Thursday, October 13, 2011

MUDA WA KUSAKA FIKRA ZAIDI

Picha kwa hisani ya blogu ya mdau Muliriye

Jumatatu ya 10.10.2011 ilitumika kufungua mwaka wa masomo Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Agostino – Mtwara. Masomo ni njia ya kumwezesha mtu kugundua vipawa vyake na kuvitumia kwa malengo yale yale ya kuweza kuitawala dunia na vilivyomo humo ilikuboresha maisha ya jamii ya wanadamu.

Elimu ya Chuo Kikuu, kwa kutumia maneno ya Mwalimu Nyerere, ni elimu hasa yenye malengo ya kumfunza mtu kuwa na fikra bayana, kuwa na uhuru wa fikra, kuchanganua, na kutatua matatizo kwa kiwango cha juu kabisa, haya ni mawazo ya Mwalimu kwa maneno yangu. Kwa hivi basi elimu ya Chuo Kikuu imjenge kijana kuwa na fikra binafsi na tena zenye nia ya kuiendeleza jamii ya wanadamu.

Kumbe elimu hiyo ya juu haina lengo la kumfanya mwanafunzi akariri, lengo kuu ni kumfanya awe na uwezo wa kujenga fikra binafsi, zenye kuweza kuijenga jamii na awe na uwezo wa kuyatetea na kuyasimamia mawazo yake, kwa kufanya hivyo ndio tunaweza kupata wagunduzi (wavumbuzi), wanasayansi na watu waliotayari kuijenga dunia.

Huko SAUT Mtwara, shughuli za kuanza mwaka wa kuendeleza ujenzi wa fikra mpya ulianza kwa kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu na kisha kufuatiwa na shughuli mbalimbali za kijamii.



Baadhi ya wageni mashuhuri wakielekea eneo la tukio


Wageni Maarufu na mashuhuri mno walikuwepo, hapa Profesa kijana akiwa na wadau wengine wakielekea eneo la tukio katika viwanja mahususi kwa tukio la siku

Hapo chini wadau wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza shughuli yenyewe

Tuesday, October 11, 2011

Falsafa - kiwanda cha fikra!















Muhula wa mwaka mpya wa masomo wa vyuo vikuu nchini Tanzania kwa kawaida huwa ni miezi ya Septemba na Oktoba. Hii ni kwa sababu wanaojiunga na vyuo humaliza masomo yao ya elimu ya sekondari mwezi Februari, na kisha matokeo yao kutoka hufuata utaratibu maalumu kuomba nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu nchini ambavyo idadi yake yazidi kuongezeka. Pamoja na vyuo vikuu nchini kuongezeka, bado vyuo hivyo haviwezi kuchukua idadi ya wanafunzi wote nchini wenye sifa za kujiunga na elimu hiyo ya kiwango cha juu. Vyuo kadhaa binafsi vinasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo hili kwa kuanzisha matawi ya vyuo hivyo sehemu mbali mbali nchini. Kwa kiasi kikubwa hii inasaidia sana kuwapatia wanafunzi wengi fursa za kuendelea na masomo katika elimu ya juu.

Katika makala hii naangazia japo kwa ufupi tu tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino kilichopo mjini Mtwara. Chuo hiki ambacho kilianza kama kituo cha masomo cha "Saint Augustine University of Tanzania" (SAUT) kimepiga hatua sasa na kuwa "University College" hatua ya juu kuelekea kuwa na mamlaka binafsi. Chuo hiki kinafundisha programu ambazo hakuna sehemu nyingine hapa nchini. Moja ya programu hizo ni ile ya falsafa na elimu. Falsafa ni somo geni kwa wanafunzi wengi wa nchi zinazotumia kiingereza kama moja ya lugha zake rasmi, hususani za Afrika Mashariki, kwa nchi zinazotumia kifaransa, somo hili hufunzwa hata katika elimu ya sekondari.

Falsafa ni chimbuko kuu la mawazo; humjengea mtu nafasi ya kuwa na fikra binafsi ambazo anaweza kuzisimamia na kuzielezea bayana. Kwa mtazamo wangu binafsi, nchi zetu za Afrika, kupitia viongozi wake, zina haja ya kubuni mikakati na fikra binafsi za kiafrika ili kutatua matatizo yanayotusibu hapa barani. Falsafa inawapatia wanafunzi fursa ya kukutana na mawazo ya watu mbalimbali toka bara ulaya, bara Asia, Marekani, na pia barani Afrika; inafanya hivyo kwa lengo la kumpatia kijana fursa ya kujenga fikra zake binafsi. Wakati kijana anapata fursa ya kujenga mawazo binafsi, anafaidika pia na kwa kujifunza masuala ya maadili, jambo ambalo lazitatiza nchini nyingi barani Afrika, hususani tatizo la rushwa.

Wakati vijana wanaanza safari yao ya kujenga na kunoa bongo zao ni vyema wakajipanga kwa kusoma mambo ambayo yatainufaisha jamii nzima ya wanadamu na hivyo kuwa kweli wajenzi wa dunia; kila mmoja wetu ana nafasi ya kuwa mjenzi wa dunia hii kwa namna yake mwenyewe kulingana na vipaji alivyojaaliwa; akiongeza na kipawa cha falsafa mambo yatakuwa mazuri zaidi.


Picha kwa hisani ya google