Thursday, October 29, 2015

AHADI ZA MTANZANIA


Google image

Chama cha TANU kilifanya kazi muhimu ya kuikomboa nchi yetu toka mikononi mwa wakoloni wa kiingereza. Haya yaliwezekana kutokana na uongozi thabiti wa kina J.K Nyerere, R.M Kawawa na viongozi wengine wazalendo, wenye utu na mapenzi makubwa kwa nchi na bara lao.

Malengo makubwa ya TANU ilikuwa ni kuleta uhuru wa waTanganyika na kushiriki katika ukombozi wa bara zima. Hapa tunakumbushana ahadi kumi za mwanaTANU ambazo zinafaa kuwa mwangaza kwa waTanzania wote bila kujali itikadi ya vyama vyetu na imani ya dini zetu. Na kwa nafasi ya kipekee ziwe mwangaza kwa viongozi popote walipo...

1. Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.

2. Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote

3. Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma.

4. Rushwa ni adui wa haki. Sitapokea wala kutoa rushwa.

5. Cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.

6. Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote.

7. Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu.

8. Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.

9. Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU na raia mwema wa Tanganyika na Afrika.

10. Nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Tanganyika.


Chanzo:http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/97717-ahadi-kumi-10-za-mwana-tanu-na-tanzania-yetu-ya-sasa.html

Wednesday, October 14, 2015

JULIUS NYERERE NA FIKRA IMARA

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1922-1999), waziri mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru, rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika na kisha rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni kiongozi wa kipekee sana kuwahi kutokea nchini Tanzania, barani Afrika na duniani kote kwa ujumla.

Mwalimu Nyerere, alikuwa kiongozi wa kipekee kutokana na mitazamo, misimamo, na maamuzi yake. Ndugu huyu kamwe hakuwa malaika aliyeshuka toka mbinguni kuja kuishi nafasi la hasha! Huyu ni mwanadamu aliyetambua vipawa na uwezo wake na akavitumia vizuri kwa faida zake na kwa taifa aliloliongoza na kulipenda. Binadamu ni kiumbe cha kipekee mno. Tumeumbwa tukiwa na uwezo mkubwa kufanya mambo mengi yaliyo mapya kabisa, lakini wengi hatufanyi hivyo. Hatufanikiwi kwa kuwa hatuishughulishi akili yetu na vipaji vyetu kwa kiashi cha kutosha.

Katika makala haya naomuongelea kwa ufupi kabisa jinsi Mwalimu Nyerere alivyoutumia uwezo wa kiakili kufanya mambo ambayo kamwe hayakuwa yamefanyika hapa nchini kwa jinsi yeye na viongozi wenzake walivyofanya. Naongelea sera za ujamaa. Hizi ni sera ambazo zimeandikwa na wanazuoni, wanahabari na watu anuwai kote duniani, wanaompenda na wanaomchukia Nyerere, wanaozipenda na wanaozichukia sera hizo.  

Ujamaa ilijengwa kwa dhana ya kihistoria, kifkra na kitaaluma ikiupinga ubepari kwa kuwa ulilenga kujenga jamii yenye furaha kwa kukandamiza kundi moja la watu ambapo wengi walifanya kazi kwa faida za mabwana wachache. Halikadhalika, iliupinga ujamaa wa kisanyansi kwa kuwa ulitaka kujenga jamii yenye furaha kwa njia ya mapigano. Mwalimu hakukubaliana na njia hizi katika kujenga jamii ya watu wenye kushirikiana, kupendana na kujitegemea.

Ujamaa uliotangazwa kupitia Azimio la Arusha, na ulishabihiana kifkra na baadhi ya siasa za Plato mwanafalsafa wa kale wa Kigiriki, mfano kwenye maadili ya uongozi kwa mwanasiasa. Ujamaa ulijengwa kupitia njia kuu mbili: utaifishaji wa njia kuu za uzalishaji mali binafsi na vijiji vya ujamaa. 

