SUPA STAA WA MUZIKI |
Hivi
karibuni, huko jijini Dar es Salaam, kulikuwa na shangwe za tuzo kwa wasanii
bora wa music mwaka 2013 nchini Tanzania maarufu
kwa jina la “Kilimanjaro Tanzania Music Awards”. Naambiwa (sikuwepo ukumbini) kuwa sherehe hizo zilifana hasa. Lengo la
mjumuiko huo lilikuwa kuwatambua na kuwatuza wanamuziki wa kitanzania wa muziki
anuwai ndani ya Jamhuri ya Muungano na pia wa nje ya nchi; kulikuwa na kipengele
cha mwanamuziki bora Afrika Mashariki. Yalipangwa makundi mbalimbali ya aina kwa
aina kwa kadri ilivyoonekana inafaa kuwapanga wasanii hao. Ama kwa hakika mtenda kazi anastahili ujira wake!
Kimsingi
muziki nchini Tanzania kwa kiasi kikubwa unatazamwa kama ajira ama shughuli ya
vijana; hivyo ni sherehe za kutambua mchango wa vijana katika tasnia na sanaa
ya muziki Tanzania. Baadhi ya vipengele ilikuwa ni pamoja na “Hip hop”, Zuku,
Muziki laini, Taarabu na kadhalika. Kulikuwa na nafasi pia ya kuwatambua
waandaaji muziki nchini. Washindi walikuwa wengi; kwa uchache tu: Naseeb …. Ama
Diamond; ambaye alitia fora kwa kupata tuzo nyingi zaidi, wengine ni Faridi
Kubanda ama Fid Q, Judith Wambura ama Lady Jay D, MzeeYusufu, na wengine lukuki.
Tunawapongeza sana wote waliochangia kuboresha Tasnia ya Muziki Tanzania;
waliopata tuzo na hata wasiopata, kwani zawadi lazima ziwekwe mipaka ili kuleta
maana; kila msanii akipata tuzo basi tunakosa maana ya ushindani. Wanaitwa wengi ilihali wanachaguliwa
wachache!
Hata
hivyo, wito wangu kwa vijana wa sanaa mbalimbali Tanzania, hususani wale wa muziki, wajifunze kutawala ala za muziki; jifunzeni kupiga muziki wa vyombo. Muziki wa
vyombo una uhai mkubwa zaidi kuliko muziki wa maabara. Hiyo inathibitishwa na
kazi za siku nyingi za kina MbarakaMwishehe soma maisha ya Mwinshehe hapa, Marijani Rajabu, Sikinde bendi, OTTU bendi, Vijana Jazz, Mwenge Jazz
na bendi nyingine nyingi za kale (hata kama hawakupata pesa nyingi
kama vijana wa leo). Kazi zao zina
umri mkubwa lakini zina ubora kwa maana ya ujumbe na melodi nzuri kuliko kazi nyingi za hivi karibuni (zenye maisha mafupi mno). Ni kweli kabisa kila
kitabu na zama zake! Lakini kuna vitabu vingine vipo zama zote. Hata hivyo kwa mara
nyingine nawapongeza sana wanatasnia ya burudani nchini Tanzania kwa kutambua
vipaji na mchango wa vipaji hivyo kwa urithi wa nchi, nikisema hivyo nageukia
tasnia zingine nchini Tanzania.
Makala
hii/haya yanahusu hasa TUZO ZA WASOMI BORA TANZANIA. Nimesubiri
kusikia kutuzwa kwa wasomi bora nchini Tanzania kwa muda sasa; leo nimeamua
kutoa dukuduku langu. Nimekuwa nikijiuliza hivi nchini kuna wasomi wanaofanya
mambo yenye mchango wa maisha ya kila siku ya mtanzania na hivi wasomi hao
kustahili kupewa tuzo? Sijapata jibu na nadhani swali hili linahitaji hadhira
kubwa zaidi kuliko kichwa kimoja;kwani naamini penye
wengi haliharibiki jambo!
Mara
nyingine ninapokutana na kero kadhaa nchini huhisi pengine kweli hakuna wasomi
wanaostahili kutuzwa. Hebu fikiria mfano Tanzania kukutwa na uhaba wa chakula.
Foleni kubwa jijini Dar na kwingineko (japokuwa magari hayo hatutengenezi
wenyewe), rushwa katika nyanja
na huduma mbalimbali nchini, upungufu maadili katika jamii, kushuka viwango na
ubora wa elimu, kuongezeka ubinafsi, mauaji ya vikongwe, albino na madhira na
maovu mengine lukuki litania hiyo ni ndefu hasa…Wakati shida na maovu haya
yanalisonga taifa; tuna wasomi wengi wenye ujuzi husika kulingana na matatizo tajwa na hata yasiyosemwa hapa, tuna
rasilimali nyingi zinazohitajika kutatua matatizo tuliyonayo; pamoja na hayo
yote tunaendelea kudidimia, ama ndo kama wahenga walivyonena? Penye miti mingi hapana wajenzi? (enzi hizo nyumba nyingi/ zote zikijengwa kwa miti).
