Thursday, September 29, 2011

Vijana wa CCM na CHADEMA


Picha kwa hisani ya mmiliki-Mtwara















Hawa ni vijana na wanafunzi; wataalamu wa leo na baadaye. Wana uwezo na nguvu nyingi zinazo hitaji kuelekwezwa sehemu sahihi kinyume na hapo ni maafa. Vijana kwa asili yao ni watu motomoto. Wana nguvu na hazina nyingi miilini na akilini mwao ambayo wanahitaji kuvifanyia kazi ili nguvu hizo ziwe na manufaa kwa jamii ya wanadamu.

Ili waweze kufanikiwa kuzitumia nguvu zao vyema ni lazima wapatiwe mafunzo ili watambue namna ya kuzigundua na kuzitumia vyema nguvu hizo; leo hii kuna AZAKI nyingi zinazotoa STADI ZA MAISHA kwa vijana.


Hilo ni jambo jema kwani bila kufanya hivyo huweza kuzitumia nguvu hizo vibaya. Wakitokea waharibifu wachache wenye kutambua vyema nguvu nyingi walizonazo vijana, huweza kuwaharibia kabisa  malengo yao ya maisha bila huruma. Hivi leo hapa Tanzania kwa sababu kadha wa kadha, baadhi ya vijana wanaingia kwenye Siasa kwa malengo ya kusaka ajira; siasa kwao ni ajira. Siasa, na hasa Siasa Safi (JK.Nyerere) ni muhimu na lazima kwa maendeleo ya watu. Lakini siasa isipokuwa safi ndipo hapo utasikia vijana wamefanya vurugu zilizohamasishwa na itikadi za kisiasa. Bila kuvurugwa na makundi ya wabinafsi wachache wenye kulenga kujinufaisha kupitia nguvu kazi na akili ya vijana, kundi la vijana ni hazina kuu kwa taifa lolote duniani, na halina haja ya fujo.Hayo yamedhihirishwa na makala hii ya Habari Leo: Vijana Chadema, CCM hawataki vurugu Igunga


MWANAFUNZI BORA


                                          Imepakuliwa hapa :https://www.youtube.com/watch?v=Y1JhL9FTA8Y                
Hapo juu wanafunzi wa moja ya shule za msingi hapa Tanzania. Mwanzo kabisa wa safari ndefu ya miaka kadhaa... wana mahitaji mengi kufanikisha ndoto zao.

Mwanzoni mwa mwaka huu shirika binafsi la HakiElimu lilitoa shindano la kuandika sifa za mwanafunzi bora. Shindano lilimtaka mshiriki aandike insha ama achore picha juu ya mada hiyo. Hatimaye hivi leo mshindi amepatika; unaweza kusoma mada hiyo kwenye Habari Leo Hapa  chini ni moja ya insha zilizoshiriki shindano hilo:

Mada hii ni muhimu kwa kuwa ni mwanzo wa maendeleo ya nchi yoyote duniani. Mwanafunzi mwenye sifa bora hufanya vyema katika masomo yake na kupata ujuzi wa aina fulani wenye manufaa kwa nchi. Mwanafunzi mwenye sifa bora hufaulu vyema masomo yake na kufaulu kwake ni lulu kwa nchi kwani kupitia ujuzi na weledi wake katifa fani aliyonayo huchangia katika maendeleo ya taifa lake.

Mwanafunzi ni mtu anayetafuta elimu ama maarifa fulani . Kwa kawaida mtu huanza kupata elimu toka utotoni. Ni vyema ikawa hivyo kwa kuwa mtoto anapokuwa mdogo ana uwezo mkubwa kwa maana ya wepesi wa kujifunza na kuelewa mambo mengi mapya kwa urahisi zaidi. Wakati wa umri mdogo mtoto anahitaji uangalizi wa karibu kabisa wa mzazi/ mlezi wake. Uangalizi huo ni vyema ukaangalia pia suala kujifunza kwa mtoto. Hivyo kujifunza kwa mwanafunzi wakati angali na umri mdogo ina maana kuwa huwahusisha pamoja naye mwenyewe, mwalimu, mzazi/mlezi, na familia yote kwa ujumla wake. Pamoja na hayo yote kuna vigezo na mazingira ambayo ni muhimu kwa mwanafunzi kuweza kutafuta maarifa kwa usahihi zaidi.

Ili mwanafunzi aweze kufanya vyema katika masomo yake na hivyo kuweza kuchangia katika maendeleo ya taifa lake na ya jamii yote ya wanadamu kwa ujumla wake, mara baada ya kupata ujuzi, ni lazima awe na sifa kadhaa. Sifa za mwanafunzi bora ndio hasa mada ya insha hii. Mwanafunzi bora anatakiwa awe na aina mbili ya sifa. Awe na sifa za ndani na za nje; nitazielezea kwa unagaubaga hapa chini.

