Saturday, March 31, 2012

KIFO: UKAMILIFU WA UBINADAMU

Sehemu ya umati uliofika kumuaga mwanachuo aliyeaga dunia
















Kama ilivyo kwa mawiyo na macheyo ya jua, ndivyo ilivyo kwa kuzaliwa na kifo. Msemo mmoja wa kiafrika wasema: "Kamwe ardhi haichoki kutupokea" ama kama inavyojidhihiri katika vitabu vitakatifu; kuna muda wa kila jambo: kupanda na kuvuna, kuzaliwa na kufa... ama tena binadamu u mavumbi na mavumbini utarudi. Na zaidi na pengine muhimu kupindukia; mbegu isipoanguka ardhini na kufa hubaki kama ilivyo, lakini ikianguka na kufa huzaa zaidi na zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla. Mbegu ya mmea wowote inaweza kufananishwa na maisha ya binadamu.

Inafaa kukumbushana kuwa mara tu binadamu anapotungwa kwenye tumbo la mamaye, tayari anakuwa na sifa za kuaga dunia, kufa. Hii inadhihirisha kwa maisha ya vichanga ambavyo hata kabla ya kuzaliwa, hufariki dunia. Vijana wengi hudhani ya kuwa kifo ni kwaajili ya wazee; watu walioishi kwa miongo kadhaa hapa duniani. Ni vyema tuambiane kuwa hii si kweli, kila binadamu yupo tayari, ameiva, amepevuka kwaajili ya kifo. Kama isemwavyo hivi leo kila mtu ni marehemu mtarajiwa. Kwa mantiki hiyo basi hatuna haja ya kuogopa. Kinyume chake inafaa tujiandae kwa tukio hilo la uhakika kama ilivyo kwa kuchomoza jua bila juhudi zetu kila asubuhi, kwa uzoefu tu twafahamu kuwa jua litachomoza. Pamoja na kujua ukweli huo bado hatuzoei suala hili.


Jeneza likiwa ndani ya ndege tayari kwa safari

Kamwe hatuzoei kifo kwa sababu kila kinapotokea, kinatokea kwa mtu ambaye hajawahi kufa. Najua hili si jambo geni lakini huo ndo ukweli wenyewe, je ni kwanini? Jambo hili li hivyo? Bila shaka ni kwa sababu kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kiimani twaelewa kuwa binadamu ameumbwa na Mungu na kuwa binadamu nd'o kazi nzuri kuliko kazi nyingine zote za Mungu na ni kwa sababu hiyo kila anapofariki dunia mwenzetu basi sisi hupatwa na simanzi lisiloelezeka, hata wale wenye mioyo migumu huguswa pia na kifo cha mpendwa ama mwanadamu ambaye walimfahamu, kuishi naye na kadhalika. Kifo ni sehemu ya ukamilifu wa binadamu.

Katika vitabu vitakatifu twaambiwa ya kuwa Mwenyezi alitufahamu hata kabla ya kuiumba dunia hii, kama nilivyoeleza hapo awali, binadamu kwa hakika ni kazi bora kabisa ya Mwenyezi Mungu. Twajua pia kuwa binadamu huanza kibaiolojia pale yai la mwanamke linaporutubishwa na mbegu ya mwanamume: kuanzia hapo safari ya binadamu fulani kibaiolojia huanza, na maisha yake huanza hapa duniani kwa kuzaliwa. Binadamu anazaliwa anaishi na hatimaye lazima afariki dunia. Kupitia kifo mzunguko wa binadamu unakamilika. Hivyo tukichukulie kifo kama ukamilifu wa ubinadamu wetu. Hata hivyo jambo la msingi hapa ni je, maisha hayo tunayaishi vipi hapa duniani?

Hivi leo wengi tunadhani kazi yetu katika sayari hii ya dunia ni kukusanya na kujilimbikizia mali nyingi iwezekanavyo. Tunajisahau, ukweli na wito wa binadamu ni kutoa mchango wa kuiboresha zaidi dunia kwaajili ya utukufu wa Mungu kama asemavyo Inyasi wa Loyola (1491-1556) . Tunaweza kuiboresha dunia kila mmoja kwa nafasi yake; mwalimu afanye kzi yake ya ualimu vyema, mwanasiasa afanye kazi yake vizuri, mwandishi, mkulima, mwanasayansi, mwanafalsafa, mwanafunzi na kila mmoja wetu afanye vyema kabisa kazi yake. Kushidwa kufanya vyema ama kutimiza wajibu wetu ni sawa na kushindwa kuitikia wito wa maisha yetu na tukishindwa kufanya hivyo basi maisha yetu yanakosa maana!

