Showing posts with label VIDEO. Show all posts
Showing posts with label VIDEO. Show all posts

Friday, January 29, 2016

JE AFRIKA TUNAWEZA KUMUDU ELIMU BORA NA BURE?


JE, AFRIKA INAWEZA KUMUDU ELIMU BURE?
imepakuliwa hapa: https://www.youtube.com/watch?v=D6zlTJ9xUp4

Mjadala umeendelea kote barani Afrika kupitia mtandao wa Bbc. Swali hili ni muhimu kwa Tanzania pia. Je, tunaweza kumudu elimu bure? Elimu hiyo ya bure inafaa iendane na ubora pia si tu elimu bure lakini yenye ubora bure pia.

Kwenye picha iliyochukuliwa mtandao wa bbc wanaonekana watoto wakiwa kwenye darasa la chini ya mti, wakiwa wamekalia mawe ili hali wapita njia wakiendelea na shughuli zao. Ama kwa hakika hapa ni ngumu mno kupata elimu bora hata kama itakuwa bure...
http://www.bbc.co.uk/programmes/p03g5pbx

Wednesday, January 20, 2016

SABABU ZA UGUMU WA MAISHA MTWARA ZATAJWA...


Mkoa wa Mtwara ni moja kati ya mikoa 26 ya Tanzania. Mkoa huu una sifa lukuki moja ya sifa hizo ni ugumu wa maisha; mkoa huu unasifika kwa bei kubwa za bidhaa ikilinganishwa na mikoa mingine ya nchi. Kwenye moja ya vipindi vyake maarufu vya jioni kituo cha redio PRIDE FM kilichopo mkoani humo siku ya Jumanne tarehe 19 Januari 2016 iliendesha kipindi ambacho pamoja na mambo mengine kilihoji kwanini maisha bidhaa mbalimbali katika mkoa huo ukilinganisha na mikoa mingine ni aghali zaidi?

Washiriki waliopiga simu walikuwa na majibu anuwai; mmoja kati ya wapiga simu hao alisema ni kweli kwamba maisha ni magumu Mtwara ikilinganishwa na mikoa mingine na sababu hasa ni uvivu wa wakazi wa mkoani humo. Wakazi wengi wanaojishughulisha na kilimo hulima eneo dogo tu la shamba na kutaka kuendesha maisha yao kupitia shamba hilo. Jambo hilo huwalazimu wakulima hao kupanga bei kubwa za mazao yao pindi wakati wa kupeleka bidhaa sokoni unapofika.

Mchangia mada mwingine alisema sababu hasa ni zile za kihistoria kwamba bidhaa zilizotoka mikoa ya jirani zilipangiwa bei kubwa kwa kuwa barabara kwenda mkoani humo zilikuwa mbovu mno na hivyo kufanya gharama za usafirishaji kuwa kubwa jambo liliongeza bei ya bidhaa.

Wito umetolewa kwa serikali kulitazama upya suala la bei za bidhaa mkoani humo kwa kuwa barabara imejengwa kwa kiwango cha lami na hivyo hakuna tena sababu ya gharama kubwa za usafirishaji.


Imepakuliwa hapa https://www.youtube.com/watch?v=-Wc0bwtAONY

Sunday, January 17, 2016

JIMBO KATOLIKI MTWARA LAPATA ASKOFU


Titus Joseph Mdoe, amesimikwa rasmi hivi leo kuwa askofu wa tano wa jimbo katoliki Mtwara. Askofu Mdoe aliteuliwa mwaka 2015 na Papa Fransisko kuliongoza jimbo hilo kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa askofu wa jimbo hilo Gabriel Mmole. Askofu Mmole ambaye amelitumikia jimbo la Mtwara kwa miaka 31 anastaafu kisheria kwa mujibu wa kanuni za kanisa.