Sifa za ndani ni za kimaumbile, hizi ni zile ambazo binadamu anazaliwa nazo. Hafanyi chochote kuzipata ni zawadi ya uumbaji na ni sifa za lazima kabisa; nazo ni akili na utashi. Akili ni ule uwezo wa kupokea, kuzisoma na kuzitafsiri taarifa zote toka nje ya mwili wa binadamu. Utashi ni ule uwezo wa binadamu kuamua kufanya jambo moja ama jingine baada ya utashi huo kupewa na akili taarifa zote zihusianazo na jambo fulani kabla ya kulifanyia maamuzi. Akili inampatia mwanafunzi uwezo wa kujifunza mambo mapya na kuyatunza kama ujuzi; hivyo ni jukumu la mwanafunzi, kupitia utashi, kuamua kujifunza. Sifa hiyo inatufikisha kwenye utashi; kazi ya utashi ni kuamua kufanya hili ama lile kisha kupewa taarifa zote muhimu. Hivyo basi, kwa sifa hii, mwanafunzi ana hiari ya ama kujifunza ama kutojifunza.

Sifa za nje za mwanafunzi bora ni usikivu, udadisi, heshima na matumizi sahihi ya ujuzi alioupata. Kijana wa kike ama wa kiume ili aweze kujifunza vyema hana budi kuwa msikivu. Asikilize kwa makini maagizo ya mzazi/mlezi nyumbani, mafunzo ya mwalimu shuleni na ni vyema pia milango yake yote ya fahamu ikawa na usikivu ili maarifa mapya yapatikane. Picha ya mtu mwenye masikio makubwa inaweza kuwakilisha twasira ya mwanafunzi mwenye usikivu.

Udadisi; hali ya kutafuta jambo kwa kuulizauliza . Kwa hakika hii ni sifa muhimu kwa mwanafunzi bora. Pamoja na kufundishwa na mzazi/mlezi nyumbani na mwalimu darasani, mwanafunzi mwenyewe inamlazimu ajifunze kutafuta elimu, mambo mbalimbali juu ya mafunzo yake bila ya kuwa tegemezi kwa mwalimu tu. Mwanafunzi mdadisi anaweza kuomba na kujiunga uanachama katika maktaba mahalia kwa lengo la kusaka mambo mbalimbali kwa kina zaidi.

Heshima, thamani ya utu, adabu ; hii ni sifa nyingine muhimu kwa mwanafunzi bora. Sifa hii humfanya mwanafunzi awe mwenye mahusiano mazuri na wazazi /walezi na walimu wake. Mahusiano mazuri ni kigezo na kichocheo cha muhimu cha udadisi na kujifunza. Mwanafunzi mwenye mahusiano mema na mwalimu wake hana hofu kuuuliza ama kutoa maoni yake juu ya mada fulani darasani.

Matumizi sahihi ya ujuzi alioupata. Mwanafunzi bora, si yule mwenyekukariri kila afundishwacho na kwa kurudia aliyoweka kichwani hupata alama nzuri katika mitihani, bali ni yule mwenye uwezo wa kutafsiri nadharia na masomo yake kwenda kwenye vitendo halisi. Mfano, kwenye somo la Sayansi kimu, mwanafunzi anajifunza juu ya utunzaji wa vyakula; swala hilo anaweza kulifanya kuwa kitendo halisi kwa kuwashirikisha wazazi wake kama simulizi inayoweza kufanyiwa kazi na hivyo kuipatia familia mbinu ya kuhifadhi chakula.

Kuhitimisha insha hii; wazazi/walezi na walimu wao pia wana majukumu makubwa juu ya wanafunzi wao. Kubwa na muhimu zaidi ni kuwajengea mazingira ya kujifunza na kuwatia shime ili wawe na hamu ya kuzitumikisha sifa zote za ndani na za nje. Akili, utashi wa kujifunza, usikivu, udadisi, heshima na matumizi sahihi ya ujuzi mpya ni sifa za mwanafunzi bora. Sifa hizi huleta matokeo mazuri mno pale zinapopatiwa mazingira na fursa sahihi na hiyo huweza kudhihirisha uwezo wa mwanafunzi bora.

Thursday, September 15, 2011

Chanzo cha Mapato kwa Wananchi

Hii ni sehemu ya soko la Samaki mkoani Mtwara.
Hapa ni sehemu samaki wanapochuuzwa mara  baada ya kuvuliwa.