Utaifishaji wa njia kuu za uzalishaji mali kwa kiasi kikubwa kabisa ulichochewa na mfumo wa kibepari ambao Tanganyika iliupitia kwa takribani miaka sita 1961-1967. katika upepari huo wananchi wengi waliendelea kuishi katika umasikini mkubwa na kunyonywa kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni. Wananchi waliendelea kuvuja jasho kwa kuwafanyia kazi matajiri wale wale waliowafanyia kazi kipindi cha ukoloni. Kwa ufupi uchumi ulikuwa mikononi mwa Watanganyika matajiri na wageni wachache wenye asili ya Uingereza na bara Asia. Kwahiyo Watanganyika wa kawaida, wanafunzi chuo kikuu, wanaharakati wachache na Mwalimu walianza kuhoji kwanini walikuwa hawaoni tofauti ya kipindi cha ukoloni na kipindi cha uhuru. Uchumi huo wa kibepari uliongozwa na  misingi ya soko huru na huria ambapo serikali ya Tanganyika na baadaye Tanzania haikuwa na mamlaka juu yake. Hivyo ubinafsishaji lilikuwa ni suluhuhisho la msingi la kuanza upya. Jambo hilo halikuwa jepesi hata kidogo, lakini Mwalimu kwa mapenzi makubwa ya nchi yake alichukua uamuzi huo mgumu. 
Ubinafsishaji ulilenga kuipatia serikali uwezo wa kumiliki njia kuu za uchumi na kujaribu kujenga uchumi wa viwanda; uchumi ambao ungetoa ajira nyingi zenye staha kwa watanganyika na ambavyo vingetumia bidhaa ghafi toka mashamba ya Watanzania wenyewe. Mwalimu na wenzake walilenga pia kujenga taifa la kijamaa na MUHIMU hapa lenye KUJITEGEMEA, ndiyo maana njia nyingine ya kujaribu kujenga ujamaa ikawa ni kupitia vijiji vya ujamaa.

Vijiji vya ujamaa vililenga kuwaleta watu ili waishi pamoja na kufanya kazi kwa kushirikiana kama familia moja katika mashamba makubwa ya vijiji vya ujamaa. Na zaidi Wananchi walikusanywa kwa kuwa idadi ya watu ilikuwa ndogo na waliishi sehemu tofauti tofauti na mbalimbali ambapo ilikuwa vigumu kwa serikali kuwapatia huduma za kijamii. Kuhamia vijiji vya ujamaa ilikuwa hiari lakini baadaye nguvu ilitumika pale wananchi walipojivuta mno kutekeleza agizo hilo.

Sera za ujamaa na kujitegemea ambazo ziligusa nyanja zote za maisha yaani kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa kiasi fulani zilifanikiwa vyema na kwa kiasi kingine zilifeli vibaya. 

Kisiasa na kijamii jaribio la kujenga taifa la kijamaa lilifanikiwa sana. Mwalimu na wenzake walijenga taifa moja linaloundwa na zaidi ya makabila mia moja na ishirini. Walifanikiwa kuvunja kasumba za makabila makubwa na madogo. Walifanikiwa kushawishi watu wengi watumie lugha moja ya KISWAHILI, walifanikiwa kufanya watu waowane toka makabila na dini tofauti na zao. Kwa ujumla walifanikiwa kujenga moyo wa kindugu na mshikamano mkubwa baina ya watanzania. Kwenye huduma za kijamii nchi ilifanikiwa kupiga hatua kwenye elimu ya msingi ambapo watu wengi karibu wote walifanikiwa kujua kusoma na kuandika, huduma za afya pia zilikuwa nzuri na zilitolewa pia vyema bila ubaguzi. Kazi hii haikuwa ya Mwalimu Nyerere peke yake ni kazi aliyoifanya akishirikiana na viongozi wengine wengi kwa uchache tu hapa Abeid Karume, Rashidi Kawawa, Abdul Jumbe, George Kahama, Rupia, bibi Titi, Mwakawago na wengine wengi. Hata hivyo kiongozi mkuu alikuwa ni Mwalimu Nyerere. Kiongozi mwadilifu, imara na mpenda nchi huifanya nchi yake iwe na msimamo na kujijengea lulu na baraka za aina kwa aina kama amani na upendo miongoni mwa Watanzania. Kiongozi mkuu wa nchi akiwa mwadilifu, nchi hata kama ina matatizo bado ataweza kutoa mwelekeo mzuri kwa taifa lake.


Kiuchumi, jaribio la kujenga nchi ya kijamaa liliuharibu kabisa uchumi wa Tanzania. Nchi ilipoteza kabisa uwezo wake iliokuwa nao kabla ya kujaribu kuingia ujamaa. Uzalishaji wa chakula ulishuka, uzalishaji viwandani uliporomoka, bidhaa za matumizi ya kawaida kabisa kama mswaki, dawa ya meno, sabuni, nguo, unga viliadimika kabisa na uchumi kushuka chini kabisa. Hii ilichangiwa na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na vita dhidi ya Iddi Amini wa Uganda, mfumuko mkubwa wa bei za mafuta, ukame ulioikumba nchi, lakini hasa sera mbovu za uchumi zilizosababishwa na jaribio la kujenga uchumi wa kijamaa, hata hivyo hujuma toka kwa Waingereza, waliokuwa na hofu ya kusambaa kwa ujamaa kote Afrika Mashariki na hivyo kuleta athari kwenye mali zao hususani katika mabenki yao, nayo pia ilichangia kwenye kufanya jaribio la kujenga ujamaa lishindikane na uchumi uharibike kabisa.

