Saturday, November 15, 2014

MAISHA NI NINI? - What is Life? - Qu'est-ce que la vie?



Image by google

Hivi karibuni nimesikia kutoka radio Maria Tanzania kuwa wana mpango wa kuanzisha kipindi kipya juu ya maisha. Nimesikia wanauliza maisha ni nini? Swali hilo limenivutia kufanya tafakari. Kisha tafakari hiyo nikaona vyema kuwashirikisha watakaopata fursa ya kutembelea ukurasa huu.

Maisha ni nini? Ni swali linalohitaji kufikiria ili kulijibu na hakika mtu hawezi kutoa jibu la maana kama atafanya hivyo bila tafakari. Swali hili lahitaji maelezo ya utangulizi kabla ya kueleza maana ya maisha. Maisha yanahusu viumbe hai, swali letu linamlega hasa binadamu nami nitamuelezea binadamu bila kwenda kwenye falsafa ya ndani ya binadamu - philosophical anthropology, nitamuelezea binadamu kwa lugha nyepesi kabisa ili kila msomaji aelewe. Hivyo basi kwa kuanza na kiumbe huyu, binadamu ni kiumbe mwenye akili na utashi zaidi kuliko viumbe wengine. 

Kiumbe huyu huanza safari ya maisha baada ya mtu mume na mtu mke kushiriki tendo la ndoa na kutungwa mimba. Kisha kutungwa mimba kiumbe kipya kinaanza kuishi ndani ya mji wa uzazi wa mwanamke. Kuishi kwa kiumbe ndani ya mwanamke kunatupatia fursa ya kurudi kwenye swali letu la msingi la maisha, yaani maisha ni nini hasa?

Maisha ni jumla ya shughuli zote azifanyazo binadamu toka kutungwa mimba hadi pale moyo (kiungo chenye kazi ya kusukuma damu mwilini sehemu zote za mwili na hivyo kuurutubisha mwili kwani damu ndiyo njia kuu ya usafirishaji mwilini) utakapokoma kufanya kazi yake.

Katika maisha ya kila binadamu kuna shughuli zinazofanana kwa viumbe wote na kuna shughuli zinazotofautiana toka binadamu mmoja hadi mwingine. Kwa kawaidaa shughuli zote za kimaumbile za binadamu hufanana. Shughuli hizo ni pamoja na zile zifanyikazo ndani ya mwili wa binadamu; ndani ya mwili wa binadamu kuna mifumo zaidi ya kumi inayoshirikiana kati yao na pia ikipata ushirikiano na idara kadhaa mwilini. Baadhi ya mifumo iliyo mwilini kwa binadamu ni pamoja na mfumo wa usafirishaji ambapo moyo na mishipa mwilini husafirisha damu na vyakula sehemu zote za mwili. Upumuaji ni mfumo unaotumia idara za pua, mapafu na kadhalika kuwezesha upumuaji wa mwili. Utoaji taka mwilini huhusisha idara kadhaa na hata mifumo mingine kufanya kazi hiyo...

Pamoja na shughuli zinazofanana kwa binadamu wote kuna mahitaji ya lazima ambayo ni muhimu kwa viumbe wote hao bila kuzingatia nafasi zao kijamii, kiuchumi na kadhalika. Chakula, hewa safi, na hifadhi ya namna fulani ni kati ya mahitaji ya lazima kwa binadamu wote.

Ili aweze kuishi vyema na mwili wake ufanye kazi, binadamu analazimika kula; lazima apate chakula katika kipindi fulani ili mwili wake uendelee kupata mahitaji na virutubisho vinavyouwezesha mwili kuendelea kuishi, hali kadhalika kwa hewa safi. Ili mwili uendelee na kazi zake lazima upate hewa safi ili kubadilishana kwa hewa safi (Okisijeni O2)  na hewa chafu (Kaboni diokisaidi CO2) kuendelee kufanyika. Binadamu wote huhitaji hifadhi ya namna fulani; toka kwenye mavazi hadi nyumba ya kujihifadhi, ni ubora tu ndiyo hutofautiana toka mmoja hadi mwingine.

Tunapojiuliza maisha ni nini kuna jambo la lazima kuligusa pia. Nini lengo la maisha? LENGO KUU LA MAISHA NI KUTAFUTA FURAHA. Kwenye dini tunaambiwa lengo kuu la maisha ni kumtumikia Mungu kupitia huduma kwa binadamu wenzetu na mwisho turudi kwa Mungu. Kwahiyo, kwa mara nyingine, kwa binadamu wote lengo kuu la maisha ni kutafuta furaha. Binadamu wote shughuli zetu zote, ama kwa kujua ama kwa kutokufahamu, ni harakati za kutafuta furaha na hivyo basi maisha ni jumla ya shughuli zote binadamu anazozifanya katika harakati za kusaka furaha.

Binadamu wote bila kasoro, lengo la maisha yetu ni kusaka furaha. Tuliona mwanzoni kuwa binadamu ni kiumbe mwenye akili na utashi mkubwa kuliko viumbe wengine wote. Utashi na akili nyingi aliyonayo binadamu humpatia fursa ya kuitafuta furaha kwa namna ya kipekee kwa jinsi ya maumbile na muundo wake unaotokana na mpangilio wa 'genes' zake, ushawishi wa mazingira aliyolelewa na pia aina na ubora wa chakula alacho hasa toka utotoni. Ndiyo maana kuna wenye hutafuta furaha kwa kufanya kazi halali kwa bidii, wengine kwa kufanya kazi haramu kwa bidii (kazi haramu huleta furaha ya muda tu kwa kuwa huwadhuru binadamu wengine), wengine kwa namna yao kulingana na vipaji vyao na wengine kwa namna zao kwa namna namna.

Hivyo basi maisha ni jumla ya shughuli zote azifanyazo binadamu katika harakati za kusaka furaha katika kipindi chote ambapo moyo unafanya kazi ya kusukuma damu mwilini!

Martin Mandalu
Alice, Eastern Cape
15/11/2014

Wednesday, November 5, 2014

Thursday, October 16, 2014

Wasomi wahoji kwa nini Mwl Nyerere ahujumiwe? Ni katika Tuzo ya Nobeli, Ulaya watiliwa shaka

