PICHA KWA HISANI YA BLOGU WAANDAA TAMASHA |
Nyama
choma ni chakula cha kitamaduni kwa baadhi ya jamii nyingi barani Afrika na
hata duniani. Historia inaonyesha kuwa jamii ama makabila mengi hapo kale
ziliishi/yaliishi kwa uwindaji wa wanyama pori. Hivyo nyama choma imekuwa
ikiliwa toka enzi za kale barani ila katika baadhi ya jamii tu. Jamii nyingine
ziliishi kwa kula mizizi na matunda pori. Wanahistoria wanaweza kutusaidia
katika hili, kuibuka kwa shughuli kuu na maalumu kwa jamii mbalimbali zama za
hivi karibuni ama nyuma kidogo, kulisababishwa na shughuli zale za uwindaji naukusanyaji mizizi na matunda pori.
Baadhi
ya makabila yakawekeza nguvu na muda wao katika uwindaji na baadaye kuwa
wafugaji, na mengine katika ukusanyaji mizizi na matunda pori na kisha kuwa
wakulima.Na kulikuwa na wavuvi halikadhalika na leo waendelea pia. Kwa hivi
basi wawindaji na baadaye wafugaji bila shaka hawa walikuja kuwa wala nyama ila
hali wakusanya mizizi na matunda pori baadaye wakawa wakulima wa mazao mbali
mbali. Mambo haya yalitokea zama za kale za mawe na chuma. Mawe na baadaye
chuma kilikuwa chombo cha kuwindia wanyama na pia zana ya kutifua ardhi na
kulimia mashamba. Hayo yalifanyika enzi hizo; hivi leo mambo haya yamebadilika.
Siku hizi kila mtu anakula nyama na tena kuna matamasha ya nyama choma. Ila
kabla ya matamasha ya nyama choma ya kisasa tuangalie nyama choma za sehemu chache nilizozifahamu miaka ya tisini.
Miaka
hiyo nilikuwa mwanafunzi mkoani Iringa. Nilisafiri kwa treni ya kati toka
Shinyanga, mara nyingine toka Mwanza hadi Dar es Salaam na mara nyingine
nilishukia Dodoma. Toka Dar es Salaam nilipanda basi hadi Iringa, ama nilipanda
treni ya Tazara mpaka Makambako na kisha kwenda mjini Mafinga, ambako palikuwa
nyumbani kwangu kwa miaka mitano. Safari kwa treni ya Tazara ilikuwa ya kitalii
na ya kuvutia, kwani nilipata fursa kuwaona wanyama wengi: swala, twiga, tembo
n.k. Ama niliposhuka Dodoma nilikwenda Iringa kwa njia ya “Ny’ang’oro” barabara
iliyokuwa na kona nyingi za kutisha na tena njia hiyo ilikuwa ni ya hatari,
kwani mara nyingine magogo yaliwekwa njiani na majambazi na kisha abiria
kunyang’anywa mali zao baaada ya basi kusimama. Namshukuru Mungu sikuwahi
kukutana na dhahama hiyo. Njia hii pamoja na kadhia zake ilinifurahisha kwani
nilikuwa na uhakika wa kula samaki watamu pale Mtera. Sijui mambo yanakwendaje
huko siku hizi kwani sijafuatilia taarifa za huko na sijapita huko tena miaka
mingi sasa.
Toka
kanda ya ziwa kwa treni watu wengi tulifurahia ujuzi wa wenyeji wa Saranda wa
kuandaa “nyama choma.” Kile kituo cha treni Saranda wengine hupaita
“Kilimanjaro Hotel”. Kila zama na kitabu
chake, enzi hizo Kilimanjaro Hotel ilikuwa ndiyo Hotel pekee? ya
hadhi ya juu zaidi jijini Dar es Salaam na wageni wengi maarufu walifikia pale.
Saranda, moja ya vituo vya treni ya kati kilichopo mkoani Singida, ni maarufu
mno kwa uuzaji wa kuku wa kienyeji. Hivyo hapo tulikula nyama choma, sikumbuki bei ya kuku wale wasioisha, iwe masika iwe kiangazi
bado utawapata. Bei ya kuku wale abiria wengi daraja la tatu tuliimudu,
sifahamu abiria waliokuwa mabehewa ya daraja la kwanza na la pili kama wao pia
walikula nyama choma ile. Kwa daraja la tatu, sina shaka, naelewa vyema kwani
nilishuhudia abiria wengi wakila “nyama choma” ya Saranda.
