Monday, October 31, 2011

KIBANGA AMPIGA MKOLONI

Na. Maisha na Mafanikio
Zamani za ukoloni, palitokea Mzungu mmoja. Mzungu huyo hakuwa mtu mwema. Alikuwa mkali na mkatili sana. Kwa ajili ya ukatili wake watu walimwita mkoloni. Wanancgi wote walimchukia sana popote pale alipokwenda.


Mzungu huyo alikuwa Bwana Shamba. Alikuwa na bakora iliyokuwa imetengenezwa kwa mkwaju. Kila alipokwenda kukagua mashamba, alikuwa na bakora hiyo mkononi. Alipendelea sana kuitwa "Bwana Mkubwa". Mkolono huyo alifurahia sana kupiga watu. Aliwapiga watu waliposhindwa kupalilia mashamba. Aliwapiga pamba yao ilipokuwa chafu. Aliwapa taabu sana.

Friday, October 28, 2011

Mtwara by Night

Mmoja wa mitaa ya mji wa Mtwara ukiwa ndani ya giza licha ya umeme wa uhakika mkoani humo- mipango miji wako wapi?

















Mkoa wa Mtwara ni moja kati ya mikoa michache nchini Tanzania isiyofahamu kadhia ya mgawo wa umeme. Mkoa haujaunganishwa kwenye mfumo mmoja wa taifa, hapa ni kwa faida ya wakazi wa Mtwara. Kwani hakuna maana kuwa chanzo cha umeme na usiupate umeme huo. Kwa Mtwara ni tofauti na maeneo yenye utajiri mkubwa ilihali watu wake hohehahe wa kutupwa.

Mkoani Mtwara kuna umeme utokanao na gesi asilia; gesi hii asilia inapatikana mkoni humu na hii inajidhihirisha kwa wakazi wa mkoani humo kwani hakuna mgao. Nafahamu kuwa hii ni hali ambayo wakazi wa mikoa mingi wangependa kuiishi. Na katika hali ya kawaida, ungetarajia kukutana na mitaa yenye kumulikwa vyema na taa nzuri za barabarani nyakati za usiku, lakini hali si hiyo. Nyakati za usiku mjini Mtwara kuna giza kubwa sawa sawa na mikoa yenye mgao wa nishati hiyo muhimu kwa maendeleo ya binadamu. Wazo kwa wahusika wakuu hususani wapanga maendeleo ya mji, wajipange na kuweka taa za barabarani katika mitaa ya mji huo wa kusini mwa nchi yetu ili kuupendezesha mji huo, kuongeza usalama wa mji na hivyo kuvutia wawekezaji wengi zaidi mjini humo.

Elimu kwa Maendeleo

Wanafunzi wa Stella Maris Mtwara University Collegge wakijisomea katika maktaba mpya ya chuo hicho.

Tuesday, October 18, 2011

WASANII WATOA ELIMU

Msanii wa Kundi la Orijino Komedi, Lucas Mhavile ‘Joti’ akisisitza jambo wakati akizungumzia Changamoto anazokumbana nazo kwenye Sanaa ya Vichekesho anayoifanya.


 
 
Picha na maelezo kwa hisani ya BASATA

BASATA NA HAKI ZA WASANII

Meneja Mzalishaji wa Kundi la Vichekesho la Orijino Komedi, Sekion David ‘Seki’ (aliyesimama) akiongea na wadau wa Jukwaa la Sanaa wiki kwenye Ukumbi wa BASATA.Wengine kutoka kulia ni Kaimu Mratibu wa Jukwaa hilo, Aristide Kwizela, Msanii Lucas Mhavile ‘Joti’ na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari, BASATA Godfrey Mungereza.

Picha zote na maelezo kwa hisani ya mwandishi wa BASATA

BASATA YAWATAKA WASANII KUJITAMBUA

Na Mwandishi  BASATA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kujitambua kwa kuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu katika kazi zao na kutambua thamani yao.

