Saturday, July 26, 2014

SOKO LA KIBEPARI NA PANDE ZAKE MBILI

Wachumi na wapiga debe wa “mfumo wa uchumi wa soko wenye ubinadamu” ( The market friendly approach ) [Tafsiri hii ni yangu binafsi ] ambao lengo lao ni kuona uchumi unakuwa, kupitia mabadiliko katika taasisi, kupunguza rushwa, na kuhakikisha maisha ya watu kupitia huduma muhimu kama afya, elimu, uhakika wa chakula na kadhalika yanakuwa bora zaidi. Njia hii ni mbadala wa njia zingine zilizotangualia (sitaki kuingia katika nadharia hii ya Neo-liberalism kwa ndani).

Nadharia hii yenye kulenga kupunguza umasikini inazishauri nchi “masikini” kushirikisha Serikali na sekta ya umma kukuza uchumi na kupambana na umasikini. Kwa hiyo wadau wakubwa wa kujenga uchumi na kupunguza umasikini katika jamii ni wadau hao wawili; serikali na sekta binafsi. Nadharia hiyo inashauri uchumi kwa kiasi kikubwa uendeshwe na sekta binafsi ilhali serikali iandae miundo mbinu na mazingira yenye kuiwezesha sekta binafsi katika shughuli za kujenga uchumi; lakini serikali inapewa jukumu na fursa ya kuirekebisha sekta hiyo binafsi yenye jukumu kubwa la kuzalisha uchumi. Kwahivi serikali kazi yeke kuu ni kusisimua, kuibua fursa, kujenga mazingira na kurekebisha wazalishaji pale wanapoelekea kupotoka.

Nadharia hii ina mashabiki na pia wapinzani wa kutosha tu: lengo la makala hii hata hivyo si kuichambua nadharia hii bali kuongelea kwa ufupi tu mfumo wa biashara nchini Afrika Kusini. Naongea kupitia uzoefu wangu wa miezi michache nchini Afrika Kusini; nitaandika kwa uhuru kama nilivyokuwa nikifanya wakati wa kuandika insha shule ya msingi hadi kidato cha kwanza. Tuliandika kwa uhuru mkubwa na kutumia vizuri zaidi hisia, kumbukumbu na uzoefu wetu. Hatukubanwa na takwimu, ambazo kwenye makala za baada ya shule ya msingi tumefundishwa kuwa ni muhimu na mara nyingine lazima. Sasa tuangalie biashara nchini Afrika kusini.

Afrika Kusini ina mfumo wa kipepari; uchumi wake kwa kiasi kikubwa unaendeshwa na soko. Natazama hapa soko la mahitaji ya kila siku ya binadamu. Moja ya sifa ya nchi za kibepari ni kuunganisha bidhaa za mashambani katika mfumo wa soko wa bidhaa za viwandani. Kwahiyo masoko yanakuwa na bidhaa za mashambani na viwandani hali kadhalika. Hivyo katika soko moja utakuta viatu, nguo na kadhalika [n.k] (bidhaa za viwandani), nyanya, maboga, mahindi mabichi, n.k (bidhaa za mashambani). Najua masoko yetu pia yanafanya hivyo ila kuna tofauti kubwa iliyopo kati ya masoko yetu Tanzania na ya Afrika Kusini [A.K].

Masoko nchini Afrika Kusini ambayo mengi ni mtandao wa wamiliki kadhaa wenye nguvu ya uchumi yamewekwa katika namna ambayo hupatikana katika miji karibu yote. Masoko hayo makubwa kwa kawaida hupatikana katika miji midogo, mikubwa na majiji. Eneo moja huweza kuwa na makampuni kadhaa ya kibiashara, kulingana na ukubwa wa mji na uchumi wa eneo husika. Kwa Tanzania mfano sahihi ni ule wa soko la Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Soko la Mlimani City, Dar es Salaam
Kama ilivyo kwa Mlimani City, Dar es Salaam, masoko ya A.K hujumuisha makampuni kadhaa ndani yake. Muhimu na kubwa zaidi ni kuwa masomo hayo, kwa kawaida, yameunganishwa na mfumo wa kibenki ambapo wateja wana uhuru wa kuingia na pesa taslimu ama kadi za benki zenye pesa ndani yake. Mteja huchagua bidhaa anazotaka na kulipia kwa njia iliyo muafaka kwake; kwa pesa taslimu ama kwa kuchanja kadi yake ya benki.