Askofu Mdoe amesimikwa rasmi mbele ya umati mkuu wa maaskofu toka pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa ngazi mbalimbali za serikali na halaiki kuu ya waumini na watu wenye mapenzi mema mkoani Mtwara.
imepakuliwa hapa...https://www.youtube.com/watch?v=PX8-nyXfnPg

Tuesday, January 12, 2016

MAPINDUZI DAIMA

Picha na mtandao
Imepakuliwa hapa: https://www.youtube.com/watch?v=-sMDkCSC_5g

Leo 12 Januari 2016 ni kumbukumbu ya 52 ya  siku ya mapinduzi yaliyofanyika visiwani Zanzibar mwaka 1964. Mapinduzi hayo yalifanyika ili kufanikisha utawala wa wengi dhidi ya utawala wa wachache. Mapinduzi hayo yalifanyika kuuong'oa utawala wa Sultan wa kiArabu aliyekuwa amepata uhuru toka mikononi mwa Waingereza. Waarabu walikuwa wachache lakini wakapewa mamlaka na Waingereza, Wazinzibar wenyeji na wenye asili ya Afrika wakafanya mapinduzi hayo kuchukua haki yao.

Mapinduzi Daima ndiyo hasa salaam rasmi kwa siku hii na hii inakubaliana na maneno ya Heraclitus mwanafalsafa wa kale wa Kigiriki aliyekuwa wa mwanzo kusema hakuna kinachodumu ila mabadiliko, ama mapinduzi hivyo ni hakika na sahihi kusema mapinduzi daima.

Tunawapongeza wananchi wote waZanzibar na Tanzania kwa ujumla wao. Aidha maadhimisho haya yawe ni chachu ya kutanzua mgogoro wa kisiasa unaoendelea visiwani humo ili nchi indelee kuwa ya amani na salama.
Mungu ibariki Tanzania na watu wake...

Thursday, January 7, 2016

DHANA YA KUTUMBUA MAJIPU IMETOKA WAPI?

Picha kwa hisani ya mtandao
imepakuliwa hapa:https://www.youtube.com/watch?v=xCjZLhxsOcA
Wakati wengi wetu tukiendelea kumpongeza Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ndugu JPMagufuli kwa kushughulikia vilivyo matatizo yanayoisibu nchi, wachache tu kati yetu tumejiuliza kwanini kaamua kutumia dhana hiyo aliyoichagua kutatua matatizo yanayoikumba nchi Dr JPM ameamua kutumia dhana ya kutumbua majipu kama kiwakilishi cha utatuzi wa matatizo mazito, sugu na yaliyo kero kubwa kwa wananchi wa Tanzania. Wengi wetu tuliisikia kauli na dhana hiyo siku alipoongea na wabunge wa bunge wa la Jamhuri ya Muungano siku ya uzinduzi wa bunge.

Kupata jibu kwanini aliamua kutumia dhana hiyo, kuna njia kuu mbili; ya kwanza ni kumuuliza yeye mwenyewe ndugu JPM na ya pili ni kuutumikisha ubongo kufanya shughuli hiyo. Njia ya kwanza japokuwa ni fupi, nyepesi na inatoa jibu sahihi, si njia tunayoitamani. Hatuitaki njia hiyo kwakuwa haijengi uwezo wa kufikiria kwa namna sahihi. Ila hali njia ya pili ni ndefu, inashughulisha, inaimarisha uwezo wa ubongo, inakomaza uwezo wa ubunifu na kadhalika. Zaidi njia hii ya pili inachosha lakini hasa ndiyo tunapaswa kuifuata kwa kuwa inazalisha faida nyingi zaidi mbali ya jibu ambalo huenda lisiwe sahihi licha ya kutumia muda mrefu kulipata. Hiyo ndiyo hasa kazi ya falsafa; kujenga uwezo kuuliza maswali sahihi na kupitia njia sahihi za tafakari kujenga fikra sahihi ili hali ikiwa ni kutafuta UKWELI.

