Monday, June 27, 2011

UTANDAWAZI NA MALEZI

Na. Mdee Mwanahiza

Picha kwa hisani ya mtandao

Kamusi ya Kiswahili sanifu toleo la pili (2010) imeelezea maana ya utandawazi kua ni mfumo wa uhisiano wa kimataifa katika nyanja mbalimbali kama vile biashara, uchumi au siasa uliowezeshwa na maendeleo ya teknolojia ya habari yanayofanya mataifa kuwasiliana kiurahisi


Malezi ni njia ya ukuzaji wa mtoto kwa kutarajiwa kufuata tabia na mwenendo unaostahiki, makuzi na mafunzo.kwa watoto na vijana wanaokua katika jamii husika. Kwa ujumla utandawazi ni hali ya mabadiliko katika nyanja mbalimbali za kimaisha ya mwanadamu kama vile Uchumi, Siasa Jamii na Utamaduni na kuwa katika hali ya mfanano mmoja duniani kote. Mabadiliko haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kukua na kuenea kwa sayansi na teknolojia ambayo imesambaa kwa kiasi kikubwa sana na kugusa karibu kila sekta ya maisha ya mwanadamu.

1:1 CHANGAMOTO KATIKA MALEZI

Kutokana na kukua na kuenea kwa utandawazi kumeathiri suala zima la malezi na kupelekea watu hasa watoto na vijana kukosa mwelekeo bora wa kimaisha kutokana na kulega kwa wakala wa malezi.

1:2 WAKALA WA MALEZI

Wakala wa malezi ni vyombo vinavyofanya kazi kwa niaba ya jamii husika katika kuhakikisha kwamba watoto na vijana wanapata malezi na mafunzo mema yanayoendana na jamii hiyo kama vile heshima, nidhamu, staidi mbalimbali za kimaisha ili waweze kujiandaa na maisha yao ya baadae na kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji bila kupotoka na mambo mabaya yasiyostahiki katika jamii.

Hapo awali wakala wa malezi walikua ni familia, shule na dini pamoja na jamii yote kwa ujumla. Lakini kutokana na jamii kuzidi kukua na kuongezeka katika masuala ya uzalishaji, biashara na kupelekea kukua kwa miji kumesababisha kuongezeka kwa wakala wengine wa malezi kama vile vyombo vya habari hasa runinga, tovuti na simu za mkononi, magazeti na majarida mbalimbali. Makundi rika ambayo yanatokana na kukua na kuenea kwa sayansi na teknologia nayo yamekua ni miongoni mwa wakala wa malezi.. Hivyo kwa pamoja tunaweza kusema kisosholojia kwamba kuna wakala watano wa malezi ambao ni Familia,Dini ,Shule, Vyombo vya habari pamoja na makundi rika.

Wakala hawa wa malezi kila mmoja ana nafasi yake katika suala zima la kutoa malezi kwa vijana na watoto wa jamii husika. Kutokana na kipaumbele cha jamii hiyo kwa vijana na watoto.

1:3 FAMILIA

Kisosholojia familia ni muunganiko wa Baba, Mama na Watoto pamoja na ndugu wengine wa karibu. Kimsingi familia ndiyo muhimili mkubwa katika jamii yoyote ile. Mtoto anapozaliwa huanza kupata malezi kutoka kwa Baba na Mama yake pamoja na ndugu wengine wanaoizunguka jamii hiyo ili aweze kukua kwa kufuata mila na desturi za kimaisha katika jamii yake. Mtoto hufunzwa mambo muhimu kama vile heshima,Utii, adabu na nidhamu mbele ya wazazi wake na watu wengine nje ya familia yake pia hufundishwa stadi mbalimbali za Kimaisha na kujiingiza katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ndani na nje ya familia.