Kwa kawaida Masoko hayo huwa na umeme wa uhakika muda wote; kwa kuwa kuna bidhaa zenye kuhitaji majokofu. Nyama, Samaki, vinywaji mbalimbali n.k. Lakini pia mfumo wa malipo huhitaji umeme muda wote. Zaidi masoko haya ni chanzo kikubwa cha ajira; watu wengi hupata fursa za kufanya kazi za aina mbalimbali. Unaweza kuorodhesha nafasi chache tu hapa: wauzaji (wapokea pesa), wapanga bidhaa, wakagua bidhaa, wasukuma mikokoteni, n.k

Masoko ya A.K yana sifa nyingine muhimu ya kuwa na wateja wenye kupenda kufanya manunuzi (nadhani hii ni kutokana na uimara wa uchumi na aina ya utamaduni); wananchi wengi wana uwezo kununua bidhaa nyingi na kulipia kila bidhaa walioichagua. Utakumbuka mfumo wa soko wa aina hii unauza karibu kila kitu kinachohitajika katika matumizi ya mwanadamu. Wakati sehemu nyingi nchini Tanzania uchumi wetu unaruhusu mtu kujipatia mahitaji yake toka vyanzo vingine mbali na soko; mfano kwenye bustani yake atakula machungwa, maembe n.k, toka shambani kwake atakula viazi, mihogo n.k. Nchni A.K bidhaa nyingi kwa watu wengi hupatikana kwenye masoko hayo tu.

Ni utamaduni wenye uzuri na ubaya wake pia; si lengo langu kukugusa mada hii kwa undani hivi leo, lakini inafaa kusema chochote juu yake. Mfumo huu wa soko una faida lukuki lakini pia mapungufu hayakosekani. Nitaelezea jambo moja tu kwa kila upande uzuri na udhaifu wake.

Mfumo huu wa soko, ni njia ya uhakika ya ukusanyaji kodi. Serikali kupitia mamlaka zake husika hukusanya kodi kwa uhakika kabisa. Kodi, twafahamu ni muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote duniani. Ni kupitia kodi ndio serikali inapata nguvu ya kuwapatia wananchi wake hudumu za msingi kama hospitali, shule, n.k

Mfumo huu wa soko, kwa maoni yangu, una shida kwenye bidhaa za vyakula. Wahitaji wa bidhaa kadhaa mara nyingine ni wengi kuliko uzalishaji wa asili unavyoweza kumudu mahitaji ya wateja hao. Ili kukidhi mahitaji hayo basi ni lazima kutafuta njia ya uzalishaji ambayo ni ya bandia, matumizi ya teknolojia yanaingia hapo. Si kila jambo linalotumia teknolojia ni jema. Chukua uzalishaji wa mayai kwa njia ya asili. Kwa kawaida kuku anapotaga yai basi kwa siku ni yai moja tu. Lakini kuna watu wanakula zaidi ya yai moja kwa siku. Hivyo basi ili kukidhi haja ya walaji lakini na ili kupata faida haraka ni lazima teknolojia iingie kati na kuzalisha mayai mengi kwa siku moja. Mfano huu unaweza kutumika kwa bidhaa nyingine za vyakula. Mfumo huu unalzimu bidhaa nyingi za vyakula kuzalishwa kwa teknolojia. Hivyo bidhaa nyingi za vyakula zinakosa virutubisho na viini asilia ambavyo sehemu nyingi nchini Tanzania bado tunaendelea kuvifurahia…

