|
Picha ya Sarah Baartman |
Tunaishi
katika zama mpya. Zama za ubepari uliochukua sura ya uliberali mamboleo. Ipo
tofauti kati ya ubepari halisi na uliberali-mamboleo. Ubepari halisi ulijikita
katika kutengeneza faida kwa kuzalisha bidhaa viwandani. Uliberali mamboleo ni
ubepari wa kikasino. Katika zama za uliberali-mamboleo uzalishaji bidhaa siyo
tena msingi wa ubepari
Upepari
wa kikasino ni ule wa kutengeneza faida na kulimbikiza mtaji bila kujihusisha
katika uzalishaji-mali. Uzalishaji-mali hufanyika mashambani na viwandani.
Katika ubepari wa kikasino na kiporaji, mtu hutengeneza
pesa kwa biashara za udalali, ununuaji na uuzaji hisa, ukopeshaji, kamari,
upaishaji wa bei za vitu, n.k.
Katika uliberali mamboleo, ambao ni awamu ya ubepari
uliofilisika, kila kitu hugeuzwa bidhaa na kuuzwa au kununulika sokoni. Huduma
za jamii (afya, elimu, makazi na maji) hugeuzwa bidhaa na kuuzwa sokoni kama itokeavyo
kwa manukato, nguo au magari. Ubidhaishaji umevuka mipaka, kiasi kwamba hata viumbe
vinabidhaishwa. Katika makala haya nitazungumzia ubidhaifishaji wa muoneko wa
viungo vya binadamu, hususun akinamama ufanyikao katika mfumo wa uliberali
mamboleo.
Agnes Masogange
Jina
la Agnes Gerald “Masogange” sio geni katika masikio ya Watanzania. Ni mwanadada
mrembo. Lakini warembo wapo wengi. Masogange ni maarufu. Akina dada warembo na
maarufu wapo wengi pia. Lakini umaarufu wa Masogange ni tofauti. Umaarufu wake
umepatikana kutokana na anavyoonekana katika video za wanamuziki, na sehemu ya
mwili wake inayompatia umaarufu ni makalio yake.
Mara
kadhaa amekwishahojiwa naye akajisifia kuwa anajisikia raha kuwa na makalio
makubwa: “Hakuna sehemu
ninayoipenda kama makalio, yamekaa vizuri, nayapenda, najidai kupitia sehemu
hiyo niliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu,” alisema Agnes katika moja ya mahojiano
yake yaliyochapishwa Machi 29, 2014 katika blogu ya Global Publishers.
Ukiingia katika mtandao
utaona picha na video za Masogange. Nyingi ya hizo zinaonyesha “sehemu hiyo
aliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu”. Ameenda mbali hata kuweka picha na video
zinazoonyesha utupu wake. Huko mtandaoni kuna wanaomlaani. Lakini hawa ni
wachache. Wengi, hasa vijana, wanamsifia.
Lakini ole wako ewe
msomaji mwema. Kama ulidhani kuwa makala haya yamelenga kumlaani ama kumsifia
Masogange basi umekosea. Makala haya hayamzungumzii Masongange kama mtu bali
yanazungumzia mfumo katili wa uliberali mamboleo. Nitatumia pia mfano wa
“Masogange wa Kenya” aitwaye Vera Sidika. Afrika nzima kuna “akina Verana
Masogange” wanaoibuka na kujizolea umaarufu na pesa. Huko Ulaya na Marekani
idadi ya mabinti wa aina hiyo imekithiri. Katika kona mbalimbali za dunia, wapo
mabinti wanaotamani kuwa na umbile kama la Vera Sidika au Masogange ili wawe
maarufu na kujizolea pesa. Je, ni nini chanzo cha wimbi hili la ubidhaishaji wa
maumbile ya binadamu? Nani mwenye maslahi katika wimbi hili? Makala haya
yamelenga kujibu maswali hayo.
Kwa kuanzia, ningependa kujadili
kisa cha Sarah Baartman, bintiwa kiafrikaaliyezaliwa nchini Afrika Kusini mwaka
1789. Alifariki mwaka 1815, jijini Paris, Ufaransa, akiwa na umri wa miaka 26.
Je, alifikaje Paris?
