Monday, October 5, 2015

SIKU YA WALIMU DUNIANI

PG4A3893
Picha kwa hisani ya dewjiblog.com
Leo ni Siku ya Walimu Duniani. Ni siku mahususi kuwapongeza walimu kwa mchango wao mkubwa kwenye sekta zote za ujuzi. Kila mtaalamu duniani amepata mafunzo toka kwa mwalimu wa aina moja ama nyingine. Hakuna ujuzi hivi hivi bila kupitia kwa mtu anayeitwa mwalimu; hata wenye mlengo wa ujuzi, ama kupata elimu bila kutumia milango mitano ya hisia, hawawezi kulikwepa hili. Kwa mujibu wa "rationalists" kuna mambo ambayo tunaweza kuyajua kwa hisia tu. Hata kwa wadau hawa, lazima warejeshe shukrani kwa wazazi wao kama walimu wa mwanzo kabisa na hata kwa muungano mzuri wa chembe chembe hai za ubongo wao. Hivyo kwa ufupi kabisa, hakuna ujuzi bila mwalimu.

Tunaposherehekea ama kukumbuka siku hii kuna mengi ya kujiuliza. Mswali machache tu hapa; hivi mwalimu ana mazingira gani ya kufundishia; mazingira hayo ni salama na rafiki kwake? Je, hivi mwalimu aliye nguzo kubwa kwa ujuzi anapata stahiki zake kama inavyotakiwa? Je, huyu ndugu ana furaha ya kweli anapoifanya kazi yake? Walimu kote duniani wanakumbwa na shida na misukosuko inayowafanya washindwe kutekeleza majukumu yao vilivyo. Matatizo ya walimu yapo kwenye nchi zilizoendelea na zinazoendelea pia.

Kwenye baadhi ya nchi zilizoendelea, mwalimu anakutana na shida kubwa ya utovu wa nidhamu na maadili mabovu ya wanafunzi. Na nafasi ya mwalimu kuwarekebisha watoto imebanwa kwa kutumia lugha ya haki za watoto. Mwalimu hana nafasi wala mamlaka ya kumwadhibu mtoto kwa kuwa ni kinyume na haki za binadamu. Waingereza wana msemo wao, usipomchapa mtoto utampoteza. Hii ni tafsiri huru. Lakini Waingereza wenyewe na nchi nyingine zilizopiga hatua kubwa zaidi kimandeleo zina shida kubwa ya utovu wa nidhamu katika kundi la vijana ambao wanalindwa na haki za binadamu. Haki za binadamu ni muhimu kwa ustawi wa jamii lakini maadili na adhabu kiasi toka kwa mwalimu muhimu. Najua suala la kiasi ni gumu kulipima. Walimu wanakumbana pia na tatizo la tishio la usalama toka wanafunzi wenye silaha.

Katika nchi zetu zinazoendelea shida za walimu zipo za"kutosha" pia. Ni hivi karibuni tu walimu wa nchini Kenya ndiyo wamemaliza mgogoro wao na serikali. Miezi michache iliyopita walikutana na matatizo ya ukosefu wa usalama eneo la mpakani na Somalia. Nchini Tanzania walimu wana shida zao pia. Si lengo langu kuziorodhesha hapa hivi leo. Bali katika ukurasa huu, kwa maneno machache tu ni kutaka kukumbushia haki za walimu, kuhimiza uboreshwaji wa mazingira ya kufanyia kazi ndugu hawa ili wapate kufanya kazi kwa juhudi na maarifa zaidi kadri ya vipawa vyao.

Wasalaam,

No comments:

Post a Comment