Monday, December 28, 2015

MAISHA NI MALENGO




                                              Imepakuliwa hapa:https://www.youtube.com/watch?v=G23nC6i5jl8
Leo ni mwanzo wa juma jipya, mwezi mpya, mwanzo wa miezi mipya kumi na mbili ama maarufu zaidi mwaka mpya.

Mwanzoni mwa mwaka ni kipindi kizuri kufanya tathmini ya kile tulichokuwa tukikifanya kama hatukufanya hivyo mwishoni mwa mwaka. Ama yaweza kuwa fursa ya kuweka malengo mapya ama kuyapitia yaliyotangulia kwaajili ya muda mpya unaoanza mbele yetu.

Kufanya tathmini ama kujiwekea malengo katika maisha ni suala la msingi mno kama tunataka kuishi katika namna inayoeleweka na yenye tija na mchango katika dunia yetu. Lengo la maisha kwa kila binadamu awe anafahamu ama la ni kuwa na furaha maishani. Aristotle, mwanafalsafa wa kale anasema hivyo pia; ili mtu awe na furaha basi hana budi kujiwekea malengo. Malengo huwekwa na watu wa kila kada.

Mwalimu shuleni hujiwekea malengo yake, mwanafunzi, mwanasiasa, mwanamichezo, mwanasanaa, mwanauchumi, msomi, mwanazuoni, mwanasheria, mkufunzi, mfanyabiashara, mkulima, mchungaji kanisani, shehe msikitini, imamu sinagogini, na kadhalika…watu wote makini wa kada zote hujiwekea malengo maishani. Kutokuwa na malengo maishani ni mithili ya muuza duka bila daftari, ambapo twajua mali bila daftari hupotea bila habari. Maisha bila malengo hupotea bila taarifa.

Kujiwekea malengo ni utamaduni ambao inafaa watu wote tuwe nao. Kwa kusema hivyo nafahamu fika kuwa kuna ndugu wasio na mazoea ya kufanya hivyo; watu hao mara nyingine hufananishwa na bendera fuata upepo hufuata chochote kitakachokuwa mbele yao. Bila ubishi si utaratibu mzuri wa maisha. Kwa wasio na utaratibu huo ni wakati sawia kuuanzisha.

Dini nyingi hutueleza kuwa hapa duniani ni sehemu tu ya mpito - twapita tu na kwamba makao yetu halisi yapo kwa muumba wetu. Hivyo wakati tukiandika malengo yetu ya maisha ni vyema tukamshirikisha huyo muumbaji kwa kuwa sisi hatujui siku wala saa ya kuyahama makazi ya hapa duniani, japokuwa hatutakiwi kuogopa kifo.

Unapoandaa malengo fanya hivi:

Kwa wanandoa, ama watarajiwa, wawashirikishe wenzi wao. Malengo haya si yako peke yako. Kwa hiyo nafsi ya kwanza ni Mwenyezi Mungu na pili ni mwenzi wako wa maisha; mkeo, mumeo ama mchumba wako. Muombe(ni) Mungu ili awaangazie kufanya malengo ya kweli.

Hatua ya pili ni kuwa mkweli na hali yako halisi; weka malengo ambayo yana uhalisia wa maisha yako. Mfano haina maana kwako mwanafunzi wa Tanzania kuwa na lengo la kuwa rais wa Pakstani miaka mitano ijayo. Weka malengo ambayo kwa kiasi fulani una nafasi ya kuyatekeleza. Mfano kusoma kozi ya Kifaransa kwa undani mara baada ya kumaliza masomo yako mwezi wa Juni.

Weka malengo yenye kukujenga na yatakayohitaji juhudi zako kuyatimiza.

Usiogope kuwa na malengo mengi bora tu ni muhimu katika makuzi na utu wako, mwisho wa muda wa kuyatimiza utakapowadia utakuwa na wasaa wa kujitathmini na kujua wapi ulihitaji ama utahitaji juhudi zaidi. Mara nyingine tukiwa na malengo mengi na yenye kudai juhudi zetu zaidi ndipo ambapo huwa na mafanikio zaidi maishani.

Usiwe mtu wa kujihurumia; kuona kuwa malengo haya ni mengi na magumu mno siwezi kuyatimiza. Usishindwe kujaribu, jaribu kutenda na ukishindwa wakati ukitenda ni tofauti kabisa na ukishindwa kujaribu kufanya chochote.

Jiamini na usijilaumu. Fanya utakachoweza kwa juhudi zako na mambo yakienda kombo, bila shaka utapata fursa nyingine ya kutenda tena!



Kila la heri na Mungu akubariki!

Mandalu
01/01/2012