Thursday, October 16, 2014

Wasomi wahoji kwa nini Mwl Nyerere ahujumiwe? Ni katika Tuzo ya Nobeli, Ulaya watiliwa shaka

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
UTOAJI wa Tuzo maarufuna muhimu za Nobeli kwa watu mashuhuri na wenye mafanikio ya kipekee katika maendeleo na amani ya dunia umeanza kutiliwa shaka na baadhi ya wasomi barani Afrika, na hususan wanazuoni katika baadhi ya vyuo vikuu Kusini mwa Jangwa la Sahara, Raia Mwema, imebaini.
Mijadala ya chini chini imeanza kurindima miongoni mwa wanazuoni, wakihoji kulikoni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa kiungo katika ukomboni barani Afrika na hata kushiriki kuratibu harakati za vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, asipewe tuzo ya amani.
Wakati tayari tuzo hizo zimekwishatolewa kwa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, mwaka 2011, kwa kupigania haki za wanawake ili washiriki kujenga amani, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, mwaka 2001, Askofu Desmond Tutu na Nelson Mandela, hoja zimeanza kuibuka kwa nini si Mwalimu Nyerere?
Wasomi hao sasa wanakosoa tuzo hizo na kudai kwamba Mwalimu ananyimwa kwa sababu aliyapinga mataifa ya magharibi alipokuwa akiongoza harakati za kudai uhuru kusini mwa nchi za Afrika na akishiriki kuunganisha nchi hizo, sambamba na kutetea haki za binadamu, akiwa kiongozi aliyeishi kwa mfano mbele ya raia wake.
Wengi wanaamini Mwalimu ni kiongozi wa mfano katika kuthamini usawa wa binadamu jambo ambalo ndilo msingi wa amani ya dunia na kwa hiyo, alistahili kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobeli.
Tuzo hizo zilizoanzishwa na raia Norway, hutolewa na kutambulika kimataifa ili kuwapa heshima watu mashuhuri waliosaidia dunia katika nyanja mbalimbali za uchumi, amani, fasihi na masuala ya sayansi kama fizikia, kemia, hisabati na mengineyo.
Wahadhiri wakosoa
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), chuo ambacho Mwalimu alikianzisha na mara kwa mara kufika hapo kwa ajili ya mijadala na wanafunzi kuhusu uhuru na maendeleo ya Afrika na dunia kwa ujumla, Bashiru Alli, anaamini Mwalimu anastahili tuzo hiyo lakini ananyimwa kutokana na kuyaudhi mataifa ya magharibi wakati aliongoza harakati za kudai haki za binadamu na uhuru wa mataifa ya Afrika.
“Kuhusu maoni yangu juu ya namna baadhi media (vyombo vya habari), wanazuoni na watu mashuhuri wa nchi za magharibi wanavyopuuza mchango wa Mwalimu katika medani za mfumo wa siasa uchumi duniani na siasa za mahusiano ya kimataifa. Maoni yangu ni kwamba Mwalimu alikuwa mpinzani mkubwa wa mifumo yote kandamizi hususan mfumo dume, ukaburu na ubeberu.
“Upinzani wa Mwalimu dhidi ya mifumo hii ulimjengea heshima miongoni mwa wanyonge duniani kote, vile vile alikuwa na maadui wengi ingawa maadui wake hawakufanikiwa kuutoa uhai wake kama ilivyotokea kwa Patrice Lumumba wa Congo.
“Hata kama Mwalimu hakuwa mmoja wa washindi wa Nishani ya Amani ya Nobel kama vile Neslon Mandela, lakini mchango wake katika mapambano ya ukombozi hasa barani Afrika hauwezi kupuuzwa. Hata kama mchango huo wa Mwalimu hautangazwi sana na vyombo vingi vya habari vya magharibi au wasomi wengi wa nchi za Magharibi lakini maandishi yake, hotuba zake na msimamo wake dhidi ya dhuluma, unyonyaji na ukandamizji ni urithi usiokifani wa dunia. Sio rahisi urithi huu wa dunia hauwezi kupotea hivi hivi,” anasema Mhadhiri Bashiru Alli.
Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Stefano Moshi Memorial, Dk. Gaspar Mpehongwa, anasema vyombo habari vya nchi za magharibi havikuwahi kumpa nafasi Mwalimu Nyerere kwa sababu alikuwa “mwiba” kwa mataifa ya magharibi kutokana na hatua yake ya kukosoa kila mara, sera zao za kibepari na ukoloni mambo leo dhidi ya nchi masikini za dunia ya tatu.
Alisema kuwa sera za Mwalimu za Ujamaa na Kujitegemea ziliendana na zile za mataifa ya na nchi za kikomunisti za China na Urusi, hivyo mataifa ya Ulaya Magharibi yenye kufuata sera za kibepari na uchumi huria yalimtenga.
“Mwalimu alikuwa black listed na mataifa ya Ulaya Magharibi na Marekani kutokana na kuegemea zaidi katika siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na hata vyombo vyao vya habari havikuwahi kumsema vizuri,” alieleza Mhadhiri huyo.
Alisema Mwalimu Nyerere alipinga sera hizo hasa Shirika la Fedha la Dunia(IMF) na Benki ya Dunia (WB) taasisi ambazo zililenga kukandamiza nchi masikini hasa za dunia ya tatu, Tanzania miongoni.
“Kwa bahati nzuri pamoja na changamoto hiyo ya nchi za Ulaya Magharibi Mwalimu aliendelea kutambuliwa kama moja wa mashujaa wa Afrika ambao walipigania maslahi ya nchi zao mbele ya Jumuiya ya Kimataifa”
“Afrika iliheshimika sana wakati huo kutokana na kuwa na viongozi wenye mtazamo chanya katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa tofauti na viongozi wa sasa ambao huitikia na kucheza kila wimbo kutoka taasisi za Bretton Woods (mfumo wa kibiashara na kifedha wa mataifa makubwa),”aliongeza.
“Kwa mfano leo hata ukitaka uongozi wa umma vigezo vinavyotumika ni fedha badala ya uwezo wa mtu na tabia hii imesababisha kuwa na aina ya viongozi katika sekta za umma wanaojilimbikizia mali na madaraka,” alisema Mpehongwa.
“Na factor (kigezo) ya uongozi ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi angalia mfano nchi ndogo kama Uswisi imeendelea kutokana na uongozi thabiti lakini Tanzania yenye rasilimali nyingi kuliko Uswisi imeendelea kubaki kuwa moja ya nchi maskini na serikali yake inajiendesha kwa kutegemea hisani ya nchi za Ulaya,” alisema.
Kwa upande wake, Mwananahabari mkongwe na mwandishi wa vitabu nchini, ambaye baadhi ya vitabu alivyoandika ni pamoja na “Harakati za Nchi zilizo Mstari wa Mbele na Unyanyo wa Julius Nyerere,” Mkwabi Ng’wanakilala, anasema inawezekana kwa mfano, Nelson Mandela na Mwalimu Julius Nyerere walikuwa katika mizani tofauti ya kimtazamo na kwamba ndiyo sababu inayowafanya wapate heshima tofauti hasa kwa watu wa Magharibi.
Kwa upande wa Nelson Mandela, anasema, hali yake ilikuwa ngumu kwa sababu hakuwa anafukuza wakoloni isipokuwa alikuwa anapigania maslahi sawa ya Waafrika Kusini weusi dhidi ya makaburu, wakati kwa upande wa Nyerere kazi ilikuwa ni kuwafukuza wazungu waondoke Tanganyika.
“Mandela alionekana kama mtu ambaye hatakuwa na madhara makubwa kwa uwekezaji na maslahi ya wazungu na makaburu Afrika Kusini, walijua wanaweza kumpa anachotaka bila kupoteza chochote, na ndiyo hali inavyoonekana mpaka leo, Waafrika weusi bado wana hali ngumu kiuchumi kama ilivyokuwa wakati ubaguzi,” anaeleza.