Akizungumza wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika makao makuu ya BASATA, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari, Godfrey Mungereza alisema kuwa, kujitambua kwa msanii ni mwanzo wa kuipa kazi yake thamani kubwa kuliko ilivyo sasa ambapo wasanii wamekuwa wakikubali kulipwa malipo kidogo.

“Sanaa ni kazi, sanaa inalipa, ni lazima wasanii wawe na mipango ya muda mfupi na mrefu. Muhimu ni kwa wasanii kutambua thamani yao na kazi wanazozifanya. Ifike mahali wasanii watambue thamani yao ni nini” alieleza Mungereza...

Friday, October 14, 2011

Julius Kambarage NYERERE (1922-1999)







Huko Tanzania, Oktoba 14 ya kila mwaka imetangazwa kuwa siku mahususi ya kumkumbuka na kumuenzi Julius Kambarage Nyerere, maarufu zaidi, Mwalimu Nyerere, ni siku aliyofariki huko Uingereza mwaka 1999. Rais wa kwanza wa nchi hiyo, MwanaAfrika na mjengadunia halisi; mpigania uhuru wa nchi nyingi barani humo, mwanafalsafa, mwandishi, mzalendo, mcha Mungu na binadamu mwadilifu.

Mwalimu ni mmoja kati ya viongozi wachache wa kiafrika aliyekuwa kwenye mamlaka kwa muda mrefu. Alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Tanganyika mara tu baada ya kupata uhuru 1961  (1962 -1985) bila kujilimbikizia mali kama wafanyavyo viongozi wengi barani humo, mwalimu hakuwa mbinafsi. Alijitahidi kuishi vyema na kufuata misingi ya fikra za ujamaa na kujitegemea alizoziasisi.




Mwalimu pamoja na wenzake aliasisi Azimio la Arusha ambalo lilitoa maelekezo ya kuliongoza taifa ikiwa ni pamoja na maadili ya viongozi. Hii ilisaidia kuongoza nchi kwa uadilifu na ubadhilifu ulidhibitiwa kwa umakini, “Awamu ya kwanza rushwa ilikuwepo, lakini mtoa na mpokea rushwa wote walitiwa msukosuko mkubwa,… aliyebainika kupokea rushwa alicharazwa viboko 24, kumi na viwili kabla ya kwenda gerezani na kumi na viwili akimaliza kifungo chake ili akamwonyeshe mke wake…”

Julius Nyerere alikuwa na fikra binafsi ambazo aliziasisi, moja ya fikra hizo ni ile ya Ujamaa na kujitegemea. Katika nadharia hii Mwalimu alilenga kujenga taifa lenye uwezo wa kujipatia mahitaji yake lenyewe bila kutegemea sana mataifa ya ng’ambo. Mwalimu alijaribu kusimamia nadharia hiyo kwa mfano hata kama haikufanikiwa kama ambavyo angependa.

Zaidi Mwalimu aliwaunganisha watanzania wenye makabila zaidi ya miamoja na ishirini; wakati Tanganyika ikipata uhuru, kulikuwa na vijitaifa vingi, hivyo kazi aliyoifanya Mwalimu na viongozi wenzake ilikuwa ni kuunganisha mataifa hayo madogo madogo kuwa taifa moja kubwa. Kazi hiyo nzuri ilisaidia kuliepusha taifa hili la Tanganyika, na kisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar 26. 04. 1964, Tanzania, toka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe ambazo zimesambaa kote barani Afrika.

J.K Nyerere aliasisi mbio za Mwenge kwa tukio lenye hisia, kumbukumbu, na ujumbe mzuri hasa. Mwenge huo wa uhuru ulisimikwa kileleni mwa mlima mrefu kuliko yote barani Afrika; Kilimanjaro. Ni kapteni Alex Nyirenda wa jeshi la wananchi wa Tanganyika ndiye aliyefanya kazi hiyo nzuri. Akihutubia mjumuiko wa Umoja wa mataifa Mwalimu Nyerere alisema sisi tumeamua kuuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale walipokata tama, heshima palipojaa dharau (si maneno halisi)…………Ni dhahiri kuwa makala hii ni fupi mno kumuelezea mmoja wa waasisi wa taifa tukufu la Tanzania. Hata hivyo jambo la msingi ni je, tunamuenzi  kwa kiasi gani Mwalimu Julius Nyerere?

