Tuesday, August 23, 2011


Baadhi ya wadau wa Vijana tukisimama kwa picha ya pamoja

Wadu wa Vijana

Hapa ni Moro nikiwa na wadau wa vijana.
Hawa ni wadau toka mikoa mbalimbali waliokutana kujadili masuala ya afya ya uzazi na maendeleo ya vijana kwa ujumla.

Picha kwa hisani ya kiongozi wa mradi wa masuala ya vijana wa fhi









Saturday, August 20, 2011

Vijana Maji Moto

Picha kwa Hisani ya mtandao
Hivi karibuni tumeshuhudia harakati kubwa za vijana sehemu mbalimbali duniani. Harakati hizo zimekuwa na dhima na vyanzo tofauti tofauti. Harakati za vijana mashariki ya kati na Afrika kaskazini zilisababishwa na kukosa mahitaji yao muhimu hususani kukosa nafasi za kazi na kutokuwa na uhakika wa mustakabali wa maisha yao. Giza hilo kwa mustakabali wa maisha ya vijana ulisababishwa na ubinafsi wa viongozi wa nchi hizo. Kiongozi wa Tunisia, Ben Ali amekuwa madarakani kwa muda mrefu na amejikusanyia mali nyingi mno na hivyo kuharibu matumaini ya vijana na wananchi wake kwa ujumla. Hali kadhalika, Misri, Libya, Yemen na kwingineko mashariki ya kati.

Vijana wa Uingereza wao nao walisababisha fujo ama varangati (Kiswahili cha kizamani) lakini wao sababu ilikuwa tofauti. Makala ya mwandishi kutoka London Macha, inatoa sababu ambazo zinawapambanua vijana wa Uingereza na wale wa Mashariki ya kati. Wachambuzi wengine husema kuwa vijana wa dola hiyo kuu zamani, wanafundishwa tu/ ama zaidi juu ya haki zao, hawafahamu kuhusu wajibu wao kwa jamii. Hili ni tatizo kubwa. Vijana wanapokua ni vyema tukawajuza haki zao, lakini muhimu kabisa watambue pia namna ya kuwajibika kwa jamii zao. Hili ni jambo la kila mahali Tanzania na nchi nyingine zote duniani, na tena muhimu kwa wananchi na pia serikali kutoa mchango wo kwa maendeleo ya vijana.

Tanzania kuna asasi zisizo za kiserikali (AZAKI) lukuki zinazojihusisha na masuala ya vijana. AZAKI hizo zimeanzishwa na wananchi kwa malengo lukuki, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia vijana. Hili ni jambo jema kwani vijana ni moja ya makundi yaliyo muhimu kwa maendeleo ya jamii ya wanadamu. Hata hivyo katika siku za nyuma kidogo kulizuka AZAKI nyingi ambazo hazikujali masilahi ya walengwa husika bali waanzilishi kujijaza mapesa.

Serikali yetu Tanzania, imepiga hatua kubwa hasa kwa kuwa na utashi muhimu wa kisiasa na kuazisha shule za sekondari kila kata. Bila ubishi hii ni hatua kubwa sana ya kuelekea maendeleo ya kweli. Elimu mwanzo wa ustaarabu wote duniani; elimu kwa upana wake si tu ile ya darasani. Hata hivyo changamoto kubwa kwa serikali ya Tanzania na wananchi wake kwa ujumla wao ni kuziboresha shule hizo lukuki za kata. Ni muhimu kufanya hivyo kinyume na hapo tunapata taifa la watu walioelimika nusu nusu. Hii elimu nusu ni hatari sana, pengine afadhali asiyeipata kabisa; mwenye elimu nusu hatokubalika katika kundi la wajinga kabisa kwani ana maarifa kiasi na hivyo kuwa tofauti na wasiosoma kabisa, lakini hawezi changamana pia na walioiva vilivyo kielimu kwake itakuwa ni kujinyanyapaa – “kujichora” (maarufu kwa vijana) mbele ya wasomi. Ni hatari kama nusu wasomi hawa watakuwa wengi; watadai haki kwa njia zisizokubalika kwani elimu yao yawatuma hivyo.

Hivyo AZAKI zilenge kuwasaidia vijana wapate stahili yao. Wananchi wote kwa ujumla na serikali kwa maana ya dola tujipange kuziboresha shule hizi haraka iwezekanavyo kama inavyoelezewa kwenye MKUKUTA II ili kuepukana na nusu wasomi na matatizo mengi toka kwa vijana wetu siku zijazo.

Wednesday, August 3, 2011

Familia Inafaa - Families Matter Program! FMP

Hapa nikiwa na mratibu wa Mradi wa Familia Inafaa huko mkoa wa Ruvuma. Wanakikundi ni wadau wa Familia Inafaa katika mkoa wa mashujaa wa kingoni, nyumbani kwa simba wa vita 



Hapa nikiwa na raia wa siku nyingi hapa Tanzania. Mzee huyu ananipatia somo juu ya malezi kulingana na uzoefu wake wa siku nyingi duniani hapa- asante mzee! 



      
                                                                                                                                                               Hapa nikiwa na wadau wa Familia Inafaa mkoani Mtwara; hapa ni kijiji cha Nanguruwe Mtwara Vijijini!


Familia Inafaa – Families Matter Program! (FMP)













Huu ni mradi unaongozwa na Kampuni ya T-MARC. Mradi huu unawalenga wazazi, walezi na wadau wa malezi ya watoto ambao bado hawajabalehe kwa wavulana na hawajavunja ungo kwa mabinti. Familia Inafaa! Ni mradi ambao tayari umeshaanza kutoa huduma kwa wazazi na walezi wa mikoa ya Mtwara na Ruvuma.
• Lengo la msingi kabisa la FMP ni kuwatia shime wazazi katika juhudi zao za kuwalea watoto wao ili wakue katika afya njema.

• FMP ni program mahususi kwa ajili ya wazazi. Imeandaliwa katika namna ambayo inawasaidia wazazi kutumia mbinu ambazo zinaweza kuwalinda watoto wao dhidi ya tabia hatarishi za afya ya jinsia, hivi sasa na wakati ujao pia.

• FMP inaamini kuwa wazazi wana nafasi yenye ushawishi mkubwa wa kujenga, katika namna chanya tabia za kiafya za watoto wao.

• Lakini hata hivyo ushawishi huo ni lazima ushindane na ujumbe wanaoupata watoto wao toka kwenye vyombo vya habari, vijana wenzao, na jamii yote kwa ujumla.

• Mawasiliano ya wazazi yanaweza kuwalinda watoto, kujenga uwezo wa kufanya maamuzi yafaayo, na kufikisha ujumbe sahihi.

• FMP inataka kuwasaidia wazazi “kuongeza ujuzi wao” kwa kuwapatia vifaa na mbinu mahususi kabisa ili waweze kuwa na mtindo bora wa afya katika familia zao.