Tuesday, January 31, 2012

Mgomo wa madaktari Tanzania

Baadhi ya matabibu na wauguzi wa hospitali ya
Muhimbili wakijadiliana mambo kadhaa picha kwa
hisani ya rfi Kiswahili

















Tunawapa pole wote wanaoathiriwa na mgomo huu!

Binadamu, kulingana na biolojia tunayoifahamu sisi wanadamu hivi leo, ndio mnyama mwenye ubongo mkubwa na wenye kufanya kazi vyema zaidi kuliko wanyama wengine. Bila shaka ukweli huu upo kwa lengo mahususi na si kwa bahati mbaya.

Binadamu mara tu anapozaliwa ana jukumu muhimu kwa dunia hii, hiyo ni moja kati ya sababu nyeti za uwepo wake hapa duniani - la raison d'être. Hali hiyo ni lazima kwa kila kilicho!

Hivyo basi, lazima tujiulize hivi nini hasa sababu ya uwepo na wajibu wa serikali kwa wananchi wake, ikiwa ni pamoja na madaktari? Nini sababu ya uwepo na wajibu wa madaktari hapa duniani?

Bila shaka kwa kutumia ubongo wenye uwezo mkubwa wa kupambanua magumu, tunaweza kupata suluhu ya tatizo hili...  

Sunday, January 29, 2012

KUSOMA VITABU KWAJENGA SANA


Hatimaye nimemaliza kusoma  "The Innocent Man"  cha John Grisham

Kitabu hiki kinajadili mambo mengi ya msingi mno kwa maisha ya binadamu. Mawili kati ya hayo ni; mosi jinsi ambavyo mfumo wa sheria, niruhusu kusema duniani, unavyoweza kuwa na mapungufu ya kutoa haki kwa binadamu, pili jinsi ambavyo watoa huduma wengine walivyo makini kuona haki inadhihirika na binadamu anatendewa haki katika mfumo wa sheria. Jambo la pili limenifurahisha sana!

Ni kitabu kizuri mno ambacho kinaweza kuamsha na kujenga moyo na usawasha wa kutenda mema katika jamii. Moyo wa kuona ukweli ukipatikana unaweza kuwa katika nyanja anuwai ama zote za maisha ya binadamu. Asante ndugu Grisham kwa kutushirikisha mawazo mazuri kabisa, huu ndo uzuri wa ubinadamu! 

Tuesday, January 17, 2012

DAWA BANDIA ZA MALARIA NI KIFO KWA AFRIKA...

Tabibu akitoa huduma kwa Mtoto mgonjwa wa malaria













Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la bidhaa nyingi bandia... karibu kila kitu unachonunua ni kama kuna mbadala wake ambao ni bandia. Hali hii imeonekana kuwa ni kitu cha kawaida na hali inayokubalika kimaisha. Hali hii la hasha haijakubalika kisheria, ambapo kuna nyaraka rasmi kwamba kuanzia sasa tuwe na bidhaa bandia, lakini kulingana na jinsi mambo yanavyokwenda basi tunaweza kusema ni hali iliyokubalika. Bidhaa bandia nyingi zinasemekana kutoka nchi za mashariki zinazoendelea kiuchumi.

Inasemekana kuwa katika nchi hizo za mashariki hususani Uchina; unaweza kutengenezewa bidhaa ya aina yoyote kulingana na uwezo wako wa kifedha. Tatizo hili linasababishwa na wafanyabiashara wenye uchu wa kujitajirisha haraka... utajiri si jambo baya ila utajiri kwa njia isiyo sahihi ni makosa. Lazima mambo haya ya bidhaa BANDIA TUYAKEMEE, na katika afya ni hatari zaidi.

Dawa bandia kwa hakika ni kifo kwa bara la Afrika, takwimu za shirika la afya duniani WHO linaonyesha kuwa Malaria ndo ugonjwa unaoongoza vifo vya watu wengi zaidi barani humo, bara linawekwa kwenye orodha za umasikini duniani. Kuzuka kwa wimbi la dawa bandia za ugonjwa huo unaoongoza kwa vifo barani ni sawa na kutoa hukumu ya kifo kwa waafrika hususani wale wenye kipato duni; sehemu kubwa ya Waafrika. Jambo la kusikitisha hapa ni kuwa hukumu hii inatolewa na ndugu zetu wa barani humu.