Mambo mengi ndivyo yalivyo, kama sarafu, yana pande mbili…

Baadhi ya makampuni ya kibiashara nchini Afrika Kusini, ambayo baadhi yake hupatikana pia Afrika Mashariki ni pamoja na  Picnpay, Spar,Checkers, Shoprite, Pep, mrprice, edgers, kfc, lewis, steers, jetmart


Sunday, July 13, 2014

UBIDHAISHAJI WA MAUMBILE YA BINADAMU: Toka Sarah Baartman mpaka Agnes “Masogange” Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Picha kwa hisani ya mtandao

Picha ya Sarah Baartman 

Picha hii imetolewa kaatika blogu hii






Tunaishi katika zama mpya. Zama za ubepari uliochukua sura ya uliberali mamboleo. Ipo tofauti kati ya ubepari halisi na uliberali-mamboleo. Ubepari halisi ulijikita katika kutengeneza faida kwa kuzalisha bidhaa viwandani. Uliberali mamboleo ni ubepari wa kikasino. Katika zama za uliberali-mamboleo uzalishaji bidhaa siyo tena msingi wa ubepari

Upepari wa kikasino ni ule wa kutengeneza faida na kulimbikiza mtaji bila kujihusisha katika uzalishaji-mali. Uzalishaji-mali hufanyika mashambani na viwandani. Katika ubepari wa kikasino na kiporaji, mtu hutengeneza pesa kwa biashara za udalali, ununuaji na uuzaji hisa, ukopeshaji, kamari, upaishaji wa bei za vitu, n.k.

Katika uliberali mamboleo, ambao ni awamu ya ubepari uliofilisika, kila kitu hugeuzwa bidhaa na kuuzwa au kununulika sokoni. Huduma za jamii (afya, elimu, makazi na maji) hugeuzwa bidhaa na kuuzwa sokoni kama itokeavyo kwa manukato, nguo au magari. Ubidhaishaji umevuka mipaka, kiasi kwamba hata viumbe vinabidhaishwa. Katika makala haya nitazungumzia ubidhaifishaji wa muoneko wa viungo vya binadamu, hususun akinamama ufanyikao katika mfumo wa uliberali mamboleo.

Agnes Masogange
Jina la Agnes Gerald “Masogange” sio geni katika masikio ya Watanzania. Ni mwanadada mrembo. Lakini warembo wapo wengi. Masogange ni maarufu. Akina dada warembo na maarufu wapo wengi pia. Lakini umaarufu wa Masogange ni tofauti. Umaarufu wake umepatikana kutokana na anavyoonekana katika video za wanamuziki, na sehemu ya mwili wake inayompatia umaarufu ni makalio yake.

Mara kadhaa amekwishahojiwa naye akajisifia kuwa anajisikia raha kuwa na makalio makubwa: “Hakuna sehemu ninayoipenda kama makalio, yamekaa vizuri, nayapenda, najidai kupitia sehemu hiyo niliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu,” alisema Agnes katika moja ya mahojiano yake yaliyochapishwa Machi 29, 2014 katika blogu ya Global Publishers.

Ukiingia katika mtandao utaona picha na video za Masogange. Nyingi ya hizo zinaonyesha “sehemu hiyo aliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu”. Ameenda mbali hata kuweka picha na video zinazoonyesha utupu wake. Huko mtandaoni kuna wanaomlaani. Lakini hawa ni wachache. Wengi, hasa vijana, wanamsifia.

Lakini ole wako ewe msomaji mwema. Kama ulidhani kuwa makala haya yamelenga kumlaani ama kumsifia Masogange basi umekosea. Makala haya hayamzungumzii Masongange kama mtu bali yanazungumzia mfumo katili wa uliberali mamboleo. Nitatumia pia mfano wa “Masogange wa Kenya” aitwaye Vera Sidika. Afrika nzima kuna “akina Verana Masogange” wanaoibuka na kujizolea umaarufu na pesa. Huko Ulaya na Marekani idadi ya mabinti wa aina hiyo imekithiri. Katika kona mbalimbali za dunia, wapo mabinti wanaotamani kuwa na umbile kama la Vera Sidika au Masogange ili wawe maarufu na kujizolea pesa. Je, ni nini chanzo cha wimbi hili la ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu? Nani mwenye maslahi katika wimbi hili? Makala haya yamelenga kujibu maswali hayo.

