Saturday, July 23, 2011

Tunu bora ni Msingi wa Maendeleo ya Watu:Je, Za Afrika ni zipi?

Mlima Kilimanjaro - TANZANIA, paa la Afrika, na Twiga, ambao hupatikana kwa wingi nchini Tanzania.
 Bila shaka hizi ni alama muhimu zinazoitambulisha TANZANIA na bara Afrika.
Hivi tunu za Afrika ya leo ni zipi hasa? Tunu za Afrika ya kina Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Patrice Lumumba, Kenneth Kaunda, Houphouët-Boigny, Frantz Fanon, Nelson Mandela, n.k zilikuwa za umoja, kuungana, kushirikiana, uzalendo kwa bara letu, na kufanya kazi kwa bidii. Tunu za leo ni kuhakikisha kuwa kiongozi anashinda uchanguzi kwa mbinu zozote zile halali ama haramu, mashindano ya kujilimbikizia mali kwa wingi iwezekanavyo. Kwa majumuisho ni ushindani wa ubinafsi. Viongozi na raia wanajenga ubinafsi kwa gharama yoyote ile ikiwa ni pamoja na kuzifanya nchi zetu kuwa vyama wanavyoweza kuvitawala kwa mihula mingi wapendayo wenyewe na mashwahiba wao. Nchi zetu nyingi hatujui hasa nini tunataka kukifanya; tuna maandishi, vielelezo na miongozo mingi mizuri lakini isivyofuatwa katu. Jambo tunalopaswa kujiuliza hapa ni je, kwa tunu hizi za kibinafsi bara Afrika linaweza kweli kuwa mshirika wa maendeleo ya dunia?


Afrika, nyumbani kwa watu zaidi ya milioni 900. Bara hili ni mama ya nchi zaidi ya hamsini. Wenyeji wa bara hilo huitwa Waafrika. Waafrika hawa wana asili mbalimbali; waafrika weusi, waafrika wenye asili ya bara asia, waafrika wa asili bara ulaya. Uanuwai huu unalifanya bara kuwa na utajiri wa tamaduni na hivyo kumiliki tunu kedekede. Kufuatia bahari hiyo ya tofauti, utaona kuwa kuna nafasi ya kupata tunu zilizo bora kabisa mithili ya mbegu za kisasa zenye kufanyiwa tafiti katika maabara na mashamba darasa ya wataalam wa kilimo.


Bara Afrika, kisayansi – daktari Leaky, lasemekana kuwa ndio nyumbani kwa binadamu wa mwanzo hapa duniani. Kwa mantiki hiyo bara hili ilifaa liwe limepiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo katika nyanja mbalimbali kama vile (kv) kisayansi, kijamii, na kadhalika kuliko ilivyo hivi sasa. Barani Afrika nyanja iliyopiga hatua kubwa zaidi ni ile ya kijamii. Nyanja nyingine zingali nyuma mno. Sayansi na teknolojia, elimu bora kwa ujumla wake vingali nyuma mno.


Uwanda wa masuala ya kijamii umepiga hatua kubwa barani humo. Ni hulka ya wanyama wote, wawe wa mwituni ama binadamu mwenyewe, kuwalea na kuwatunza watoto wao na pia kuishi katika jamii. Utaona kuwa kwenye eneo hili Afrika imepiga hatua kubwa hasa. Jamii nyingi katika Afrika bado huishi pamoja watu, familia kadhaa zinazotengeneza ukoo bado huishi pamoja. Ni jambo la kawaida kwenye familia za Kiafrika kuona ndugu wa mbali kabisa ama msaidizi akiishi na kutendewa vyema kama mtoto wa familia mwenyeji. Ni barani humo ndo kijana wa miaka hata thelathini huendelea kuishi kwa baba na mama akiwa tegemezi kabisa. Tamaduni za sehemu nyingine duniani humtaka kijana wa miaka kumi na nane aanze kujitegemea; ajitenge na aanze kujenga maisha yake mwenyewe. Ndugu wa mbali katu hathubutu kuishi na familia ya mbali naye. Tamaduni zote hizi zina mazuri na mapungufu yake, hata hivyo hii si mada ya leo. Kwa leo tuendelee na suala la sayansi na teknolojia hapa barani.