Tukirejea kwenye swali letu la msingi je kwanini JPM ametumia dhana ya kutumbua majipu? Ama ametoa wapi dhana hii? Katika falsafa na jinsi ninavyoamini pia kila kitu tumekipata maishani, ama tumekiishi sisi wenyewe, ama tumeona kwa wengine, ama tumesikia, ama kuhisi toka kwa wengine, ama kwa ufupisho huyapata mambo haya kupitia milango yetu ya fahamu za hisia (kuona, kusikia, kunusa, kuhisi na kuonja) haya ndiyo mafundisho ya wanafalsafa kadhaa wakiongozwa na Aristotle. Kwa upande wa wale wanaoongozwa na Plato; mwalimu wa Aristotle na mwanafunzi wa Socrates, wao wanaamini kuwa tuliishi sehemu nyingine kabla ya kuja hapa duniani na hivyo tulifahamu mambo yote huko tulikoishi. Hivyo mambo yote tunayofanya hivi sasa ikiwa ni pamoja na elimu ni juhudi tu za kujikumbusha tuliyoyaishi hapo kabla katika ukamilifu wa maisha. Unaweza kutumia mtazamo wowote kati ya hii miwili kupata jibu. Kwa Makala hii/haya twatumia mtazamo wa kiAristotle kupata jibu na hivyo ndugu JPM katumia dhana ya kutumbua majipu toka kwenye Hasina ya kumbukumbuu zake.
google image

Kwahiyo basi dhana ya kutumbua majipu ndugu JPM ama ameiishi yeye mwenyewe, ama kaishuhudia kwa mtu mwingine, ama alipata kusimuliwa juu ya dhana hiyo na mtu mwingine. Pengine kabla ya kuendelea tujiulize kwanza jipu ni nini? Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Dar es Salaam (TUKI), jipu ni uvimbe mkubwa unaotunga usaha. Na usaha ni ute wa rangi y manjano iliyopauka unaotunga aghalbu katika vidonda na majipu. Kamusi hii inaeleza tu maana ya jjipu na usaha. Lakini katika uhalisia wa maisha jipu ni adha inayousumbua mwili na kuufanya ufanye kazi zake kwa taabu. Zaidi uvimbe huu mara nyingi, bila shaka kuna sababu za kitabibu, huvimba maeneo yenye kumkosesha Amani na kumpatia binadamu usumbufu uliokithiri. Unaweza kukuta jipu limempata mtu kwenye makalio, mgongoni, sehemu zake za siri na kadhalika. Fikiria mtu mwenye kazi ya inayomlazimu kuketi muda mwingi, apatwe na jipu kwenye makalio…bila shaka unapata picha ya adha kubwa ndugu huyo atakayoipata.

google
Mtu huyo anahitaji matibabu ya haraka ili aendelee na kazi zake ili kutumia vipawa vyake,  kuitegemeza familia, jamaa zake, na taifa lake, kinyume na hapo familia jipu litamhangaisha na familia yake itaathirika, nchi itakosa mchango wake wa kimaendeleo. Kuepuka yote hayo mgonjwa anakwena hospitali kutumbuliwa jipu hilo. Kutumbua jipu hilo ni moja ya njia za kutibu uvimbe huo, nyingine inaweza kuwa vidonge vya kupunguza uvimbe na hatimaye kuisha. Kati ya njia hizi mbili, madaktari wanaweza kutujuza kama zipo njia nyinge murua zaidi yaa hizi mbili, ile ya kutumbua jipu ni bora zaidi kwa kuwa njia hii huasaidia kuondoa pia kiini cha jipu na hivyo kuzuia jipu hilo kuhamia sehemu nyingine ya mwili.