Tafakari hii imenijia baada ya kuona nyuso nyingi za huzuni wakati wa kumsindikiza mwanachuo wa stemmuco hivi karibuni baada ya kukamilisha safari yake hapa duniani.

Saturday, March 17, 2012

Mkanganyiko wa Maisha: Misitu ama Maisha?


Baiskeli hii TZ MKAA ikiwa imeengesha bidhaa kusubiri wahitaji mjini Mtwara
Kuishi kwenye jumuiya ya wasomi ni faida kubwa. Msomi, kwa tafsiri yangu ni mtu yeyote mwenye elimu kuanzia darasa la saba, ama kwa upana zaidi anayejua kusoma na kuandika, lakini mwenye moyo wa utafiti, kujisomea na kuwashirikisha wengine taarifa ya anachosoma ama anachotafiti.

Mwanachuo wa Stella Maris Mtwara University College (STEMMUCO), ambao kwa maelezo yangu ni wasomi, wapo katika harakati za kuandika taarifa, ripoti ya tafiti walizofanya sehemu mbalimbali hapa nchini. Kuna mada nyingi karibu kadri ya idadi ya watafiti hao. Kuna ripoti juu ya hali ya uchumi nchini, hali ya hisabati shuleni, nafasi ya sayansi katika elimu ya tanzania, hali ya elimu nchini, ushiriki wa wasichana katika elimu, jando na maendeleo, kwa ufupi nyanja zote muhimu zimeguswa, kuanzia siasa, uchumi, sayansi, na jamii. Zaidi tasnifu hizo za wasomi zimeangazia makundi mbalimbali katika jamii; wazee, wanawake, walemavu, vijana na kadhalika.

kwa ufupi, makala hii inagusia mkanganyiko unaowakuba vijana wanaofikia kundi la kujitegemea maishani. Hili ni kundi muhimu mno; hii ndio nguvu kazi hitajika ya ujenzi wa taifa letu. Tafiti zinaonyesha kuwa kundi kubwa la vijana karibu ya vijana milioni mbili na laki tatu (2.3), takwimu rasmi za serikali ya Tanzania 2005, hawana ajira zinazoeleweka. Kumbuka hii ni idadi ya makadirio tu, kuna idadi kubwa sana ambayo mara nyingi haijumuishwi kwenye taarifa rasmi, kwa hivi basi, vijana wengi hawana kazi. na wanakumbana na mkanganyiko wa maisha.

Baadhi ya sera zinakataza ama zinapiga vita shughuli ambazo vijana huzitegemea kuendesha maisha yao. Bishara ya mkaa ni moja ya biashara zinazopigwa vita kwa vile watayarishaji mkaa wengi huvuna miti kwaajili ya kuni bila mpangilio maalumu. Ni kweli zao la mkaa linaharibu mazingira na kuhatarisha dhana ya maendeleo endelevu. Wakati zao hili linapigwa vita, mahitaji na matumizi yake ndo kwanza yanazidi kuongezeka kila uchao. Na hii ni dhahiri kuwa mkaa ni bidhaa ambayo itaendelea kutumika kwa miaka mingi ijayo; kama wasemavyo vijana wa Bongo Flava; mkaa bado tutakuwa nao kwa muda mrefu sana. kumbe tufanye nini sasa.

1. Mosi, maafisa misitu, ama wataalamu wa maliasili waweke utaratibu wa kupanda miti kuwe na maeneo maalumu ya kupanda miti na vijana wavuna miti kwaajili ya mkaa wapewe maeneo ya kupanda miti na kuitunza ili hali waonyeshwe eneo maalumu la kuvuna miti ya kazi yao hiyo.

2. Pili, mamlaka husika zenye kujihusisha na gesi ya kupikia majumbani waangalie uwezekano wa kupunguza kwa kiasi kikubwa kodi za chanzo hicho mahususi cha nishati hitajika ili wananchi wengi ikiwa ni pamoja na mashambani waweze kuitumia pia.

3. Tatu, tafiti zifanyike kuangalia upunguzaji wa bei ya umeme ili walio na fursa ya kutumia nishati toka shirika la taifa la umeme watumie pia kwa kupikia; kwa sasa bei yake ni kubwa mno kwa mwananchi mwenye kipato cha wastani kumudu gharama hizo.

Mpanda baiskeli akitafuta wahitaji wa biadhaa yake manispaa ya Mtwara-Mikindani
Nchini Tanzania hali halisi ndivyo ilivyo vijana wengi wamejiajiri kuuza mazao ya miti

Tukifanya haya kuna uwezekano wa kufikia ndoto tuliyonayo ya kuwa na Watanzania wa daraja la kati ifikapo 2025 kama inavyoelezwa kwenye mpango wa maendeleo wa taifa. Kinyume na hivyo vijana wetu wataendelea kuwa kwenye mkanganyiko mkubwa wa misitu ama maisha ya leo; je nikate miti ili nichome mkaa ama nisikate na kufa njaa? 