Wanaoingiza nchi dawa bandia za Malaria ni ndugu zetu waafrika, kwa hili tusimame pamoja tuwaambie acheni kuua ndugu zetu- wafanyabiashara wanaoingiza, wanaoagiza dawa bandia hawana utu na ni wauaji - waache kufanya hivyo!

Taarifa hizi zinapatikana pia kwenye wavuti wa Bbc Kiswahili

MZEE JANGALA AONGELEA SANAA

  Na Mwandishi wa BASATA
 Msanii Nguli wa sanaa za maonesho, Bakari Kassim
Mbelemba (Mzee Jangala) aikizungumza na
wadau wa sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa


Msanii nguli wa Sanaa za Maonesho, Bakari Kassim Mbelemba (Mzee Jangala) amesema kuwa programu ya Jukwaa la Sanaa inayoendeshwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ni chuo tosha kwa wasanii katika kuwapa elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali ya sekta ya Sanaa.

Akizungumza wiki hii, kwenye programu hiyo katika ukumbi wa BASATA, Ilala Sharif Shamba, Jangala alisema kuwa, Jukwaa la Sanaa ni jambo la kujivunia na ni chachu ya kukua kwa Sanaa.

“Jukwaa la Sanaa ni programu inayonifanya nithubutu kusema, sasa Sanaa ni kazi, maana kazi yoyote ili ifanywe kwa ufanisi inahitaji elimu, uratibu na mwongozo, hivyo wasanii tuitumie fursa hii adimu” Jangala alisema.

Aliongeza kuwa, programu hii imekuwa ikiwaleta wataalam na wadau mbalimbali wenye uzoefu katika sekta ya Sanaa hivyo, kwa wasanii ambao wamekuwa wakihudhuria toka mwanzo wamepata mambo mengi ambayo yatawasaidia katika kukuza na kuendeleza vipaji vyao.

Alisisitiza kuwa, Sanaa inabadilika na kumezwa na teknolojia mpya zinazokuwa zinajitokeza hivyo, ni lazima wasanii wajenge utamaduni wa kutafuta maarifa mapya na kuwa wabunifu huku wakizingatia maadili ya kitanzania.

Kuhusu wasanii kulewa umaarufu na sifa, alishauri kuwa ni vema wakabadilika na kufanya kazi zao kwa bidii na ubunifu zaidi kwani, sifa ya msanii inakuja yenyewe kutokana na kazi anazozalisha na kupeleka kwa jamii inayomzunguka.

“Sifa ya mpishi hutolewa na mlaji, kwa hiyo wasanii wanapotengeneza kazi zao wasijisifu wenyewe bali wasubili kusifiwa na msikilizaji au mtazamaji” alishauri Mzee Jangala.

Alizungumzia pia suala la wasanii kutegemea vipaji tu pasipo kuingia darasani na kusema kuwa hilo haliwezi kukuza sekta ya sanaa na badala yake tutakuwa na kazi zinazoandaliwa kwa msukumo wa soko na si taaluma ya Sanaa

“Wasanii ni lazima watambue kuwa, mbolea ya kipaji chochote kile ni elimu. Ni vigumu sana kutegemea kipaji tu pasipo kukipalilia kwa taaluma ya sanaa husika”

Kwa upande wake, kaimu mwenyekiti wa Jukwaa la Sanaa, Vivian Nsao Shalua alishauri wasanii kulitumia Jukwaa la Sanaa ili kuzijua sheria, taratibu na mbinu mbalimbali zitakazo waongoza katika shughuli zao za Sanaa.

Wednesday, January 11, 2012

MAVAZI YA AIBU YALALAMIKIWA

Picha toka mtandaoni
imepakuliwa hapa https://www.youtube.com/watch?v=wxBwsU9u6vw
Picha kwa hisani ya google
                                                                                                                                                          
Wafaransa wana msemo wao, "L'habit ne fait pas le moine" unaotafsiriwa kwa kiingereza "Clothes don't make the man" ama kwa tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi, "si mavazi yanayofanya mtu kuwa mtu".



