Thursday, April 26, 2012

MASHINDANO YA SU-SAUT KATIKA PICHA

Kikundi cha uhamasishaji STEMMUCO
Mashabiki katika mduara wa sherehe
Mchezo baina ya STEMMUCO NA JUCO UKIENDELEA
Mashabiki wa STEMMUCO wakishangilia ushindi wa timu yao


                                                                                                                                  
   
                                                        

                          

Wednesday, April 25, 2012

Siku ya Malaria Duniani

Ugonjwa wa malaria ambao ni wakitropiki, unaendelea kuuwa watu wengi duniani na hasa barani Afrika hususani kusini mwa jangwa la Sahara. Ungonjwa huu ambao inasemekana umekuwa ukimsumbua binadamu kwa zaidi ya miaka 50'000 ni tishio kwa afya za Waafrika wengi.

Malaria huuwa zaidi kina mama na watoto
picha hii kwa hisani ya blogu hili
Asilimia 90% ya vifo vyote vya malaria hutokea barani mwetu, ambapo asilimia sitini ya vifo vyote huwa ni watoto wadogo chini ya miaka mitano. Mara nyingi malaria huambatanishwa na umasikini, na huenda ukawa moja ya vyanzo vya umasikini barani. Kuhusiswa huko na umasikini ni kutokana familia nyingi barani kushindwa kumudu manunuzi ya dawa za kuzuia maambukizi lakini pia mara nyingine kukosa uelewa wa namna ya kujikinga hususani vijijini na mijini kwenye familia zenye elimu na kipato cha kadri ama chini .
Chandarua chaweza kuzuia maambukizi
Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia chandarua kilichotiwa dawa ya kuua mbu na wadudu wengine, kusafisha vyema mazingira ya maeneo tunayoishi ili kuharibu mazalia ya mbu, kukausha na kuondoa maji yote yaliyotuama. na kadhalika.

Ugonjwa wa malaria unazuilika na inawezekana kufanya hivyo kama usemavyo ujumbe wa kataa Malaria. Na ukweli huu umedhihirika huko Zanzibar na Zambia ambapo katika ripoti za hivi karibuni, ugonjwa huo umedhibitiwa kwa asilimia zaidi ya hamsini.

Kwa kumbukumbu ya siku hii tujihadhari zaidi na kuhadharisha wenzetu wawe makini na ugonjwa huu unaoendelea kuuwa binadamu wengi zaidi mithiri ya vita.  

Taarifa za Malaria zaidi zinaweza kupatikana katika blogu hii pia. na katika blogu la unicef, who nk




Sunday, April 22, 2012

JE UMEANDIKA NINI?

Kipanya kikitoa huduma ya usafiri kwa umma. Picha toka blogu

















Hivi karibuni nilikuwa kwenye basi dogo la usafiri wa umma daladala; toka Mtwara kwenda Mikindani. Usafiri maarufu kwa daladala za Mtwara ni vipanya; vibasi vidogo vidogo ambavyo nadhani vingi ni mitumba toka Dar es Salaam. Vipanya vingi mjini hapa vimechoka na vinakwenda kwa mwendo wa kusuasua vinapokuwa barabarani. Hakuna mabasi makubwa mithili ya yale ya Mwenge Posta kwa Dar es Salaam, pamoja na hayo ule udaladala upo pale pale. Daladala ama vipanya hivi vinajaza kama ilivyo ada ya daladala sehemu nyingi Tanzania. Hapo juu nimegusia Mikindani; huu ni mji mkongwe, mji wa zamani ambao kwa bahati mbaya umesahaulika, hauendelezwi tena. Pengine kwa kuwa neema ya gesi mjini hapa imefunguliwa basi mambo huenda yakawa sawia  kwa mji huu wa kihistoria.Sasa nirejee kwenye mada ya makala hii.