Takribani miongo mitatu imepita tangu tulipopata mafanikio ya sayansi na teknologia ambayo yamekua ni chachu ya mageuzi katika familia zetu na maisha ya jamii nzima kwa ujumla. Mageuzi haya yameziathiri sana familia zetu katika suala zima la malezi, hi imesababisha baba na mama kuwaacha watoto wao wadogo na kwenda kufanya kazi za Ofisini mbali na nyumbani kwa siku nzima na kuwaacha watoto na walezi wengine..Hapo awali mwanamke ndiye aliyekua mlezi mkubwa wa familia wakati baba alikua anatoka nyumbani na kumuacha mama na kwenda kutafuta riziki kwa ajili ya familia yote. Mabadiliko haya ya baba na mama wote kwenda kutafuta riziki mbali na familia yao yameleta mmomonyoko wa maadili kwa watoto kwa kiasi kikubwa na kupelekea familia nyingi kusambaratika. wazazi wenyewe kwa wenyewe kulaumiana mwishowe tunaona wazazi wanaanza kupeana talaka.

Wazazi kuachana imekua ni jambo la kawaida katika karne hii ya utandawazi ambako kumepelekea athari mbalimbali katika familia kama vile.

i) Watoto kukosa malezi ya wazazi sahihi

ii) Ongezeko la familia za mzazi mmoja

iii) Ndoa za mikataba

iv) Kuongezeka kwa Umasikini katika ngazi ya kaya na Taifa kwa ujumla.

Kutokana na huu utandawazi tumeona wazazi hawawanyonyeshi watoto wao kwa wakati muafaka unaoshauriwa na wataalamu wa afya ili aweze kuendelea na majukumu yake ya kazini alipoajiriwa au kujiajiri. Hii inapelekea watoto na vijana kupoteza uwezo wao wa kufikiri na kushuka kwa kinga na hivyo kupelekea kupatwa na maradhi ya mara kwa mara na kushindwa kuwa wabunifu wanapokua wakubwa.

Na pia kutokana na huu utandawazi wazazi wanaona kua suala la kulea ni sawa na kupoteza muda wao kwani wana majukumu bora na mazuri kwao wao wenyewe na wala sio kwa watoto wao na kuona kwamba kulea ni kupoteza. bora wawe bize makazini. Hii .inachangia watoto kukosa mwongozo wa maisha yao na kushindwa kutatua matatizo yanayowakabili mbele yao na kushindwa kuendeleza vipaji vyao vya asili kwa ajili ya ;.

i) Kutokujua lugha zao za asili

ii) Kushindwa kumiliki miili yao

iii) Kutokufahamu taratibu na sheria za kijamii

iv) Kutojua mila na tamaduni zao

v) Kutokua na huruma kwa ndugu zao

vi) Uvunjifu wa maadili na kupoteza kabisa malengo ya kimaisha.

Utandawazi huu umeweza kusambaratisha familia zetu moja kwa moja ambapo hapo awali mtoto alikua ni mali ya jamiinzima, anaongozwa na kujirekebisha. Huu utandawazi umesababisha watoto kujitegemea na kujilea wenyewe pasipo kujua mwenendo mzima wa maadili ya jamii zao na matokeo yake ni kama vile.

i) Vijana kutosaidiana na kuthaminiana wao wenyewe.

ii) Kukosa umoja na mshikamano kama ndugu wa moja.

iii) Vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya jamii moja.

vi) Umimi, Udini, Ukabila na Ukanda vimeyatawala maisha yetu

1:4 MAKUNDI RIKA

Rika ni watu ambao wana umri unaokaribiana na kulingana. Kundi rika anaweza kuwa rafiki ,yako jirani yako au hata mwanafunzi mwenzako. Watu wa kundirika wana uwanda mpana wa mazungumzo tofauti na mazungumzo katika familia au jamii kwa ujumla. Makundi rika ya zamani yaliongozwa na mafunzo ya jamii ya jando na unyago. Walifundishwa namna ya kuishi katika hali ya usawa, upendo, uvumilivu na maarifa mbalimbali ili waweze kukabiliana na changamoto za kimaisha pindi watakapokua na familia zao wenyewe ili nao waweze kuwalea watoto wao katika misingi hiyo hiyo yenye tija kubwa katika maisha yao. Kulingana na mabadiliko ya kimaisha yaliyoletwa na utandawazi yameharibu maana halisi ya mafunzo ya jando na unyago kwa vijana katika jamii nyingi za kiafrika ikiwemo Tanzania.