Hapo kale tumesoma katika historia ya kuwa wazazi wetu wa kale walijisitiri tu sehemu zao za utupu na kuwa hiyo ilikuwa ni namna yao ya maisha na hakukuwa na shida yoyote. Unaweza pia kuona katika filamu ya "the gods must be crazy " Mavazi ni kwaajili ya binadamu na si vinginevyo.

Hivi karibuni jamii zetu zimekuwa na muingiliano na jamii zingine na zimepiga hatua kubwa katika nyanja anuwai ikiwa ni pamoja na kwenye suala la mavazi. Binadamu ameona ni vyema akajivika mavazi yenye heshima na yenye kumpendeza.






Picha hii kwa hisani ya
blogu la haki za binadamu
Lakini muingiliano huo haukuishia tu kwenye mambo mazuri ya kujifunza kumekuwa na mambo yasiyo ya kupendeza kwa jamii. Kuna aina ya mavazi ambayo humuacha kiumbe akiwa karibu nusu uchi, ni kweli kwamba si mavazi yanayomfanya mtu kuwa mtu, lakini ni vyema kukubaliana na kile jamii inachotaka. Jamii ya leo Tanzania inahitaji mavazi yenye kusitiri vyema maungo, basi natufanye hivyo.

Kutoka Dodoma Mwandishi wa Tanzania Daima anaandika zaidi

BAADHI ya wakazi wa mji wa Dodoma wamesema kuwa wanakerwa na tabia ya baadhi ya wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu wanaovalia mavazi ambayo yanaonyesha maungo yao na hivyo kuleta aibu kwa jamii.

Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, walisema kuwa tabia za wasomi hao haziendani na jinsi jamii inavyowachukulia kwani badala ya wao kuwa kioo kwa jamii wamegeuka kuwa chukizo.

Mmoja wa wakazi hao, Twaha Kivale, alisema kuwa kwa sasa mavazi ambayo yanavaliwa na wanavyuo hususan wa kike katika mkoa wa Dodoma ni ya aibu na yanaleta picha mbaya kwa wadogo wao wa elimu ya chini kama vile shule za msingi na sekondari.

“Tunategemea kuwaona wasomi wakiwa na tabia njema lakini cha kushangaza wasomi hao wanavaa nguo mbaya ambazo zinaonyesha maumbile yao ya ndani, hii ni sawa na kutembea uchi bila aibu tena mchana.

Tunashindwa kutofautisha wasomi na makahaba kutokana na mambo ambayo yanafanyika, kama kweli wasomi ambao tunawategemea kuongoza nchi wanavaa hivi kinyume kabisa na maadili yetu kuna maana gani ya kuelimika,” alihoji Kivalle.

Naye, mchungaji Evance Lucas wa Kanisa la EAGT, Siloam Ipagala, akizungumzia suala hilo alisema kuwa kitendo cha baadhi ya wanafunzi wa kike kuvaa nguo hizo ni mpango kamili wa shetani.

Alisema kuwa kwa sasa shetani anawatumia sana watu ambao wanaonekana kuwa wasomi na wasipoweza kujitambua ni wazi kuwa watajikuta wakishindwa kufikia malengo ambayo wameyakusidia.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, katika hilo alisema kuwa hata yeye anakerwa na tabia hiyo ambayo kimsingi inadhalilisha utu wa mwanamke.

Dk. Nchimbi alisema pamoja na kuwa mji wa Dodoma una vyuo vikuu vingi na kuonekana kama sehemu ya maendeleo lakini kwa sasa hali ni mbaya kwani zimekuwepo tabia ambazo zinatia aibu katika jamii.

Hata hivyo alisema ili kuondokana na tabia hiyo kunatakiwa kuwepo kwa ushirikiano mkubwa kati ya viongozi wa dini na serikali ili kuhakikisha tabia ya namna hiyo inakomeshwa.