Kwa kuanzia, ningependa kujadili kisa cha Sarah Baartman, bintiwa kiafrikaaliyezaliwa nchini Afrika Kusini mwaka 1789. Alifariki mwaka 1815, jijini Paris, Ufaransa, akiwa na umri wa miaka 26. Je, alifikaje Paris?

Sarah alikuwa mtumwa huko Afrika Kusini. Mmiliki wake mwenye asili ya kikaburu aliamua kumuuza kwa daktari wa kiingereza aliyeitwa Alexander Dunlop. Dunlop alikuwa ameona ‘fursa za kiuchumi’ katika umbilela Sarah, na hasa makalio yake makubwa. Hivyo akamshawishi mmiliki wa Sarah amwuzie “bidhaa” hiyo adimu ili akaitumie kutengeneza pesa huko Ulaya.

Sarah alipelekwa katika nchi kadhaa za Ulaya, hasa Uingereza na Ufaransa. Huko alipelekwa katika kumbi za maonyesho akiwa uchi, na wazungu wakawa wanalipa viingilio kuja kushuhudia weusi wa ngozi yake na ukubwa wa makalio yake na sehemu zake za siri.

Ili kutengeneza pesa zaidi, mmiliki wa Sarah akawa akimuuza kwa wanaume wa kizungu waliotaka “kumvumbua” zaidi mwanadada huyowa Kiafrika. Sarah akafariki kwa ugonjwa wa zinaa. Hata baada ya kufariki viungo vya mwili wake vilikatwa na kuwekwa katika makumbusho huko Paris ili wazungu wakajionee. Sarah aliendelea kuwa bidhaa na kivutio cha utalii hata baada ya kufa.

Tofauti ya Sarah na “ma-modo” wa sasa
Je, kuna tofauti kati ya Sarah na“mamodo” wa sasa?
Sarah aliishi katika kipindi ambacho biashara ya utumwa ilikuwa imeshika hatamu. Waafrika waligeuzwa bidhaa, wakauzwa na kununuliwa sokoni, kama vile mtu anunuavyo nyanya, nguo au kuku. Wakapelekwa huko Amerika kuzalisha mashambani na migodini. Nguvu-jasho ya Waafrika hawa ndiyo iliyozijenga na kuzistawisha nchi za Ulaya na Marekani ambazo leo tunakwenda kuomba misaada ya hali na mali.

Kwa hiyo, kama ilivyokuwa kwa babu na bibi zetu wengine waliopelekwa utumwani, Sarah hakwenda Ulaya kwa hiari yake. Alilazimishwa. Alikuwa ni bidhaa.
Usipofanya uchambuzi wa kina, unaweza kusema kuwa “ma-modo” wetu wa leo wanaotumia maumbo yao kama vivutio hufanya hivyo kwa hiyari yao. Lakini ukweli ni kwamba kuna nguvu ya kimfumo inayowalazimisha kufanya hivyo wafanyavyo. Nitajadili.

Maumbile ya Sarah yalikuwa ni ya asili. Mwili wake ni ule aliojaaliwa na Muumba. Katika zama zetu, wapo mamodo wenye maumbile ya asili. Lakini wapo wengi pia ambao wamelazimika kubadili maumbile yao. Ukuzaji wa makalio na matiti, uchubuaji wa ngozi, na hata ubadilishaji wa jinsia yamekuwa ni mambo ya kawaida.

Kiini macho na nguvu ya soko
Ukiingia mtandaoni, utakuta kampuni kadhaa zikitangaza bidhaa za kukuza makalio na matiti. Kwa wanaume, zipo dawa za kunenepesha na kurefusha uume, kukuza misuli, n.k. Kampuni hizi za kibepari ndizo kiini hasa cha ubidhaishaji waviungo vya binadamu, na hasa makalio na matiti. Ili bidhaa zao zikubalike, kampuni hizi sharti zitengeneze soko za bidhaa zao.