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
UTOAJI wa Tuzo maarufuna muhimu za Nobeli kwa watu mashuhuri na wenye mafanikio ya kipekee katika maendeleo na amani ya dunia umeanza kutiliwa shaka na baadhi ya wasomi barani Afrika, na hususan wanazuoni katika baadhi ya vyuo vikuu Kusini mwa Jangwa la Sahara, Raia Mwema, imebaini.
Mijadala ya chini chini imeanza kurindima miongoni mwa wanazuoni, wakihoji kulikoni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa kiungo katika ukomboni barani Afrika na hata kushiriki kuratibu harakati za vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, asipewe tuzo ya amani.
Wakati tayari tuzo hizo zimekwishatolewa kwa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, mwaka 2011, kwa kupigania haki za wanawake ili washiriki kujenga amani, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, mwaka 2001, Askofu Desmond Tutu na Nelson Mandela, hoja zimeanza kuibuka kwa nini si Mwalimu Nyerere?
Wasomi hao sasa wanakosoa tuzo hizo na kudai kwamba Mwalimu ananyimwa kwa sababu aliyapinga mataifa ya magharibi alipokuwa akiongoza harakati za kudai uhuru kusini mwa nchi za Afrika na akishiriki kuunganisha nchi hizo, sambamba na kutetea haki za binadamu, akiwa kiongozi aliyeishi kwa mfano mbele ya raia wake.
Wengi wanaamini Mwalimu ni kiongozi wa mfano katika kuthamini usawa wa binadamu jambo ambalo ndilo msingi wa amani ya dunia na kwa hiyo, alistahili kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobeli.
Tuzo hizo zilizoanzishwa na raia Norway, hutolewa na kutambulika kimataifa ili kuwapa heshima watu mashuhuri waliosaidia dunia katika nyanja mbalimbali za uchumi, amani, fasihi na masuala ya sayansi kama fizikia, kemia, hisabati na mengineyo.
Wahadhiri wakosoa
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), chuo ambacho Mwalimu alikianzisha na mara kwa mara kufika hapo kwa ajili ya mijadala na wanafunzi kuhusu uhuru na maendeleo ya Afrika na dunia kwa ujumla, Bashiru Alli, anaamini Mwalimu anastahili tuzo hiyo lakini ananyimwa kutokana na kuyaudhi mataifa ya magharibi wakati aliongoza harakati za kudai haki za binadamu na uhuru wa mataifa ya Afrika.
“Kuhusu maoni yangu juu ya namna baadhi media (vyombo vya habari), wanazuoni na watu mashuhuri wa nchi za magharibi wanavyopuuza mchango wa Mwalimu katika medani za mfumo wa siasa uchumi duniani na siasa za mahusiano ya kimataifa. Maoni yangu ni kwamba Mwalimu alikuwa mpinzani mkubwa wa mifumo yote kandamizi hususan mfumo dume, ukaburu na ubeberu.
“Upinzani wa Mwalimu dhidi ya mifumo hii ulimjengea heshima miongoni mwa wanyonge duniani kote, vile vile alikuwa na maadui wengi ingawa maadui wake hawakufanikiwa kuutoa uhai wake kama ilivyotokea kwa Patrice Lumumba wa Congo.
“Hata kama Mwalimu hakuwa mmoja wa washindi wa Nishani ya Amani ya Nobel kama vile Neslon Mandela, lakini mchango wake katika mapambano ya ukombozi hasa barani Afrika hauwezi kupuuzwa. Hata kama mchango huo wa Mwalimu hautangazwi sana na vyombo vingi vya habari vya magharibi au wasomi wengi wa nchi za Magharibi lakini maandishi yake, hotuba zake na msimamo wake dhidi ya dhuluma, unyonyaji na ukandamizji ni urithi usiokifani wa dunia. Sio rahisi urithi huu wa dunia hauwezi kupotea hivi hivi,” anasema Mhadhiri Bashiru Alli.
Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Stefano Moshi Memorial, Dk. Gaspar Mpehongwa, anasema vyombo habari vya nchi za magharibi havikuwahi kumpa nafasi Mwalimu Nyerere kwa sababu alikuwa “mwiba” kwa mataifa ya magharibi kutokana na hatua yake ya kukosoa kila mara, sera zao za kibepari na ukoloni mambo leo dhidi ya nchi masikini za dunia ya tatu.
Alisema kuwa sera za Mwalimu za Ujamaa na Kujitegemea ziliendana na zile za mataifa ya na nchi za kikomunisti za China na Urusi, hivyo mataifa ya Ulaya Magharibi yenye kufuata sera za kibepari na uchumi huria yalimtenga.
“Mwalimu alikuwa black listed na mataifa ya Ulaya Magharibi na Marekani kutokana na kuegemea zaidi katika siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na hata vyombo vyao vya habari havikuwahi kumsema vizuri,” alieleza Mhadhiri huyo.
Alisema Mwalimu Nyerere alipinga sera hizo hasa Shirika la Fedha la Dunia(IMF) na Benki ya Dunia (WB) taasisi ambazo zililenga kukandamiza nchi masikini hasa za dunia ya tatu, Tanzania miongoni.
“Kwa bahati nzuri pamoja na changamoto hiyo ya nchi za Ulaya Magharibi Mwalimu aliendelea kutambuliwa kama moja wa mashujaa wa Afrika ambao walipigania maslahi ya nchi zao mbele ya Jumuiya ya Kimataifa”
“Afrika iliheshimika sana wakati huo kutokana na kuwa na viongozi wenye mtazamo chanya katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa tofauti na viongozi wa sasa ambao huitikia na kucheza kila wimbo kutoka taasisi za Bretton Woods (mfumo wa kibiashara na kifedha wa mataifa makubwa),”aliongeza.
“Kwa mfano leo hata ukitaka uongozi wa umma vigezo vinavyotumika ni fedha badala ya uwezo wa mtu na tabia hii imesababisha kuwa na aina ya viongozi katika sekta za umma wanaojilimbikizia mali na madaraka,” alisema Mpehongwa.
“Na factor (kigezo) ya uongozi ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi angalia mfano nchi ndogo kama Uswisi imeendelea kutokana na uongozi thabiti lakini Tanzania yenye rasilimali nyingi kuliko Uswisi imeendelea kubaki kuwa moja ya nchi maskini na serikali yake inajiendesha kwa kutegemea hisani ya nchi za Ulaya,” alisema.
Kwa upande wake, Mwananahabari mkongwe na mwandishi wa vitabu nchini, ambaye baadhi ya vitabu alivyoandika ni pamoja na “Harakati za Nchi zilizo Mstari wa Mbele na Unyanyo wa Julius Nyerere,” Mkwabi Ng’wanakilala, anasema inawezekana kwa mfano, Nelson Mandela na Mwalimu Julius Nyerere walikuwa katika mizani tofauti ya kimtazamo na kwamba ndiyo sababu inayowafanya wapate heshima tofauti hasa kwa watu wa Magharibi.
Kwa upande wa Nelson Mandela, anasema, hali yake ilikuwa ngumu kwa sababu hakuwa anafukuza wakoloni isipokuwa alikuwa anapigania maslahi sawa ya Waafrika Kusini weusi dhidi ya makaburu, wakati kwa upande wa Nyerere kazi ilikuwa ni kuwafukuza wazungu waondoke Tanganyika.
“Mandela alionekana kama mtu ambaye hatakuwa na madhara makubwa kwa uwekezaji na maslahi ya wazungu na makaburu Afrika Kusini, walijua wanaweza kumpa anachotaka bila kupoteza chochote, na ndiyo hali inavyoonekana mpaka leo, Waafrika weusi bado wana hali ngumu kiuchumi kama ilivyokuwa wakati ubaguzi,” anaeleza.
Anafafanua kuwa pamoja na kwamba Mandela ni mpigania uhuru na ukombozi wa Afrika na amekaa jela miaka 27 kwa ajili ya kupigania ukombozi wa mtu mweusi, lakini ni kama nchi za Magharibi zilimtumia kimkakati kwa mantiki kwamba anaweza akawafanya wakaishi kwa amani kwa kuwa atakubalika na wote, weusi na makaburu.
“Hata ukiangalia release (kuachiwa toka jela) yake ni kama ilikuwa staged (ilipangwa kimkakati) ili kuweza kukidhi matakwa yao kutokana na shinikizo lilikuwapo wakati huo, na walipomwachia amekuwa Rais na haki za weusi kupiga kura na mambo mengine wamepata lakini kwa kweli bado kiuchumi hali haijabadilika sana ni kama ile ile tu” anasema.
Anasema kuwa huyu ni lazima asifiwe kwa kuwa ni mtu ambaye hana madhara makubwa sana kwao, kuendelea kumsifia ni kujihakikishia kuendelea kujiimarisha katika hali waliyo nayo tofauti na Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wa Mwalimu Nyerere anasema alikuwa anataka uhuru kamili katika nyanja zote, na alikuwa anawaambia ukweli bila kujali watamtafsiri vipi, na kwamba ilifikia kipindi wakaumuona kama mkomunisti lakini kimsingi hakuwa mkumnisti yeye alibaki kuwa mjamaa hata kama alikuwa na marafiki China na Cuba.
“Mwalimu kama ilivyokuwa kwa Nkrumah walitaka kuvunja vunja kabisa mizizi ya unyonyaji, wamchukia kwa sababu ya impact (matokeo) ya misimamo yake, he was very disturbing (alikuwa msumbufu sana) kwao, haikuwa rahisi kumfanyaia ujanja ujanja” alisema.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk. Charles Kitima, anasema kuwa Mwalimu Nyerere hawezi kuwa maarufu na kusifiwa na watu ambao aliongoza juhudi za kuwakatia mirija ya kunyonya rasilimali za Afrika.
Anasema Mwalimu Nyerere aliongoza juhudi za nchi zilizo mstari wa mbele kwa kuwaunganisha Waafrika kupinga aina zote za unyonyaji wa wakoloni na koloni mamboleo kitu ambacho hakikufurahiwa na wakubwa wengi wa Magharibi.
“Asingeweza kuwa maarufu kwa watu ambao aliwanyang’anya ulaji, kumbuka ni juhudi zake ndiyo ziliwaunganisha Waafrika nay eye akawa Mwenyekiti wan chi zilizo mstari wa mbele kuwapinga hawa,kwao mtu wa namna hi hawezi kuwa shujaa hata siku moja” alisema.
Anasema kwa Afrika kwa kiasi kikubwa inajitahidi kumkumbuka na kumuenzi ambapo sasa baadhi ya nchi kama Rwanda wana maadhimisho rasmi ya kumuenzi Mwalimu na Umoja wa Afrika umeanzisha Scholarship kwa heshima ya Mwalimu.
Mwalimu Nyerere African Union Sholarship Scheme imeanzishwa kwa ushirkiano na India kuwasomesha Wanafunzi wa Afrika katika vyuo mahiri Afrika, katika fani ya sayansi na teknolojia kwa ngazi za shahada, shahada za uzamili na uzamivu.
Chuo Kikuu cha Edinburgh ambako Mwalimu alichukua shahada yake ya uzamili mwaka 1949, kilianzisha The Julius Nyerere Master’s Scholarship mwaka 2009, kwa ajili ya wanafunzi wa Tanzania kusoma katika chuo hicho.
Dk. Kitima anasema kuwa sababu nyingine ambayo inafanya Mwalimu asipate heshima hiyo ni jinsi serikali inavyosimamia masuala ya msingi aliyoyaanzisha, kwamba udhaifu huo ndiyo unafanya hata watu wengine wasione mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Afrika huru.
Ameshauri ni muhimu serikali kurejesha somo la historia shuleni ili wanafunzi wajifunze historia ya nchi yao na kuwatambua mashujaa wao na hapo ndipo wanaweza kusimama kidete na kuitetea hadhi ya taifa lao.
Naye Mwanasheria Edward Lekaita alieleza kuwa mataifa ya magharibi pamoja na vyombo vya vya habari hayakuweza kutambua mchango wa Mwalimu kutokana na tabia yao ya kujali masuala yenye maslahi na mataifa yao.
“Vyombo vya habari vya magharibi siku zote ajenda yao kubwa ni kuandika habari zenye maslahi na mataifa yao hasa habari nyingi za mataifa masikini Afrika na yale ya Bara la Asia”
“Walikuwa double standard (ndimi mbili) katika masuala mengi ya msingi kwa mfano walitambua umuhimu wa Nelson Mandela baada ya kutoka gerezani na kuioongoza Afrika ya Kusini huru lakini kabla ya hapo walimtabua kama gaidi.”
Alisema Mwalimu na wenzake kama Nkwame Nkrumah wa Ghana, Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini, Lepold Senghor wa Senegal walijitahidi kuwaunganisha wananchi ili kuondoa ukoloni na ubaguzi katika nchi zao.
“Ni aibu mambo yanayofanyika sasa ni kinyume na dhamira iliyowasukama viongozi wetu wa zamani kupigani uhuru kutoka kwa wakoloni hata wakati mwingine kuhatarisha maisha yao”alisema.
Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Mbeya waliozungumza na mwandishi wetu wanamueleza Nyerere kama masikini jeuri, kwamba katika harakati zake za kupigania haki na utu kwa wanadamu wote hakujali mabavu ya mataifa makubwa wala uwezo wao mkubwa kifedha.
“Nyerere alikuwa masikini jeuri, alikataa kufanya biashara na Makaburu wa Afrika Kusini, hatua inayotugharimu hadi leo, lakini heshima ya msimamo wake tunavivunia hadi leo,” anasema mkazi wa jiji hilo, Newton Kyando.
Kyando anatoa mifano zaidi kuonyesha ujasiri wa Nyerere kupigania haki za wanyonge duniani, akikumbuka namna Mwalimu alivyokataa kuitambua serikali ya Mlowezi Ian Smith, alipojitangazia uhuru wa Zimbabwe, wakati huo ikijulikana kama Northern Rhodesia. Mbali na uamuzi huo, Nyerere akipata kuvunja uhusiano na Israel akipinga uonevu dhidi ya wananchi wa Palestine.
“Nyerere alivuka mipaka ya dini, alikuwa mkristo safi, tena mkatoliki, lakini alivunja uhusiano na Israel kupinga uonevu dhidi ya Wapalestina ambao wengi ni Waislamu, alichokizingatia yeye ni haki za wanyonge na utu wa mtu,” anasema Kyando kisha anaendelea akisema, “Pamoja na Chama cha ANC cha Afrika Kusini kilitangulia kuanzishwa, ilikuwa ni TANU iliyokijenga kufikia pale ilipofikia leo hadi kufanikiwa kupatikana kwa uhuru wa Afrika Kusini, na unapotaja TANU unamtaja Mwalimu Nyerere,” anasema Kyando.
Wananchi hao wanakumbuka pia mchango wa Mwalimu Nyerere kwenye medani ya kimataifa, ikiwamo kuwa msemaji wa “South South Commission,” pamoja na ukweli kwamba yalikuwamo mataifa makubwa na yenye nguvu za kiuchumi kama vile China na Indonesia.
“Alikuwa ni Mwalimu na Helmut Kohl wa Ujerumani Magharibi wakati huo, waliokuja na wazo la haki sawa ya kiuchumi kwa wote duniani, hivyo kunzaliwa kwa “International Economic Order.”
Marekani kinara Tuzo za Nobeli
Rekodi zinaonyesha kuwa Marekani ndiyo inayoongoza kwa kuwa na watu waliopata tuzo nyingi zaidi za Nobeli, wakifikia watu 334, ikifuatiwa na Uingereza tuzo 117, Ujerumani tuzo 102.
Katika Afrika, mbali ya Ellen Sirlef wa Liberia aliyechangia tuzo hiyo na mwenzake, Leymah Gbowee, wengine waliopewa tuzo hizo ni Wangari Maathai wa Kenya, Wole Soyinka wa Nigeria (katika fasihi mwaka 1986), Kofi Annan wa Ghana (katika amani-2001), Nelson Mandela na Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini. Misri pia imetwaa tuzo nne.