Makundi rika ya sasa hayana mafunzo yoyote ya kimaadili kwa wakubwa na wadogo zao, yametawaliwa na jaziba, hasira, chuki majivuno na dharau kutunushiana misuli mizozo isiyokua na tija kwao, fujo subira imepotea kabisa. Umaarufu ndio ngao ya maisha yao, kudai haki bila kufanya kazi, hawajui wajibu wao sio kwa wao wenyewe kwa familia zao wala kwa jamii zao. Mwelekeo potevu kwa makundi rika haya ni kutokana na utandawazi ambao umepelekea kulega na kupotea kwa mafunzo yetu ya asili ya jando na unyago na kutekwa kwa kiasi kikubwa na tamaduni za kimagharibi hivyo kujishughulisha zaidi na mambo ya kuiga na kushindwa kufanya mambo yao ya ubunifu na kusahau kabisa tamaduni zao katika suala zima la malezi na kujishughulisha na mambo ambayo hayana tija katika maisha yao.

1:5 TAASISI ZA ELIMU

Taasisi za elimu zinajishughulisha na malezi na mafunzo kwa niaba ya jamii husika. Husaidia vijana na watoto kupata mafunzo na stadi mbalimbali za maisha, taaluma na ujuzi ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha pindi wanapohitimu mafunzo yao.

Taasisi hizi huongozwa na sera na mafunzo mbalimbali ambapo wakati mwingine hubadilika kutokana na huu utandawazi tulionao hivi sasa. Utandawazi huu kwa kiasi kikubwa umechangia kuwa na mabadiliko katika sekta ya elimu kama vile mabadiliko ya mara kwa mara katika mitaala yetu ya masomo na kusababisha kubadilika kwa mwenendo mzima wa utoaji elimu katika jamii husika. Kwa mfano hapa kwetu Tanzania kuongezeka kwa mtaala na teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama) ambapo imepelekea watoto na vijana kuweza kutumia tovuti mbalimbali ambapo zingine hazina maadili kwa umri wao na hivyo kuwapelekea kuiga na kufanya vitendo ambavyo havina maadili katika jamii yetu.

Kwa upande mwingine vijana hawa ndiyo wanakua waalimu wa shule hapo baadae ambapo inapeleka ukosefu wa maadili shuleni kwani tayari wameshajifunza mambo tofauti ambayo yameathiri saikolojia zao na hivyo kuwafanya wanafunzi ambao ni watoto kuiga mienendo mibaya ya walimu wao na kupelekea utovu wa nidhamu kwa wanafunzi dhidi ya waalimu wao na kusababisha wanafunzi kutowasikiliza waalimu wao na hivyo kupelekea kuwa na matokeo mabaya katika masomo yao, kupata mimba wakiwa bado shuleni, matumizi ya simu darasani huku mwalimu akiwa anafundisha na kufuta ile dhana ya hapo awali kwamba mwanafunzi ni sawa na mtoto wa mwalimu lakini kutokana na utandawazi mwanafunzi anamwona mwalimu kama rafiki yake wa mtaani tu.

1:6 DINI

Dini ni mojawapo ya wakala wa malezi katika jamii toka jadi mpaka sasa. Dini zinatoa mafundisho mbalimbali ya kimwili na kiroho kwa watu wote hasa hasa watoto na vijana ili waweze kuwa na tabia na mienendo mema katika jamii kama vile namna kuabudu, kuheshimu wakubwa, nidhamu katika kazi na huduma nyingine za kimalezi katika jamii.