Miaka kadhaa baada ya kifo cha Mwalimu, Tanzania inaendelea kumuenzi mzee huyu aliyefanya mambo mengi makubwa kwa taifa hili la Afrika Mashariki, lenye utajiri mkubwa japokuwa utajiri wake hauwafikii wote kwa usawa. Taifa linaendelea kumuenzi sana Mwalimu kwa sifa na sherehe zenye mbwembwe nyingi kote nchini. Lakini hatumuenzi Mwalimu kwa mambo ambayo yeye mwenyewe aliyataja kama muhimu kufikia maendeleo ya kweli ya watu. Kwani lengo kuu la kuongoza nchi ni kuleta maendeleo kwa wananchi; mwalimu alisema ili tuendelee tunahitaji mambo manne;

1. Watu,

2. Ardhi,

3. Siasa safi na

4. Uongozi bora

Ili nchi zetu ziweze kuendelea tunawahitaji watu wenye elimu nzuri, afya njema, chakula cha kutosha na mahitaji yao muhimu ya kila siku ili kushiriki katika ujenzi wa taifa lao, jamii ya wanadamu na dunia kwa ujumla wake. Lakini hivi leo watu wengi wa nchi hiyo bado hawana huduma za lazima kufikia wanapotaka kufika.
















Ardhi, ni chanzo cha vyakula vingi anavyotumia binadamu na ni sehemu ambapo shughuli za kijamii na kimaendeleo za binadamu hufanyikia. Hii leo hiyo yenye utajiri, rutuba na mengine muhimu wanapatiwa wananchi wachache wenye pesa nyingi na wageni wenye mapesa na ushawishi mkubwa.

Siasa safi na uongozi bora ni tunu muhimu na za lazima kwa maendeleo ya watu…tunu hizo zimepiga hatua kubwa kwa malengo nia ile ile ya kuleta maendeleo kwa watanzania. Hata hivyo bado kuna mapungufu katika nyanja hiyo ya siasa safi na uongozi bora; kwa hivi kuna haja ya kuendelea kufanya marekebisho kwenye suala hili la uongozi. Hivi leo huko Tanzania, siasa inaonekana kama ni ajira yenye kuleta kipato kikubwa kwa haraka, matokeo yake watu wengi wenye kutaka utajiri wa haraka haraka, ikiwa ni wasomi, wafanyabiashara, wakulima hukimbilia siasa hata kama hawana wito huo. Viongozi wengi hivi leo hawana maadili sahihi ya uongozi, wameingia siasa kwa malengo mbalimbali; wengine wameingia kulinda biashara zao, wengine kujiongezea heshima tu na kulinda malengo yao binafsi. Azimio la Arusha lilitoa mwongozo namna gani kiongozi aongoze watu wake. Siasa safi na uongozi bora ni muhimu mno kwa maendeleo ya kweli ya WATANZANIA WOTE! Hivyo lazima kuwe na namna flani ya Azimio la Kujenga maadili ya viongozi nchini!

Picha kwa hisani ya tovuti ya nyerere.info

Thursday, October 13, 2011

MUDA WA KUSAKA FIKRA ZAIDI


Mtaalamu wa burudani za mafunzo akiburudisha na kuelimisha wageni waalikwa siku ya hiyo ya ufunguzi wa mwaka wa masomo.

         MJ wa Mtwara hakukosa kwenye orodha ya waelimisha jamii wa siku                                      
   



                                                                                                                                                                
Burudani hii murua ilitufunza namna ya kupokea tofauti na vipaji vyetu na kuendelea kuishi kati jumuiya moja kwa upendo na mafanikio. Burudani nyingi zilitolewa na kundi hili maarufu la SAUT TRAVELLING GROUP (STG)




MUDA WA KUSAKA FIKRA ZAIDI

Picha kwa hisani ya blogu ya mdau Muliriye

Jumatatu ya 10.10.2011 ilitumika kufungua mwaka wa masomo Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Agostino – Mtwara. Masomo ni njia ya kumwezesha mtu kugundua vipawa vyake na kuvitumia kwa malengo yale yale ya kuweza kuitawala dunia na vilivyomo humo ilikuboresha maisha ya jamii ya wanadamu.

