Wednesday, May 30, 2012

BASATA YAWATAKA WASANII KUONGEZA THAMANI KATIKA KAZI ZAO



Na Mwandishi wa BASATA

Huku kukiwa na juhudi za kutambuliwa na kuthaminiwa kazi za wasanii ndani na nje ya nchi, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kuongeza thamani kwenye kazi zao ili kuzipa ubora zaidi.

Wito huo umetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari wa BASATA Godfrey Lebejo wakati akihitimisha programu maalum iliyohusu Ubunifu, Utengenezaji na Uongezaji thamani katika Kazi za Sanaa kupitia Jukwaa la Sanaa.

Alisema kuwa, ubora katika Sanaa unapatikana pia kwa Wasanii kuangalia wenzao wanafanya nini na wao kupata ubunifu mpya kwa kuongeza vionjo, uthamani na ubunifu binafsi katika kuifanya kazi ya Sanaa kwanza kupendwa na baadaye kupewa thamani kubwa sokoni.

“Ni wazi Wasanii wetu wanapaswa kuzingatia uongezaji uthamani kwenye kazi wanazozifanya. Kubuni kazi ni suala moja lakini kuongeza uthamani katika kazi yako ili ivutie wengi na kuuzika kwa thamani kubwa ni suala lingine la kuzingatia” alisistiza Lebejo.

Aliongeza kuwa, kwa sasa kuna taarifa za Wakenya kununua kazi za Wasanii wetu kwa bei ya chini na baadaye kuziongezea ubunifu, thamani na kuziuza nje kwa bei kubwa. Katika hili anasema, inatokana na wasanii wetu kutokuzingatia falsafa hiyo ya ubunifu na uongezaji thamani wa kazi zao.

“Tuna bahati ya kuwa na malighafi nyingi sana, baadhi zimeoneshwa hapa lakini suala hapa ni sisi kutumia ipasavyo malighafi hizo katika kubuni kazi zenye ubora na kuhakikisha tunazipa thamani stahiki tunapozisafirisha nje” alizidi kusisitiza.

Awali akiendesha darasa hilo maalum ambalo wiki hii lilikuwa mahsusi kwa ajili ya wasanii na wajasiriamali wa Sanaa za mikono (Handcrafts), Haroun Sabili kutoka asasi ya Musoma Handcraft alisema kuwa, Sanaa hizo zinahitaji ubunifu na umakini mkubwa kwani kinyume chake ni kutokuvutia na kupoteza uthamani.

Alitoa wito kwa Wasanii kujiunga katika vikundi na kuwa rasmi ili kuhakikisha kwanza,wanajenga mazingira ya kuwezeshwa lakini pia kupata mafunzo mbalimbali ambayo yatawafanya wazalishe kazi za Sanaa zenye ubora na thamani kubwa.

“Ni ngumu sana kuhudumia msanii mmoja-mmoja lakini mkiwa kwenye umoja ni rahisi sana kupata fursa za uwezeshaji hususan mafunzo katika kuongeza ubunifu na uthamani wa kazi zenu” alishauri Haroun.

Katika programu hiyo iliyohudhuriwa na wadau 72, elimu kuhusu ubunifu na uongezaji thamani kwenye kazi za Sanaa ilitolewa sambamba na malighafi mbalimbali na jinsi zinavyoweza kutumika kuzalisha kazi za mikono kuoneshwa.

Tuesday, May 22, 2012

NAFASI ZA MASOMO ZAIDI (UZAMILI)

Nchini Tanzania, idadi ya vyuo vikuu imeogezeka kutoka chuo kikuu kimoja tu cha umma mwaka 1961 hadi kufikia zaidi ya vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 60 mwaka 2012. Takwimu hizi ni kulingana na kitabu cha mwongozo wa kuomba nafasi za masomo vyuo vikuu toka mamlaka ya kudhibiti vyuo vikuu nchini TCU.

Kuongezeka huko kwa vyuo vikuu nchini pamoja na kuja kutokana na sheria ya kuruhusu vyuo hivyo, imekuja hasa baada ya kuonekana mahitaji dhahiri nchini. Idadi ya watu, hususani wanafunzi imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Makadirio yanaonyesha kuwa kuna zaidi ya wananchi milioni arobaini hapa Tanzania, na wengi kati ya watanzania hao ni vijana. Na zaidi, kuanzishwa kwa shule nyingi za kata, japo nyingi zingali duni kiubora, kumeongeza idadi ya vijana wenye uhitaji wa elimu ya chuo kikuu. Na ukweli huo unapatikana kwa uwazi zaidi katika malengo ya kimaendeleo ya Tanzania 2025; kwamba kufikia wakati huo watanzania wengi wawe wamefikia daraja la kati.

Elimu ni njia ya uhakika ya kumuweka mtanzania wa kawaida kwenye daraja la kati kuliko njia nyingine nyingi zinazofahamika. Kwa mantiki hiyo inafaa zaidi watanzania wengi wapate elimu yenye lengo la kuwakomboa, kifikra na kiujuzi na hatimaye waelimike kwa lengo la kuwasaidia kwa maana ya kuwatumikia wananchi wenzao wengi.

Kwa mantiki hiyo vijana ama wanafunzi wengi wanahitajika kujikita vyema katika masomo wanayoyafanya, wabobee kwa uhakika hasa. Wanaokwenda kazi wakafanye kazi kwa bidii na ujuzi zaidi wanaotaka kuendelea na masomo zaidi wafanye vivyo hivyo kwa bidii bobevu. Hapa ni nafasi moja kwa wanaopenda kuendelea na masomo zaidi. Wasome hapa kuna nafasi za kutoa udhamini kwenye masomo ya juu zaidi. Udhamini wa masomo - Sholarship hapa...