Tuesday, October 14, 2014

Nyerere kupata tuzo ya Nobel ya Amani Mwaka 2100

The Nobel Peace Prize Medal. Registered trademark of the Nobel Foundation. © ® The Nobel Foundation
Medali ya tuzo ya Nobel
Tuzo za Nobel ni maarufu zaidi katika orodha ya tuzo mbalimbali duniani. Tuzo hizo ambazo zilianza kutolewa mwaka 1901, ni matokeo ya wosia alioucha Mswidi Alfred Nobel (1833-1896) mwaka 1895. Alipofariki alikuwa na utajiri mkubwa ambao alipenda uwaendee watu waliotoa mchango katika ujenzi na uboreshaji wa maisha ya binadamu katika dunia yetu. 

Tuzo za Nobel zimegawanywa katika makundi sita; watu wenye kutoa mchango uliotukuka kwenye Fizikia, Kemia, Biolojia(Tiba), Riwaya (Uandishi), Uchumi na wale wenye kujishughulisha na masuala ya amani.Tuzo hizi hupewa mtu ama taasisi/ asasi yeyote iliyo/ aliyefanya kazi bora katika moja ya maeneo tajwa hapo juu lakini pia asiyepingana/isiyopingana walau wazi wazi na fikra za kibepari na asionekane tishio kwa mfumo huo wa maisha.

Tuzo hizi wamepokea watu toka takribani mabara yote duniani. Hapa naangazia, japo kwa ufupi tu, tuzo ya amani ya Nobel. Ukitazama orodha ya wapokea tuzo hiyo ya amani utaona wapo waume kwa wake, wenye kujishughulisha na kazi anuwai, watu wa imani tofauti, wazee kwa vijana. Na kijana mdogo zaidi kuliko wote kuwahi kupokea tuzo hiyo ni bi Malala Yousafzai (1997). Binti Yousafzai ameshinda tuzo hiyo pamoja na mwanaharakati mwingine kwa mchango wao katika kutetea/kupigania haki ya elimu kwa vijana.

Litania ya washindi wa tuzo hii ya amani ni ndefu na yenye majina makubwa. Kwa uchache utamkuta Martin Luther King JrMama Tereza wa Kalkuta, Elie Wiesel n.k. Afrika ina uwakilishi mkubwa ambapo nchi ya Afrika Kusini ikiwa imetoa watuzwa wengi zaidi barani humo. Kwa uchache tu kuna Albert Lithuli(1898-1967); mmoja wa marais wa ANC na Mwafrika wa kwanza kupata tuzo hiyo, Nelson Mandela (1918-2013), Desmond Tutu n.k. Afrika Mashariki yupo kwenye orodha hiyo hayati Wangari Maathai (1940-2011 ) mwanamke wa kwanza barani kupokea tuzo hiyo kwa mchango wake kwenye upandaji miti.

Julius Kambarage Nyerere (1922- 1999) kiongozi wa kwanza mzalendo wa Tanganyika huru na baadaye Tanzania, ni mmoja ya viongozi walioshiriki kujenga utu wa mtu duniani. Ushahidi wa mchango wake kutetea utu wa mwanadamu hususani binadamu mwafrika upo wa kutosha. Kwenye imani na kanuni za mwanaTANU, kanuni moja inasema binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja (sisemi kwa mpangilio kama ilivyo). Kiongozi huyu, kupitia sera ya chama na nchi yake, alijitoa kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa huru. Mchango wake ulikuwa mkubwa zaidi kwa nchi za kusini mwa bara hili la kitropiki, bara lenye kuandamwa na magonjwa ya kila namna ya asili na hata ya majaribio.