Mikindani chakavu, picha na blobu ya wadau wa safari


















Katika kipanya nilichokuwa abiria, utakumbuka kuwa kwenye daladala huwa kuna mada nyingi, kondakta wetu alikuwa muongeaji kupindukia. Kodakta, konda ndivyo wanavyofahamika zaidi, huyu hatofautiani na wengi walio mikoa mingine; ni kijana aliyevalia sare chakavu ya kazi na ambapo kama walivyo wengi wao suruali yake ilikuwa ikining'inia zaiki kuliko kuvaliwa, namna hiyo ya kuvalia huitwa na vijana wa leo "kata k". Koda yule katika utani na abiria mmoja ndani ya daladala letu, ambaye nadhani ni shwahiba wake kwa jinsi walivyokuwa wameshibana kwa simulizi za kutosha bila shaka kwa lengo la kufupisha safari. Basi yule konda alimtupia rafiki yake swali ambalo hasa nd'o linabeba kichwa habari cha mada hii, hivi wewe toka umalize shule ya msingi umeandika chochote kweli?
Hivi wewe umeandika chochote kweli? Kwa hakika hili ni swali dogo sana na lategemea uzito ambao mtu ataamua kulitilia mkazo. Lakini ni jambo kubwa na muhimu sana pia. Mtu anayeandika kwa kawaida ni mtu anayesoma pia. Kwa hivi swali la konda lauliza pia, je, umesoma nini hivi karibuni? Sina hakika kama yeye mwenyewe ameandika ama amesoma chochote hivi karibuni. Tafiti na ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa moyo na tabia ya kujisomea kwa watu wengi imepotea ama inapotea kwa kasi kubwa . Hapo zamani ilikuwa ni lazima kuandika barua ili kujua nini kinaendelea nyumbani kwa wazazi wako walio mbali nawe, siku hizi inatosha kuweka salio katika simu ya mkoni, simu hizo karibu kila mmoja anayo yake; hii ni moja ya sekta ambazo Tanzania imepiga hatua kubwa sana, na kuanza kuongea. Anayejua kuandika ataongea kama asiyejua kuandika halikadhalika. Kukua kwa tekinolojia ya habari nako kwa kiasi kikubwa kinachangia kushuka kwa moyo wa kuandika na kusoma kama hapo awali. Hivi leo hata zile huduma za kibenki ambazo humlazimu mtumiaji kuandika japo sentensi mbili tatu zinafanywa kwa wepesi na urahisi kabisa kupitia simu ya mkononi hata na mtu asiyejua kusoma na kuandika ila tu masuala ya lazima hususani yahusuyo pesa. Maendeleo ya tekinolojia ya habari ni muhimu lakini tuendelee kujifunza kusoma na kuandika.

Hivi wewe umeandika chochote toka uhitimu elimu ya msingi, sekondari, chuo kikuu, toka upate udaktari wa falsafa?Swali hili la konda mhitimu wa darasa la saba lamgusa kila mmoja wetu toka wale wa shule ya msingi hadi madaktari wasiotimu watu ila falsafa. Nchini Tanzania pamoja na juhudi nyingi za wasomi wetu mahitaji ya vitabu vya mafunzo mbalimbali bado ni vichache; tunaendelea kutumia vitabu toka ng'ambo. Hili si jambo jema hata chembe.

Wito kwa kila mmoja wetu tuongeze muda wa kusoma vitabu zaidi na kufanya hivyo tutapata hamu na ujumbe wa kuandika chochote kitu kwa lengo la kuielimisha jamii, ambalo ni jukumu la kila mmoja wetu.

Monday, April 16, 2012

MANENO MAKALI HAYAVUNJI MFUPA

The image by the courtesy of Google
                                   
"The smallest deed is better than the greatest intention." John Burrough.
Maneno Makali hayavunji mfupa!

Wazo hili nimelipata katika mtandao wa advance Africa. Mtandao ambao siku zote hutoa kwa wahitaji fursa za masomo na kazi zaidi . Mtandao huu ni nyenzo nzuri wa vijana walio masomoni na wanaotarajia kumaliza masomo yao na kujiunga na ulimwengu wa kazi.

Mtandao huu huonyesha fursa za kazi kwenye nchi mabalimbali ikiwa ni pamoja na ughaibuni. Kwanza nieleweke vyema kuwa jambo muhimu kwa mwenye kuweza kulifanyia kazi, ni mtu binafsi kujiajiri ni vyema akafanya hivyo japokuwa si vibaya kama atafanya kazi sehemu nyingine kwanza ili apate mtaji wa kuanzisha shughuli zake binafsi. Kwa wale wanaopenda kufanya kazi za kuajiriwa, wanaweza pia kufikiria kazi za hapa nchini na pia zile za kimataifa. Vijana wetu wafahamu kuwa kazi hizo zipo pia kwaajili yao si tu kwa watu wa mataifa mengine. Hata hivyo ili kuweza kupata fursa hizo ni vyema kuzingatia masuala kadhaa yenye umuhimu usio kifani. Weledi, uaminifu, kujiamini na kujituma, ujuzi wa lugha za kigeni, utayari kuishi katika tamaduni mchanganyiko na kadhalika.

