Monday, December 24, 2012

HERI YA NOELI NA MWAKA MPYA


Picha kwa hisani ya blogu wadau

Saa chache zijazo sherehe ya Noeli ama maarufu zaidi kama "krismas" itaanza kwa Misa, ibada na karamu mbalibali kusheherekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita.
Sherehe za siku kuu hii huwa ni kubwa pengine kuliko sherehe nyingine katika nchi zinazotumia kalenda ya Kigregory inayosoma mwaka huu kuwa ni 2012. Sherehe hizi huwa kubwa kwa sababu kadhaa; chache kati ya hizo ni sherehe ya kiimani kuzaliwa kwa mkombozi; yeye ambaye alikubali kujitoa kwa hiari ili kusaidia wengine, shughuli kubwa za kibiashara zafanyika wakati huu, na tatu inaungana na zingine ni mwisho wa mwaka.
Mwisho wa mwaka ni kipindi mwafaka kwa karibu binadamu wote; ni kipindi cha kufanya mahesabu, je, mambo yamekwenda kama tulivyotarajia katika shughuli zetu?, wapi tuboreshe, ama turekebishe? Wapi tumefanikiwa na tuna haja na haki ya kujipongeza? Tukifanya sherehe hizi tunawajibika kulinda afya na usalama wetu.
Kuwa na afya njema ni jukumu letu la kwanza kabisa. Kupitia afya njema ndo mengine yaliyo mengi ama karibu yote hufanyika. Hivyo wakati tukisheherekea tunalazimika kufanya sherehe zetu kwa kadri, tusifuje kila akiba tuliyonayo kwenye sherehe hii, tufurahie ili hali tukiwa na akili zetu timamu; wanywaji tufanye hivyo kwa kiasi sana. Wote twale; tule kwa kiasi tule kwa afya. Tunaosafiri; madereva wote waendeshe kwa umakini zaidi kuliko pengine vipindi vingine vya mwaka. Kamwe dereva usinywe kinywaji chenye kilevi na kuendesha. Tukifanikisha haya yote kwa hakika tutakuwa tunajipanga vyema zaidi kuuanza mwaka mwingine kwa mafanikio.

                                 Kila la heri ya Noel, Merry Christmas na Joyeux Noël

Tuesday, December 11, 2012

SACCOS suluhisho la Mitaji kwa Wasanii


Picha kwa hisani ya mtandao Mkurugenzi wa Basata ndugu Ghonche Materegho na Mbunifu mahiri wa sanaa ya mitindo ya mavazi nchini Tanzania ndugu Mustafa Hassanal  
Picha kwa hisani ya Tanzaniatoday 
Na Mwandishi wa BASATA

Wasanii nchini wametakiwa kutumia vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) ili kujiwekea akiba itakayowawezesha kukopa ili kuendeleza kazi zao za Sanaa.

Akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu iliyopita, Mwenyekiti wa SAA Saccos ambayo inamilikiwa na washereheshaji (Mc’s) na wachezeshaji muziki (Dj’s), Emmanuel Urembo, amesema saccos ni suluhisho la mitaji kwa kazi za wasanii ambao wengi wao wameshindwa kukamilisha kazi zao kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha.

Saccos zinaweza kuwasaidia kupata mitaji na kujikwamua kiuchumi kwa kupata mikopo yenye riba nafuu ili kuendeleza ubunifu walionao, kwa kuwa wasanii wamekuwa hawana sifa za kukopesheka na benki mbalimbali kutokana na kutokuwa na fedha na dhamana za zinazowezesha mkopaji kupewa mikopo, lakini kwa kupitia saccos zao wenyewe wanaweza kujikopesha na kujiendeleza zaidi.

Aidha Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa nchini, Ghonche Materegho, aliwasisitiza wasanii kuanza kujizoesha kujiwekea akiba. Aliwahimiza wasanii kujifunza kwa SAA ambao wameshaanza katika mfumo huu wenye kuleta maendeleo na tija katika sekta ya sanaa, “kuendelea kulia juu ya ukosefu wa mitaji ya kufanyia kazi zetu na miradi ya sanaa hakutusaidii kusonga mbele, bali tunapaswa kujikwamua wenyewe kwa kuanzisha vyama hivi vya kuweka na kukopa kwa maendeleo yetu wenyewe” alitilia mkazo zaidi.