Hivyo basi utaona kuwa dhana ya Rais Magufuli ya kutumbua majipu imejengwa toka katika uhalisisa wa maisha yanayofahamika kwa watu wengi. Hivyo umithirishaji wa matatizo yanayoikumba jamii ya watanzania na tatizo la majipu mwilini ni dhana inayoeleweka kwa urahishi na hivyo inaweza kuimarisha na kuhamasisha uungwaji mkono na ushiriki wa watanzania wengi zaidi katika jitihada za kutumbua majipu (juhudi za kutatua matatizo yanayowaumiza wananchi na kubana fursa zao za kujiletea maendeleo). Kwa hiyo basi ndugu JPMagufuli huenda akawa anatumia dhana hiyo kwa kuwa anafahamu kero za majipu mwilini na jinsi ambavyo huwa kero kubwa na kubana fursa za mhanga kufanya shughuli zake za kila siku. 


Mandalu

Monday, December 28, 2015

MAISHA NI MALENGO




                                              Imepakuliwa hapa:https://www.youtube.com/watch?v=G23nC6i5jl8
Leo ni mwanzo wa juma jipya, mwezi mpya, mwanzo wa miezi mipya kumi na mbili ama maarufu zaidi mwaka mpya.

Mwanzoni mwa mwaka ni kipindi kizuri kufanya tathmini ya kile tulichokuwa tukikifanya kama hatukufanya hivyo mwishoni mwa mwaka. Ama yaweza kuwa fursa ya kuweka malengo mapya ama kuyapitia yaliyotangulia kwaajili ya muda mpya unaoanza mbele yetu.

Kufanya tathmini ama kujiwekea malengo katika maisha ni suala la msingi mno kama tunataka kuishi katika namna inayoeleweka na yenye tija na mchango katika dunia yetu. Lengo la maisha kwa kila binadamu awe anafahamu ama la ni kuwa na furaha maishani. Aristotle, mwanafalsafa wa kale anasema hivyo pia; ili mtu awe na furaha basi hana budi kujiwekea malengo. Malengo huwekwa na watu wa kila kada.

Mwalimu shuleni hujiwekea malengo yake, mwanafunzi, mwanasiasa, mwanamichezo, mwanasanaa, mwanauchumi, msomi, mwanazuoni, mwanasheria, mkufunzi, mfanyabiashara, mkulima, mchungaji kanisani, shehe msikitini, imamu sinagogini, na kadhalika…watu wote makini wa kada zote hujiwekea malengo maishani. Kutokuwa na malengo maishani ni mithili ya muuza duka bila daftari, ambapo twajua mali bila daftari hupotea bila habari. Maisha bila malengo hupotea bila taarifa.

Kujiwekea malengo ni utamaduni ambao inafaa watu wote tuwe nao. Kwa kusema hivyo nafahamu fika kuwa kuna ndugu wasio na mazoea ya kufanya hivyo; watu hao mara nyingine hufananishwa na bendera fuata upepo hufuata chochote kitakachokuwa mbele yao. Bila ubishi si utaratibu mzuri wa maisha. Kwa wasio na utaratibu huo ni wakati sawia kuuanzisha.

Dini nyingi hutueleza kuwa hapa duniani ni sehemu tu ya mpito - twapita tu na kwamba makao yetu halisi yapo kwa muumba wetu. Hivyo wakati tukiandika malengo yetu ya maisha ni vyema tukamshirikisha huyo muumbaji kwa kuwa sisi hatujui siku wala saa ya kuyahama makazi ya hapa duniani, japokuwa hatutakiwi kuogopa kifo.

Unapoandaa malengo fanya hivi:

Kwa wanandoa, ama watarajiwa, wawashirikishe wenzi wao. Malengo haya si yako peke yako. Kwa hiyo nafsi ya kwanza ni Mwenyezi Mungu na pili ni mwenzi wako wa maisha; mkeo, mumeo ama mchumba wako. Muombe(ni) Mungu ili awaangazie kufanya malengo ya kweli.

Hatua ya pili ni kuwa mkweli na hali yako halisi; weka malengo ambayo yana uhalisia wa maisha yako. Mfano haina maana kwako mwanafunzi wa Tanzania kuwa na lengo la kuwa rais wa Pakstani miaka mitano ijayo. Weka malengo ambayo kwa kiasi fulani una nafasi ya kuyatekeleza. Mfano kusoma kozi ya Kifaransa kwa undani mara baada ya kumaliza masomo yako mwezi wa Juni.