Sera za Tanganyika na baadaye Tanzania ziliruhusu wapigania uhuru wa nchi kadhaa za kusini mwa Afrika kuweka makazi yao na kufungua vituo vyao vya mafunzo nchini Tanzania. Mfano ni wapigania uhuru wa Afrika Kusini kule Morogoro, wapigania uhuru wa Msumbiji kule Mtwara na kadhalika. Zaidi wapigania uhuru na haki za watu kadhaa waliifanya Tanzania kuwa nyumbani kwao kwa namna moja ama nyingine ambapo walijipanga na kuweka mikakati ya ukombozi wa nchi zao. Unaweza kuwataja wachache tu hapa Laurent Kabila (1939-2001) wa Kongo-Kinshasa, John Garang (1945-2005) wa Sudan, Yoweri Museveni (1944) wa Uganda

Tanzania kwa miaka mingi imekuwa nyumbani kwa wakimbizi toka nchi mbalimbali zenye machafuko ya wenyewe kwa wenyewe.Tanzania na Zambia zinatajwa na mwandishi Crawford Young kwenye kitabu chake cha "The Postcolonial State in Africa: Fifty years of independence. 1960-2010" cha mwaka 2012, kuwa ni mataifa yenye makabila mengi lakini mataifa haya yameendelea kuwa ni nchi zenye amani na demokrasia. Nikiongelea AMANI ya Tanzania, pamoja na kwamba kuna tofauti lukuki kwa wananchi wake katika masuala ya imani, makabila na hivi karibuni itikadi tofauti za kisiasa, ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na viongozi wa mwanzo wa Tanganyika na baadaye Tanzania na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa miongoni mwao. Amani hiyo, pamoja na kuwa zawadi toka kwa Muumba, ilijengewa mazingira ya kustawi na viongozi hao wa mwanzo. Matumizi ya lugha moja - KISWAHILI, kwa taifa kubwa lililokuwa na vitaifa vingi (makabila) kabla na mara baada ya kupata uhuru, ni mbinu na mchango mkubwa uliostawisha na kuendelea kustawisha amani na mshikamano kwa Watanzania na pia kutoa hifadhi kwa binadamu wa mataifa mengine.

Mchango wa Tanzania kumfukuzilia mbali kiongozi wa mabavu wa zamani nchini Uganda Idi Amin Dada ilikuwa mchango mkubwa wa kazi ya amani kwa Tanzania, Uganda, Afrika na duniani kwa ujumla. 

Orodha hii inaweza kuwa ndefu zaidi, tukomee hapa kwa leo lakini tujiulize swali kwanini pamoja na mchango mkubwa amabao Tanzania imetoa katika masuala ya amani kwa ustawi wa binadamu nchi hii haijapewa zawadi hiyo na Nobel ya amani. Si kwamba bila tuzo hiyo maisha hayaendi la hasa, hata bila tuzo hiyo tunaendelea kuishi kwa mshikamano na udugu. Twauliza swali hilo kwa kuwa vigezo vinavyotumika kuwapima watu mbalimbali duniani inatakiwa ziwe kwenye mizani iliyo sawa.

Binadamu, kama ilivyo kwa maji huwa ana tabia ya kufuata mkondo katika maamuzi yake. Tanzania, kupitia Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wa zama zake, ilikuwa ikifuata mfumo wa ujamaa na kujitegemea. Mfumo huu si rafiki sana kwa nchi za magharibi na hivyo Norway na hususani wakfu wa Nobel hata kama wanakubaliana na mchango wa Mwalimu Julius Nyerere si rahisi kwao kutaka kujihusisha na nchi ama kiongozi mwenye kujitangaza hadharani kuwa ni mjamaa, mfumo wenye kupingwa kwa nguvu zote na Marekani, Uingereza na jumuiya za kibepari zenye "kuufadhili" wakfu huo.

Mwalimu Julius Nyerere, kwa mtazamo wangu kupitia mchango wake kutetea haki ya wanyonge kwa mfano wake wa kujinyima, anastahili kupata tuzo hiyo ya amani. Tatizo ni kizazi hiki za watoa tuzo hizo na "wafadhili wao" wana upofu kwenye masuala yenye kugusa ujamaa na upofu huo nadhani utakwisha 2099 karne moja baada ya kifo chake. Ila wahenga walinena vyema mno na ni vyema kufuata maelekezo yao: Tenda wema nenda zako...  

Martin Mandalu
Alice, 14/10/2014

Saturday, September 20, 2014

Baadhi ya Miamba Afrika



Mwanamuziki Mkongwe wa Kameruni
Emmanuel N'Djoke Dibango - maarufu zaidi  Manu Dibango (12 .12. 1933) ni mwanamuziki mkongwe wa Kameruni. Maarufu mno kwa vyombo vya kupuliza.

Mwanamuzi mashuhuri wa Kongo - Hayati Franco
Franco Luanzo Makiadi (6.6.1938 - 12.10.1989) alikuwa mwanamuziki mashuhuri mno nchi Kongo-Kinshasa, Afrika na duniani kwa ujumla.


Mwanamuziki Mashuhuri wa Nigeria Hayati Fela Kuti
Fela Anikulapo Kuti (15.10.1938 - 2.08.1997) Alikuwa mwanamuziki mashuhuri sana huko Nigeria. Aliweza kutumia vyombo anuwai vya muziki.

Mwanamuziki wa Zimbabwe Mashuhuri Oliver Mtukudzi
Oliver Mtukudzi (22.09.1952). Ni mmoja kati ya wanamuziki Maarufu nchini Zimbabwe na barani Afrika kwa ujumla.

Mwanamuziki wa zamani Tanzania Frank Humplick
Frank Humplick (03.04.1927- 25.08.2007) Mwanamuziki mTanzania ambaye hajulikani sana na kizazi cha wapenda muziki nchini Tanzania. Hapa historia yake inaelezewa na mtandao wa jamii forums


Mwanamuziki nguli wa Mali Salif Keita
Salif Keita (25.08.1949) Mwanamuziki mashuhuri kutoka Mali


Mwanamuziki wa Senegal
Youssou N'Dour (1.10.1959) ni mwanamuziki kutoka Senegali 

Mwanamuziki Maarufu nchini Tanzania hayati Marijani Rajabu
Marijabu Rajabu ( Kuzaliwa?  - kifo  23.03.1995) hapa anaelezewa vyema na mtandao wa  kwanzajamii

Mwanamuziki Mashuhuri nchini Tanzania hayati Mbaraka Mwaruka Mwinshehe
Mbaraka Mwaruka Mwinshehe (Kuz - Kifo  )



Saturday, August 30, 2014

NYAMA CHOMA NA UCHUMI WA TANZANIA



President John Magufuli
PICHA KWA HISANI YA BLOGU WAANDAA TAMASHA
Nyama choma ni chakula cha kitamaduni kwa baadhi ya jamii nyingi barani Afrika na hata duniani. Historia inaonyesha kuwa jamii ama makabila mengi hapo kale ziliishi/yaliishi kwa uwindaji wa wanyama pori. Hivyo nyama choma imekuwa ikiliwa toka enzi za kale barani ila katika baadhi ya jamii tu. Jamii nyingine ziliishi kwa kula mizizi na matunda pori. Wanahistoria wanaweza kutusaidia katika hili, kuibuka kwa shughuli kuu na maalumu kwa jamii mbalimbali zama za hivi karibuni ama nyuma kidogo, kulisababishwa na shughuli zale za uwindaji naukusanyaji mizizi na matunda pori.

Baadhi ya makabila yakawekeza nguvu na muda wao katika uwindaji na baadaye kuwa wafugaji, na mengine katika ukusanyaji mizizi na matunda pori na kisha kuwa wakulima.Na kulikuwa na wavuvi halikadhalika na leo waendelea pia. Kwa hivi basi wawindaji na baadaye wafugaji bila shaka hawa walikuja kuwa wala nyama ila hali wakusanya mizizi na matunda pori baadaye wakawa wakulima wa mazao mbali mbali. Mambo haya yalitokea zama za kale za mawe na chuma. Mawe na baadaye chuma kilikuwa chombo cha kuwindia wanyama na pia zana ya kutifua ardhi na kulimia mashamba. Hayo yalifanyika enzi hizo; hivi leo mambo haya yamebadilika. Siku hizi kila mtu anakula nyama na tena kuna matamasha ya nyama choma. Ila kabla ya matamasha ya nyama choma ya kisasa tuangalie nyama choma za sehemu chache nilizozifahamu miaka ya tisini.

Miaka hiyo nilikuwa mwanafunzi mkoani Iringa. Nilisafiri kwa treni ya kati toka Shinyanga, mara nyingine toka Mwanza hadi Dar es Salaam na mara nyingine nilishukia Dodoma. Toka Dar es Salaam nilipanda basi hadi Iringa, ama nilipanda treni ya Tazara mpaka Makambako na kisha kwenda mjini Mafinga, ambako palikuwa nyumbani kwangu kwa miaka mitano. Safari kwa treni ya Tazara ilikuwa ya kitalii na ya kuvutia, kwani nilipata fursa kuwaona wanyama wengi: swala, twiga, tembo n.k. Ama niliposhuka Dodoma nilikwenda Iringa kwa njia ya “Ny’ang’oro” barabara iliyokuwa na kona nyingi za kutisha na tena njia hiyo ilikuwa ni ya hatari, kwani mara nyingine magogo yaliwekwa njiani na majambazi na kisha abiria kunyang’anywa mali zao baaada ya basi kusimama. Namshukuru Mungu sikuwahi kukutana na dhahama hiyo. Njia hii pamoja na kadhia zake ilinifurahisha kwani nilikuwa na uhakika wa kula samaki watamu pale Mtera. Sijui mambo yanakwendaje huko siku hizi kwani sijafuatilia taarifa za huko na sijapita huko tena miaka mingi sasa.

