Saturday, July 28, 2012

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU KUSUDIO LA WALIMU KUGOMA


SERIKALI kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi leo, Ijumaa, Julai 27, 2012 majira ya saa tisa alasiri, imepokea notisi ya saa arobaini na nane (48) ya kusudio la walimu wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kugoma kuanzia Jumatatu tarehe 30 Julai 2012 saa moja na nusu asubuhi.

Kabla ya notisi hii kutolewa, Serikali imekuwa ikifanya jitihada nyingi za kujadiliana na viongozi wa CWT kuhusu jinsi ya kuboresha maslahi ya walimu kwa nia ya kumaliza suala hili kwa maelewano kwa kutumia vyombo na ngazi mbali mbali za kisheria.

Kwa sasa, shauri hili liko Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na leo hii siku ya Ijumaa tarehe 27 Julai, 2012 majira ya saa sita mchana pande zote mbili zilifika Mahakamani, na Mahakama ikaamuru kwamba pande zote zikamilishe maelezo yao ifikapo siku ya Jumanne tarehe 31 Julai, 2012 saa sita mchana, ili kuiwezesha Mahakama kuendelea kusikiliza shauri hilo na hatimaye kutoa uamuzi.

Kwa hiyo, Mgomo huu siyo halali kwa sababu shauri hili bado liko Mahakamani.

Kwa msingi huo hatua ya CWT kutoa notisi ya kuanza kwa mgomo kabla ya kukamilika kwa shauri hili ni kukiuka taratibu halali za Kimahakama ambazo kila mmoja anawajibika kuziheshimu.

Serikali inapenda kuwafahamisha walimu wote kuwa kujihusisha na mgomo huu ni kwenda kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za kazi. Hivyo, walimu wanapaswa kupima madhara ya mgomo huu usiokuwa halali na Serikali inawataka walimu kupuuza mgomo huo na kutokujihusisha nao. Walimu wote wanatakiwa waendelee na kazi kama kawaida.



Peniel M. Lyimo
KAIMU KATIBU MKUU KIONGOZI
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
27 Julai, 2012

Tuesday, July 17, 2012

MKUTANO WA WAKUU AFRIKA WAMALIZIKA


Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika Jijini Addis Ababa.
Viogozi wa Afrika wakimaliza mkutano wa 19 wa kawaida wa Umoja wa bara hilo makao makuu ya Umoja huo jijini Addis Ababa. Pamoja na kumchangua kiongozi mpya mtendaji bi Nkosazana Dlamini-Zuma, ambaye anakuwa mwanamke wakwanza kuuongoza umoja huo, viongozi hao wamekubaliana pia kuangalia na kuifanyia kazi migogoro mikubwa miwili inayoendelea barani humo. Mgogoro ule wa kaskazini mwa Mali na ule wa Mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kiongozi mpya wa Umoja wa Afrika
bi Nkosazana Dlamini Zuma picha kwa hisani ya blogu wadau

Mama Nkosazana Dlamini Zuma akifurahia jambo. Picha na wadau