Soko lenyewe hutengenezwa kwa kubadili mtazamo na fikra zawatu, na hasa vijana, juu ya dhana ya urembo, mapenzi na mahusiano ya kimwili. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na kampuni za utengenezaji wa filamu za ngono, kampuni za kurekodi video za muziki, wamiliki wa vilabu na makasino, magazeti na televisheni za udaku, hospitali za binafsi za upasuaji wa plastiki, kampuni za uzalishaji wa dawa hizi zimewezesha kukubalika kwamba makalio na matiti makubwa ni urembo, lakini pia ni hazina murua kwa shughuli za ujasiriamali.

Kwa hiyo, katika zama zetu hizi binti mrembo anasemekana kuwa ni yule aliye na makalio makubwa, matiti makubwa, na ngozi nyeupe. Ikitokea hukuzaliwa na vitu hivi basi usikonde: utavipata kwa kutumia dawa au kwa kufanyiwa upasuaji wa plastiki. Binti mwenye sifa hizi anaaminishwa kuwa ana “rasilimali”ambayo anaweza kuitumia kutengeneza pesa iwe ni kwa kujiuza sokoni ama kwa kuwa na mpenzi mwenye pesa.

Hivyo basi, wapo wanenepeshao viungo vyao ili kuwaridhisha wapenzi wao. Wapo wafanyao hivyo ili “kwenda na wakati”. Lakini wengi pia hufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya soko. Soko lenyewe sio lazima liwe la kujiuza kimwili. Ni soko la kuuza “makalio”, watu wakayaona iwe ni katika klabu za usiku, magazeti ya udaku au video za muziki, na mwenye nayo akatengeneza pesa.

Tarehe 10 Februari 2011, gazeti la MailOnline la nchini Uingereza liliripoti kifo cha Claudia Aderotimi, mwanafunzi wa nchini Uingereza, aliyefariki huko Marekani akiwa ameenda kufanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio. Claudia, ambaye alikuwa na ndoto ya kuwa mnenguaji katika video za wanamuziki wakubwa, aliwahi kukosa tenda kwa kutokuwa na makalio makubwa. Aliambiwa kuwa ili afanikiwe ni lazima awe na makalio yaliyobinuka kama ya mwanamuziki Beyonce. Hivyo, mfumo tulio nao unawatengenezea mabinti kiini-macho (illusion) cha “kuwa na umbo kama la Beyonce ili ufanikiwe”.

Hapa Afrika, wapo akina-dada wachache ambao kutokana na maumbile yao, yawe ya asili ama “yaliyokarabatiwa” kwa dawa au upasuaji, waliofanikiwa kujipatia pesa, Maisha yao ni ghali: toka nguo wavaazo, manukato wajifukizayo, magari waendeshayo na kumbi za starehe waingiazo. Wengi wao huenda kufanya “shopping” Dubai au Afrika Kusini.

Vera Sidika: “Mwili wangu ni dili”
Katika kipindi cha The Trendkirushwacho na kituo cha NTV nchini Kenya, Vera Sidika,ambaye amejizolea umaarufu nchini Kenya kutokana na umbile la makalio yake, alisema kuwa huenda kufanya “shopping” ya kati ya dola 10,000 hadi 50,000 (yaani kati ya Tshs. milioni 16 hadi milioni 80). Viatu alivyokuwa amevaa siku hiyo vinaghatimu Tshs. milioni 5 na laki 6, na nywele zake za bandia ni Tshs. milioni 3 na laki 7.

Ngozi ya Vera sio ya asili. Ilichubuliwa kitaalamuna akawa mweupe. Vera anajitapa kuwa ubadilishaji wa rangi ya ngozi yake ulitumia zaidi ya shilingi milioni 15 za Kenya (takribani shilingi milioni 300 za Tanzania). Vera anasisitiza kuwa tangu apate ngozi nyeupe, kwake imekuwa “baraka”. Anatengeneza pesa zaidi, na anaalikwa nchi mbalimbali kwenda kusherehesha vilabu vya usiku (club hosting).
Vera anasema kwamba ukimwona klabu ujue amekwenda kutengeneza pesa. Hufanyaje hasa? “Huwa nasimama pale, na kutabasamu, na kupiga picha na mashabiki,” alifafanua. “Mwili wangu ni biashara yangu na ninautumia kutengeneza pesa,” Veera alijitapa.