Naye mwanachuo mmoja wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambaye hakutaka kutaja jina lake, alipoulizwa alisema kuwa mavazi ni hiari ya mtu na kuongeza kuwa licha ya wananchi kulalamika bado wataona mambo mengi kwani kila mtu ana uhuru wa kuvaa atakavyo.

Kwa sasa katika mkoa wa Dodoma kuna vyuo vya elimu ya juu vya Udom, St.Johns, Chuo cha Mipango na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).










Tuesday, January 10, 2012

BASATA YAONYA MAPROMOTA WABABAISHAJI

Na Mwandishi wa BASATA
Mkurugenzi Idara ya Ukuzaji Sanaa BASATA, Vivian Nsao Shalua
   akizungumza na wadau wa Sanaa katika Jukwa la Sanaa linalofanyika
kila wiki makao makuu ya Baraza hilo. Kulia ni Afisa Habari wa
BASATA Aristide Kwizela.


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewaonya wakuzaji sanaa nchini kuacha mara moja ubabaishaji wanapokuwa wanaendesha matukio na matamasha mbalimbali ya Sanaa.

Onyo hilo limetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa wa Baraza hilo, Vivian Nsao Shalua wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kwenye ukumbi wa BASATA uliopo Ilala Sharifu Shamba.

Shalua alisema kuwa, Mapromota wamekuwa wakiwarubuni wasanii kwa kuwafanyisha kazi zisizo na mikataba huku wao wakinufaika na kuwaacha wasanii wakishindwa kujikwamua kimaisha.

“Utaratibu uliopo sasa kila mdau yeyote anapoandaa tamasha au tukio lolote linalohusisha wasanii lazima aje na mikataba na wasanii hao, aoneshe uwezo wake kifedha katika kuendesha tukio lakini pia awe na kamati inayoeleweka ya uendeshaji” alisisitiza Shalua.

Aidha, aliongeza kuwa, kumekuwa na ukiukwaji kanuni na taratibu za uendeshaji matukio hayo ambapo Baraza limekuwa likiwapa onyo na kuwafungia wahusika lakini akasisitiza kuwa, njia pekee ya kuepuka hali hii ni kwa mapromota kufuata taratibu zilizopo.

Akizungumzia kuhusu suala la mikataba, aliwataka Wasanii kuhakikisha hawashiriki tukio au onyesho bila kuwa na mkataba na waandaaji kwani hali hiyo inawafanya wadhulumiwe na kushindwa kudai haki zao kwa mujibu wa makubaliano.

“Ni lazima sasa wasanii wadai mikataba. Sisi tunawabana wakuzaji sanaa (mapromota) kuambatanisha mikataba yao kabla hatujawapa kibali lakini lazima na wasanii waoneshe wajibu wao kwa kudai mikataba na kutoshiriki maonyesho bila makubaliano ya maandishi” alionya Shalua.

Alisisitiza kuwa, Baraza litakuwa makini katika kufuatilia wadau wanaopewa vibali vya kuendesha matamasha na matukio mbalimbali ya Sanaa na mara taratibu na kanuni zitakapokiukwa halitasita kuchukua hatua za makusudi.

Wednesday, January 4, 2012

Masomo Zaidi...?

Elimu haina mwisho ndivyo usemavyo mmoja wa semi za wahenga wetu.
Kujiendeleza kielimu ni muhimu kabisa kwa wale wenye kupenda kufanya hivyo.

Mtandao wa Advance Africa lengo lao kuu ni kufanya hivyo; hebu sasa wale wenye moyo na nia ya kufanya hivyo wasome zaidi hapa. Bonyeza hapa

Mbinu za kazi tofauti malengo yaleyale - safi sana!


    

Sunday, January 1, 2012

MAISHA NI MALENGO

Leo ni mwanzo wa juma jipya, mwezi mpya, mwanzo wa miezi mipya kumi na mbili ama maarufu zaidi mwaka mpya.

Mwanzoni mwa mwaka ni kipindi kizuri kufanya tathmini ya kile tulichokuwa tukikifanya kama hatukufanya hivyo mwishoni mwa mwaka. Ama yaweza kuwa fursa ya kuweka malengo mapya ama kuyapitia yaliyotangulia kwaajili ya muda mpya unaoanza mbele yetu.