Weka malengo yenye kukujenga na yatakayohitaji juhudi zako kuyatimiza.

Usiogope kuwa na malengo mengi bora tu ni muhimu katika makuzi na utu wako, mwisho wa muda wa kuyatimiza utakapowadia utakuwa na wasaa wa kujitathmini na kujua wapi ulihitaji ama utahitaji juhudi zaidi. Mara nyingine tukiwa na malengo mengi na yenye kudai juhudi zetu zaidi ndipo ambapo huwa na mafanikio zaidi maishani.

Usiwe mtu wa kujihurumia; kuona kuwa malengo haya ni mengi na magumu mno siwezi kuyatimiza. Usishindwe kujaribu, jaribu kutenda na ukishindwa wakati ukitenda ni tofauti kabisa na ukishindwa kujaribu kufanya chochote.

Jiamini na usijilaumu. Fanya utakachoweza kwa juhudi zako na mambo yakienda kombo, bila shaka utapata fursa nyingine ya kutenda tena!



Kila la heri na Mungu akubariki!

Mandalu
01/01/2012

Wednesday, December 9, 2015

UHURU NA KAZI: KAZI YA TANU - KAZI YA MAGUFULI - KAZI YA WATANZANIA

Taken from Ndomi's Page
                                          Inapatikana hapa https://www.youtube.com/watch?v=b0Roj3MFrE4
Uhuru na kazi - Kazi ya Tanu. Maneno haya ama yanayofanana na haya yalikuwa ni moja ya salaam ambazo wananchi wa Tanganyika waliitumia kusabahiana mara baada ya uhuru. Bila shaka salaam hii ilitumika kutokana na umuhimu wa wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya haraka.

Ni utamaduni mzuri kukumbushana masuala ya msingi ili kuweza kufanikisha jambo ama mambo muhimu katika jamii. Kauli mbiu ya ndugu John Pombe Magufuli (JPM), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa kampeni zake za uchaguzi mkuu  mwaka huu alitumia kauli mbiu ya HAPA KAZI TU! Kwa jinsi mambo yanavyoonekana kauli mbiu hiyo inaendelea kutumika wakati huu wa utendaji kazi zake za urais.

Kiongozi ni mtu ambaye huonyesha njia kwa kutenda. Na tena kiongozi mzuri huwa mbunifu na mweledi ili hali akitenda kwa mujibu wa sheria mama ya nchi yake. Hivi karibuni ndugu JPM alitoa agizo la maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika kwa namna ya tofauti kabisa na miaka mingine iliyotangulia. Kwa kawaida nchini Tanzania maadhimisho haya hufanyika kwa gwaride la ukakamavu toka majeshi ya ulinzi na usalama, halaiki, ngoma mbalimbali na matumbuizo anuwai. Lakini agizo la JPM mwaka huu limekuwa kwamba maadhimisho ya sikukuu ya uhuru wa Tanganyika mwaka huu yafanyike kwa kufanya usafi maeneo mbalimbali zitolewapo huduma za kijamii.

Tumeshuhudia mwitikio mkubwa toka kwa wananchi waliojitokeza kufanya usafi katika maeneo mbalimbali. Ni jambo zuri wananchi kuitikia agizo hili ambalo pia limelenga kusaidia kupambana na ugonjwa wa kipindupindu. Moja ya sifa za kiogozi mzuri tuliona kwa ufupi ni kuonyesha njia kwa mfano; pichani hapo juu JPM anaonekana akishiriki kwa dhati kabisa katika kufanya usafi. Usafi huu ni muendelezo wa kauli mbiu ya HAPA KAZI TU!