Toka kanda ya ziwa kwa treni watu wengi tulifurahia ujuzi wa wenyeji wa Saranda wa kuandaa “nyama choma.” Kile kituo cha treni Saranda wengine hupaita “Kilimanjaro Hotel”. Kila zama na kitabu chake, enzi hizo Kilimanjaro Hotel ilikuwa ndiyo Hotel pekee? ya hadhi ya juu zaidi jijini Dar es Salaam na wageni wengi maarufu walifikia pale. Saranda, moja ya vituo vya treni ya kati kilichopo mkoani Singida, ni maarufu mno kwa uuzaji wa kuku wa kienyeji. Hivyo hapo tulikula nyama choma, sikumbuki bei ya kuku wale wasioisha, iwe masika iwe kiangazi bado utawapata. Bei ya kuku wale abiria wengi daraja la tatu tuliimudu, sifahamu abiria waliokuwa mabehewa ya daraja la kwanza na la pili kama wao pia walikula nyama choma ile. Kwa daraja la tatu, sina shaka, naelewa vyema kwani nilishuhudia abiria wengi wakila “nyama choma” ya Saranda. 

Kutoka Iringa Mjini kwenda Mafinga, unapita maeneo mengi kadhaa moja muhimu huwezi kulisahau ni Tanangozi; maarufu kwa nyama choma ya aina yake. Hapa sikupata nafasi ya kula nyama choma ila nafahamu huduma hiyo ilikuwepo. Mjini Dodoma, kule Mnadani kulikuwa na nyama choma za uhakika, sijui siku hizi, tena bei yake ilikuwa rafiki kwani wananchi wa kipato cha kawaida waliimudu. Naambiwa baadhi ya ndugu wabunge walifika kule kupata nyama choma pia. Najua kuna maeneo mengine mengi yaliyokuwa yakitoa huduma hii kwa wahitaji tena kwa bei maridhawa.

Ugumu wa maisha kipimo cha akili ama uvumbuzi mama wa maendeleo, hivi karibuni hususani jijini Dar es Salaam kumeibuka matamasha ya nyama choma. Kama tulivyoona hapo awali hili si jambo jipya na kuliona kama uvumbuzi. Upya wa nyama choma hii ni kule “kusasaishwa” ambapo kuna kuwa na eneo mahususi la kuendesha shughuli hiyo, ndani ya eneo ambamo kuna kuwa na mambo anuwai yakiendelea ikiwa ni pamoja na ajira kadhaa za muda; mama/baba lishe, biashara mbalimbali mfano uuzaji vinywaji, na bidhaa nyingine lukuki. Ili kuingia eneo hilo ni lazima kutoa kiingilio. Nimeona matangazo kiingilio mara nyingine huwa shilingi za Tanzania elfu saba 7,000/= hadi kumi elfu 10,000/=. Kiingilio hicho si tiketi ya kwenda kunufaika na kila huduma kwenye tamasha hilo, muingiaji atalazimika kuendelea kutoa pesa kwaajili ya huduma zingine. Kwa haraka haraka nyama choma hii si kama ile ya Mnadani ama Saranda, hii ni kwaajili ya watu wa tabaka maalumu.

Kwa hakika matamasha ya nyama choma ya namna hii yanawalenga watu wenye ahueni kubwa ya maisha. Ni jambo jema ama jambo baya si lengo la makala hii leo. Hapa najiuliza tu je, hizi ni dalili za kukuwa kwa uchumi wa taifa la Tanzania ambapo wananchi, baadhi yao, wanapata kipato cha matumizi ya ziada, matumizi yasiyo ya lazima? Sera ya maendeleo ya Taifa inalenga kuwa ifikiapo mwaka 2025 jamii ya Tanzania iwe na watu wenye uchumi wa kati. Hii maana yake Mtanzania mmoja anakuwa na uwezo wa kutumia kiasi cha dola za Marekani 5,960, yaani pesa ya Tanzania 9,536,000/= kwa mwaka walau kitakwimu, ama shilingi 26,126/= kwa siku. Kulingana na ripoti ya maendeleo ya binadamu ya shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa ya mwaka 2014 Mtanzania wa leo, kitakwimu, ana uwezo wa kutumia dola za kimarekani 1702, yaani wastani wa pesa ya milioni mbili laki saba ishirini na tatu elfu na mia mbili 2,723,200/= kwa mwaka, ama wastani wa shillingi elfu saba na mia nne na sitini 7,460/= kwa siku. Hii ni kama pato jumla la Taifa litagawanywa kwa kila mmoja wetu. Utagundua kuwa kwa uchumi tulionao hivi sasa kitakwimu yaani kila Mtanzania kuweka mfukoni mwake shillingi 7,460/= tamasha la nyama choma litakosa wateja. Kwahiyo, ni dhahiri kuwa matamasha ya nyama choma ni kwaajili ya watu mahususi. Lakini inawezekana pia kuwa wingi wa matamasha ya nyama choma na maisha ya mtindo huo ni kiashiria cha kukua kwa tabaka la kati katika uchumi wa Tanzania.

Swali hapa ni je uchumi wa Tanzania umekuwa kiasi cha kuwa na matamasha ya nyama choma mengi vile, ila hali uwanja wa mpira wa taifa unaweza kujazwa na watu wenye bahasha za kaki? Je, uchumi wetu umekuwa kiasi cha kutosheleza sherehe kila uchao wakati imani za kishirikina zimetujaa mpaka shingoni? Mauji ya albino yanaendelea kila uchao. Je, hii ni jamii ya watu tusioelimika? Uchumi mkubwa wa wala nyama choma hauwezi kumkata kiungo binadamu mwenzake kwa kisingizio cha kupata mali. Uchumi uliokuwa na kukomaa watu wake hufanya kazi halali kwa bidii zaidi, hulipa kodi, huheshimu tofauti zao na watu wengine katika jamii, hutimiza wajibu wao iwapasavyo na kisha huenda kwenye TAMASHA LA NYAMA CHOMA.


Tuesday, August 12, 2014

Friday, August 1, 2014

The Continent is not short of Heroes!

Dr Sheik Umar Khan
Dr. Sheik Umar Khan (1975-2014) - Photo by BBC

Doctor Sheik Umar Khan (1975-2014) is to Sierra Leone what Doctor Matthew Lukwiya (1957- 2000) is to Uganda

Dr. Matthew Lukwiya (1957-2000) Photo by Wikipedia
"It is our vocation to save life. It involves risk, but when we serve with love, that is when the risk does not matter so much. When we believe our mission is to save lives, we have got to do our work." Dr. Matthew Lukwiya


Dr. Lukwiya and Dr. Khan died while serving their people-treating patients of the EBOLA disease
This is indeed the spirit of "for my people and my country"- let political leaders in Africa take these two men as models and keep the social contract dear in their hearts as they serve their fellow citizens just like these two scientists.  

Saturday, July 26, 2014

SOKO LA KIBEPARI NA PANDE ZAKE MBILI

Wachumi na wapiga debe wa “mfumo wa uchumi wa soko wenye ubinadamu” ( The market friendly approach ) [Tafsiri hii ni yangu binafsi ] ambao lengo lao ni kuona uchumi unakuwa, kupitia mabadiliko katika taasisi, kupunguza rushwa, na kuhakikisha maisha ya watu kupitia huduma muhimu kama afya, elimu, uhakika wa chakula na kadhalika yanakuwa bora zaidi. Njia hii ni mbadala wa njia zingine zilizotangualia (sitaki kuingia katika nadharia hii ya Neo-liberalism kwa ndani).

Nadharia hii yenye kulenga kupunguza umasikini inazishauri nchi “masikini” kushirikisha Serikali na sekta ya umma kukuza uchumi na kupambana na umasikini. Kwa hiyo wadau wakubwa wa kujenga uchumi na kupunguza umasikini katika jamii ni wadau hao wawili; serikali na sekta binafsi. Nadharia hiyo inashauri uchumi kwa kiasi kikubwa uendeshwe na sekta binafsi ilhali serikali iandae miundo mbinu na mazingira yenye kuiwezesha sekta binafsi katika shughuli za kujenga uchumi; lakini serikali inapewa jukumu na fursa ya kuirekebisha sekta hiyo binafsi yenye jukumu kubwa la kuzalisha uchumi. Kwahivi serikali kazi yeke kuu ni kusisimua, kuibua fursa, kujenga mazingira na kurekebisha wazalishaji pale wanapoelekea kupotoka.