Kufanya tathmini ama kujiwekea malengo katika maisha ni suala la msingi mno kama tunataka kuishi katika namna inayoeleweka na yenye tija na mchango katika dunia yetu. Lengo la maisha kwa kila binadamu awe anafahamu ama la ni kuwa na furaha maishani. Aristotle, mwanafalsafa wa kale anasema hivyo pia; ili mtu awe na furaha basi hana budi kujiwekea malengo. Malengo huwekwa na watu wa kila kada.

Mwalimu shuleni hujiwekea malengo yake, mwanafunzi, mwanasiasa, mwanamichezo, mwanasanaa, mwanauchumi, msomi, mwanazuoni, mwanasheria, mkufunzi, mfanyabiashara, mkulima, mchungaji kanisani, shehe msikitini, imamu sinagogini, na kadhalika…watu wote makini wa kada zote hujiwekea malengo maishani. Kutokuwa na malengo maishani ni mithili ya muuza duka bila daftari, ambapo twajua mali bila daftari hupotea bila habari. Maisha bila malengo hupotea bila taarifa.

Kujiwekea malengo ni utamaduni ambao inafaa watu wote tuwe nao. Kwa kusema hivyo nafahamu fika kuwa kuna ndugu wasio na mazoea ya kufanya hivyo; watu hao mara nyingine hufananishwa na bendera fuata upepo hufuata chochote kitakachokuwa mbele yao. Bila ubishi si utaratibu mzuri wa maisha. Kwa wasio na utaratibu huo ni wakati sawia kuuanzisha.

Dini nyingi hutueleza kuwa hapa duniani ni sehemu tu ya mpito - twapita tu na kwamba makao yetu halisi yapo kwa muumba wetu. Hivyo wakati tukiandika malengo yetu ya maisha ni vyema tukamshirikisha huyo muumbaji kwa kuwa sisi hatujui siku wala saa ya kuyahama makazi ya hapa duniani, japokuwa hatutakiwi kuogopa kifo.

Unapoandaa malengo fanya hivi:

Kwa wanandoa, ama watarajiwa, wawashirikishe wenzi wao. Malengo haya si yako peke yako. Kwa hiyo nafsi ya kwanza ni Mwenyezi Mungu na pili ni mwenzi wako wa maisha; mkeo, mumeo ama mchumba wako. Muombe(ni) Mungu ili awaangazie kufanya malengo ya kweli.

Hatua ya pili ni kuwa mkweli na hali yako halisi; weka malengo ambayo yana uhalisia wa maisha yako. Mfano haina maana kwako mwanafunzi wa Tanzania kuwa na lengo la kuwa rais wa Pakstani miaka mitano ijayo. Weka malengo ambayo kwa kiasi fulani una nafasi ya kuyatekeleza. Mfano kusoma kozi ya Kifaransa kwa undani mara baada ya kumaliza masomo yako mwezi wa Juni.

Weka malengo yenye kukujenga na yatakayohitaji juhudi zako kuyatimiza.

Usiogope kuwa na malengo mengi bora tu ni muhimu katika makuzi na utu wako, mwisho wa muda wa kuyatimiza utakapowadia utakuwa na wasaa wa kujitathmini na kujua wapi ulihitaji ama utahitaji juhudi zaidi. Mara nyingine tukiwa na malengo mengi na yenye kudai juhudi zetu zaidi ndipo ambapo huwa na mafanikio zaidi maishani.

Usiwe mtu wa kujihurumia; kuona kuwa malengo haya ni mengi na magumu mno siwezi kuyatimiza. Usishindwe kujaribu, jaribu kutenda na ukishindwa wakati ukitenda ni tofauti kabisa na ukishindwa kujaribu kufanya chochote.

Jiamini na usijilaumu. Fanya utakachoweza kwa juhudi zako na mambo yakienda kombo, bila shaka utapata fursa nyingine ya kutenda tena!



Kila la heri na Mungu akubariki!

Mandalu
01/01/2012