Monday, May 19, 2014

TUZO ZA WASOMI BORA TANZANIA - MASUPA STAA WA ELIMU!

SUPA STAA WA MUZIKI
Hivi karibuni, huko jijini Dar es Salaam, kulikuwa na shangwe za tuzo kwa wasanii bora wa music mwaka 2013 nchini Tanzania maarufu kwa jina la “Kilimanjaro Tanzania Music Awards”. Naambiwa (sikuwepo ukumbini) kuwa sherehe hizo zilifana hasa. Lengo la mjumuiko huo lilikuwa kuwatambua na kuwatuza wanamuziki wa kitanzania wa muziki anuwai ndani ya Jamhuri ya Muungano na pia wa nje ya nchi; kulikuwa na kipengele cha mwanamuziki bora Afrika Mashariki. Yalipangwa makundi mbalimbali ya aina kwa aina kwa kadri ilivyoonekana inafaa kuwapanga wasanii hao. Ama kwa hakika mtenda kazi anastahili ujira wake!

Kimsingi muziki nchini Tanzania kwa kiasi kikubwa unatazamwa kama ajira ama shughuli ya vijana; hivyo ni sherehe za kutambua mchango wa vijana katika tasnia na sanaa ya muziki Tanzania. Baadhi ya vipengele ilikuwa ni pamoja na “Hip hop”, Zuku, Muziki laini, Taarabu na kadhalika. Kulikuwa na nafasi pia ya kuwatambua waandaaji muziki nchini. Washindi walikuwa wengi;  kwa uchache tu: Naseeb …. Ama Diamond; ambaye alitia fora kwa kupata tuzo nyingi zaidi, wengine ni Faridi Kubanda ama Fid Q, Judith Wambura ama Lady Jay D, MzeeYusufu, na wengine lukuki. Tunawapongeza sana wote waliochangia kuboresha Tasnia ya Muziki Tanzania; waliopata tuzo na hata wasiopata, kwani zawadi lazima ziwekwe mipaka ili kuleta maana; kila msanii akipata tuzo basi tunakosa maana ya ushindani. Wanaitwa wengi ilihali wanachaguliwa wachache!

Hata hivyo, wito wangu kwa vijana wa sanaa mbalimbali Tanzania, hususani wale wa muziki, wajifunze kutawala ala za muziki; jifunzeni kupiga muziki wa vyombo. Muziki wa vyombo una uhai mkubwa zaidi kuliko muziki wa maabara. Hiyo inathibitishwa na kazi za siku  nyingi za kina MbarakaMwishehe soma maisha ya Mwinshehe hapa, Marijani Rajabu, Sikinde bendi, OTTU bendi, Vijana Jazz, Mwenge Jazz na bendi nyingine nyingi za kale (hata kama hawakupata pesa nyingi kama vijana wa leo). Kazi zao zina umri mkubwa lakini zina ubora kwa maana ya ujumbe na melodi nzuri kuliko kazi  nyingi za hivi karibuni (zenye maisha mafupi mno). Ni kweli kabisa kila kitabu na zama zake! Lakini kuna vitabu vingine vipo zama zote. Hata hivyo kwa mara nyingine nawapongeza sana wanatasnia ya burudani nchini Tanzania kwa kutambua vipaji na mchango wa vipaji hivyo kwa urithi wa nchi, nikisema hivyo nageukia tasnia zingine nchini Tanzania.

Makala hii/haya yanahusu hasa TUZO ZA WASOMI BORA TANZANIA. Nimesubiri kusikia kutuzwa kwa wasomi bora nchini Tanzania kwa muda sasa; leo nimeamua kutoa dukuduku langu. Nimekuwa nikijiuliza hivi nchini kuna wasomi wanaofanya mambo yenye mchango wa maisha ya kila siku ya mtanzania na hivi wasomi hao kustahili kupewa tuzo? Sijapata jibu na nadhani swali hili linahitaji hadhira kubwa zaidi kuliko kichwa kimoja;kwani naamini penye wengi haliharibiki jambo!

Mara nyingine ninapokutana na kero kadhaa nchini huhisi pengine kweli hakuna wasomi wanaostahili kutuzwa. Hebu fikiria mfano Tanzania kukutwa na uhaba wa chakula. Foleni kubwa jijini Dar na kwingineko (japokuwa magari hayo hatutengenezi wenyewe), rushwa katika nyanja na huduma mbalimbali nchini, upungufu maadili katika jamii, kushuka viwango na ubora wa elimu, kuongezeka ubinafsi, mauaji ya vikongwe, albino na madhira na maovu mengine lukuki litania hiyo ni ndefu hasa…Wakati shida na maovu haya yanalisonga taifa; tuna wasomi wengi wenye ujuzi husika kulingana na matatizo tajwa na hata yasiyosemwa hapa, tuna rasilimali nyingi zinazohitajika kutatua matatizo tuliyonayo; pamoja na hayo yote tunaendelea kudidimia, ama ndo kama wahenga walivyonena? Penye miti mingi hapana wajenzi? (enzi hizo nyumba nyingi/ zote zikijengwa kwa miti). 