Biashara ya samaki ni moja kati ya maeno yenye kutoa ajira kwa wananchi wengi wa kawaida hususan kina mama. Hii ni shughuli ambayo huwapatia wananchi wengi pesa za kuweza kuendesha maisha yao na pia huweza kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi hata kama ni kiasi kidogo.

Hivi karibuni nilitembelea soko hilo kujionea jinsi lilivyo na kuangalia uwezekano wa kujipatia kitowewo. Hali niliyoikuta sokoni hapo si ya kuridhisha sana. Soko la bidhaa hiyo muhimu kwa afya ya binadamu si nzuri kiafya. Hata hivyo nilipouliza kidogo wachuuzi sokoni hapo niliambiwa kuwa kuna mikakati na ujenzi wa soko la kisasa tayari umekwishaanza. Hivyo kuna matumaini ya kupata sehemu nzuri zaidi siku za usoni.

Hii ni sehemu ya muendelezo wa soko letu la samaki mjini Mtwara, wahusika wameliona na hivyo wanaendelea kuliboresha...



Bila shaka mazingira safi ni muhimu kwa akili safi... ni muhimu marekebisho yafanyike haraka... bila shaka tutahitaji soko la kisasa kama pale Magogoni...

Wednesday, September 14, 2011

Clouds Fm hongereni lakini...


Hiki ni kivuko kinachotoka Mtwara kwenda Msanga Mkuu.
Picha inaonekana kwa mbali kiasi; vitu unavyoona vya rangi ya pinki vikipepea ni maboya ya kuokoa maisha. Unaonaje yavaliwe wakati gani?

Kituo cha redio (Mawingu) Clouds Fm cha jijini Dar es Salaam, kimeanzisha mkakati wa kuchangia ununuzi wa maboya ya kuoa maisha-mkakati huo umepewa jina la "OKOA MAISHA"  Maboya hayo "life jackets" hutumika kuokoa maisha ya abiria endapo ajali ya majini itatokea. Maboya hayo huvaliwa na abiria kwenye ndege-ili kwamba chombo hicho kikiangukia majini, husaidia kuoa maisha ya abiria, vazi hilo hutakiwa kuwepo pia kwa chombo chenye kusafirisha abiria majini. Clounds wanapiga la mgambo ili kusaidia wasafiri majini. Kwa hili binafsi nawapongeza sana. Hata hivyo kuna mambo mawili hapa ya kutafakari si tu wa mpiga mwano huu bali ni kwa watanzania wote.

Mosi, binafsi natambua kuwa kwenye ndege maboya hayo, kwa kawaida, huwatosha abiria wote; kila abiria anakuwa na life jacket chini ya kitivchake. Na hivyo kikitokea kile ambacho katu hakitamaniki, bali kila abiria hupata kutumia boya lake. Nimesafiri mara mbili kwa maji toka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, binafsi sikumbuki “boya langu” lilikuwa wapi. Kwa kusema hivi sina uhakika je, kila abiria kwenye vyombo vya maji hapa Tanzania, ana uhakika wa kupata boya lake ama, je idadi ya maboya inalingana na idadi ya abiria chomboni?

Swala la pili ni juu ya muda wa kuvaa boya hilo. Nilipokuwa mwanafunzi kule Uganda, nilipata nafasi ya kutembelea wafungwa kwenye gereza lililo kisiwani katika mji wa Jinja. Kwenda gerezani, chuo nilichosoma kiliweka utaratibu wa kila mwanafunzi kuvaa boya lake pale anapokuwa chomboni. Hi ili wanafunzi wasafiri kwa usalama na uhakika zaidi. Tunaweza kuanzisha utaratibu kama huo pia, kila abiria avae boya “life jacket” pale tu anapoingia chomboni. Najua utaratibu huu utazua hofu kwa abiria na wamiliki wa chombo.

Abiria, akivaa boya la kuokoa maisha, atajihisi kama anaingia kwenye ajali moja kwa moja na ataona kama anajiombea dua baya kwa kufanya hivyo. Mmiliki wa chombo atahisi kuwa abiria wataondoka ya maboya yake na safari inayofuata hakutakuwa na boya hata moja. Tukitaka kufanikiwa lazima tubadilishe tamaduni zinazobadilika.