Anafafanua kuwa pamoja na kwamba Mandela ni mpigania uhuru na ukombozi wa Afrika na amekaa jela miaka 27 kwa ajili ya kupigania ukombozi wa mtu mweusi, lakini ni kama nchi za Magharibi zilimtumia kimkakati kwa mantiki kwamba anaweza akawafanya wakaishi kwa amani kwa kuwa atakubalika na wote, weusi na makaburu.
“Hata ukiangalia release (kuachiwa toka jela) yake ni kama ilikuwa staged (ilipangwa kimkakati) ili kuweza kukidhi matakwa yao kutokana na shinikizo lilikuwapo wakati huo, na walipomwachia amekuwa Rais na haki za weusi kupiga kura na mambo mengine wamepata lakini kwa kweli bado kiuchumi hali haijabadilika sana ni kama ile ile tu” anasema.
Anasema kuwa huyu ni lazima asifiwe kwa kuwa ni mtu ambaye hana madhara makubwa sana kwao, kuendelea kumsifia ni kujihakikishia kuendelea kujiimarisha katika hali waliyo nayo tofauti na Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wa Mwalimu Nyerere anasema alikuwa anataka uhuru kamili katika nyanja zote, na alikuwa anawaambia ukweli bila kujali watamtafsiri vipi, na kwamba ilifikia kipindi wakaumuona kama mkomunisti lakini kimsingi hakuwa mkumnisti yeye alibaki kuwa mjamaa hata kama alikuwa na marafiki China na Cuba.
“Mwalimu kama ilivyokuwa kwa Nkrumah walitaka kuvunja vunja kabisa mizizi ya unyonyaji, wamchukia kwa sababu ya impact (matokeo) ya misimamo yake, he was very disturbing (alikuwa msumbufu sana) kwao, haikuwa rahisi kumfanyaia ujanja ujanja” alisema.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk. Charles Kitima, anasema kuwa Mwalimu Nyerere hawezi kuwa maarufu na kusifiwa na watu ambao aliongoza juhudi za kuwakatia mirija ya kunyonya rasilimali za Afrika.
Anasema Mwalimu Nyerere aliongoza juhudi za nchi zilizo mstari wa mbele kwa kuwaunganisha Waafrika kupinga aina zote za unyonyaji wa wakoloni na koloni mamboleo kitu ambacho hakikufurahiwa na wakubwa wengi wa Magharibi.
“Asingeweza kuwa maarufu kwa watu ambao aliwanyang’anya ulaji, kumbuka ni juhudi zake ndiyo ziliwaunganisha Waafrika nay eye akawa Mwenyekiti wan chi zilizo mstari wa mbele kuwapinga hawa,kwao mtu wa namna hi hawezi kuwa shujaa hata siku moja” alisema.
Anasema kwa Afrika kwa kiasi kikubwa inajitahidi kumkumbuka na kumuenzi ambapo sasa baadhi ya nchi kama Rwanda wana maadhimisho rasmi ya kumuenzi Mwalimu na Umoja wa Afrika umeanzisha Scholarship kwa heshima ya Mwalimu.
Mwalimu Nyerere African Union Sholarship Scheme imeanzishwa kwa ushirkiano na India kuwasomesha Wanafunzi wa Afrika katika vyuo mahiri Afrika, katika fani ya sayansi na teknolojia kwa ngazi za shahada, shahada za uzamili na uzamivu.
Chuo Kikuu cha Edinburgh ambako Mwalimu alichukua shahada yake ya uzamili mwaka 1949, kilianzisha The Julius Nyerere Master’s Scholarship mwaka 2009, kwa ajili ya wanafunzi wa Tanzania kusoma katika chuo hicho.
Dk. Kitima anasema kuwa sababu nyingine ambayo inafanya Mwalimu asipate heshima hiyo ni jinsi serikali inavyosimamia masuala ya msingi aliyoyaanzisha, kwamba udhaifu huo ndiyo unafanya hata watu wengine wasione mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Afrika huru.
Ameshauri ni muhimu serikali kurejesha somo la historia shuleni ili wanafunzi wajifunze historia ya nchi yao na kuwatambua mashujaa wao na hapo ndipo wanaweza kusimama kidete na kuitetea hadhi ya taifa lao.
