Hapa duniani kila jamii ina aina fulani ya burudani na hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu. Hata hivyo maisha ya nchi na watu wake ili yaweze kwenda mbele na nchi kupiga hatua za kimaendeleo ni muhimu ikawekeza kwa kiasi kikubwa zaidi katika elimu. Elimu kama tuambiawavyo nd'o ufunguo wa maisha. Elimu ndio inaweza kuwaweka sawa, kwa kiasi fulani, watoto wa tajiri na wamasikini. Ni kupitia hiyo elimu ndo mambo mengi iwe ni burudani; muziki, mpira, urembo, sana ya mavazi, iwe ni mawasiliano, sheria, tiba, taja tasnia zote; zinahitaji elimu ili kufanya vyema zaidi.
Nchini Tanzania, nchi yangu hii, kwa maoni yangu naona elimu hatuipatii fursa ya kutosha; ni kweli Serikali na wadau wengine wengi wanajitahidi kwa kiasi kikubwa kutoa huduma hiyo muhimu kwa jamii. Hata hivyo juhudi mara dufu bado yahitajika. Kuna njia na mbinu nyingi elimu inaweza kuiga toka kwenye kada nyingine hapa nchini.
Kwenye Muziki, filamu na sekta nyingine, wadau kadhaa wameanzisha tamasha maalumu kutafuta vijana wenye vipaji, na tamasha hizo zinafanywa kwa mbwembwe,ubunifu na bila shaka udhamini mkubwa na wenye gharama kubwa tu. Jambo hili ni jema sana kwani shughuli hizi zinachangia kuwakwamua vijana toka kwenye kukosa ajira na kuweza kupata kipato ambacho bila shughuli hizo wasingekipata. Hata hivyo wazo na wito wangu: kuibuke wadau wengine watakao fanya mashindano ya vijana kwenye hisabati, fizikia, baiolojia, jiografia, kiswahili... wazunguke mkoa mmoja hadi mwingine kupata wataalamu wa hisabati, na kadhalika. Kufanya hivyo kutatuwezesha kupata teknolojia na kujenga hamu ya kubobea na kujikita zaidi katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia.