Tuesday, January 17, 2012

DAWA BANDIA ZA MALARIA NI KIFO KWA AFRIKA...

Tabibu akitoa huduma kwa Mtoto mgonjwa wa malaria













Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la bidhaa nyingi bandia... karibu kila kitu unachonunua ni kama kuna mbadala wake ambao ni bandia. Hali hii imeonekana kuwa ni kitu cha kawaida na hali inayokubalika kimaisha. Hali hii la hasha haijakubalika kisheria, ambapo kuna nyaraka rasmi kwamba kuanzia sasa tuwe na bidhaa bandia, lakini kulingana na jinsi mambo yanavyokwenda basi tunaweza kusema ni hali iliyokubalika. Bidhaa bandia nyingi zinasemekana kutoka nchi za mashariki zinazoendelea kiuchumi.

Inasemekana kuwa katika nchi hizo za mashariki hususani Uchina; unaweza kutengenezewa bidhaa ya aina yoyote kulingana na uwezo wako wa kifedha. Tatizo hili linasababishwa na wafanyabiashara wenye uchu wa kujitajirisha haraka... utajiri si jambo baya ila utajiri kwa njia isiyo sahihi ni makosa. Lazima mambo haya ya bidhaa BANDIA TUYAKEMEE, na katika afya ni hatari zaidi.

Dawa bandia kwa hakika ni kifo kwa bara la Afrika, takwimu za shirika la afya duniani WHO linaonyesha kuwa Malaria ndo ugonjwa unaoongoza vifo vya watu wengi zaidi barani humo, bara linawekwa kwenye orodha za umasikini duniani. Kuzuka kwa wimbi la dawa bandia za ugonjwa huo unaoongoza kwa vifo barani ni sawa na kutoa hukumu ya kifo kwa waafrika hususani wale wenye kipato duni; sehemu kubwa ya Waafrika. Jambo la kusikitisha hapa ni kuwa hukumu hii inatolewa na ndugu zetu wa barani humu.

Wanaoingiza nchi dawa bandia za Malaria ni ndugu zetu waafrika, kwa hili tusimame pamoja tuwaambie acheni kuua ndugu zetu- wafanyabiashara wanaoingiza, wanaoagiza dawa bandia hawana utu na ni wauaji - waache kufanya hivyo!

Taarifa hizi zinapatikana pia kwenye wavuti wa Bbc Kiswahili

MZEE JANGALA AONGELEA SANAA

  Na Mwandishi wa BASATA
 Msanii Nguli wa sanaa za maonesho, Bakari Kassim
Mbelemba (Mzee Jangala) aikizungumza na
wadau wa sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa


Msanii nguli wa Sanaa za Maonesho, Bakari Kassim Mbelemba (Mzee Jangala) amesema kuwa programu ya Jukwaa la Sanaa inayoendeshwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ni chuo tosha kwa wasanii katika kuwapa elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali ya sekta ya Sanaa.

Akizungumza wiki hii, kwenye programu hiyo katika ukumbi wa BASATA, Ilala Sharif Shamba, Jangala alisema kuwa, Jukwaa la Sanaa ni jambo la kujivunia na ni chachu ya kukua kwa Sanaa.

“Jukwaa la Sanaa ni programu inayonifanya nithubutu kusema, sasa Sanaa ni kazi, maana kazi yoyote ili ifanywe kwa ufanisi inahitaji elimu, uratibu na mwongozo, hivyo wasanii tuitumie fursa hii adimu” Jangala alisema.

Aliongeza kuwa, programu hii imekuwa ikiwaleta wataalam na wadau mbalimbali wenye uzoefu katika sekta ya Sanaa hivyo, kwa wasanii ambao wamekuwa wakihudhuria toka mwanzo wamepata mambo mengi ambayo yatawasaidia katika kukuza na kuendeleza vipaji vyao.

Alisisitiza kuwa, Sanaa inabadilika na kumezwa na teknolojia mpya zinazokuwa zinajitokeza hivyo, ni lazima wasanii wajenge utamaduni wa kutafuta maarifa mapya na kuwa wabunifu huku wakizingatia maadili ya kitanzania.

Kuhusu wasanii kulewa umaarufu na sifa, alishauri kuwa ni vema wakabadilika na kufanya kazi zao kwa bidii na ubunifu zaidi kwani, sifa ya msanii inakuja yenyewe kutokana na kazi anazozalisha na kupeleka kwa jamii inayomzunguka.

“Sifa ya mpishi hutolewa na mlaji, kwa hiyo wasanii wanapotengeneza kazi zao wasijisifu wenyewe bali wasubili kusifiwa na msikilizaji au mtazamaji” alishauri Mzee Jangala.

Alizungumzia pia suala la wasanii kutegemea vipaji tu pasipo kuingia darasani na kusema kuwa hilo haliwezi kukuza sekta ya sanaa na badala yake tutakuwa na kazi zinazoandaliwa kwa msukumo wa soko na si taaluma ya Sanaa

“Wasanii ni lazima watambue kuwa, mbolea ya kipaji chochote kile ni elimu. Ni vigumu sana kutegemea kipaji tu pasipo kukipalilia kwa taaluma ya sanaa husika”

Kwa upande wake, kaimu mwenyekiti wa Jukwaa la Sanaa, Vivian Nsao Shalua alishauri wasanii kulitumia Jukwaa la Sanaa ili kuzijua sheria, taratibu na mbinu mbalimbali zitakazo waongoza katika shughuli zao za Sanaa.