Kwenye uwanja wa sayansi na teknolojia bara Afrika linashika nafasi mbili muhimu, ya mwanzo na ya mwisho kabisa; hakuna mkaganyiko, nitaelezea:

Kwenye ubunifu, ufikirivu; utengenezaji na matumizi ya bidhaa za kiteknolojia bara hilo li nyuma kuliko mabara yote.

Kwenye matumizi ya bidhaa za kiteknolojia na kwa kuwa jaa la bidhaa duni, dhaifu, mbovu, zenye  kukaribia kuisha muda wake na ambazo hutengenezwa ughaibuni, bara letu laongoza. Umeona, hakuna mkanganyiko wowote bali ni ukweli tupu ila tu wenye kuumiza.

Hivyo katika uwanda huu bara Afrika chini ya viongozi na waafrika wote kwa pamoja tunawajibika kujenga uzalendo wa kulipenda bara hili ili kuleta ustawi na maendeleo ya kweli kwa Waafrika na hivyo kutoa mchango kwa maendeleo ya dunia yetu. Kwenye moja ya mada zilizotangulia tuliona kuwa maendeleo huchangiwa kwa kiasi kikubwa na tunu zilizo mahali husika. Kwa mtiririko huo wa kimawazo basi, tujiulize je, hapa barani Afrika tunu zetu ni zipi hasa?

Aina ya maisha na jinsi mtu anavyoishi, ikiwa ni pamoja na nyanja za kijamii, sayansi na teknolojia, husaidia katika kumuainisha binadamu husika. Waafrika kwa asili yao ni wakarimu, marafiki, wenye uteremeshi, na wenye tabasamu la kweli lililo karibu mno takribani muda wote. Furaha, bashasha juu ya binadamu wengine ni tunu zilizojaa pomoni maishani mwa mwafrika. Kwenye sayansi na teknolojia ili mmoja aweze kupiga hatua kubwa kwenda mbele ni wajibu kuwa na tunu za kujali muda zaidi, kujituma na hata kuwa mtumwa wa muda kwa kupangilia kila jambo linalotakiwa kufanyika, mtu kujali na kupenda kazi aifanyayo na kubwa zaidi uzalendo kwa nchi, na bara lake. Tunu hizi na nyingine zenye kuleta tija kwa kazi ni muhimu hasa kwa kufikia malengo mahususi ya maendeleo. Tunu hizi zipo pia barani Afrika lakini zimefichwa mno mithili ya vinasaba dhaifu visivyo na athari yoyote katika maisha ya binadamu. Kisha maelezo hayo basi ni muhimu mno kuimarisha tunu zinazoweza kuchochea maendeleo ya kweli.

Bara Afrika kongwe kwenye tunu za ukarimu, upendo, undugu, n.k limeishangaza dunia baada ya kutumbukia katika lindi la kuporomoka kwa utu na upendo barani humo. Kwa miaka kadhaa kumekuwa na vita pande nyingi barani humo. Vita nyingi barani humo zimechochewa na sababu nyingi za kibinafsi; uroho wa mali nyingi kupindukia, uchu wa mamlaka, na hata hamu ya utukufu binafsi. Jamii ambazo zilitazamwa kama zenye wema, upendo na utu wa hali ya juu ziliingia kwenye janga la mauaji na kusababisha ulemavu wa kudumu kwa watu wao. Kumekuwa na vita pande zote; kaskazini, kusini, magharibi na mashariki hali kadhalika. Wakati jamii nyingi duniani kote zinaungana, baadhi ya jamii za kiafrika zinatengana, zinawindana na kudhoofishana badala ya kusaidiana kuleta maendeleo kwa watu wao.Tumeona kuwa watu hutambulika na kuainishwa kupitia tunu zao.

Hivi tunu za Afrika ya leo ni zipi hasa? Tunu za Afrika ya kina Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Patrice Lumumba, Kenneth Kaunda, Houphouët-Boigny, Fanon, Nelson Mandela, n.k zilikuwa za umoja, kuungana, kushirikiana, uzalendo kwa bara letu, na kufanya kazi kwa bidii. Tunu za leo ni kuhakikisha kuwa kiongozi anashinda uchanguzi kwa mbinu zozote zile halali ama haramu, mashindano ya kujilimbikizia mali kwa wingi iwezekanavyo. Kwa majumuisho ni ushindani wa ubinafsi. Viongozi na raia wanajenga ubinafsi kwa gharama yoyote ile ikiwa ni pamoja na kuzifanya nchi zetu kuwa vyama wanavyoweza kuvitawala kwa mihula mingi wapendayo wenyewe na mashwahiba wao. Nchi zetu nyingi hatujui hasa nini tunataka kukifanya; tuna maandishi, vielelezo na miongozo mingi mizuri lakini isivyofuatwa katu. Jambo tunalopaswa kujiuliza hapa ni je, kwa tunu hizi za kibinafsi bara Afrika linaweza kweli kuwa mshirika wa maendeleo ya dunia?

