Saturday, April 19, 2014

Vijana wa Kitanzania jijini Pretoria


Pretoria ni mji mkuu wa nchi ya Afrika Kusini. Ni mji wa shughuli muhimu nyingi za nchi hii iliyoendelea kwa kiasi kikubwa katika nyaja kadhaa za maisha ya mwanadamu. Mji huu una waAfrika Kusini weupe wengi zaidi kuliko weusi. Ndani ya mji huu ndo unakutana na balozi karibu zote zenye mahusiano na Afrika Kusini. Sina hakika sana, nimeambiwa kuna nchi zingine zina balozi zao kule Jo'berg, jambo hili haishangazi sana kila nchi hutazama maslahi yake. Kule Uganda nchi ya Misri ina ubalozi wake pale Jinja; bila shaka kwa lengo la kulinda maslahi yake kwa mto Nili, ambao ni uhai kwa Misri.



 Pretoria ni mji wenye mchanganyiko mkubwa wa watu toka mataifa mengi toka bara Afrika na kwingineko: kwa muda wa siku chache nimekutana na watu toka nchi kadhaa: Tanzania, Zimbabwe, Kenya, Burundi, Ethiopia, Somalia, DRC, Ethiopia, Msumbiji, Pakstani, Uchina, Afrika Kusini wenyewe n.k. Wengi wa hawa niliokutana nao ni vijana; mji huu pia umejaa vyuo lukuki vinavyoufanya mji upambwe na vijana zaidi. Hivyo mji umejaa mitindo ya kila aina; toka mavazi, nywele, milo, lugha, n.k.Japokuwa kuna lugha kadhaa zinaoongelewa katika mji huo, Kiingereza, kwa wageni, ndio hasa lugha kuu ya mawasiliano.

Mji huu wa Pretoria ni mji wa kibepari hasa; ni biashara muda wote- ni kuuza na kununua tu. Kila kitongoji kina maduka makubwa ya kibiashara, mithili ya Mlimani City kwa Dar es Salaam, Tanzania ila majengo haya ya biashara makubwa kupindukia. Maeneo haya ya biashara yamenishangaza, ukiacha mbali wanaofanya biasha hapa (hiyo ndo kazi na wapo kazini ), kuna watu wengi karibu muda wote, unajiuliza ni muda upi watu hawa huenda kufanya kazi zao. Wengi wa watu unaokutana nao ni vijana wakienda na kurudi, wakinunua na kuuza, wakila na kunywa...

Ukiacha vijana wanafunzi waliofika mjini hapo kufuata masomo, wapo wengi zaidi ambao wamefika kutafuta maisha kwa kufanya kazi. Hapo nd'o napokutana na vijana waozungumza kiswahili fasaha na unapodadisi ni vijana toka Tanzania, Kenya, Burundi n.k. Vijana kadhaa ambao nimekutana nao wanaweza kuongea kiingereza cha msingi kile tu amabacho kinawawezesha kueleweka japo kwa taabu. Nimekutana na kijana mmoja maeneo ya Sunny Park moja kati ya maeneo yaliyojaa vijana weusi wa kiafrika toka kona nyingi za bara hili. Kijana huyu mtanzania, anafanya kazi kwenye moja ya maduka ya mjini hapa. Huyu ni mjuzi wa teknohama- anaweledi mkubwa kwenye mambo hayo na tena anaoengea lugha ya kiingereza kwa ufasaha mkubwa kabisa. Ananivutia na katika usaili nagundua kuwa alisomea nchi ya jirani ambapo alipata fursa ya kumudu lugha ya kiingereza.

Kijana huyu, ambaye ni muwazi na mjuzi wa masuala kadhaa, ananieleza 'Pretoria kuna kazi nyingi sana tu, na vijana wengi toka nchi zinazoongea kiingereza huko kwao ndio hasa huchukua  nafasi hizi za ajira'. Vijana wengi wa kitanzania ananiambia, hawawezi kumudu kiingereza na hivyo kushindwa kuaminika na kufanya kazi na wenye mitaji. Vijana wa kitanzania wenye kuimudu lugha wana shughuli zao hata wameajiri wengine pia. Wapo wenye migahawa ambapo huandaa vyakula vyenye radha ya Afrika Mashariki, wapo madereva wa taksi, wapo vinyozi n.k. Bahati mbaya sana kuna kundi la vijana wa kitanzania na sehemu zingine wanaojishughulisha na biashara haramu ya dawa za kulevya- kundi hili linahitaji msaada!

Siku nyingine panapo fursa tutaangalia usafiri na usafirishaji jiji Pretoria.

1 comment:

  1. Thanks for sharing, nice post! Post really provice useful information!

    Giaonhan247 chuyên dịch vụ vận chuyển hàng đi mỹ cũng như dịch vụ ship hàng mỹ từ dịch vụ nhận mua hộ hàng mỹ từ trang ebay vn cùng với dịch vụ mua hàng amazon về VN uy tín, giá rẻ.

    ReplyDelete