Wednesday, March 14, 2012

Siku ya Wanawake STEMMUCO - MTWARA


Sehemu ya wanawake wakifuatilia matukio

Wajumbe wakifuatialia mtiririko wa matukio
Akina mama wakifanya utambulisho siku ya kimataifa ya wanawake duniani



http://www.stemmuco.ac.tz/index.php

Sunday, March 11, 2012

Mashindano ya PRO-LIFE - MTWARA

Picha kwa hisani ya google
Mashindano ya Pro life, ambayo yanaanza kujenga mizizi mjini Mtwara, kwa mwaka huu 2012 yamefunguliwa rasmi hapo jana. Mashindano hayo yanajumuisha taasisi kadhaa za elimu mjini Mtwara.

Moja ya malengo la mashindano haya ni kujenga uhusiano baina ya wanavyuo katika manispaa ya mji huu wa kusini mashariki mwa Tanzania. Yanatumika pia kama sehemu ya matumizi sahihi ya nguvu za vijana; kundi la watu wenye nguvu kubwa za mwili. Mashindano ni sehemu ya mazoezi muhimu yanayohitajika kwaajili ya kujenga na kuulinda mwili.

 Pamoja na malengo mengine mahususi na mazuri mno yaliyotajwa; Jina la mashindano haya lengo lake hasa ni kutetea na kulinda uhai kama jinsi ilivyo kwa malengo halisi ya "Pro-life". Pro life ni vuguvugu lenye lengo mahususi la kutetea na  kulinda uhai wa binadamu. Binadamu huanzia kwenye muungano wa yai la mama na mbegu ya baba, na hapo safari ya mwanadamu mpya huanza. Kwa hiyo binadamu anaanzia tumboni mwa mama hata kabla ya kuzaliwa. Kutokana na maelezo hayo basi utaona kuwa Prolife hutetea uhai wa mtoto anayekuwa tumboni mwa mama na kwa hivi hupinga utoaji mimba kwa lengo la kutetea na kulinda uhai.

Kwa hiyo basi vijana wa kike na wa kiume wanaalikwa kuheshimu uhai wa mwanadamu kwa kujizuia kabisa kushiriki katika utoaji mimba. Kunaweza kuwa na sababu lukuki za kuhalalisha utoaji mimba lakini ukweli ni ule ule kwamba utoaji mimba ni uuaji ni uharibifu wa maisha. Vijana hivi leo wanashindwa kujizuia kushawishiwa kutoa mimba; njia rahisi ya kuepuka kujiingiza kwenye kosa hilo ni kuwa na mahusiano yenye heshima. Mvulana na msichana wawe marafiki ili kusaidiana kukua kikamilifu katika ubinadamu (mwanaume hujifunza toka kwa mwanamke na kinyume chake pia) mahusiano ya kimwili yasubiri vijana watakapofunga ndoa na kutambulika mbele ya jamii na mwenyezi kuwa wao ni bwana na bibi fulani. Kufanya hivyo kutasaidia kuondoa utoaji mimba-uuaji!

Katika tafsiri ya leo ya kutetea na kulinda uhai vijana tunaalikwa kuacha mambo yote ambayo yanapunguza maana ya maisha yetu. Vijana tupunguze ama kuacha kabisa unywaji wa pombe, tuache uvutaji wa sigara kwa kuwa hasara na matatizo yanayosababishwa na uvutaji ni makubwa kuliko furaha ya uvutaji. Kwa wale tunaotumia dawa za kulevya tuache na tuwashawishi rafiki zetu waache ushiriki na utumiaji wa vitu hivi vinavyopingana na maisha. Tukifanikiwa katika hayo amani, upendo na mafanikio vitatamalaki kote duniani, lakini vianzie kwa kila mmoja wetu.

Kwa hivi basi mashindano ya "STEMMUCO Pro-life 2012" yanalenga kutetea na kulinda uhai wa binadamu. Vijana wote walio mashindanoni wanapaswa kufahamu hilo na kwamba wao tayari wanakuwa ni mabalozi wa uhai-ni watetezi na walinzi wa uhai. Mashindano mema!!!

