Monday, July 18, 2011

Siku ya Nelson Rolihlahla Mandela

Leo Jumatatu, 18 Julai ni kumbukumbu ya kuzaliwa Mzee Nelson Mandela, rais wa kwanza wa Afrika Kusini ya Kidemokrasia (18.07.1918). Kadri ya kumbukumbu zangu huyu ndiye mtu pekee ambaye Umoja wa Mataifa umemtengea siku katika mwaka mahususu kwa heshima yake. Hivi leo anatimiza miaka 93 toka azaliwe; ni mmoja kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameishi kwa muda mrefu.

Nelson Mandela ni mtu anayepewa heshima kubwa duniani kote kwa wanaomfahamu na hata wasiomfahamu. Watu wengi hasa nje ya Afrika hususani katika jamii zinazopenda kusoma vitabu wamfahamu kupitia kitabu chake cha "Long Walk to Freedom". Hiki ni kitabu kinachoelezea historia ya maisha yake kwa kina kabisa. Sehemu kubwa ya kitabu hicho ameiandika yeye mwenyewe na tena akiwa gerezani. Hili ni moja ya mambo ya kujifunza toka kwa mzee huyu-maktaba kubwa duniani kote. Tujipange tuandike historia zetu sahihi ili kuiachia jamii na dunia kwa ujumla utajiri wa mawazo kama alivyofanya mzee Mandela. Wengine tulimfahamu mzee Madiba toka enzi za utoto; tukiwa shule ya msingi tuliimba nyimbo za kutaka Mandela achiwe huru na serikali ya makaburu. Utawala wa makabulu ulitawala Afrika Kusini kwa mabavu na kwa misingi ya kibaguzi ya rangi za binadamu; ni udhalimu wa aina yake kwa ustawi wa wanadamu.

Kwanini mzee huyu ni maarufu vile?

Saturday, July 16, 2011

Uhuru wa wahadhiri kimawazo

Makala ya Profesa Mbele juu ya uhuru wa kimawazo wa wahadhiri, kwa hakika, imenitia hamu kubwa kuendelea kuijadili. Nadhani ni suala la msingi kabisa kulitazama hasa hivi leo ambapo kuna vyuo vikuu lukuki hapa nchini. Ni muhimu kuupongeza uongozi wa nchi kwa kuruhusu kuanzishwa kwa vyuo vikuu vingi hapa nchini. Vyuo vikuu vingi moja kwa moja vinamaanisha kukua kwa wigo wa fikra nchini. Kuongezeka kwa fikra ni mwanzo wa ugunduzi na kichocheo kikuu cha maendeleo.

Moja ya masuala makuu katika kipindi cha " Scholarsticism" karne ya 12 na 13 ilikuwa ni kuibuka kwa wingi kwa vyuo vikuu vilivyotoa maarifa ya aina mbalimbali. Kipindi hicho Kanisa lilikuwa na mamlaka makubwa hata juu ya kilichofunzwa vyuo vikuu. Matokeo yake kazi za mwanafalsa Aristotle (384—322 BCE) zilikataliwa, hata hivyo kukataliwa huko kulikuwa kwa muda mfupi tu kwani baadaye kazi za gwiji huyo zilianza kufundishwa katika vyuo vikuu na kuboresha zaidi mawazo kwa wanavyuo na wanazuoni.

Kwahiyo basi ni vyema kwa viongozi wa nchi yetu kulitambua hilo na kuwaacha huru wahadhiri wafanye kazi yao, ambayo kimsingi hulenga kujenga wananchi wenye ukomavu wa kujenga hoja na kuzisimamia ili kuendeleza nchi yao na dunia kwa ujumla.

Kupata mawazo zaidi ya Profesa Mbele soma makala hiyo murua kabisa hapa








.