Nafahamu fika kuwa kuna wasomi wanaojituma na wametoa mapendekezo kupata ufumbuzi wa matatizo yanayolisonga taifa. Hata hivyo ushauri na ujumbe wao umepuuzwa. Poleni wale mliokutwa na kukatishwa tamaa huko. Hata hivyo nadhani haitoshi kutoa ushauri ukikataliwa na wenye mamlaka kumfanya msomi makini  akae kimya. Kukaa kimya ni mbaya mno; watu wema wakikaa kimya uovu unaongezeka, na watu wema hapa tunamaanisha wasomi jadidi. Msomi silaha yake kuu ni maandishi. Ndugu wasomi andikeni suluhu za matatizo yanayolisonga taifa ili nchi iwe na kumbukumbu ya suluhu hizo pengine wenye mamlaka kesho watayatumia.

Suluhu hizo zinaweza kuandikwa kwenye magazeti yanayosomwa na wananchi wengi, ama likaanzishwa jarida mahususi kwaajili hiyo. Nani atafanya kazi hiyo? Pengine hili ndo swali tunalojiuliza watu wengi. Sifahamu, nani alianzisha tuzo za wanasanaa Tanzania... Nchini Tanzania hivi sasa kuna vyuo vikuu lukuki, hii ni dalili nzuri ya kupata wasomi wengi. Chombo kinachosimamia ubora wa vyuo hivyo bila shaka wanaendelea kufanya kazi yao vizuri; ili tupate wasomi wengi na bora. Chombo hicho kinaweza kuanzisha jarida ambalo suluhu za matatizo nchini zinaweza kuandikwa humo; suluhu hizo zinaweza kutoka vyuo vikuu vilivyopo nchini na hata nje ya nchi, zinaweza pia kutoka kwa mtu yeyote ila tu zitasimamiwa na chombo chenye mamlaka juu ya vyuo vikuu. Jukumu hili tunapendekeza liende kwa chombo hicho kwa kuwa kazi ya vyuo vikuu pamoja na mambo mengine, kama alivyosema Mwalimu Julius K. Nyerere, ni kumsaidia binadamu aweze kuujenga ama kuuboresha zaidi uwezo wake wa kufikiria ili aweze kuleta suluhu kwa matatizo yanayomkabili binadamu (tafsiri isiyo rasmi na naweka maneno yangu zaidi). Kama msomi atatoa na ataandika suluhu ya kero iyao/zinazowakabili  binadamu wanaoishi Tanzania, na kweli suluhu hiyo ikafanya kazi, basi msomi huyu atastahili kutuzwa kama alivyotuzwa Diamond, Mzee Yusufu, Lady Jay D, Fid Q na wengine. Tanzania si kisiwa cha binadamu, na nd’o maana haitakuwa nchi ya kwanza kutoa zawadi kwa wanazuoni.


Tuzoza Nobel kwa magwiji wa Kemia, Fizia, Baiolojia ni maarufu duniani, kwa kuwa tupo duniani huenda suluhu zetu kwa matatizo yetu zikasaidia matatizo ya binadamu wengine hapa duniani. Naamini tuzo za wasomi nchini zitachochea kuibuka kwa ari mpya ya usomi, watu wakazunguka na kutambiana, bila majivuno, kwa kuwa wamesoma kitabu hiki na kitabu kile. Nilikuwa nikimsikia baba yangu anaongelea vitabu vya tamthilia ya Kiswahili maarufu kipindi hicho, Kikosi cha Kisasi, Kamlete akibisha mlipue, Simu ya Kifo, n.k. Nilimsikia baba yangu mzazi akitusimulia (watoto wake) hadithi za kusisimua toka kwenye Biblia Takatifu hadithi za kusisimua mfano simulizi ya kijiti kinachowaka bila kuteketea; bila shaka kuna wengine pia wamesimuliwa hadithi toka Kuruhani Tukufu na hiyo ikawajengea hamu ya kusoma Kuruhani ama Biblia ili kupata kujifunza mwenyewe na kukutana na simulizi nyingi zaidi mwenyewe. TUZO ZA WASOMI TANZANIA zitaamsha ari ya kupata "MASUPA STAA" wa elimu pia! Kwani kwa jinsi mambo yalivyo hivi sasa supa staa ni ama mwanamuzi, mwanafilamu, mrembo, mwingizaji na kadhalika, hukutani na masupa staa kwenye fizikia, kemia, baiolojia, geografia, uchumi, falsafa n.k inatakiwa tukutane na masupa staa wasomi pia! Wasalaaam!