Weledi ni kigezo cha uhakika kwa mtu kufanya kazi popote apendapo. Weledi ni msamiati ulioibuka hivi karibuni ukimaanisha ujuzi na uwezo wa kufanya kazi. Wanachuo ama mtu yeyote anayetaka kufanya kazi ni vyema awe na ujuzi wa kile anachotaka kufanya hii ni muhimu hasa. Hapa linaibuka swali la mtu anapata vipi uwezo na ujuzi wa kazi ili hali ndo kwanza anatoka masoni? Swali hili lafaa kujibiwa na fursa za kujitolea; vijana wanafunzi, wanavyuo tujenge utamaduni wa kujitolea kufanya kazi katika makampuni, mashirika na hata kati taasisi za kidini ili mradi kuwe na fursa ya kujijenga katika utendaji kazi na hapo hakutakuwa na ukosefu wa ujuzi.

Uaminifu; ni moja ya mahitaji muhimu katika ulimwengu wa kazi na ujasiriamali. Katika ulimwengu wa mtaji jamii "social capital" uaminifu ni suala la lazima katika mafanikio, ili ufanikiwe ni lazima uwe na mtandao mkubwa na mpana, huwezi kupata mtandao mkubwa vile kama wewe si mwaminifu. Kwa hivi basi ni lazima kujifunza kuwa mwaminifu. Tunu ya uaminifu ni moja kati ya zawadi amabazo watu wengi hujifunza toka katika familia zetu; huwatazama wazazi wetu jinsi wanavyoishi na hii hurithi toka kwao. Hata hivyo kulingana na uwezo mkubwa wa ubongo wa binadamu; unaweza kujifunza kila kitu mradi tu upatiwe mazingira na kuwe na nia na ulazima wa kufanya hivyo.

Kujiamini na kujituma; hivi ni vigezo muhimu katika mafanikio. Ili uweze kufanya jambo fulani ni lazima kwanza wewe mwenyewe ujiamini kuwa unaweza kulifanya, lakini kujiamini peke yake haitoshi ni lazima kujituma katika kile unachonuia kukifanya. Tunu hivi mbili ukiziweka pamoja basi una uhakika wa kufanikiwa. Msemo wa Kiswahili Penye nia pana njia unafaa uwe kielelezo na mwongozo katika malengo yako maishani.

Ujuzi wa lugha za kigeni; hiki ni kitendea kazi muhimu hasa hususani katika zama zetu za utandawazi. Katika nyakati hizi watu wengi zaidi husafiri, kufanya hivyo kuna walazimu kujifunza lugha kadhaa. Wewe huna sababu ya kutojifunza lugha muhimu za maitaifa mengine hasa zile zenye ushawishi kwa mataifa mengi. Unaweza kujifunza na kutawala vyema zaidi Kiingereza, Kifaransa, Kispanyola, na sasa kwa sababu za kiuchumi, watu wanajifunza kichina. Ujuzi wa lugha nyingi utakufanya uwe mshindani mkubwa na kujitofautisha na hata wale waliofanya kazi siku nyingi.

Utayari kuishi katika tamaduni mchanganyiko; binadamu sisi ni wamoja kwa namna zote muhimu. Binadamu ana undwa kwa chembe hai ndogo ndogo ambazo ni sawa kwa kila binadamu, ana mifumo kadhaa ambayo hufanya kazi sawa sawa na kadhalika. Hata hivyo tamaduni, mazingira, makuzi n.k huleta tofauti tulizonazo katika jamii za binadamu zilizosambaa katika uso wa sayari ya dunia. Tofauti hizi muhimu ndo hutufanya tufanikiwe kwani hutujengea ushindani mioyoni mwetu. Sasa kama unataka kufanikiwa ni lazima ujifunze kuishi na watu wa jamii zingine; kupitia wao utajifunza taaluma na tekinolojia za watu wengine. Ukipata fursa hiyo; itumie vyema kwani unaweza kuibadilisha dunia toka duniani kote!

Kwa wanaotafuta nafasi za kazi na masomo nje ya nchi tafuta kwa kubonyeza hapa