Nafahamu fika kuwa kuna wasomi wanaojituma na
wametoa mapendekezo kupata ufumbuzi wa matatizo yanayolisonga taifa. Hata hivyo
ushauri na ujumbe wao umepuuzwa. Poleni wale mliokutwa na kukatishwa tamaa
huko. Hata hivyo nadhani haitoshi kutoa ushauri ukikataliwa na wenye mamlaka kumfanya msomi makini akae kimya. Kukaa kimya ni mbaya mno; watu
wema wakikaa kimya uovu unaongezeka, na watu wema hapa tunamaanisha wasomi jadidi.
Msomi silaha yake kuu ni maandishi. Ndugu wasomi andikeni suluhu za matatizo
yanayolisonga taifa ili nchi iwe na kumbukumbu ya suluhu hizo pengine wenye mamlaka kesho watayatumia.
Suluhu
hizo zinaweza kuandikwa kwenye magazeti yanayosomwa na wananchi wengi, ama
likaanzishwa jarida mahususi kwaajili hiyo. Nani atafanya kazi hiyo? Pengine
hili ndo swali tunalojiuliza watu wengi. Sifahamu, nani alianzisha tuzo za
wanasanaa Tanzania... Nchini Tanzania hivi sasa kuna vyuo vikuu lukuki, hii ni dalili nzuri
ya kupata wasomi wengi. Chombo kinachosimamia ubora wa vyuo hivyo bila shaka
wanaendelea kufanya kazi yao vizuri; ili tupate wasomi wengi na bora. Chombo hicho kinaweza kuanzisha jarida
ambalo suluhu za matatizo nchini zinaweza kuandikwa humo; suluhu hizo zinaweza
kutoka vyuo vikuu vilivyopo nchini na hata nje ya nchi, zinaweza pia kutoka kwa
mtu yeyote ila tu zitasimamiwa na chombo chenye mamlaka juu ya vyuo vikuu.
Jukumu hili tunapendekeza liende kwa chombo hicho kwa kuwa kazi ya vyuo vikuu
pamoja na mambo mengine, kama alivyosema Mwalimu Julius K. Nyerere, ni kumsaidia binadamu aweze kuujenga ama
kuuboresha zaidi uwezo wake wa kufikiria ili aweze kuleta suluhu kwa matatizo
yanayomkabili binadamu (tafsiri isiyo rasmi na naweka maneno yangu zaidi). Kama msomi atatoa na ataandika suluhu ya kero
iyao/zinazowakabili binadamu wanaoishi
Tanzania, na kweli suluhu hiyo ikafanya kazi, basi msomi huyu atastahili
kutuzwa kama alivyotuzwa Diamond, Mzee Yusufu, Lady Jay D, Fid Q na wengine.
Tanzania si kisiwa cha binadamu, na nd’o maana haitakuwa nchi ya kwanza kutoa
zawadi kwa wanazuoni.
Tuzoza Nobel kwa magwiji wa Kemia, Fizia, Baiolojia ni maarufu duniani, kwa kuwa
tupo duniani huenda suluhu zetu kwa matatizo yetu zikasaidia matatizo ya
binadamu wengine hapa duniani. Naamini tuzo za wasomi nchini zitachochea
kuibuka kwa ari mpya ya usomi, watu wakazunguka na kutambiana, bila majivuno, kwa kuwa wamesoma
kitabu hiki na kitabu kile. Nilikuwa nikimsikia baba yangu anaongelea vitabu
vya tamthilia ya Kiswahili maarufu kipindi hicho, Kikosi cha Kisasi, Kamlete akibisha mlipue, Simu ya Kifo, n.k.
Nilimsikia baba yangu mzazi akitusimulia (watoto wake) hadithi za kusisimua toka kwenye Biblia Takatifu hadithi za kusisimua mfano simulizi ya kijiti kinachowaka bila kuteketea; bila shaka kuna wengine pia
wamesimuliwa hadithi toka Kuruhani Tukufu na hiyo ikawajengea hamu ya kusoma Kuruhani ama Biblia ili kupata kujifunza mwenyewe na kukutana na simulizi
nyingi zaidi mwenyewe. TUZO ZA WASOMI TANZANIA zitaamsha ari ya kupata "MASUPA STAA" wa
elimu pia! Kwani kwa jinsi mambo yalivyo hivi sasa supa staa ni ama mwanamuzi,
mwanafilamu, mrembo, mwingizaji na kadhalika, hukutani na masupa staa kwenye
fizikia, kemia, baiolojia, geografia, uchumi, falsafa n.k inatakiwa tukutane na
masupa staa wasomi pia! Wasalaaam!