Kutoka
Iringa Mjini kwenda Mafinga, unapita maeneo mengi kadhaa moja muhimu huwezi
kulisahau ni Tanangozi; maarufu kwa nyama choma ya aina yake. Hapa sikupata
nafasi ya kula nyama choma ila nafahamu huduma hiyo ilikuwepo. Mjini Dodoma,
kule Mnadani kulikuwa na nyama choma za uhakika, sijui siku hizi, tena bei yake
ilikuwa rafiki kwani wananchi wa kipato cha kawaida waliimudu. Naambiwa baadhi
ya ndugu wabunge walifika kule kupata nyama choma pia. Najua kuna maeneo
mengine mengi yaliyokuwa yakitoa huduma hii kwa wahitaji tena kwa bei
maridhawa.
Ugumu wa maisha kipimo cha akili ama uvumbuzi
mama wa maendeleo, hivi karibuni hususani jijini Dar es Salaam kumeibuka
matamasha ya nyama choma. Kama tulivyoona hapo awali hili si jambo jipya na kuliona
kama uvumbuzi. Upya wa nyama choma hii ni kule “kusasaishwa” ambapo kuna kuwa
na eneo mahususi la kuendesha shughuli hiyo, ndani ya eneo ambamo kuna kuwa na
mambo anuwai yakiendelea ikiwa ni pamoja na ajira kadhaa za muda; mama/baba
lishe, biashara mbalimbali mfano uuzaji vinywaji, na bidhaa nyingine lukuki.
Ili kuingia eneo hilo ni lazima kutoa kiingilio. Nimeona matangazo kiingilio
mara nyingine huwa shilingi za Tanzania elfu saba 7,000/= hadi kumi elfu 10,000/=.
Kiingilio hicho si tiketi ya kwenda kunufaika na kila huduma kwenye tamasha
hilo, muingiaji atalazimika kuendelea kutoa pesa kwaajili ya huduma zingine.
Kwa haraka haraka nyama choma hii si kama ile ya Mnadani ama Saranda, hii ni
kwaajili ya watu wa tabaka maalumu.
Kwa
hakika matamasha ya nyama choma ya namna hii yanawalenga watu wenye ahueni kubwa
ya maisha. Ni jambo jema ama jambo baya si lengo la makala hii leo. Hapa
najiuliza tu je, hizi ni dalili za kukuwa kwa uchumi wa taifa la Tanzania
ambapo wananchi, baadhi yao, wanapata kipato cha matumizi ya ziada, matumizi
yasiyo ya lazima? Sera ya maendeleo ya Taifa inalenga kuwa ifikiapo mwaka 2025
jamii ya Tanzania iwe na watu wenye uchumi wa kati. Hii maana yake Mtanzania
mmoja anakuwa na uwezo wa kutumia kiasi cha dola za Marekani 5,960, yaani pesa
ya Tanzania 9,536,000/= kwa mwaka walau kitakwimu, ama shilingi 26,126/= kwa
siku. Kulingana na ripoti ya maendeleo ya binadamu ya shirika la maendeleo la
Umoja wa Mataifa ya mwaka 2014 Mtanzania wa leo, kitakwimu, ana uwezo wa
kutumia dola za kimarekani 1702, yaani wastani wa pesa ya milioni mbili laki
saba ishirini na tatu elfu na mia mbili 2,723,200/= kwa mwaka, ama wastani wa
shillingi elfu saba na mia nne na sitini 7,460/= kwa siku. Hii ni kama pato
jumla la Taifa litagawanywa kwa kila mmoja wetu. Utagundua kuwa kwa uchumi
tulionao hivi sasa kitakwimu yaani kila Mtanzania kuweka mfukoni mwake shillingi
7,460/= tamasha la nyama choma litakosa wateja. Kwahiyo, ni dhahiri kuwa matamasha
ya nyama choma ni kwaajili ya watu mahususi. Lakini inawezekana pia
kuwa wingi wa matamasha ya nyama choma na maisha ya mtindo huo ni kiashiria cha
kukua kwa tabaka la kati katika uchumi wa Tanzania.
Swali
hapa ni je uchumi wa Tanzania umekuwa kiasi cha kuwa na matamasha ya nyama choma mengi vile, ila hali uwanja wa mpira wa
taifa unaweza kujazwa na watu wenye bahasha za kaki? Je, uchumi wetu umekuwa
kiasi cha kutosheleza sherehe kila uchao wakati imani za kishirikina zimetujaa
mpaka shingoni? Mauji ya albino yanaendelea kila uchao. Je, hii ni jamii ya watu
tusioelimika? Uchumi mkubwa wa wala nyama choma hauwezi kumkata kiungo binadamu
mwenzake kwa kisingizio cha kupata mali. Uchumi uliokuwa na kukomaa watu wake
hufanya kazi halali kwa bidii zaidi, hulipa kodi, huheshimu tofauti zao na watu
wengine katika jamii, hutimiza wajibu wao iwapasavyo na kisha huenda kwenye
TAMASHA LA NYAMA CHOMA.