Tuvae maboya mara tunapoanza safari majini; kwa kufanya hivyo ndo tutakuwa tunajali maisha hofu za kimazingaombwe kamwe haziwezi kutusaidia. Mmiliki wa chombo majini, aweke utaratibu wa kukusanya maboya mwisho wa safari; kila aingiaye chomboni apate boya na kila anapotelemka akabidhi, kama hana alipe gharama ya boya hilo hata kama hakuvaa. Kuokoa maisha ni lazima tuwe wabunifu, makini lakini pia wakali kwenye utekelezaji. Utaratibu huu kwa kiasi fulani unafanyika pale kituo cha mabasi, Ubungo, Dar es Salaam.(Kukagua abiria kama wamefunga mikanda)

Mandalu

Uzembe ukipungua ajali pia zitapungua !

Google Image
                                          Inapakiwa hapa https://www.youtube.com/watch?v=MpzE7flW9_A
Wakati tukiendelea na tafakari juu ya ajali ya meli kule Nungwi ni wasaa mwafaka kwa watanzania na wanadamu wote kwa ujumla na hasa wenye kutumia vyombo mbalimbali kusafirisha binadamu wennzao, iwe ni vya ardhini, majini ama angani, kuwa waangalifu zaidi. Ajali ya meli ya abiria LCT Spice Islanders, iliyokuwa ikitoka Unguja kwenda Pemba, imesababisha vifo vya ndugu zetu wengi. Ni msiba mkubwa kuona watu wengi wenye afya njema na ambao ni  nguvu kazi muhimu kwa ujenzi wa Taifa, wakiaga dunia.Tunamwomba Mwenyezi Mungu kwa huruma yake awapokee ndugu hawa kwenye makazi ya kudumu, na wafiwa na wajeruhi wote wapate faraja na kupona haraka! Kutokana na tukio hili serikali na wananchi wote kwa ujumla wetu tunapenda kuona wamiliki vyombo vya kusafirishia abiria, mamlaka za kudhibiti vyombo vya usafiri na wasafiri wenyewe wakiongeza umakini...

Tuesday, September 13, 2011

Vijana na Mabadiliko

Makala ya Mwandishi Ahmed Rajab; Vijana wa Afrika wanawaperemba tu viongozi... imejaa mambo anuai ambayo yana manufaa mengi kwa kijana mwenye malengo ya kuchangia katika jamii yake.

Mwandishi anaongelea mwamko mpya wa vijana barani Afrika katika kudai haki za jamii zao, aidha anatoa picha ya jinsi viongozi wabadhilifu wanavyo tumia vibaya mali za umma kwa manufaa binafsi.

Monday, September 12, 2011

Tandahimba Pia


















Sekondari ya Milongodi ilikuwa na walimu wetu pia. Hapa mkuu msaidizi wa shule hiyo akitushirikisha jambo kuhusu sekondari hiyo ambayo ingali ikikuwa kabisa.

Katika shule hii kidato kimoja kina wanafunzi wa kiume tu bila binti hata mmoja, Zaidi ya hayo walimu, kama ilivyo katika shule nyingine nyingi, ni wachache mno. Kwahiyo, walimu mafunzoni ilikuwa ni ukombozi mkubwa kwa shule nyingi za wilayani Newaala na Tandahimba, mkoani Mtwara. Pengine muda wa mazoezi uongezwe, ili huduma hiyo iendelee kwa muda mrefu zaidi? Tutawauliza walimu hawa mafunzoni.

Walimu mafunzoni

Nilipata fursa ya kukutana na walimu-mafunzo
sekondari ya kutwa Newala mjini

Alaa kumbe ni NEWALA !














Hapa nikijiandaa kuanza safari asubuhi na mapema- mjini Newala! Picha na Eric Wamalwa

Nipo wilayani Newala. Hii ndo wilaya ya kwanza kuandikishwa hapa Tanzania, ni moja ya wilaya tano za mkoa wa Mtwara. Wilaya hii, kama jinsi ilivyo kwa maeneo mengine, ina mahitaji ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kuna makundi yote ya lazima katika jamii; watu wazima, vijana, na watoto.

Kijamii; maji ni shida (jamii imejenga utamaduni wa kuvuna maji ya mvua: karibu kila familia ina mikingio maji kwaajili hiyo – huu ni utamaduni wa kuigwa hasa na sehemu zenye mvua za kutosha. Maji hayo ya akiba yaweza kuwa na matumizi kedekede. Mfano kumwagilia bustani za mboga mboga, kuanzisha mabwawa ya samaki n.k )

Elimu: wilaya ina shule kadha wa kadha; karibu kila kata ina shule yake. Hili ni moja ya mambo mazuri ya serikali iliyopo madarakani. Ni vyema kuwa na shule za kuweza kuandikisha wanafunzi wengi iwezekanavyo. Vijana wengi wakiandikishwa shule za sekondari ndo hasa mwanzo mzuri na wa uhakika wa kupiga vita umasikini kwa vitendo. Hata hivyo mtaala wa elimu uzingatie mfumo wenye vitendo zaidi kuliko nadharia kama ilivyo hivi sasa. Vijana wetu wengi wakimalima masomo yao, kwa mfumo tulio nao hivi sasa, hulazimika kusubiri ajira. Mfumo unaofaa ni ule wa kumuandaa kijana ili aweze kujiajiri; hilo hasa ndo liwe lengo la elimu yetu. Tukirejea mada yetu; shule nyingi huko Newala zina watenda kazi wachache sana.