Naye Mwanasheria Edward Lekaita alieleza kuwa mataifa ya magharibi pamoja na vyombo vya vya habari hayakuweza kutambua mchango wa Mwalimu kutokana na tabia yao ya kujali masuala yenye maslahi na mataifa yao.
“Vyombo vya habari vya magharibi siku zote ajenda yao kubwa ni kuandika habari zenye maslahi na mataifa yao hasa habari nyingi za mataifa masikini Afrika na yale ya Bara la Asia”
“Walikuwa double standard (ndimi mbili) katika masuala mengi ya msingi kwa mfano walitambua umuhimu wa Nelson Mandela baada ya kutoka gerezani na kuioongoza Afrika ya Kusini huru lakini kabla ya hapo walimtabua kama gaidi.”
Alisema Mwalimu na wenzake kama Nkwame Nkrumah wa Ghana, Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini, Lepold Senghor wa Senegal walijitahidi kuwaunganisha wananchi ili kuondoa ukoloni na ubaguzi katika nchi zao.
“Ni aibu mambo yanayofanyika sasa ni kinyume na dhamira iliyowasukama viongozi wetu wa zamani kupigani uhuru kutoka kwa wakoloni hata wakati mwingine kuhatarisha maisha yao”alisema.
Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Mbeya waliozungumza na mwandishi wetu wanamueleza Nyerere kama masikini jeuri, kwamba katika harakati zake za kupigania haki na utu kwa wanadamu wote hakujali mabavu ya mataifa makubwa wala uwezo wao mkubwa kifedha.
“Nyerere alikuwa masikini jeuri, alikataa kufanya biashara na Makaburu wa Afrika Kusini, hatua inayotugharimu hadi leo, lakini heshima ya msimamo wake tunavivunia hadi leo,” anasema mkazi wa jiji hilo, Newton Kyando.
Kyando anatoa mifano zaidi kuonyesha ujasiri wa Nyerere kupigania haki za wanyonge duniani, akikumbuka namna Mwalimu alivyokataa kuitambua serikali ya Mlowezi Ian Smith, alipojitangazia uhuru wa Zimbabwe, wakati huo ikijulikana kama Northern Rhodesia. Mbali na uamuzi huo, Nyerere akipata kuvunja uhusiano na Israel akipinga uonevu dhidi ya wananchi wa Palestine.
“Nyerere alivuka mipaka ya dini, alikuwa mkristo safi, tena mkatoliki, lakini alivunja uhusiano na Israel kupinga uonevu dhidi ya Wapalestina ambao wengi ni Waislamu, alichokizingatia yeye ni haki za wanyonge na utu wa mtu,” anasema Kyando kisha anaendelea akisema, “Pamoja na Chama cha ANC cha Afrika Kusini kilitangulia kuanzishwa, ilikuwa ni TANU iliyokijenga kufikia pale ilipofikia leo hadi kufanikiwa kupatikana kwa uhuru wa Afrika Kusini, na unapotaja TANU unamtaja Mwalimu Nyerere,” anasema Kyando.
Wananchi hao wanakumbuka pia mchango wa Mwalimu Nyerere kwenye medani ya kimataifa, ikiwamo kuwa msemaji wa “South South Commission,” pamoja na ukweli kwamba yalikuwamo mataifa makubwa na yenye nguvu za kiuchumi kama vile China na Indonesia.
“Alikuwa ni Mwalimu na Helmut Kohl wa Ujerumani Magharibi wakati huo, waliokuja na wazo la haki sawa ya kiuchumi kwa wote duniani, hivyo kunzaliwa kwa “International Economic Order.”
Marekani kinara Tuzo za Nobeli
Rekodi zinaonyesha kuwa Marekani ndiyo inayoongoza kwa kuwa na watu waliopata tuzo nyingi zaidi za Nobeli, wakifikia watu 334, ikifuatiwa na Uingereza tuzo 117, Ujerumani tuzo 102.
Katika Afrika, mbali ya Ellen Sirlef wa Liberia aliyechangia tuzo hiyo na mwenzake, Leymah Gbowee, wengine waliopewa tuzo hizo ni Wangari Maathai wa Kenya, Wole Soyinka wa Nigeria (katika fasihi mwaka 1986), Kofi Annan wa Ghana (katika amani-2001), Nelson Mandela na Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini. Misri pia imetwaa tuzo nne.