Nadharia hii ina mashabiki na pia wapinzani wa kutosha tu: lengo la makala hii hata hivyo si kuichambua nadharia hii bali kuongelea kwa ufupi tu mfumo wa biashara nchini Afrika Kusini. Naongea kupitia uzoefu wangu wa miezi michache nchini Afrika Kusini; nitaandika kwa uhuru kama nilivyokuwa nikifanya wakati wa kuandika insha shule ya msingi hadi kidato cha kwanza. Tuliandika kwa uhuru mkubwa na kutumia vizuri zaidi hisia, kumbukumbu na uzoefu wetu. Hatukubanwa na takwimu, ambazo kwenye makala za baada ya shule ya msingi tumefundishwa kuwa ni muhimu na mara nyingine lazima. Sasa tuangalie biashara nchini Afrika kusini.

Afrika Kusini ina mfumo wa kipepari; uchumi wake kwa kiasi kikubwa unaendeshwa na soko. Natazama hapa soko la mahitaji ya kila siku ya binadamu. Moja ya sifa ya nchi za kibepari ni kuunganisha bidhaa za mashambani katika mfumo wa soko wa bidhaa za viwandani. Kwahiyo masoko yanakuwa na bidhaa za mashambani na viwandani hali kadhalika. Hivyo katika soko moja utakuta viatu, nguo na kadhalika [n.k] (bidhaa za viwandani), nyanya, maboga, mahindi mabichi, n.k (bidhaa za mashambani). Najua masoko yetu pia yanafanya hivyo ila kuna tofauti kubwa iliyopo kati ya masoko yetu Tanzania na ya Afrika Kusini [A.K].

Masoko nchini Afrika Kusini ambayo mengi ni mtandao wa wamiliki kadhaa wenye nguvu ya uchumi yamewekwa katika namna ambayo hupatikana katika miji karibu yote. Masoko hayo makubwa kwa kawaida hupatikana katika miji midogo, mikubwa na majiji. Eneo moja huweza kuwa na makampuni kadhaa ya kibiashara, kulingana na ukubwa wa mji na uchumi wa eneo husika. Kwa Tanzania mfano sahihi ni ule wa soko la Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Soko la Mlimani City, Dar es Salaam
Kama ilivyo kwa Mlimani City, Dar es Salaam, masoko ya A.K hujumuisha makampuni kadhaa ndani yake. Muhimu na kubwa zaidi ni kuwa masomo hayo, kwa kawaida, yameunganishwa na mfumo wa kibenki ambapo wateja wana uhuru wa kuingia na pesa taslimu ama kadi za benki zenye pesa ndani yake. Mteja huchagua bidhaa anazotaka na kulipia kwa njia iliyo muafaka kwake; kwa pesa taslimu ama kwa kuchanja kadi yake ya benki.

Kwa kawaida Masoko hayo huwa na umeme wa uhakika muda wote; kwa kuwa kuna bidhaa zenye kuhitaji majokofu. Nyama, Samaki, vinywaji mbalimbali n.k. Lakini pia mfumo wa malipo huhitaji umeme muda wote. Zaidi masoko haya ni chanzo kikubwa cha ajira; watu wengi hupata fursa za kufanya kazi za aina mbalimbali. Unaweza kuorodhesha nafasi chache tu hapa: wauzaji (wapokea pesa), wapanga bidhaa, wakagua bidhaa, wasukuma mikokoteni, n.k

Masoko ya A.K yana sifa nyingine muhimu ya kuwa na wateja wenye kupenda kufanya manunuzi (nadhani hii ni kutokana na uimara wa uchumi na aina ya utamaduni); wananchi wengi wana uwezo kununua bidhaa nyingi na kulipia kila bidhaa walioichagua. Utakumbuka mfumo wa soko wa aina hii unauza karibu kila kitu kinachohitajika katika matumizi ya mwanadamu. Wakati sehemu nyingi nchini Tanzania uchumi wetu unaruhusu mtu kujipatia mahitaji yake toka vyanzo vingine mbali na soko; mfano kwenye bustani yake atakula machungwa, maembe n.k, toka shambani kwake atakula viazi, mihogo n.k. Nchni A.K bidhaa nyingi kwa watu wengi hupatikana kwenye masoko hayo tu.

Ni utamaduni wenye uzuri na ubaya wake pia; si lengo langu kukugusa mada hii kwa undani hivi leo, lakini inafaa kusema chochote juu yake. Mfumo huu wa soko una faida lukuki lakini pia mapungufu hayakosekani. Nitaelezea jambo moja tu kwa kila upande uzuri na udhaifu wake.

Mfumo huu wa soko, ni njia ya uhakika ya ukusanyaji kodi. Serikali kupitia mamlaka zake husika hukusanya kodi kwa uhakika kabisa. Kodi, twafahamu ni muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote duniani. Ni kupitia kodi ndio serikali inapata nguvu ya kuwapatia wananchi wake hudumu za msingi kama hospitali, shule, n.k

Mfumo huu wa soko, kwa maoni yangu, una shida kwenye bidhaa za vyakula. Wahitaji wa bidhaa kadhaa mara nyingine ni wengi kuliko uzalishaji wa asili unavyoweza kumudu mahitaji ya wateja hao. Ili kukidhi mahitaji hayo basi ni lazima kutafuta njia ya uzalishaji ambayo ni ya bandia, matumizi ya teknolojia yanaingia hapo. Si kila jambo linalotumia teknolojia ni jema. Chukua uzalishaji wa mayai kwa njia ya asili. Kwa kawaida kuku anapotaga yai basi kwa siku ni yai moja tu. Lakini kuna watu wanakula zaidi ya yai moja kwa siku. Hivyo basi ili kukidhi haja ya walaji lakini na ili kupata faida haraka ni lazima teknolojia iingie kati na kuzalisha mayai mengi kwa siku moja. Mfano huu unaweza kutumika kwa bidhaa nyingine za vyakula. Mfumo huu unalzimu bidhaa nyingi za vyakula kuzalishwa kwa teknolojia. Hivyo bidhaa nyingi za vyakula zinakosa virutubisho na viini asilia ambavyo sehemu nyingi nchini Tanzania bado tunaendelea kuvifurahia…

Mambo mengi ndivyo yalivyo, kama sarafu, yana pande mbili…

Baadhi ya makampuni ya kibiashara nchini Afrika Kusini, ambayo baadhi yake hupatikana pia Afrika Mashariki ni pamoja na  Picnpay, Spar,Checkers, Shoprite, Pep, mrprice, edgers, kfc, lewis, steers, jetmart


Sunday, July 13, 2014

UBIDHAISHAJI WA MAUMBILE YA BINADAMU: Toka Sarah Baartman mpaka Agnes “Masogange” Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Picha kwa hisani ya mtandao

Picha ya Sarah Baartman 

Picha hii imetolewa kaatika blogu hii






Tunaishi katika zama mpya. Zama za ubepari uliochukua sura ya uliberali mamboleo. Ipo tofauti kati ya ubepari halisi na uliberali-mamboleo. Ubepari halisi ulijikita katika kutengeneza faida kwa kuzalisha bidhaa viwandani. Uliberali mamboleo ni ubepari wa kikasino. Katika zama za uliberali-mamboleo uzalishaji bidhaa siyo tena msingi wa ubepari

Upepari wa kikasino ni ule wa kutengeneza faida na kulimbikiza mtaji bila kujihusisha katika uzalishaji-mali. Uzalishaji-mali hufanyika mashambani na viwandani. Katika ubepari wa kikasino na kiporaji, mtu hutengeneza pesa kwa biashara za udalali, ununuaji na uuzaji hisa, ukopeshaji, kamari, upaishaji wa bei za vitu, n.k.

Katika uliberali mamboleo, ambao ni awamu ya ubepari uliofilisika, kila kitu hugeuzwa bidhaa na kuuzwa au kununulika sokoni. Huduma za jamii (afya, elimu, makazi na maji) hugeuzwa bidhaa na kuuzwa sokoni kama itokeavyo kwa manukato, nguo au magari. Ubidhaishaji umevuka mipaka, kiasi kwamba hata viumbe vinabidhaishwa. Katika makala haya nitazungumzia ubidhaifishaji wa muoneko wa viungo vya binadamu, hususun akinamama ufanyikao katika mfumo wa uliberali mamboleo.