Elimu ya Chuo Kikuu, kwa kutumia maneno ya Mwalimu Nyerere, ni elimu hasa yenye malengo ya kumfunza mtu kuwa na fikra bayana, kuwa na uhuru wa fikra, kuchanganua, na kutatua matatizo kwa kiwango cha juu kabisa, haya ni mawazo ya Mwalimu kwa maneno yangu. Kwa hivi basi elimu ya Chuo Kikuu imjenge kijana kuwa na fikra binafsi na tena zenye nia ya kuiendeleza jamii ya wanadamu.

Kumbe elimu hiyo ya juu haina lengo la kumfanya mwanafunzi akariri, lengo kuu ni kumfanya awe na uwezo wa kujenga fikra binafsi, zenye kuweza kuijenga jamii na awe na uwezo wa kuyatetea na kuyasimamia mawazo yake, kwa kufanya hivyo ndio tunaweza kupata wagunduzi (wavumbuzi), wanasayansi na watu waliotayari kuijenga dunia.

Huko SAUT Mtwara, shughuli za kuanza mwaka wa kuendeleza ujenzi wa fikra mpya ulianza kwa kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu na kisha kufuatiwa na shughuli mbalimbali za kijamii.



Baadhi ya wageni mashuhuri wakielekea eneo la tukio


Wageni Maarufu na mashuhuri mno walikuwepo, hapa Profesa kijana akiwa na wadau wengine wakielekea eneo la tukio katika viwanja mahususi kwa tukio la siku

Hapo chini wadau wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza shughuli yenyewe

Tuesday, October 11, 2011

Falsafa - kiwanda cha fikra!















Muhula wa mwaka mpya wa masomo wa vyuo vikuu nchini Tanzania kwa kawaida huwa ni miezi ya Septemba na Oktoba. Hii ni kwa sababu wanaojiunga na vyuo humaliza masomo yao ya elimu ya sekondari mwezi Februari, na kisha matokeo yao kutoka hufuata utaratibu maalumu kuomba nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu nchini ambavyo idadi yake yazidi kuongezeka. Pamoja na vyuo vikuu nchini kuongezeka, bado vyuo hivyo haviwezi kuchukua idadi ya wanafunzi wote nchini wenye sifa za kujiunga na elimu hiyo ya kiwango cha juu. Vyuo kadhaa binafsi vinasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo hili kwa kuanzisha matawi ya vyuo hivyo sehemu mbali mbali nchini. Kwa kiasi kikubwa hii inasaidia sana kuwapatia wanafunzi wengi fursa za kuendelea na masomo katika elimu ya juu.

Katika makala hii naangazia japo kwa ufupi tu tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino kilichopo mjini Mtwara. Chuo hiki ambacho kilianza kama kituo cha masomo cha "Saint Augustine University of Tanzania" (SAUT) kimepiga hatua sasa na kuwa "University College" hatua ya juu kuelekea kuwa na mamlaka binafsi. Chuo hiki kinafundisha programu ambazo hakuna sehemu nyingine hapa nchini. Moja ya programu hizo ni ile ya falsafa na elimu. Falsafa ni somo geni kwa wanafunzi wengi wa nchi zinazotumia kiingereza kama moja ya lugha zake rasmi, hususani za Afrika Mashariki, kwa nchi zinazotumia kifaransa, somo hili hufunzwa hata katika elimu ya sekondari.