Tuesday, October 14, 2014

Nyerere kupata tuzo ya Nobel ya Amani Mwaka 2100

The Nobel Peace Prize Medal. Registered trademark of the Nobel Foundation. © ® The Nobel Foundation
Medali ya tuzo ya Nobel
Tuzo za Nobel ni maarufu zaidi katika orodha ya tuzo mbalimbali duniani. Tuzo hizo ambazo zilianza kutolewa mwaka 1901, ni matokeo ya wosia alioucha Mswidi Alfred Nobel (1833-1896) mwaka 1895. Alipofariki alikuwa na utajiri mkubwa ambao alipenda uwaendee watu waliotoa mchango katika ujenzi na uboreshaji wa maisha ya binadamu katika dunia yetu. 

Tuzo za Nobel zimegawanywa katika makundi sita; watu wenye kutoa mchango uliotukuka kwenye Fizikia, Kemia, Biolojia(Tiba), Riwaya (Uandishi), Uchumi na wale wenye kujishughulisha na masuala ya amani.Tuzo hizi hupewa mtu ama taasisi/ asasi yeyote iliyo/ aliyefanya kazi bora katika moja ya maeneo tajwa hapo juu lakini pia asiyepingana/isiyopingana walau wazi wazi na fikra za kibepari na asionekane tishio kwa mfumo huo wa maisha.

Tuzo hizi wamepokea watu toka takribani mabara yote duniani. Hapa naangazia, japo kwa ufupi tu, tuzo ya amani ya Nobel. Ukitazama orodha ya wapokea tuzo hiyo ya amani utaona wapo waume kwa wake, wenye kujishughulisha na kazi anuwai, watu wa imani tofauti, wazee kwa vijana. Na kijana mdogo zaidi kuliko wote kuwahi kupokea tuzo hiyo ni bi Malala Yousafzai (1997). Binti Yousafzai ameshinda tuzo hiyo pamoja na mwanaharakati mwingine kwa mchango wao katika kutetea/kupigania haki ya elimu kwa vijana.

Litania ya washindi wa tuzo hii ya amani ni ndefu na yenye majina makubwa. Kwa uchache utamkuta Martin Luther King JrMama Tereza wa Kalkuta, Elie Wiesel n.k. Afrika ina uwakilishi mkubwa ambapo nchi ya Afrika Kusini ikiwa imetoa watuzwa wengi zaidi barani humo. Kwa uchache tu kuna Albert Lithuli(1898-1967); mmoja wa marais wa ANC na Mwafrika wa kwanza kupata tuzo hiyo, Nelson Mandela (1918-2013), Desmond Tutu n.k. Afrika Mashariki yupo kwenye orodha hiyo hayati Wangari Maathai (1940-2011 ) mwanamke wa kwanza barani kupokea tuzo hiyo kwa mchango wake kwenye upandaji miti.

Julius Kambarage Nyerere (1922- 1999) kiongozi wa kwanza mzalendo wa Tanganyika huru na baadaye Tanzania, ni mmoja ya viongozi walioshiriki kujenga utu wa mtu duniani. Ushahidi wa mchango wake kutetea utu wa mwanadamu hususani binadamu mwafrika upo wa kutosha. Kwenye imani na kanuni za mwanaTANU, kanuni moja inasema binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja (sisemi kwa mpangilio kama ilivyo). Kiongozi huyu, kupitia sera ya chama na nchi yake, alijitoa kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa huru. Mchango wake ulikuwa mkubwa zaidi kwa nchi za kusini mwa bara hili la kitropiki, bara lenye kuandamwa na magonjwa ya kila namna ya asili na hata ya majaribio.