Agnes Masogange
Jina la Agnes Gerald “Masogange” sio geni katika masikio ya Watanzania. Ni mwanadada mrembo. Lakini warembo wapo wengi. Masogange ni maarufu. Akina dada warembo na maarufu wapo wengi pia. Lakini umaarufu wa Masogange ni tofauti. Umaarufu wake umepatikana kutokana na anavyoonekana katika video za wanamuziki, na sehemu ya mwili wake inayompatia umaarufu ni makalio yake.

Mara kadhaa amekwishahojiwa naye akajisifia kuwa anajisikia raha kuwa na makalio makubwa: “Hakuna sehemu ninayoipenda kama makalio, yamekaa vizuri, nayapenda, najidai kupitia sehemu hiyo niliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu,” alisema Agnes katika moja ya mahojiano yake yaliyochapishwa Machi 29, 2014 katika blogu ya Global Publishers.

Ukiingia katika mtandao utaona picha na video za Masogange. Nyingi ya hizo zinaonyesha “sehemu hiyo aliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu”. Ameenda mbali hata kuweka picha na video zinazoonyesha utupu wake. Huko mtandaoni kuna wanaomlaani. Lakini hawa ni wachache. Wengi, hasa vijana, wanamsifia.

Lakini ole wako ewe msomaji mwema. Kama ulidhani kuwa makala haya yamelenga kumlaani ama kumsifia Masogange basi umekosea. Makala haya hayamzungumzii Masongange kama mtu bali yanazungumzia mfumo katili wa uliberali mamboleo. Nitatumia pia mfano wa “Masogange wa Kenya” aitwaye Vera Sidika. Afrika nzima kuna “akina Verana Masogange” wanaoibuka na kujizolea umaarufu na pesa. Huko Ulaya na Marekani idadi ya mabinti wa aina hiyo imekithiri. Katika kona mbalimbali za dunia, wapo mabinti wanaotamani kuwa na umbile kama la Vera Sidika au Masogange ili wawe maarufu na kujizolea pesa. Je, ni nini chanzo cha wimbi hili la ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu? Nani mwenye maslahi katika wimbi hili? Makala haya yamelenga kujibu maswali hayo.

Kwa kuanzia, ningependa kujadili kisa cha Sarah Baartman, bintiwa kiafrikaaliyezaliwa nchini Afrika Kusini mwaka 1789. Alifariki mwaka 1815, jijini Paris, Ufaransa, akiwa na umri wa miaka 26. Je, alifikaje Paris?

Sarah alikuwa mtumwa huko Afrika Kusini. Mmiliki wake mwenye asili ya kikaburu aliamua kumuuza kwa daktari wa kiingereza aliyeitwa Alexander Dunlop. Dunlop alikuwa ameona ‘fursa za kiuchumi’ katika umbilela Sarah, na hasa makalio yake makubwa. Hivyo akamshawishi mmiliki wa Sarah amwuzie “bidhaa” hiyo adimu ili akaitumie kutengeneza pesa huko Ulaya.

Sarah alipelekwa katika nchi kadhaa za Ulaya, hasa Uingereza na Ufaransa. Huko alipelekwa katika kumbi za maonyesho akiwa uchi, na wazungu wakawa wanalipa viingilio kuja kushuhudia weusi wa ngozi yake na ukubwa wa makalio yake na sehemu zake za siri.

Ili kutengeneza pesa zaidi, mmiliki wa Sarah akawa akimuuza kwa wanaume wa kizungu waliotaka “kumvumbua” zaidi mwanadada huyowa Kiafrika. Sarah akafariki kwa ugonjwa wa zinaa. Hata baada ya kufariki viungo vya mwili wake vilikatwa na kuwekwa katika makumbusho huko Paris ili wazungu wakajionee. Sarah aliendelea kuwa bidhaa na kivutio cha utalii hata baada ya kufa.

Tofauti ya Sarah na “ma-modo” wa sasa
Je, kuna tofauti kati ya Sarah na“mamodo” wa sasa?
Sarah aliishi katika kipindi ambacho biashara ya utumwa ilikuwa imeshika hatamu. Waafrika waligeuzwa bidhaa, wakauzwa na kununuliwa sokoni, kama vile mtu anunuavyo nyanya, nguo au kuku. Wakapelekwa huko Amerika kuzalisha mashambani na migodini. Nguvu-jasho ya Waafrika hawa ndiyo iliyozijenga na kuzistawisha nchi za Ulaya na Marekani ambazo leo tunakwenda kuomba misaada ya hali na mali.

Kwa hiyo, kama ilivyokuwa kwa babu na bibi zetu wengine waliopelekwa utumwani, Sarah hakwenda Ulaya kwa hiari yake. Alilazimishwa. Alikuwa ni bidhaa.
Usipofanya uchambuzi wa kina, unaweza kusema kuwa “ma-modo” wetu wa leo wanaotumia maumbo yao kama vivutio hufanya hivyo kwa hiyari yao. Lakini ukweli ni kwamba kuna nguvu ya kimfumo inayowalazimisha kufanya hivyo wafanyavyo. Nitajadili.

Maumbile ya Sarah yalikuwa ni ya asili. Mwili wake ni ule aliojaaliwa na Muumba. Katika zama zetu, wapo mamodo wenye maumbile ya asili. Lakini wapo wengi pia ambao wamelazimika kubadili maumbile yao. Ukuzaji wa makalio na matiti, uchubuaji wa ngozi, na hata ubadilishaji wa jinsia yamekuwa ni mambo ya kawaida.

Kiini macho na nguvu ya soko
Ukiingia mtandaoni, utakuta kampuni kadhaa zikitangaza bidhaa za kukuza makalio na matiti. Kwa wanaume, zipo dawa za kunenepesha na kurefusha uume, kukuza misuli, n.k. Kampuni hizi za kibepari ndizo kiini hasa cha ubidhaishaji waviungo vya binadamu, na hasa makalio na matiti. Ili bidhaa zao zikubalike, kampuni hizi sharti zitengeneze soko za bidhaa zao.

Soko lenyewe hutengenezwa kwa kubadili mtazamo na fikra zawatu, na hasa vijana, juu ya dhana ya urembo, mapenzi na mahusiano ya kimwili. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na kampuni za utengenezaji wa filamu za ngono, kampuni za kurekodi video za muziki, wamiliki wa vilabu na makasino, magazeti na televisheni za udaku, hospitali za binafsi za upasuaji wa plastiki, kampuni za uzalishaji wa dawa hizi zimewezesha kukubalika kwamba makalio na matiti makubwa ni urembo, lakini pia ni hazina murua kwa shughuli za ujasiriamali.

Kwa hiyo, katika zama zetu hizi binti mrembo anasemekana kuwa ni yule aliye na makalio makubwa, matiti makubwa, na ngozi nyeupe. Ikitokea hukuzaliwa na vitu hivi basi usikonde: utavipata kwa kutumia dawa au kwa kufanyiwa upasuaji wa plastiki. Binti mwenye sifa hizi anaaminishwa kuwa ana “rasilimali”ambayo anaweza kuitumia kutengeneza pesa iwe ni kwa kujiuza sokoni ama kwa kuwa na mpenzi mwenye pesa.

Hivyo basi, wapo wanenepeshao viungo vyao ili kuwaridhisha wapenzi wao. Wapo wafanyao hivyo ili “kwenda na wakati”. Lakini wengi pia hufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya soko. Soko lenyewe sio lazima liwe la kujiuza kimwili. Ni soko la kuuza “makalio”, watu wakayaona iwe ni katika klabu za usiku, magazeti ya udaku au video za muziki, na mwenye nayo akatengeneza pesa.

Tarehe 10 Februari 2011, gazeti la MailOnline la nchini Uingereza liliripoti kifo cha Claudia Aderotimi, mwanafunzi wa nchini Uingereza, aliyefariki huko Marekani akiwa ameenda kufanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio. Claudia, ambaye alikuwa na ndoto ya kuwa mnenguaji katika video za wanamuziki wakubwa, aliwahi kukosa tenda kwa kutokuwa na makalio makubwa. Aliambiwa kuwa ili afanikiwe ni lazima awe na makalio yaliyobinuka kama ya mwanamuziki Beyonce. Hivyo, mfumo tulio nao unawatengenezea mabinti kiini-macho (illusion) cha “kuwa na umbo kama la Beyonce ili ufanikiwe”.

Hapa Afrika, wapo akina-dada wachache ambao kutokana na maumbile yao, yawe ya asili ama “yaliyokarabatiwa” kwa dawa au upasuaji, waliofanikiwa kujipatia pesa, Maisha yao ni ghali: toka nguo wavaazo, manukato wajifukizayo, magari waendeshayo na kumbi za starehe waingiazo. Wengi wao huenda kufanya “shopping” Dubai au Afrika Kusini.