Utandawazi umeibua taasisi mbalimbali za kidini ambazo zimekua na mitazamo tofauti tofauti kuhusiana na suala zima la Kimungu na kimalezi katika jamii kama vile kuamini kuwa maombi yanaweza kumsaidia mtu awe na hali nzuri na ustawi wa kijamii katika maisha yake bila kufanya kazi. Hali hii imewafanya watu wengi kuacha kufanyakazi za kijamaa za uzalishajimali na malezi kwenye familia zao na kwenda kwenye vituo mbalimbali vya mahubiri na kukaa huko kwa muda mrefu huku wakiwa na imani kwamba watafanikiwa kimaisha kwa njia ya mahubiri na kumkemea shetani kama ndiye adui mkubwa wa hali ngumu ya maisha yao. Viongozi wa madhebu haya wameshindwa kuwafunza watu mbinu mbalimbali za kupambana na hali ngumu ya maisha kama vile kujituma bila kukata tama na kua waadilifu na waaminifu katikakazi mbalimbali za maendeleo katika jamii zao. Kwa mfano kwa sasa kuna vipindi vingi sana vya maombi na mahubiri kwa njia ya runinga kama vile Saa ya Maajabu.Tutashinda, Joshua Tv, Emanuel Tv ,ukiangalia vile vipindi kuna watu wengi wamehudhuria na sisi wengine huku nje tumekuwa watazamaji hivyo wote kwa pamoja tunaibiwa muda wetu badala ya kwenda kujishughulisha na shughuli zingine za uzalishajimali. Pia kuna baadhi makanisa yanaidhinisha kufunga ndoa za jinsia moja. Huu ni upotoshaji wa maadili kwa viongozi wa dini dhidi ya wafuasi wao wanaowaamini kama sehemu ya malezi kwao na jamii kwa ujumla.

1:7 VYOMBO VYA HABARI

Vyombo vya habari ni pamoja na runinga, tovuti ,magazeti , simu za mkononi na majarida mbalimbali. Vyombo hivyo ni sehemu mojawapo ya malezi na mafundisho kwa watu wa jamii mbalimbali, huelimisha, huburudisha na vilevile huonya kwa kupitia vipindi mbalimbali vinavyooneshwa kwenye runinga kama vile taarifa za habari vipindi vya uzalishaji mali, miradi mbalimbali vipindi vizuri vya watoto na elimu,.kwenye magazeti huandikwa habari na makala mbalimbali. Husaidia kuibua matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii yetu kuonya na kukosoa viongozi wetu kuanzia ngazi ya kaya. hadi Taifa kwa ujumla.

Kwa upande mwingine vyombo hivi vimeweza kupotosha watoto na vijana ambao hawana muongozo mzuri katika matumizi ya vyombo hivi. Kuna mambo mengine yanaoneshwa na kuandikwa katika vyombo vya habari ambavyo havina maadili mazuri katika jamii yetu. Watoto na vijana wasiokua na muongozo ndio waathirika wakubwa kwani hutumia muda wao mwingi kuangalia na kusoma mambo haya kama vile picha za ngono kwenye filamu na tovuti, kusoma majarida ya udaku na kimapenzi, kuangalia tamthilia na vichekesho mbalimbali kama vile Vichekesho vya Hinye Gwedegwede ambvyao kwa sasa imepigwa marufuku. Hali hii imechangia uvunjifu wa maadili kwa kiasi kikubwa sana kwa watoto na vijana wa Taifa letu.

Utandawazi umepelekea vijana kuiga tabia na mienendo mibaya kama vile hisia za kimapenzi na utumiaji wa madawa ya kulevya na kujiingiza katika vitendo vya uhalifu. Hii ni kutokana na kuoneshwa kwa filamu za kiuhalifu na ngumi katika runinga zetu ambayo inapunguza ubunifu na kuendeleza vitendo vya uigaji na vijana kushindwa kujiingiza kwenye shughuli za uzalishaji mali na hatimaye kuwa wahalifu na kushindwa kufanya mambo yenye manufaa katika jamii.