Thursday, March 8, 2012

Siku ya Wanawake duniani katika matukio Mtwara

Vazi rasmi siku hiyo ilikuwa kitenge - Naam kina mama wanapendeza
na kuongeza staha sana kwa mwanamke pale wanapovalia mavazi ya heshima




























Hii ni siku mahususi kwa wanawake duniani. Hutumika kuwakumbusha wanawake wenyewe, watunga sera, na jamii yote kwa ujumla juu ya haki na nafasi ya mwanamke katika nyanja zote za maisha.































Tafiti nyingi hapa Tanzania zinaonyesha kuwa mwanamke hususani yule wa kijijini anafanya kazi nyingi kuliko mwananchi mwingine yeyote. Pamoja na mchango huo mkubwa wa wanawake, mara nyingi juhudi zao hazitambuliki vya kutosha na wala hawathaminiwi na jamii kwa kiasi stahiki. Hivyo kwa siku ya leo ni fursa kuikumbusha jamii na wanawake wenyewe hasa wale wa mashambani. Ni dhahiri kuwa wanawake wengi vijijini wanafanya kazi nyingi kwa kuwa tamaduni nyingi, zenye mfumo dume, zinawalazimu kufanya hivyo.





























Tunawaomba na kuwapa changamoto wanawake wa mijini, kulihamasisha kundi hili lenye mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi yetu. Mwaka huu, kwa kutambua nafasi ya elimu kuleta mabadiliko kwa jamii, wito umeelekezwa kwa ushiriki wa mtoto wa kike katika elimu kama kichocheo kikubwa kuleta maendeleo ya jamii.

Saturday, March 3, 2012

Duh angurumapo simba mcheza nani?


Hii toka kwa kaka michuzi
Hakuna ubishi kuwa watu wengi tunapenda mchezo wa soka hapa Tanzania.

kupitia huu upenzi wa mpira kwanini tusibuni njia ya kuhamasishana kwenye elimu kupita soka ili kiwango na ubora wa elimu yetu vikue pamoja na soka hasa la kina mama; soka la kina mama Tanzania ni bora zaidi kuliko la kina baba, kwa kigezo cha matokeo. Taifa Stars imewahi kuifunga timu nyingine mabao matano?


Hii ni keki tuliyokula siku ya ufunguzi wa Simba TV. Hata hivyo TV hiyo inayorusha vipindi vyake kupitia clouds tv inaishia tu mikocheni, haifiki walipo watazamaji wa mdenga, Mtwara, Lindi, Mazoo, Shytown, Ta etc fikisheni mapema basi! 

Harakati za Ubunifu wa vazi la Taifa?




Picha zote kwa hisani ya blogu la UDADISI

Thursday, March 1, 2012

Mtazamo Chanya Humjenga Binadamu!

Maneno haya ya kiingereza juu ya rais huyu wa Marekani ni fundisho la aina yake
tujifunze kupenda tunachofanya na tukifanye kwa moyo wote matokeo yake ni furaha na amani
Ujumbe huu nimeupata toka kwenye e-mail niliyotumiwa na Edward Ezekiel, kwa hakika ni ujumbe mzuri na wa maana mno.

Huu unawafaa vijana wote ambao ni wepesi wa kukatishwa tamaa na watu wengine. Kumbuka hakuna mtu mwenye mamlaka ya kukufanya ukose furaha, ili ukose furaha, ukasirike ama uwe kwenye aina yote ya hisia ni lazima wewe mwenyewe uamue; Lincoln ni mfano mzuri mno. Maneno ya watu wengine si yenye kutubomoa.

Fundisho la pili ni kufanya kazi zetu kwa uadilifu, ubunifu, umakini na zaidi ya yote upendo. Mambo hayo husaidia kuvumbua mbinu mpya za kurahisisha maisha na kuleta maendeleo kwa watu haraka. Ndugu huyu japo si Mwafrika na atukumbushe kutenda mema!

Je Afrika imejididimiza yenyewe?

Ndugu zangu salam,
Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere kinawakaribisha wote kwenye , Malumbano ya Hoja baina ya Wanafunzi wa Sekondari na Chuo Kikuu, mada ni " Handira hii inaamini kwamba Afrika imejididimiza yenyewe" ikifuatiwa na filamu ya "The Last Days of Walter Rodney" hapa UDSM-katika ukumbi wa Nkrumah, tarehe 03.03.2012 siku ya Jumamosi kuanzia saa 4:00 asubuhi mpaka 8:15 mchana. Malumbano haya ya hoja yatakuwa katika lugha ya Kiswahili. Nawaombeni tusambaze tangazo hili kwenye mitandao yetu ya jamii. Karibuni sana.
Nimeambatanisha ratiba na bango bonyeza hapa.

Walter Rodney Luanda
Mwalimu Nyerere Chair-Senior Administrative Officer