Sera za Tanganyika na baadaye Tanzania ziliruhusu wapigania uhuru wa nchi kadhaa za kusini mwa Afrika kuweka makazi yao na kufungua vituo vyao vya mafunzo nchini Tanzania. Mfano ni wapigania uhuru wa Afrika Kusini kule Morogoro, wapigania uhuru wa Msumbiji kule Mtwara na kadhalika. Zaidi wapigania uhuru na haki za watu kadhaa waliifanya Tanzania kuwa nyumbani kwao kwa namna moja ama nyingine ambapo walijipanga na kuweka mikakati ya ukombozi wa nchi zao. Unaweza kuwataja wachache tu hapa Laurent Kabila (1939-2001) wa Kongo-Kinshasa, John Garang (1945-2005) wa Sudan, Yoweri Museveni (1944) wa Uganda

Tanzania kwa miaka mingi imekuwa nyumbani kwa wakimbizi toka nchi mbalimbali zenye machafuko ya wenyewe kwa wenyewe.Tanzania na Zambia zinatajwa na mwandishi Crawford Young kwenye kitabu chake cha "The Postcolonial State in Africa: Fifty years of independence. 1960-2010" cha mwaka 2012, kuwa ni mataifa yenye makabila mengi lakini mataifa haya yameendelea kuwa ni nchi zenye amani na demokrasia. Nikiongelea AMANI ya Tanzania, pamoja na kwamba kuna tofauti lukuki kwa wananchi wake katika masuala ya imani, makabila na hivi karibuni itikadi tofauti za kisiasa, ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na viongozi wa mwanzo wa Tanganyika na baadaye Tanzania na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa miongoni mwao. Amani hiyo, pamoja na kuwa zawadi toka kwa Muumba, ilijengewa mazingira ya kustawi na viongozi hao wa mwanzo. Matumizi ya lugha moja - KISWAHILI, kwa taifa kubwa lililokuwa na vitaifa vingi (makabila) kabla na mara baada ya kupata uhuru, ni mbinu na mchango mkubwa uliostawisha na kuendelea kustawisha amani na mshikamano kwa Watanzania na pia kutoa hifadhi kwa binadamu wa mataifa mengine.

Mchango wa Tanzania kumfukuzilia mbali kiongozi wa mabavu wa zamani nchini Uganda Idi Amin Dada ilikuwa mchango mkubwa wa kazi ya amani kwa Tanzania, Uganda, Afrika na duniani kwa ujumla. 

Orodha hii inaweza kuwa ndefu zaidi, tukomee hapa kwa leo lakini tujiulize swali kwanini pamoja na mchango mkubwa amabao Tanzania imetoa katika masuala ya amani kwa ustawi wa binadamu nchi hii haijapewa zawadi hiyo na Nobel ya amani. Si kwamba bila tuzo hiyo maisha hayaendi la hasa, hata bila tuzo hiyo tunaendelea kuishi kwa mshikamano na udugu. Twauliza swali hilo kwa kuwa vigezo vinavyotumika kuwapima watu mbalimbali duniani inatakiwa ziwe kwenye mizani iliyo sawa.

Binadamu, kama ilivyo kwa maji huwa ana tabia ya kufuata mkondo katika maamuzi yake. Tanzania, kupitia Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wa zama zake, ilikuwa ikifuata mfumo wa ujamaa na kujitegemea. Mfumo huu si rafiki sana kwa nchi za magharibi na hivyo Norway na hususani wakfu wa Nobel hata kama wanakubaliana na mchango wa Mwalimu Julius Nyerere si rahisi kwao kutaka kujihusisha na nchi ama kiongozi mwenye kujitangaza hadharani kuwa ni mjamaa, mfumo wenye kupingwa kwa nguvu zote na Marekani, Uingereza na jumuiya za kibepari zenye "kuufadhili" wakfu huo.

Mwalimu Julius Nyerere, kwa mtazamo wangu kupitia mchango wake kutetea haki ya wanyonge kwa mfano wake wa kujinyima, anastahili kupata tuzo hiyo ya amani. Tatizo ni kizazi hiki za watoa tuzo hizo na "wafadhili wao" wana upofu kwenye masuala yenye kugusa ujamaa na upofu huo nadhani utakwisha 2099 karne moja baada ya kifo chake. Ila wahenga walinena vyema mno na ni vyema kufuata maelekezo yao: Tenda wema nenda zako...  

Martin Mandalu
Alice, 14/10/2014