NINI KIFANYIKE ILI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO HIZI

• Wazazi watambue umuhimu na wajibu wao katika suala zima la malezi kwa watoto wao kwani wao ndio walezi wa kwanza katika jamii yoyote ile.Kwani wazazi ndio muhimili mkuu katika familia na taifa kwa ujumla,hivyo waoombwa wayajue na kuyatafakari upya majukumu yao kama wazazi ili waende sambamba na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia pamoja na changamoto zake katika malezi ya familia na taifa kwa ujumla.

• Walimu inawapasa kutambua kwamba wanafunzi wa sasa ni mayatima,wengine hulelewa na baba au mama tu pia wengine wanatoka katika familia zenye migogoro,hivo wanahitaji msaada wao si wa kielimu tu bali hata wa kimalezi ili nao waelewe misingi ya maisha ya jamii zao pindi wanapohitimu masomo yao.Nahii itawasaidi kupambana na hali mbaya za maisha yao ya huko majumbani mwao na kuweza kuishi kwa kufuata mila na tamaduni za jamii zao.

• Viongozi wa dini waache tabia ya kumkemea shetani kana kwamba yeye ndiye chanzo cha matatizo na migogoro katika jamii zetu bali watumie nafasi zao kuwakeme wale ambao ni wafuasi wao katika kuwafunza zaidi masuala yanayotukabili kwa sasa na mienendo mema katika jamii ili nao weweze kuwaunza wanaowategemea na kumuomba mungu awape wepesi katika katika shunguli zao za kila siku na si kumkemea tu shetani.

• Serikali itilie mkazo na isimamie uuzaji wa filamu za ngono na urushaji wa vipindi ambavyo haviendani na maadili ya jamii yetu.isiangalie tu maslahi na haki za watunzi wa tunzi wa mambo haya bali wapige vita mambo ambayo yanaipotosha jamii.Wazazi nao wawaongoze watoto wao katika vipindi vyenye manufaa kwao na kwa jamii kwa ujumla.

• Wazazi na walezi wanatakiwa kuwafahamu kwa undani marafiki wa watoto wao.,na pia wajue walipo watoto wao na wanafanya nini.vilevile watumie muda wao mwingi wa kukaa na watoto waokuliko kuwaacha watumie muda wao mwingi kucheza na marafiki.Hii itawaepushi watoto kujiingiza katika mienendo mibaya.

HITIMISHO

Wakala hawa wa malezi huweza kujenga na pia kubomoa misingi ya jamii.hivyo vinahitaji ushirikiano wangu na wako katika malezi ya jamii ili kuleta maendeleo ya familia zetu na taifa kwa ujumla.

ASANTENI KWA USIKIVU WENU

.

Tuesday, June 7, 2011

Tasnia Ya Muziki Mkombozi wa Vijana

    Tasnia ya Muziki
Mkombozi wa Vijana

Hiki ni kitabu ambacho kinatokana na utafiti uliofanywa kitaalam. Kitabu hiki kinaelezea tatizo la ajira nchini Tanzania. Ukosefu wa ajira ndo hasa tatizo linalowakabili vijana wa Tanzania.

Vijana wengi huko Tanzania wanajituma ili kuepukana na tatizo hili la ukosefu wa ajira. Vijana wa mijini huko Tanzania, wameingia katika tasnia ya Muziki, hususani katika muziki wa vijana al maarufu Bongo flava. Muziki huu unachukuliwa na vijana hao kama aina ya ajira na kwa hiyo basi ilitarajiwa kuwa kazi hii ingekuwa ni mkombozi kwao. Taarifa ambapo hazikuwa zimefanyiwa utafiti zilionyesha kuwa vijana hao hawakunufaika kama ambavyo ilifaa wanufaike. Hali hii kwa hakika ilionyesha ombwe la maelezo; ni kwa sababu ya kutaka kutoa maelezo ndo hasa utafiti ulifanyika ili kuelezea kilichojiri.

Katika ukurasa huu tutakuwa na mfululizo kukielezea kitabu ambazo kinatoa mchango wa namna ya kukabiliana na tatizo hili la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu hapa Tanzania.