Monday, July 18, 2011

Siku ya Nelson Rolihlahla Mandela

Leo Jumatatu, 18 Julai ni kumbukumbu ya kuzaliwa Mzee Nelson Mandela, rais wa kwanza wa Afrika Kusini ya Kidemokrasia (18.07.1918). Kadri ya kumbukumbu zangu huyu ndiye mtu pekee ambaye Umoja wa Mataifa umemtengea siku katika mwaka mahususu kwa heshima yake. Hivi leo anatimiza miaka 93 toka azaliwe; ni mmoja kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameishi kwa muda mrefu.

Nelson Mandela ni mtu anayepewa heshima kubwa duniani kote kwa wanaomfahamu na hata wasiomfahamu. Watu wengi hasa nje ya Afrika hususani katika jamii zinazopenda kusoma vitabu wamfahamu kupitia kitabu chake cha "Long Walk to Freedom". Hiki ni kitabu kinachoelezea historia ya maisha yake kwa kina kabisa. Sehemu kubwa ya kitabu hicho ameiandika yeye mwenyewe na tena akiwa gerezani. Hili ni moja ya mambo ya kujifunza toka kwa mzee huyu-maktaba kubwa duniani kote. Tujipange tuandike historia zetu sahihi ili kuiachia jamii na dunia kwa ujumla utajiri wa mawazo kama alivyofanya mzee Mandela. Wengine tulimfahamu mzee Madiba toka enzi za utoto; tukiwa shule ya msingi tuliimba nyimbo za kutaka Mandela achiwe huru na serikali ya makaburu. Utawala wa makabulu ulitawala Afrika Kusini kwa mabavu na kwa misingi ya kibaguzi ya rangi za binadamu; ni udhalimu wa aina yake kwa ustawi wa wanadamu.

Kwanini mzee huyu ni maarufu vile?

Saturday, July 16, 2011

Uhuru wa wahadhiri kimawazo

Makala ya Profesa Mbele juu ya uhuru wa kimawazo wa wahadhiri, kwa hakika, imenitia hamu kubwa kuendelea kuijadili. Nadhani ni suala la msingi kabisa kulitazama hasa hivi leo ambapo kuna vyuo vikuu lukuki hapa nchini. Ni muhimu kuupongeza uongozi wa nchi kwa kuruhusu kuanzishwa kwa vyuo vikuu vingi hapa nchini. Vyuo vikuu vingi moja kwa moja vinamaanisha kukua kwa wigo wa fikra nchini. Kuongezeka kwa fikra ni mwanzo wa ugunduzi na kichocheo kikuu cha maendeleo.

Moja ya masuala makuu katika kipindi cha " Scholarsticism" karne ya 12 na 13 ilikuwa ni kuibuka kwa wingi kwa vyuo vikuu vilivyotoa maarifa ya aina mbalimbali. Kipindi hicho Kanisa lilikuwa na mamlaka makubwa hata juu ya kilichofunzwa vyuo vikuu. Matokeo yake kazi za mwanafalsa Aristotle (384—322 BCE) zilikataliwa, hata hivyo kukataliwa huko kulikuwa kwa muda mfupi tu kwani baadaye kazi za gwiji huyo zilianza kufundishwa katika vyuo vikuu na kuboresha zaidi mawazo kwa wanavyuo na wanazuoni.

Kwahiyo basi ni vyema kwa viongozi wa nchi yetu kulitambua hilo na kuwaacha huru wahadhiri wafanye kazi yao, ambayo kimsingi hulenga kujenga wananchi wenye ukomavu wa kujenga hoja na kuzisimamia ili kuendeleza nchi yao na dunia kwa ujumla.

Kupata mawazo zaidi ya Profesa Mbele soma makala hiyo murua kabisa hapa








.

Tuesday, July 12, 2011

MITUME WA BWANA KATIKA MAZIWA MAKUU


Hiki ni kitabu kinachoelezea safari za mwanzo kabisa za wamisionari wa shirika la wamisionari wa Afrika. Shirika hilo la dini lilianzishwa na Kadinali wa Algiers Charles-Martial Allemand Lavigerie wa Ufaransa.