Nyuma ya Vera, zipo kampuni za kurekodi video za muziki, wanamuziki, magazeti, redio, vituo vya televisheni, vilabu vya usiku, kampuni za kuzalisha kemikali za kubadili rangi ya ngozi, hospitali za binafsi zifanyazo uchubuaji wa ngozi, kampuni za vipodozi na mavazi ya kisasa, hoteli za kifahari, n.k. Wote hawa humtumia Vera kutengeneza faida.

Lakini tusisahau watu wa msingi wamfanyao binti huyu ajivune: hawa ni wale anaowaita “my fans”, yaani mashabiki wake. Kila siku Vera huweka picha za nusu uchi, zionyeshazo makalio yake, katika mtandao ili kukonga nyoyo za mashabiki wake. Aendapo Klabu hujiachia na kupiga nao picha za “ajabu” ili waendelee kumshabikia. Mashabiki hawa pia tayari wamekwishatekwa na mfumo, nao wakaamini juu ya urembo utokanao na kuwa na umbo kama la Vera.

Mtandao wa Kibiashara
Zipo nchi nyingi, mathalani Venezuela na Ufaransa, ambako ukuzaji-makalio na matiti vimetia fora kiasi cha wananchi kuzipigia serikali zao kelele ili zidhibiti vitendo hivyo. Lakini hii ni kazi bure kama tusipoelewa kiini cha tatizo lenyewe.

Gazeti la mtandaoni liitwalo “The Revolution” linalomilikiwa na cha Chama cha Kikomunisti cha Marekani liliwahi kufanya uchambuzi wa biashara ya upachikaji wa matiti ya bandia kwa wanawake. Nchini Uingereza pekee kati ya wanawake 20,000 hadi 30,000 hukuza matiti kwa njia hiyo kila mwaka, na biashara hiyo huingiza pato la zaidi ya dola milioni 150 (takribani shilingi bilioni 240 za kitanzania) kwa mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa plastiki nchini Marekani, idadi ya watu wanaojihusisha na upasuaji wa plastiki iwe ni katika kukuza au kupunguza makalio, matiti, nyusi, nywele, kubadili sura au ngozi, imeongezeka kutoka watu milioni 7.5 mwaka 2000 na kufikia watu milioni 14 mwaka 2011.

Jarida la “The Revolution” linaripoti kuwa kampuni za utengenezaji kemikali za ukuzaji matiti hutumia kemikali bandia ili kutengeneza faida zaidi. Moja ya kampuni hizo ni Poly Implant Prothese (PIP) ya nchini Ufaransa. Kutokana na madhara makubwa ya kiafya yasababishwayo na kemikali za PIP, baadhi ya nchi zimejaribu kuzipiga marufuku bidhaa za kampuni hizo bila mafanikio.

Maslahi ya kibiashara hayaishii katika kampuni tu. Ubidhaishaji wa huduma za afya umezifanya hospitali nyingi za binafsi zijiingize katika kazi ya upasuaji wa plastiki ili kukuza au kupunguza viungo vya mwili. Wateja waliopata madhara ya kiafya kutokana na kemikali za kukuza matiti na makalio wamekataliwa na hospitali zilizowapa huduma hizo. Wamiliki wa hospitali hizo, kwa mujibu wa jarida la The Revolution, “wanadai kuwa hawapashwi kuwajibishwa kutokana na kununua bidhaa zilizokuwa sokoni.”

Ubepari: toka uzalishaji hadi ubidhaishaji
Pengine cha kufikirisha ni kauli ya Vera kuwa “mwili wangu ni biashara yangu na ninautumia kutengeneza pesa”. Suala la kujiuliza ni kuwa, je, tangu lini mwili wa binadamu uligeuka kuwa bidhaa, hata ukatumika kutengeneza pesa?