Sarah alikuwa mtumwa huko
Afrika Kusini. Mmiliki wake mwenye asili ya kikaburu aliamua kumuuza kwa
daktari wa kiingereza aliyeitwa Alexander Dunlop. Dunlop alikuwa ameona ‘fursa
za kiuchumi’ katika umbilela Sarah, na hasa makalio yake makubwa. Hivyo
akamshawishi mmiliki wa Sarah amwuzie “bidhaa” hiyo adimu ili akaitumie kutengeneza
pesa huko Ulaya.
Sarah alipelekwa katika
nchi kadhaa za Ulaya, hasa Uingereza na Ufaransa. Huko alipelekwa katika kumbi
za maonyesho akiwa uchi, na wazungu wakawa wanalipa viingilio kuja kushuhudia weusi
wa ngozi yake na ukubwa wa makalio yake na sehemu zake za siri.
Ili kutengeneza pesa
zaidi, mmiliki wa Sarah akawa akimuuza kwa wanaume wa kizungu waliotaka
“kumvumbua” zaidi mwanadada huyowa Kiafrika. Sarah akafariki kwa ugonjwa wa
zinaa. Hata baada ya kufariki viungo vya mwili wake vilikatwa na kuwekwa katika
makumbusho huko Paris ili wazungu wakajionee. Sarah aliendelea kuwa bidhaa na
kivutio cha utalii hata baada ya kufa.
Tofauti ya
Sarah na “ma-modo” wa sasa
Je,
kuna tofauti kati ya Sarah na“mamodo” wa sasa?
Sarah
aliishi katika kipindi ambacho biashara ya utumwa ilikuwa imeshika hatamu.
Waafrika waligeuzwa bidhaa, wakauzwa na kununuliwa sokoni, kama vile mtu
anunuavyo nyanya, nguo au kuku. Wakapelekwa huko Amerika kuzalisha mashambani
na migodini. Nguvu-jasho ya Waafrika hawa ndiyo iliyozijenga na kuzistawisha
nchi za Ulaya na Marekani ambazo leo tunakwenda kuomba misaada ya hali na mali.
Kwa
hiyo, kama ilivyokuwa kwa babu na bibi zetu wengine waliopelekwa utumwani,
Sarah hakwenda Ulaya kwa hiari yake. Alilazimishwa. Alikuwa ni bidhaa.
Usipofanya
uchambuzi wa kina, unaweza kusema kuwa “ma-modo” wetu wa leo wanaotumia maumbo
yao kama vivutio hufanya hivyo kwa hiyari yao. Lakini ukweli ni kwamba kuna
nguvu ya kimfumo inayowalazimisha kufanya hivyo wafanyavyo. Nitajadili.
Maumbile
ya Sarah yalikuwa ni ya asili. Mwili wake ni ule aliojaaliwa na Muumba. Katika
zama zetu, wapo mamodo wenye maumbile ya asili. Lakini wapo wengi pia ambao
wamelazimika kubadili maumbile yao. Ukuzaji wa makalio na matiti, uchubuaji wa
ngozi, na hata ubadilishaji wa jinsia yamekuwa ni mambo ya kawaida.
Kiini macho na
nguvu ya soko
Ukiingia
mtandaoni, utakuta kampuni kadhaa zikitangaza bidhaa za kukuza makalio na
matiti. Kwa wanaume, zipo dawa za kunenepesha na kurefusha uume, kukuza misuli,
n.k. Kampuni hizi za kibepari ndizo kiini hasa cha ubidhaishaji waviungo vya
binadamu, na hasa makalio na matiti. Ili bidhaa zao zikubalike, kampuni hizi
sharti zitengeneze soko za bidhaa zao.