Falsafa ni chimbuko kuu la mawazo; humjengea mtu nafasi ya kuwa na fikra binafsi ambazo anaweza kuzisimamia na kuzielezea bayana. Kwa mtazamo wangu binafsi, nchi zetu za Afrika, kupitia viongozi wake, zina haja ya kubuni mikakati na fikra binafsi za kiafrika ili kutatua matatizo yanayotusibu hapa barani. Falsafa inawapatia wanafunzi fursa ya kukutana na mawazo ya watu mbalimbali toka bara ulaya, bara Asia, Marekani, na pia barani Afrika; inafanya hivyo kwa lengo la kumpatia kijana fursa ya kujenga fikra zake binafsi. Wakati kijana anapata fursa ya kujenga mawazo binafsi, anafaidika pia na kwa kujifunza masuala ya maadili, jambo ambalo lazitatiza nchini nyingi barani Afrika, hususani tatizo la rushwa.

Wakati vijana wanaanza safari yao ya kujenga na kunoa bongo zao ni vyema wakajipanga kwa kusoma mambo ambayo yatainufaisha jamii nzima ya wanadamu na hivyo kuwa kweli wajenzi wa dunia; kila mmoja wetu ana nafasi ya kuwa mjenzi wa dunia hii kwa namna yake mwenyewe kulingana na vipaji alivyojaaliwa; akiongeza na kipawa cha falsafa mambo yatakuwa mazuri zaidi.


Picha kwa hisani ya google

Wednesday, October 5, 2011

Siku ya Walimu duniani












Picha zote katika makala hii ni kwa hisani ya google
Oktoba, 5 ni siku ya walimu duniani. Siku hii ambayo kimataifa imeanza kusheherekewa 1994, ina malengo hasa ya kuikumbusha jamii ya wanadamu kuwa walimu ni muhimu kwa maendeleo ya jamii zetu na kwa dunia kwa ujumla. Ni fursa nzuri kuwakumbuka walimu ambao wamechangia sisi wote kuwa hapa tulipo.

Walimu ndio chanzo cha mafanikio katika kila sekta, kila mtaalamu, katika hali ya kawaida, huhitaji mwalimu wa aina yoyote ile ili kujifunza, kuboresha alichonacho ama kujifunza zaidi na kuwa imara zaidi. Kwa hivi hata wale wenye vipawa maalumu bado ni lazima wapate maongozo ya namna flani. Kwahiyo kimantiki, mwalimu inatakiwa awe ni mtu mwenye uwezo mkubwa sana kiakili, uwezo mkubwa wa kuwafundisha wengine na si kinyume chake. Na zaidi tunahitaji walimu wengi ili kutoa ujuzi kwa watu wengi zaidi. Vigezo hivi muhimu vyatulazimisha watanzania kutafakari kwa kina mahitaji yetu ya walimu na ubora wao.















Kwa Tanzania, tunaungana na jamii ya kimataifa kusheherekea siku hii adhimu kwa jamii ya wanadamu. Ni muhimu kwa kuwa kila mmoja wetu ana mwalimu ama walimu wake ambao kamwe hawezi kuwasahau kwa jinsi walivyomsaidia na kumjenga kitaaluma, kiutu, kijamii na kadhalika.

Kama tulivyoona hapo juu, mwalimu ni mtu mwenye (anayepaswa kuwa na) mafunzo ama ujuzi maalumu kwaajili ya kuwafunza na kuwasaidia wengine. Mtu mwenye kufanya hizo inafaa awe na uwezo mkubwa wa kuelewa na kuwasilisha ujuzi huo kwa watu wengine. Ujuzi na uwezo wa mtu, kwa bahati mbaya sana, mpaka hivi sasa hupimwa kutumia vyeti alivyonazo. Vyeti hivyo huonesha matokeo ya mitihani mbalimbali ambayo mtu huyo alifanya; binafsi siamini njia hii ya namna ya kupima uwezo wa mtu, nakumbuka HakiElimu waliwahi kusema elimu sio cheti bali uwezo. Kurejea kwenye mada yetu, swali hapa ni je, walimu wetu Tanzania wana sifa zipi na ni namna gani huwapata?

