Wednesday, February 4, 2015

TUMIA FURSA VYEMA NJE YA NCHI YAKO

Na. Theddy Matemu Sawaki

Fursa zipo kila sehemu - This image for education purpose is taken from another website

Tofauti na elimu ya darasani lakini mambo ya elimu dunia Zingatia yafuatayo.

Ø  Kujali muda.
Ø  Kuheshimu kila mtu.
Ø  Kujituma.
Ø  Kujifunza lugha na tamaduni za wenyeji.
Ø  Kuwa msikilizaji zaidi ya msemaji.
Ø  Kuwa tayari kupokea ushauri toka kwa watu wote hata wa kada za chini.

Nimekuwa nikizunguka kwenye mitaa ya Mji wa Tokyo nikaja kugundua wahindi ni watu wanaojua kucheza na fursa wanazozipata. Sio kwa nchi zinazoendelea tu hata kwa nchi zilizoendelea kama Japani.

Na nikaamini kuwa darasani tu haitoshi kukufanya ukapata maendeleo ya Kimaisha. Kwa kuwa napenda kula nimekuwa nikizunguka katika mitaa ya Tokyo kutafuta chakula ninachokipenda. Nimekutana na migahawa ya Kijapani na kihindi na kitaliano.Migahawa ya kihindi ina sehemu ndogo sana ya kufanyia biashara naamnisha ukubwa wa nyumba maana jiko liko hapo hapo na viti vya kulia wateja viko hapo hapo karibu( ila kwa huku wamejitahidi kwa usafi sio kama wanavyoutufanyia kwetu Tanzania)hapo napo ni kipengele kingine cha kujifunza kumbe kuwa wasafi wanaweza isipokuwa ni namna gani nchi husika inajali wananchi wake.

Katika kufanya utafiti wangu wa kichumi usio rasmi (mimi sio mwana uchumi) nikagundua wahindi wameweza kujenga umaarufu katika biashara ya chakula na wana wateja wengi sana wenyeji wa Japani. Nikamwuliza mmoja wa wenye migahawa wa kihindi umewezaje kufanikiwa katika kupata wateja wengi akaniambia nina miaka 30 hapa Japani na kweli anaongea kiJapani kama amezaliwa nacho.

Kwanza kabisa alipofika hapa alijifunza lugha (naweza sema kwa Japani ili uweze kuishi vizuri ni vyema ujue lugha vinginevyo utapata shida katika huduma za muhimu),pia alijifunza tamaduni na mengine muhimu katika maisha ya waJapani. Hii ilimsaidia kuweza kuwasiliana na wateja wake, kujua nini wanapenda na nini hawapendi kujua jinsi gani angeweza kuwafanya wafurahie huduma zake. Haya yote alifanikiwa pale alipoajiri wafanyakazi wa kijapani wakati akianza biashara yake na kuwafundisha jinsi ya kuandaa vyakula vya kihindi nao wakamfundisha lugha na mengine yote ya muhimu.

Alipoona biashara imeshamiri alipunguza wafanyakazi wake. Baada yakupunguza wafanya kazi biashara ikayumba sana. Akaitisha kikao na wafanya kazi wake waliobaki kutaka kujua tatizo ni nini kama unavyojua wafanyabiashara wengi wa kihindi hupenda kuamrisha zaidi na huamini watu wachache tu.
Mmoja wa wafanyakazi akamwambia bosi ili biashara ikue warudishe wale wafanyakazi uliowapunguza kwasababu wanajua siri ya kazi na wameizoea na ndio walichangia biahara kukua. Hapo ndipo alipojifunza kwamba ili upate mafanikio lazima uamini kwamba kila mtu hata kama ni mdogo kiasi gani anaweza kuwa na mchango katika maisha yako. Muda mfupi baada ya wale wafanyakazi kurudishwa kazini biashara ikainuka mpaka leo na wateja wanajaa mpaka wanasubiria nafasi ya kuketi kwa foleni.

Nimejifunza Maisha sio kukaa darasani tu bali pia na hasa namna gani unaweza kuthubutu na kufanya chochote hata kama ni nje na nchi yako na ukafanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, ili mradi kuwe na amani na utulivu katika nchi husika.