Pamoja na shida zote hizo, Mwalimu Nyerere aliendelea kuwa imara, mkweli, muwazi "mjamaa safi" ambaye kamwe hakujilimbikizia mali wala kuharibu rasilimali za taifa lake kwa manufaa binafsi kama tunavyoshuhudia hivi leo Tanzania na kote barani Afrika kwa baadhi ya wanasiasa wanavyofanya biashara kupitia dhamana ya vyeo walivyopewa na wananchi.

Tumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kujenga na kutumia fikra na vipaji vyetu vizuri kujinufaisha na hasa kuihudumia vyema jamii tunapoishi. Na kwa wenye nafasi ya uongozi popote pale toka katika ngazi ya familia tujenge uongozi bora na tuepuke ubinafsi tukifuata mfanowa Julius Kambarage Nyerere.

Martin Mandalu
Dar es Salaam,
14, 10, 2015

Monday, October 5, 2015

SIKU YA WALIMU DUNIANI

PG4A3893
Picha kwa hisani ya dewjiblog.com
Leo ni Siku ya Walimu Duniani. Ni siku mahususi kuwapongeza walimu kwa mchango wao mkubwa kwenye sekta zote za ujuzi. Kila mtaalamu duniani amepata mafunzo toka kwa mwalimu wa aina moja ama nyingine. Hakuna ujuzi hivi hivi bila kupitia kwa mtu anayeitwa mwalimu; hata wenye mlengo wa ujuzi, ama kupata elimu bila kutumia milango mitano ya hisia, hawawezi kulikwepa hili. Kwa mujibu wa "rationalists" kuna mambo ambayo tunaweza kuyajua kwa hisia tu. Hata kwa wadau hawa, lazima warejeshe shukrani kwa wazazi wao kama walimu wa mwanzo kabisa na hata kwa muungano mzuri wa chembe chembe hai za ubongo wao. Hivyo kwa ufupi kabisa, hakuna ujuzi bila mwalimu.

Tunaposherehekea ama kukumbuka siku hii kuna mengi ya kujiuliza. Mswali machache tu hapa; hivi mwalimu ana mazingira gani ya kufundishia; mazingira hayo ni salama na rafiki kwake? Je, hivi mwalimu aliye nguzo kubwa kwa ujuzi anapata stahiki zake kama inavyotakiwa? Je, huyu ndugu ana furaha ya kweli anapoifanya kazi yake? Walimu kote duniani wanakumbwa na shida na misukosuko inayowafanya washindwe kutekeleza majukumu yao vilivyo. Matatizo ya walimu yapo kwenye nchi zilizoendelea na zinazoendelea pia.

Kwenye baadhi ya nchi zilizoendelea, mwalimu anakutana na shida kubwa ya utovu wa nidhamu na maadili mabovu ya wanafunzi. Na nafasi ya mwalimu kuwarekebisha watoto imebanwa kwa kutumia lugha ya haki za watoto. Mwalimu hana nafasi wala mamlaka ya kumwadhibu mtoto kwa kuwa ni kinyume na haki za binadamu. Waingereza wana msemo wao, usipomchapa mtoto utampoteza. Hii ni tafsiri huru. Lakini Waingereza wenyewe na nchi nyingine zilizopiga hatua kubwa zaidi kimandeleo zina shida kubwa ya utovu wa nidhamu katika kundi la vijana ambao wanalindwa na haki za binadamu. Haki za binadamu ni muhimu kwa ustawi wa jamii lakini maadili na adhabu kiasi toka kwa mwalimu muhimu. Najua suala la kiasi ni gumu kulipima. Walimu wanakumbana pia na tatizo la tishio la usalama toka wanafunzi wenye silaha.

Katika nchi zetu zinazoendelea shida za walimu zipo za"kutosha" pia. Ni hivi karibuni tu walimu wa nchini Kenya ndiyo wamemaliza mgogoro wao na serikali. Miezi michache iliyopita walikutana na matatizo ya ukosefu wa usalama eneo la mpakani na Somalia. Nchini Tanzania walimu wana shida zao pia. Si lengo langu kuziorodhesha hapa hivi leo. Bali katika ukurasa huu, kwa maneno machache tu ni kutaka kukumbushia haki za walimu, kuhimiza uboreshwaji wa mazingira ya kufanyia kazi ndugu hawa ili wapate kufanya kazi kwa juhudi na maarifa zaidi kadri ya vipawa vyao.

Wasalaam,