Shule kadhaa zina walimu wawili, watano, sita, nyingi zina idadi isiyozidi walimu kumi. Hii ni changamoto kuu na kubwa mno katika sekta ya elimu. Wanafunzi wanapokuwa na walimu wa kutosha ndo inawarahisishia kujifunza kwa ufanisi zaidi. Kwa walimu wakiwa na wanafunzi kiasi, kwao inakuwa ni vyema zaidi katika utendaji kazi wao.

Ukosefu nyumba za walimu; shule nyingi za kata zipo vijijini hasa, ni sawa kwani huko ndiko wanapoishi wananchi na watanzania wengi zaidi. na vijiji vyetu vingi havina huduma kwa wageni hususani nyumba za kulala wageni. Ukosefu nyumba za kulala wageni vijijini unakwamisha hata wakaguzi na wataalamu wa kada zingine kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. Shule nyingi hizi za kata ama hazina nyumba za kutosha kwa walimu ama hazina kabisa nyumba hizo. Ni kweli walimu waliopo katika shule hizo ni wachache pengine inajieleza sawa pia kutokuwa na nyumba kwa walimu. Kuwa na nyumba za ziada kwa walimu inaweza kuwa ni fursa ya kuwavutia walimu wageni, ambao wengi wafikapo kujitambulisha na kuona mazingira ya shule hugoma kurejea shuleni huko.

Kisiasa: Newala ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hivyo huko pia kuna mfumo wa vyama vingi vya kisiasa lakini wakazi wa huko wanaishi kwa amani na undugu. Hata hivyo hii ni tathmini yangu ya juma moja tu.

Kiuchumi: zao la korosho ni uti wa mgogo wa uchumi wa wilaya hiyo; wakazi wengi hujihusisha na kilimo cha zao hilo la msimu na lenye kuhitaji matunzo ya karibu hasa. Kwa wananchi wanaoweza kufuata vyema maelekezo ya wataalamu wa kilimo hujipatia mavuno na pesa nzuri kutokana na kilimo cha zao hilo. Hata hivyo mkulima siku zote huchukua tu bei inayopangwa sokoni na watu wengine; yeye hufanya kazi ngumu ya kutunza shamba na kufuatilia ukuazi wa korosho hadi kuwa tayari na kisha hapo watu wengine wenye “utu” zaidi ya mkulima hukaa meza na kupanga bei ya zao hilo kama ilivyo kwa mazao mengine ya wakulima wetu maskini hapa Tanzania na sehemu nyingi nyingine barani Afrika. Siku moja tufikie hatua ya kupanga bei ya mazao yetu wenye kwenye hilo soko la dunia; hii ni mantiki zaidi kwa kuwa wakulima wetu ndio wanafahamu haswa gharama za kilimo.

Ajira za vijana: Vijana kundi lenye nguvu na msukumo mkubwa wa maendeleo ya wakati uliopo na ujao katika jamii. Nikiongea na vijana kadhaa wa mjini Newala niligundua kuwa kuna idadi kubwa ya vijana wa kitanzania wanofanya shughuli za kiuchumi, hususan biashara nchini Msumbiji. Newala ni wilaya ya mpakani kabisa na Msumbiji. Upande wa kaskazini ya Msumbiji haujapiga hatua kubwa kimaendeleo na hivyo kutoa fursa nyingi kwa watafuta mali: hivyo vijana wetu hupitia huko na kufanya biashara za bidhaa anuwai. Vijana niliongea nao, wanijuza kuwa vijana hao wa kitanzania huko, hususani wale wenye bidii ya shughuli zao, ni wenye mafanikio makubwa.

Nyumba za kulala wageni chache: wilaya hii ina nyumba chache za kulala wageni. Upungufu huo hivyo unatoa fursa za kiuchumi kwa wananchi kujiimarisha kiuchumi na hivyo kujiongezea pato na pia kuongeza pato la taifa kwa ujumla.Kuna changamoto lakini pia fursa anuwi za kujiimarisha kiuchumi, kujiondoa kwenye umasikini na kuchangia kwa pato jumla la taifa.