Vera Sidika: “Mwili wangu ni dili”
Katika kipindi cha The Trendkirushwacho na kituo cha NTV nchini Kenya, Vera Sidika,ambaye amejizolea umaarufu nchini Kenya kutokana na umbile la makalio yake, alisema kuwa huenda kufanya “shopping” ya kati ya dola 10,000 hadi 50,000 (yaani kati ya Tshs. milioni 16 hadi milioni 80). Viatu alivyokuwa amevaa siku hiyo vinaghatimu Tshs. milioni 5 na laki 6, na nywele zake za bandia ni Tshs. milioni 3 na laki 7.

Ngozi ya Vera sio ya asili. Ilichubuliwa kitaalamuna akawa mweupe. Vera anajitapa kuwa ubadilishaji wa rangi ya ngozi yake ulitumia zaidi ya shilingi milioni 15 za Kenya (takribani shilingi milioni 300 za Tanzania). Vera anasisitiza kuwa tangu apate ngozi nyeupe, kwake imekuwa “baraka”. Anatengeneza pesa zaidi, na anaalikwa nchi mbalimbali kwenda kusherehesha vilabu vya usiku (club hosting).
Vera anasema kwamba ukimwona klabu ujue amekwenda kutengeneza pesa. Hufanyaje hasa? “Huwa nasimama pale, na kutabasamu, na kupiga picha na mashabiki,” alifafanua. “Mwili wangu ni biashara yangu na ninautumia kutengeneza pesa,” Veera alijitapa.

Nyuma ya Vera, zipo kampuni za kurekodi video za muziki, wanamuziki, magazeti, redio, vituo vya televisheni, vilabu vya usiku, kampuni za kuzalisha kemikali za kubadili rangi ya ngozi, hospitali za binafsi zifanyazo uchubuaji wa ngozi, kampuni za vipodozi na mavazi ya kisasa, hoteli za kifahari, n.k. Wote hawa humtumia Vera kutengeneza faida.

Lakini tusisahau watu wa msingi wamfanyao binti huyu ajivune: hawa ni wale anaowaita “my fans”, yaani mashabiki wake. Kila siku Vera huweka picha za nusu uchi, zionyeshazo makalio yake, katika mtandao ili kukonga nyoyo za mashabiki wake. Aendapo Klabu hujiachia na kupiga nao picha za “ajabu” ili waendelee kumshabikia. Mashabiki hawa pia tayari wamekwishatekwa na mfumo, nao wakaamini juu ya urembo utokanao na kuwa na umbo kama la Vera.

Mtandao wa Kibiashara
Zipo nchi nyingi, mathalani Venezuela na Ufaransa, ambako ukuzaji-makalio na matiti vimetia fora kiasi cha wananchi kuzipigia serikali zao kelele ili zidhibiti vitendo hivyo. Lakini hii ni kazi bure kama tusipoelewa kiini cha tatizo lenyewe.

Gazeti la mtandaoni liitwalo “The Revolution” linalomilikiwa na cha Chama cha Kikomunisti cha Marekani liliwahi kufanya uchambuzi wa biashara ya upachikaji wa matiti ya bandia kwa wanawake. Nchini Uingereza pekee kati ya wanawake 20,000 hadi 30,000 hukuza matiti kwa njia hiyo kila mwaka, na biashara hiyo huingiza pato la zaidi ya dola milioni 150 (takribani shilingi bilioni 240 za kitanzania) kwa mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa plastiki nchini Marekani, idadi ya watu wanaojihusisha na upasuaji wa plastiki iwe ni katika kukuza au kupunguza makalio, matiti, nyusi, nywele, kubadili sura au ngozi, imeongezeka kutoka watu milioni 7.5 mwaka 2000 na kufikia watu milioni 14 mwaka 2011.

Jarida la “The Revolution” linaripoti kuwa kampuni za utengenezaji kemikali za ukuzaji matiti hutumia kemikali bandia ili kutengeneza faida zaidi. Moja ya kampuni hizo ni Poly Implant Prothese (PIP) ya nchini Ufaransa. Kutokana na madhara makubwa ya kiafya yasababishwayo na kemikali za PIP, baadhi ya nchi zimejaribu kuzipiga marufuku bidhaa za kampuni hizo bila mafanikio.

Maslahi ya kibiashara hayaishii katika kampuni tu. Ubidhaishaji wa huduma za afya umezifanya hospitali nyingi za binafsi zijiingize katika kazi ya upasuaji wa plastiki ili kukuza au kupunguza viungo vya mwili. Wateja waliopata madhara ya kiafya kutokana na kemikali za kukuza matiti na makalio wamekataliwa na hospitali zilizowapa huduma hizo. Wamiliki wa hospitali hizo, kwa mujibu wa jarida la The Revolution, “wanadai kuwa hawapashwi kuwajibishwa kutokana na kununua bidhaa zilizokuwa sokoni.”

Ubepari: toka uzalishaji hadi ubidhaishaji
Pengine cha kufikirisha ni kauli ya Vera kuwa “mwili wangu ni biashara yangu na ninautumia kutengeneza pesa”. Suala la kujiuliza ni kuwa, je, tangu lini mwili wa binadamu uligeuka kuwa bidhaa, hata ukatumika kutengeneza pesa?

Katika kitabu chake cha Das Kapital(Capitalau Mtaji) kilichochapishwa mwaka 1867, Karl Marx aliubainisha ubepari kama mfumo unaojitambulisha kupitia bidhaa. Lakini bidhaa hizo ni zile zinazozalishwa na nguvu ya binadamu na kupelekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa. Cha kushangaza ni kuwa watu hushikwa na wazimu wa bidhaa, wakazipenda na kuzithamini, lakini wasione kiini ndani ya bidhaa hizo. Kiini hicho ni nguvu-kazi ya binadamu iliyotumika kuzitengeneza. Marx alifariki mwaka 1883, yapata miongo saba baada ya Sarah kufariki. Kipindi alichoishi Marx kilikuwa ni kipindi cha ubepari wa uzalishaji bidhaa, viwandani na mashambani.
Takribani karne moja na nusu baada ya kuchapishwa kwa Das Kapital, Prof. Issa Shivji, mmoja wa wanazuoni wa Kimaksi, ameandika kuhusu ubepari wa karne ya 21, ambao umechukua sura ya uliberali mamboleo. Mfumo huu hautegemei tena uzalishaji, bali ubidhaishaji wa kila kitu.

Vitu ambavyo kwa asili yake haviwezi kuuzwa, hugeuzwa bidhaa na kuuzwa sokoni. “Utengenezaji wa bidhaa-sesere na zisizo za asili hauna mipaka katika mfumo wa uliberali-mamboleo,” anaandika Shivji katika kitabu chake kiitwacho Accumulation in an Afriacan Periphery. “Mazingira, ikolojia, na viumbe vingine wa asili (wanyama na mimea), viini vya kibaiolojia (ute wa mimea na viini-tete vya binadamu) hugeuzwa kuwa bidhaa, hali ambayo hutokea pia katika hisia na raha zihusishazo mahusiano ya kimwili. Juu ya vitu na mahusiano halisi hutengenezwa vitu-pepe na mahusiano-pepe, ambavyo pia hubidhaishwa. Katika ulimwengu wa mahusiano utaona mambo kama mabinti wa mtandaoni, vyumba vya faragha, na ufanyaji-mapenzi katika mtandao” (tafsiri yangu).

Kwa hiyo, tujifunzacho hapa ni kuwa mtandao wa watumiao miili ya vijana, na hasa wa kike, kutengeneza pesa ni mpana: vituo vya televisheni huwaalika katika mahojiano na kueneza udaku juu yao na kwa kufanya hivyo hutengeneza pesa, magazeti ya udaku hutengeneza pesa kwa kuchapisha picha na stori za mabinti hao, kampuni za utengenezaji wa kemikali za ukuzaji makalio/matiti na uchubuaji ngozi nazo hutengeza pesa, hospitali zijihusishazo na uchubuaji ngozi na upasuaji wa ukuzaji makalio hutengeneza pesa, na vilabu vya usiku viwaalikao mabinti hao navyo hutengeneza pesa, n.k. Huu ni mtandao mkubwa wa kutengeneza pesa katika zama hizi za utumwa mamboleo.

Kiini cha mtandao huuni mfumo wa uliberali mamboleo, ambao ni aina ya ubepari uliofilisika na uliochukua sura ya kikatili ya ubidhaishaji wa kila kitu, yakiwemo maumbile ya binadamu! Mfumo huu hauwezi kuwekewa viraka kwa kuhubiri juu ya maadili kwa vijana. Ni ama tuubomoe, au tuuache uendelee kutubomoa kwa kugeuza hata miili yetu kuwa bidhaa. Kama wapigania uhuru wa bara la Afrika walipambana dhidi ya ukoloni, sisi wajukuu wao hatupashwi kusalimu amri. Hatuna chaguo mbadala, ni jukumu letu sote kupambana dhidi ya uliberalimamboleo
Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.