Tuesday, November 24, 2015

MAGUFULI KURUDISHA "KATIBA YA WARIOBA?"


Ndugu John Pombe Magufuli
 Majuma machache tu toka kupata mkataba toka kwa wananchi wa Tanzania kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano, na ikiwa ni muda mfupi tu kisha kuapishwa kwake kuwatumikia wananchi, ndugu John Pombe Joseph Magufuli amefanya mambo kadhaa tofauti na ilivyokuwa imezoeleka huko nyuma.

Alichofanya ndugu JPJ Magufuli hakikinzani na katiba ya Jamhuri ya Muungano, na zaidi si kinyume na asili ya ubinadamu na kanuni za kimaumbile kwani hata Heraclitus mwanafalsafa wa kale wa Ugiriki anasema hakuna jambo la kudumu ila mabadiliko. Kwahiyo alichofanya kinaendena na kanuni za kifalsafa, ubinadamu na kanuni za kimaumbile; kila binadamu ni tofauti na wa kipekee mno na hivyo kila binadamu ana uwezo wa kufanya mambo ya kipekee na tofauti na wengine wote, hiyo ndiyo hulka sahihi ya binadamu anapokuwa na nafasi ya kujitawala.

Pamoja na mambo mengine aliyoyafanya ndugu rais, hapa hatulengi kuyaorodhesha, kusitisha safari ambazo hazina ulazima wala faida kubwa kwa taifa kwa viongozi wa serikali, kufanya mabadiliko ya matumizi ya pesa iliyokuwa imetengwa kwa sherehe za kuwapongeza wabunge na kwa kuzinduliwa rasmi kwa bunge la Tanzania. Mambo yote haya yanalenga kuongeza nidhamu ya matumizi ya pesa; hii ni stadi muhimu ambayo kila mmoja wetu inafaa ajifunze. Aidha kusitisha shamrashamra zilizozoeleka za 09/12 na badala yake kusheherekea siku hiyo ya uhuru wa Tanganyika kwa kushiriki kufanya usafi maeneo mbali mbali tunayoishi na kufanyia kazi ni jambo jema hasa. Ni dhahiri kuwa kipindu pindu hakitakwisha kwa usafi huo wa siku moja lakini agizo hilo limelenga mbali zaidi. Agizo hilo la ndugu rais linalenga mabadiliko ya tabia: jambo muhimu kwa mafanikio maishani.

Kasi ya utendaji kazi aliyoanza nayo rais Magufuli inapendeza na bila shaka tutarajie mabadiliko zaidi. Hata hivyo analazimika kuwa makini zaidi atakapokuwa “akifanya usajiri wa baraza lake la mawaziri” kwa lugha ya kisoka zaidi timu yake inafaa kuwa na wachezaji wenye viwango vya juu na wenye sifa mithili ya wachezaji wa kulipwa kama ilivyo kwa Samatta na Ulimwengu kwa TP Mazembe, Maguli kwa Stand Utd, Bocco kwa Azam, Martial, Roney kwa Man Utd, Ronaldo kwa Real Madrid, Messi, Neymar na Suarez kwa Barcelona na kadhalika na kadhalika.

Wakati wapenda maendeleo wengi wanaendelea kufurahia hatua za uchapakazi ndugu rais na hivyo kutoa pongezi kemkem kwake, nasi pia twaungana nao kumtia shime zaidi ndugu John Magufuli aendelee kufanya vyema na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu amlinde na kumuongoza zaidi. Hata hivyo tufahamu kuwa ndugu rais anatimiza wajibu wake kama kiongozi mkuu wa nchi mithili ya baba anayewajibika vyema kwa familia yake. Baba anayelipa ada kuwasomesha watoto wake katika shule ya viwango vya juu, anapotoa mahitaji stahiki kwa familia yake na kadhalika hapewi sifa na wala hapaswi kujisifu kwa vile anatimiza wajibu wake impasavyo. Pengine mazoea ya kuona baba wa jirani akikosa kuwajibika impasavyo kwa familia yake ndicho kinachosababisha kuona kuwa baba mtimiza wajibu anafanya mambo yasiyokuwa ya kawaida. Hivyo tufahamu na tumpatie ushirikiano ndugu rais aendelee kutimiza wajibu wake vizuri zaidi na zaidi.
Jaji Mstaafu Warioba
Wito wetu katika Makala hii/haya kwa rais Magufuli ni juu ya ama kujenga ama kuimarisha taasisi zetu. Taasisi zetu za uongozi inafaa ziwe imara na zenye mamlaka yaliyojitosheleza, zikiwa imara basi kiongozi yeyote akipata mkataba kuongoza nchi atalazimika kufanya kazi vizuri ama kwa utashi wake ama kwa kulazimishwa na taasisi hizo. Bila kuwa na taasisi imara utendaji kazi na uongozi utategemea hisani na hulka ya kiongozi aingiaye madarakani. Kiongozi mchapakazi na mzalendo “akiukwaa” mkataba kuongoza nchi mambo yatakwenda vyema na wanachi tutaona kama tunafanyiwa hisani ila hali akiingia kiongozi mwenye uzalendo hafifu na mwenyekujipenda yeye mwenyewe zaidi basi katika nchi tutashuhudia madudu. Hivyo basi ili tuepuke kucheza bahati nasibu ya uongozi ni vyema basi tukawa na taasisi imara. Taasisi hizo imara tunaweza kuzipata kwenye mabadiliko ya katiba yenye kushirikisha na kukubaliwa na wananchi walio wengi.


Bahati njema mabadiliko ya katiba yanayokubaliwa na wananchi tunayo kwenye chapisho la ‘katiba ya Warioba.’ Hivyo basi ndugu rais tunakuomba uturejeshee “katiba ya Warioba” ambayo itatufaa sana kwa dira ya taifa letu kwa miaka mingi ijayo.

1 comment:

  1. Kweli kabisa, tumuunge mkono ili azid kusonga mbele, tuweke itikad kando ILA HIYO KATIBA NDO KUBWA LA KUTUFANYA TUZID KUMHESHIMU, "KATIBA YA WARIOBA".

    ReplyDelete