Sina rejea sahihi kuhusiana na uwezo wa Mwalimu Julius Nyerere, ila simulizi za walimu wangu shuleni zinaonesha(hapa ni uvivu wa kufanya utafiti) kuwa alikuwa mwanafunzi hodari ndio maana akasomea ualimu. Mwalimu wangu darasani aliniambia kuwa huo ulikuwa ni utaratibu wa kikoloni kuwa wanafunzi wenye uwezo mkubwa darasani wanakwenda kusomeshwa ualimu ili wafundishe wengine. Utaratibu huu ulikuwa na mantiki na maana kubwa sana. Mtu anataka kuwa mwalimu awe ni yule aliyefaulu vyema sana katika masomo yake, kwa kutumia vyeti, tuchukue wanafunzi wenye daraja la kwanza na la pili.

Na kwa taaluma zingine, ambazo pia ni muhimu kama vile utabibu, uhandishi, sheria, wanasaikolojia n.k kuwe na utaratibu utakaofaa; wanafunzi wote wakifundishwa vyema na walimu wenye uwezo mkubwa basi madaraja yoyote kuanzia la kwanza hadi la tatu yanaweza kutoa wataalamu wenye sifa takikana kabisa. Kwa hali ilivyo hivi sasa baadhi ya watu hapa Tanzania waidharau taaluma ya ualimu, kiasi cha kushauri mwanafunzi aliyefanya vibaya mitihani kusomea ualimu. Sasa hii, si sawa, kwa kuwa mwanafunzi ambaye hana uwezo wa kutosha kuelewa inawezekana kabisa akawa na uwezo mdogo wa kuelewesha wengine. Kwa hivi basi kuna haja ya kuangalia kwa makini namna tunavyowapata walimu wetu wa baadaye ili kupata  kuwa na uhakika wa kupata wanataalamu wa fani zingine waliofunzwa na walimu wenye ujuzi na uwezo wa kufaa kuwapatia elimu hitajika. Kinyume na hapo tutapata wataalamu wasioiva sawasawa ni muhimu sana.

Ili wanafunzi wanaofanya vyema waweze kwenda kusomea ualimu na kufunza ni muhimu wakapatiwa motisha ili kuwahamasisha. Ni muhimu kufanya hivyo kuwa kila binadamu ana uhuru wa kufanya aonavyo muhimu ili mradi tu hadhuru ama haathiri haki za wengine. Kuwe na utaratibu na sheria ya namna ya kuwafanya wanafunzi waliofanya vyema zaidi kwenda kusomea ualimu. Hiyo inaweza kuwa moja ya malengo ya kimaendeleo ya taifa hasa wakati huu ambapo hapa nchini kuna shule nyingi kama zilivyo kata. Ili kuepuka kuendelea kuwa na takwimu kubwa ya shule bila ubora stahiki basi hilo tuliangalie.
Shule ya Tusiime Picha na google












Sifa stahiki za walimu zinatupeleka kwenye sifa stahiki pia kwa shule zetu. Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya elimu, japokuwa, bado kuna mengi yanatakiwa kufanyika. Kuwa na shule kila kata ni hatua nzuri mno ya kimaendeleo, lakini aina gani ya shule ni muhimu zaidi kwa kuwa shule inaweza kuwa ni ukombozi ama utumwa. Mwanafunzi aliyefunzwa vyema yeye na jamii yote ya wanadamu itakuwa imekombolewa ilhali yule asiyefunzwa barabara atakuwa mzigo mkubwa kwa jamii; kwa vile atatazamwa kama aliyekombolewa na elimu. Mtu aliepata elimu katika mazingira duni ya kitaaluma ni mtu aliyeelimika nusunusu, mtu mwenye elimu nusunusu ni hatari kweli katika jamii kwani anaweza kuutumia, ashalkumu si matusi, umbumbumbu wake kuleta madhara akidhani kuwa anatoa msaada kwa jamii. Kwa hiyo wito hapa ni kuboresha walimu na mazingira yao ili wafanye kazi kwa uzuri na hivyo kuwa chachu kwa maendeleo ya taifa lote.