasa… tufanye
hivyo, maana uwezo tunao, sio wa kutafuta, rasilimali ipo tayari… Mengi, hilo
tunaweza tukafanya.
Tatu, madawa, madawa…
Madawa hili nalo tunaliweza bwana, hivi kweli au hata vidawa vya hospitali
zetu. Ndugu Rais, kitu cha kutengeneza dawa za hospitali, maana dawa za
hospitali miaka 11 kabla ya karne ya 21 bado hatuwezi kufanya hivyo? Hivi
hatuwezi kuwa na orodha maana tulitengeneza ya madawa muhimu. Nasema madawa
haya kwetu sisi ndiyo ya lazima. Hatuwezi kuyatengeneza?... Tuzitengeneze sisi
wenyewe hapa, tuna viwanda viwili sisi hapa. Nadhani tuna viwanda viwili au
vitatu sijui vya kutengeneza dawa. Na vitengeneze ama vigawane kazi; kimoja
kitengeneze dawa hizi, hiki kitengeneze dawa hizi, hiki kitengeneze dawa hizi na
kile tusichokiweza tukitafutie uwezo, tutengeneze dawa zile za lazima.
Tunayo orodha ya madawa
muhimu, tunaweza kutengeneza. Kwa nini kwa afya ya watu wetu vilevile tuwe
tegemezi? Hata afya ya watu tunakuwa tegemezi. Vitu vidogo sana kuweza
kutengeneza dawa na tunaweza kutengeneza dawa. Najua wakubwa hawapendi. Brazil
wanatengeneza dawa, wamebanwa na Marekani; nimeambiwa kwamba ingawa
wanatengeneza dawa karibu kujitosheleza, hii sekta ya nyumbani ya dawa hii
sehemu kubwa kabisa ni ya Marekani. Lakini hata hivyo, wamekabwa na wakubwa.
Sasa dawa angalau
tutengeneze. Tujitegemee katika kitu kama dawa sio kwa kila kitu lakini kwa
madawa ya lazima. Tuna matatizo ya afya. Sasa hilo nalo tuendelee kuwa tegemezi?
Tunauziwa unga lakini miaka 11 kutoka karne ya 21 wanatuuzia vidonge vya unga
wa muhogo, sijui. Tunalisha watu wetu, wataalam, nyinyi hamuwezi kutukomboa kwa
hilo?
Vifaa vya elimu… vifaa vya elimu. Mengi, si ulianza na kalamu? Sasa tuanze, tutengeneze
karatasi. Leo tunatengeneza vifaa vya elimu vinatupa taabu tuna watoto wengi
wanaosoma. Tuna watoto wanasoma kama milioni nne. Mimi nadhani kusema kweli
tunaweza tukawa na viwanda maalum tu kwa shughuli za vifaa vya elimu.
Tunaposema kwamba tunataka watoto wa shule wavae viatu, tunajua viatu vyenyewe
vinapatikana wapi? Eh! hivi viatu tu, kusema viatu, sijui watu wana viwanda
vyao wenyewe, sijui maduka yao wenyewe? Angalao tuseme, kwa shughuli za shule,
tunatengeneza. Hivi yunifomu zinatengenezwa mahali fulani, hizi kalamu
madaftari yanatengenezwa mahali fulani. Tufanye hivyo, maana kubwa jambo hili,
ni kubwa kwetu; kusomesha watu wetu ni kubwa, na uwezo tunao, sio kwamba hilo
nalo tena ni kazi ya kuweza kutegemea Kaskazini. Hivi sasa ni balaa kupata
madaftari katika shule zetu. Watoto hawana daftari, walimu hawana ile chaki ya
kuandika.
Mwisho. Nimeyasema hayo:
chakula, mavazi, madawa ya watu na mifugo, vifaa vya elimu, na spea mbalimbali.
Yule Mhindi aliyekuwa akiniambia bomba ni za spea. Leo Tanzania mtu wa
nchi anaweza akatupa gari lake bure bure, akasema hilo gari kuchukua bure
madhali utanunua spea kwake. Kwa hiyo matumizi yetu ya spea hapa ndiyo huyu
Mhindi alikuwa akisema bomba, lile bomba… lile bomba hasa linazoa fedha
zinazokwenda nje bure. Kama lazima, sawa. Kile kitu ambacho hukitengenezi na huna
uwezo wa kukitengeneza na unataka agiza kutoka nje.
Lakini spea nyingi ni bure,
za magari yetu, za matrekta. Hayo tungetengeneza. Ndugu Rais, nimechukua muda
wenu mrefu sana na (….) matatizo. Niwashukuruni sana.
(Chanzo:
Gazeti la Mzalendo ; Jumapili Mei 21, 1989)
No comments:
Post a Comment