Soko
lenyewe hutengenezwa kwa kubadili mtazamo na fikra zawatu, na hasa vijana, juu
ya dhana ya urembo, mapenzi na mahusiano ya kimwili. Kwa hiyo, kwa kushirikiana
na kampuni za utengenezaji wa filamu za ngono, kampuni za kurekodi video za
muziki, wamiliki wa vilabu na makasino, magazeti na televisheni za udaku, hospitali
za binafsi za upasuaji wa plastiki, kampuni za uzalishaji wa dawa hizi zimewezesha
kukubalika kwamba makalio na matiti makubwa ni urembo, lakini pia ni hazina
murua kwa shughuli za ujasiriamali.
Kwa
hiyo, katika zama zetu hizi binti mrembo anasemekana kuwa ni yule aliye na
makalio makubwa, matiti makubwa, na ngozi nyeupe. Ikitokea hukuzaliwa na vitu
hivi basi usikonde: utavipata kwa kutumia dawa au kwa kufanyiwa upasuaji wa
plastiki. Binti mwenye sifa hizi anaaminishwa kuwa ana “rasilimali”ambayo anaweza
kuitumia kutengeneza pesa iwe ni kwa kujiuza sokoni ama kwa kuwa na mpenzi
mwenye pesa.
Hivyo
basi, wapo wanenepeshao viungo vyao ili kuwaridhisha wapenzi wao. Wapo wafanyao
hivyo ili “kwenda na wakati”. Lakini wengi pia hufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya
soko. Soko lenyewe sio lazima liwe la kujiuza kimwili. Ni soko la kuuza
“makalio”, watu wakayaona iwe ni katika klabu za usiku, magazeti ya udaku au
video za muziki, na mwenye nayo akatengeneza pesa.
Tarehe
10 Februari 2011, gazeti la MailOnline
la nchini Uingereza liliripoti kifo cha Claudia Aderotimi, mwanafunzi wa nchini
Uingereza, aliyefariki huko Marekani akiwa ameenda kufanyiwa upasuaji wa
kuongeza makalio. Claudia, ambaye alikuwa na ndoto ya kuwa mnenguaji katika
video za wanamuziki wakubwa, aliwahi kukosa tenda kwa kutokuwa na makalio
makubwa. Aliambiwa kuwa ili afanikiwe ni lazima awe na makalio yaliyobinuka
kama ya mwanamuziki Beyonce. Hivyo, mfumo tulio nao unawatengenezea mabinti
kiini-macho (illusion) cha “kuwa na
umbo kama la Beyonce ili ufanikiwe”.
Hapa
Afrika, wapo akina-dada wachache ambao kutokana na maumbile yao, yawe ya asili
ama “yaliyokarabatiwa” kwa dawa au upasuaji, waliofanikiwa kujipatia pesa,
Maisha yao ni ghali: toka nguo wavaazo, manukato wajifukizayo, magari
waendeshayo na kumbi za starehe waingiazo. Wengi wao huenda kufanya “shopping”
Dubai au Afrika Kusini.
Vera Sidika:
“Mwili wangu ni dili”
Katika
kipindi cha The Trendkirushwacho na
kituo cha NTV nchini Kenya, Vera Sidika,ambaye amejizolea umaarufu nchini Kenya
kutokana na umbile la makalio yake, alisema kuwa huenda kufanya “shopping” ya
kati ya dola 10,000 hadi 50,000 (yaani kati ya Tshs. milioni 16 hadi milioni
80). Viatu alivyokuwa amevaa siku hiyo vinaghatimu Tshs. milioni 5 na laki 6,
na nywele zake za bandia ni Tshs. milioni 3 na laki 7.
Ngozi
ya Vera sio ya asili. Ilichubuliwa kitaalamuna akawa mweupe. Vera anajitapa
kuwa ubadilishaji wa rangi ya ngozi yake ulitumia zaidi ya shilingi milioni 15
za Kenya (takribani shilingi milioni 300 za Tanzania). Vera anasisitiza kuwa
tangu apate ngozi nyeupe, kwake imekuwa “baraka”. Anatengeneza pesa zaidi, na
anaalikwa nchi mbalimbali kwenda kusherehesha vilabu vya usiku (club hosting).
Vera
anasema kwamba ukimwona klabu ujue amekwenda kutengeneza pesa. Hufanyaje hasa?