Kwa hivi wengi wa wamisionari hao walitoka Ufaransa na kuja kutangaza neno la Mungu. Hawa walifika eneo la maziwa makuu hasa Afrika ya Mashariki ya leo; hivyo kitabu hiki kinaelezea historia nzuri ya ndugu hao waliofika kwa mara ya kwanza mwaka 1878. Mbali na kutangaza neno la Mungu, kitabu kinatoa pia historia ya Tanzania toka Bagamoyo hadi Kagera.

Maelezo zaidi juu ya historia ya eneo na habari hizo inapatikana hapa:  http://www.africamission-mafr.org/bagamoyo.htm

Thursday, July 7, 2011

KAZI YA TANU NA TANZANIA YA LEO


Viongozi wa TANU
Flag of TANU.svg
Bendera ya TANU
Tarehe 7 mwezi Julai, 1954 (7.7.1954) ni siku ya kuzaliwa kwa chama cha kisiasa kilichosaidia kudai uhuru wa Tanganyika. Tanganyika National Union (TANU) kilikuwa Chama cha kisiasa kilichowaunganisha wananchi wengi wa kawaida wa Tanganyika na kuwa na nguvu ya pamoja kupigania uhuru wao.

Chama hicho kilikuwa na imani na ahadi za mwanachama. Nazipenda hasa ahadi za mwanaTanu. Ahadi hizo kwa hakika inafaa ziwe ndo TUNU za taifa letu la jamuhuri ya muungano wa tanganyika na Zanzibar- Tanzania. Ahadi za TANU ambazo zimeasiriwa na Chama cha Mapinduzi, (CCM), ni mali ya watanzania wote kwa sababu zililenga kuikomboa nchi na wananchi wote kwa pamoja bila kujali itikadi zao za kisiasa, rangi, dini, wala kabila. Chama cha TANU na pia CCM ndani ya mfumo wa chama kimoja kilikuwa ni mali ya waTanzania wote na hivyo basi ahadi hizo za mwanaTANU ni mali ya waTanzania wote.

Hivi leo tunapokuwa katika mfumo wa vyama vyingi ni dhahiri kuwa vyama vya kisiasa vina katiba, imani na miongozo mbalimbali ya kisiasa, hiyo ni vyema kwa ushindani wa kisiasa. Tanzania kama nchi, pmoja na kwamba ina mwongozo mama-Katiba, inafaa iwe na TUNU ambazo zitafuatwa na wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa. Ahadi za mwanaTANU zinaweza kutufaa sana.

AHADI ZA MWANATANU

(1)Binadamu wote in ndugu zangu na Afrika ni moja

(2) Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote

(3) Nitajitolea nafsi yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma.
(4) Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa.
(5) Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.
(6) Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote.
(7) Nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu.
(8) Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.
(9) Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU na raia mwema wa Tanzania na Afrika.


Tuesday, July 5, 2011

SIKU YA JUMUIYA SAUT - Mtwara

Sehemu ya kwaya ikiongoza maandamano ili kuanza ibada. Naam waimbaji walipendeza hasa! 

SIKU YA JUMUIYA SAUT - Mtwara

Sehemu ya wanajumuiya wakifuatilia matukio ya siku yao kadri yalivyokuwa yakitokea

SIKU YA JUMUIYA SAUT - Mtwara

Jumuiya za watu duniani zinajenga utamaduni wa kukutana kwa malengo mbalimbali. Kuimarisha umoja wao, kujenga uzalendo kwa jumuiya na kadhalika. SAUT Mtwara ni jumuiya ya wasomi; watu wanaoandaliwa kuwa wajenzi wa dunia. Kwa kuwa jumuiya ya aina hiyo ina jukumu kubwa la kujielimisha zaidi ili kuondoa ujinga binafsi na kuisaidia jamii yake, basi inafaa mara mojamoja kupata nafasi ya kujipumzisha. Tarehe 4 Juni, 2011 ilikuwa ni siku ya jumuiya hiyo.

Kulikuwa na shughuli kadha wa kadha kuishi siku hiyo; ikiwa ni pamoja na hotuba anuwai za kitaaluma na maonyesho toka idara za hapo chuoni.

Sehemu ya wanajumuiya ya Saut wakianza sherehe za siku yao kwa maandamano.