Katika kitabu chake cha Das Kapital(Capitalau Mtaji) kilichochapishwa mwaka 1867, Karl Marx aliubainisha ubepari kama mfumo unaojitambulisha kupitia bidhaa. Lakini bidhaa hizo ni zile zinazozalishwa na nguvu ya binadamu na kupelekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa. Cha kushangaza ni kuwa watu hushikwa na wazimu wa bidhaa, wakazipenda na kuzithamini, lakini wasione kiini ndani ya bidhaa hizo. Kiini hicho ni nguvu-kazi ya binadamu iliyotumika kuzitengeneza. Marx alifariki mwaka 1883, yapata miongo saba baada ya Sarah kufariki. Kipindi alichoishi Marx kilikuwa ni kipindi cha ubepari wa uzalishaji bidhaa, viwandani na mashambani.
Takribani karne moja na nusu baada ya kuchapishwa kwa Das Kapital, Prof. Issa Shivji, mmoja wa wanazuoni wa Kimaksi, ameandika kuhusu ubepari wa karne ya 21, ambao umechukua sura ya uliberali mamboleo. Mfumo huu hautegemei tena uzalishaji, bali ubidhaishaji wa kila kitu.

Vitu ambavyo kwa asili yake haviwezi kuuzwa, hugeuzwa bidhaa na kuuzwa sokoni. “Utengenezaji wa bidhaa-sesere na zisizo za asili hauna mipaka katika mfumo wa uliberali-mamboleo,” anaandika Shivji katika kitabu chake kiitwacho Accumulation in an Afriacan Periphery. “Mazingira, ikolojia, na viumbe vingine wa asili (wanyama na mimea), viini vya kibaiolojia (ute wa mimea na viini-tete vya binadamu) hugeuzwa kuwa bidhaa, hali ambayo hutokea pia katika hisia na raha zihusishazo mahusiano ya kimwili. Juu ya vitu na mahusiano halisi hutengenezwa vitu-pepe na mahusiano-pepe, ambavyo pia hubidhaishwa. Katika ulimwengu wa mahusiano utaona mambo kama mabinti wa mtandaoni, vyumba vya faragha, na ufanyaji-mapenzi katika mtandao” (tafsiri yangu).

Kwa hiyo, tujifunzacho hapa ni kuwa mtandao wa watumiao miili ya vijana, na hasa wa kike, kutengeneza pesa ni mpana: vituo vya televisheni huwaalika katika mahojiano na kueneza udaku juu yao na kwa kufanya hivyo hutengeneza pesa, magazeti ya udaku hutengeneza pesa kwa kuchapisha picha na stori za mabinti hao, kampuni za utengenezaji wa kemikali za ukuzaji makalio/matiti na uchubuaji ngozi nazo hutengeza pesa, hospitali zijihusishazo na uchubuaji ngozi na upasuaji wa ukuzaji makalio hutengeneza pesa, na vilabu vya usiku viwaalikao mabinti hao navyo hutengeneza pesa, n.k. Huu ni mtandao mkubwa wa kutengeneza pesa katika zama hizi za utumwa mamboleo.

Kiini cha mtandao huuni mfumo wa uliberali mamboleo, ambao ni aina ya ubepari uliofilisika na uliochukua sura ya kikatili ya ubidhaishaji wa kila kitu, yakiwemo maumbile ya binadamu! Mfumo huu hauwezi kuwekewa viraka kwa kuhubiri juu ya maadili kwa vijana. Ni ama tuubomoe, au tuuache uendelee kutubomoa kwa kugeuza hata miili yetu kuwa bidhaa. Kama wapigania uhuru wa bara la Afrika walipambana dhidi ya ukoloni, sisi wajukuu wao hatupashwi kusalimu amri. Hatuna chaguo mbadala, ni jukumu letu sote kupambana dhidi ya uliberalimamboleo
Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.