HAPA KAZI TU! ni kauli mbiu nzuri inayofaa kutumika vyema na kwa undani zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Wakati kauli mbiu hii inahamasisha watu kutenda kazi, kuna watu wengine wengi hawana kazi na hivi kauli mbiu hii inakosa mantiki kwao. Hata hivyo kauli mbiu hii kama tulivyosema inatuhusu mno watanzania kwa kuwa nchi yetu bado ina uchumi duni. Hivi karibuni wadau wa HAKI ELIMU wametoa ripoti inayoelezea jinsi sekta ya elimu ilivyotenda ndani ya miaka kumi ya uongozi wa awamu ya nne.

Ripoti ya HakiElimu inasema awamu ya nne ilifanikiwa kwenye kuongeza idadi ya vitendea kazi katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya shule za msingi na pia za sekondari, vyumba vya madarasa, mtundu ya vyoo, maabara na kadhalika. Hata hivyo ubora wa elimu katika miaka hiyo kumi imekuwa duni. Kuna wanafunzi wamemaliza masomo pasi ya kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika. Hivyo ripoti hiyo inaisihi serikali ya awamu ya tano kuwekeza zaidi katika ubora wa elimu. Katika taarifa ya ripoti hiyo watoa mada walisema serikali ya awamu ya kwanza ilifanikiwa kwenye ubora wa elimu kwa kuwa waliweka falsafa ya kutolea elimu. Falsafa iliyotumika kipindi hicho ilikuwa ni elimu ya ujamaa na kujitegemea. Kupitia elimu hiyo wanafunzi walipata mafunzo anuwai wakati wakiwa shuleni. Mwanafunzi alipohitimu masomo yake aliondoka shuleni akiwa pia na ujuzi fulani ambao ungemwezesha kujiajiri ama kufanya kazi ndogo ndogo nyumbani kwao kulingana na fani aliyojifunza na hata aliposhindwa kuendelea na masomo tayari alikuwa na fani ya kuanzia maisha.
Makamu wa Rais aikishiriki zoezi la usafi katika eneo analoishi
Serikali ya awamu ya tano inayo nafasi pia ya kuboresha elimu kwa kauli mbiu ya hapa kazi tu. Kwa mantiki hii elimu yetu inafaa ibebe kauli mbiu hii ya kazi ambapo anaweza kufuata mbinu zilizotumika awamu ya kwanza. Hivi leo elimu yetu iwajengee wanafunzi wetu moyo wa kufanya kazi, iwapatie maarifa yanayohitajika na ambayo anaweza kuyatumia maarifa hayo ama kujiajiri, kuajiri wengine ama ayatumie atakapoajiriwa. Zaidi elimu yetu iwajengee vijana wetu uthubutu wa kutenda mambo, iwajengee uwezo wa kujiamini, iwasaidie kuibua na kuvifanyia kazi vipaji vyao ili wawe na uwezo wa kushindana katika soko la ajira. Ukitazama vizuri nchini mwetu utagundua kuwa kuna watu wengi toka nchi jirani katika nafasi zenye kulipa vizuri katika sekta binafsi kadhaa, sababu ya wageni kupata fursa hizo ni uwezo wa kujieleza kwa ufasaha katika lugha za kigeni hususani kiingereza. 
Waziri Mkuu akishiriki zoezi la usafi wa mazingira
Hivyo, wakati mjadala wa lugha ya kufundishia ukiendelea, wataalamu wa mitaala watazame mbinu za kuwezesha ufundishaji lugha mbali mbali kwa ufanisi. Ushahidi unaonyesha kuwa mwanafunzi anaweza kusoma vizuri na kumudu vyema kabisa lugha zaidi ya mbili. Ni dhahiri kuwa inatengemea pia kipaji cha mtu mmoja hadi mwingine lakini uwezo huo upo kwa binadamu na upo kwa mtanzania pia. Hivyo basi hapa kazi tu, Uhuru na kazi, kazi ya Magufuli, Kazii ya Mtanzania itakuwa na maana zaidi pale itakapowekwa katika falsafa ya kuongoza elimu yetu.

Mandalu Martin