“Huwa nasimama pale, na kutabasamu, na kupiga picha na mashabiki,” alifafanua.
“Mwili wangu ni biashara yangu na ninautumia kutengeneza pesa,” Veera
alijitapa.
Nyuma ya Vera, zipo kampuni za kurekodi
video za muziki, wanamuziki, magazeti, redio, vituo vya televisheni, vilabu vya
usiku, kampuni za kuzalisha kemikali za kubadili rangi ya ngozi, hospitali za
binafsi zifanyazo uchubuaji wa ngozi, kampuni za vipodozi na mavazi ya kisasa,
hoteli za kifahari, n.k. Wote hawa humtumia Vera kutengeneza faida.
Lakini tusisahau watu wa msingi
wamfanyao binti huyu ajivune: hawa ni wale anaowaita “my fans”, yaani mashabiki
wake. Kila siku Vera huweka picha za nusu uchi, zionyeshazo makalio yake,
katika mtandao ili kukonga nyoyo za mashabiki wake. Aendapo Klabu hujiachia na
kupiga nao picha za “ajabu” ili waendelee kumshabikia. Mashabiki hawa pia
tayari wamekwishatekwa na mfumo, nao wakaamini juu ya urembo utokanao na kuwa
na umbo kama la Vera.
Mtandao wa
Kibiashara
Zipo
nchi nyingi, mathalani Venezuela na Ufaransa, ambako ukuzaji-makalio na matiti
vimetia fora kiasi cha wananchi kuzipigia serikali zao kelele ili zidhibiti
vitendo hivyo. Lakini hii ni kazi bure kama tusipoelewa kiini cha tatizo
lenyewe.
Gazeti
la mtandaoni liitwalo “The Revolution” linalomilikiwa na cha Chama cha
Kikomunisti cha Marekani liliwahi kufanya uchambuzi wa biashara ya upachikaji
wa matiti ya bandia kwa wanawake. Nchini Uingereza pekee kati ya wanawake
20,000 hadi 30,000 hukuza matiti kwa njia hiyo kila mwaka, na biashara hiyo huingiza
pato la zaidi ya dola milioni 150 (takribani shilingi bilioni 240 za
kitanzania) kwa mwaka.
Kwa
mujibu wa taarifa ya chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa plastiki nchini
Marekani, idadi ya watu wanaojihusisha na upasuaji wa plastiki iwe ni katika
kukuza au kupunguza makalio, matiti, nyusi, nywele, kubadili sura au ngozi,
imeongezeka kutoka watu milioni 7.5 mwaka 2000 na kufikia watu milioni 14 mwaka
2011.
Jarida
la “The Revolution” linaripoti kuwa kampuni za utengenezaji kemikali za ukuzaji
matiti hutumia kemikali bandia ili kutengeneza faida zaidi. Moja ya kampuni
hizo ni Poly Implant Prothese (PIP) ya nchini Ufaransa. Kutokana na madhara
makubwa ya kiafya yasababishwayo na kemikali za PIP, baadhi ya nchi zimejaribu
kuzipiga marufuku bidhaa za kampuni hizo bila mafanikio.
Maslahi
ya kibiashara hayaishii katika kampuni tu. Ubidhaishaji wa huduma za afya
umezifanya hospitali nyingi za binafsi zijiingize katika kazi ya upasuaji wa
plastiki ili kukuza au kupunguza viungo vya mwili. Wateja waliopata madhara ya
kiafya kutokana na kemikali za kukuza matiti na makalio wamekataliwa na
hospitali zilizowapa huduma hizo. Wamiliki wa hospitali hizo, kwa mujibu wa
jarida la The Revolution, “wanadai
kuwa hawapashwi kuwajibishwa kutokana na kununua bidhaa zilizokuwa sokoni.”
Ubepari: toka uzalishaji hadi ubidhaishaji
Pengine cha kufikirisha ni kauli ya
Vera kuwa “mwili wangu ni biashara yangu na ninautumia kutengeneza pesa”. Suala
la kujiuliza ni kuwa, je, tangu lini mwili wa binadamu uligeuka kuwa bidhaa,
hata ukatumika kutengeneza pesa?
Katika kitabu chake cha Das Kapital(Capitalau Mtaji) kilichochapishwa
mwaka 1867, Karl Marx aliubainisha ubepari kama mfumo unaojitambulisha kupitia
bidhaa. Lakini bidhaa hizo ni zile zinazozalishwa na nguvu ya binadamu na
kupelekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa. Cha kushangaza ni kuwa watu hushikwa na
wazimu wa bidhaa, wakazipenda na kuzithamini, lakini wasione kiini ndani ya
bidhaa hizo. Kiini hicho ni nguvu-kazi ya binadamu iliyotumika kuzitengeneza.
Marx alifariki mwaka 1883, yapata miongo saba baada ya Sarah kufariki. Kipindi alichoishi
Marx kilikuwa ni kipindi cha ubepari wa uzalishaji bidhaa, viwandani na
mashambani.
Takribani karne moja na nusu baada ya
kuchapishwa kwa Das Kapital, Prof.
Issa Shivji, mmoja wa wanazuoni wa Kimaksi, ameandika kuhusu ubepari wa karne
ya 21, ambao umechukua sura ya uliberali mamboleo. Mfumo huu hautegemei tena uzalishaji,
bali ubidhaishaji wa kila kitu.
Vitu ambavyo kwa asili yake haviwezi
kuuzwa, hugeuzwa bidhaa na kuuzwa sokoni. “Utengenezaji wa bidhaa-sesere na
zisizo za asili hauna mipaka katika mfumo wa uliberali-mamboleo,” anaandika
Shivji katika kitabu chake kiitwacho Accumulation
in an Afriacan Periphery. “Mazingira, ikolojia, na viumbe vingine wa asili
(wanyama na mimea), viini vya kibaiolojia (ute wa mimea na viini-tete vya
binadamu) hugeuzwa kuwa bidhaa, hali ambayo hutokea pia katika hisia na raha
zihusishazo mahusiano ya kimwili. Juu ya vitu na mahusiano halisi hutengenezwa
vitu-pepe na mahusiano-pepe, ambavyo pia hubidhaishwa. Katika ulimwengu wa
mahusiano utaona mambo kama mabinti wa mtandaoni, vyumba vya faragha, na
ufanyaji-mapenzi katika mtandao” (tafsiri yangu).
Kwa hiyo, tujifunzacho hapa ni kuwa
mtandao wa watumiao miili ya vijana, na hasa wa kike, kutengeneza pesa ni
mpana: vituo vya televisheni huwaalika katika mahojiano na kueneza udaku juu
yao na kwa kufanya hivyo hutengeneza pesa, magazeti ya udaku hutengeneza pesa
kwa kuchapisha picha na stori za mabinti hao, kampuni za utengenezaji wa
kemikali za ukuzaji makalio/matiti na uchubuaji ngozi nazo hutengeza pesa,
hospitali zijihusishazo na uchubuaji ngozi na upasuaji wa ukuzaji makalio
hutengeneza pesa, na vilabu vya usiku viwaalikao mabinti hao navyo hutengeneza
pesa, n.k. Huu ni mtandao mkubwa wa kutengeneza pesa katika zama hizi za utumwa
mamboleo.
Kiini cha mtandao huuni mfumo wa
uliberali mamboleo, ambao ni aina ya ubepari uliofilisika na uliochukua sura ya
kikatili ya ubidhaishaji wa kila kitu, yakiwemo maumbile ya binadamu! Mfumo huu
hauwezi kuwekewa viraka kwa kuhubiri juu ya maadili kwa vijana. Ni ama
tuubomoe, au tuuache uendelee kutubomoa kwa kugeuza hata miili yetu kuwa
bidhaa. Kama wapigania uhuru wa bara la Afrika walipambana dhidi ya ukoloni,
sisi wajukuu wao hatupashwi kusalimu amri. Hatuna chaguo mbadala, ni jukumu
letu sote kupambana dhidi ya uliberalimamboleo
Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma.
Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.